Habari
Naibu Katibu Mkuu Mmuya ahimiza Wajasiriamali nchini kutangaza bidhaa zao.
Wajasiriamali nchini wameshauriwa kutumia fursa ya Maonesho ya 21 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Afrika Mashariki kutangaza bidhaa wanazozalisha na kutafuta masoko ya bidhaa hizo ndani na nje ya nchi ili kukuza biashara zao na kuwa wafanyabiashara wakubwa.
Hayo yameelezwa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Uratibu na Bunge Bw. Kaspar Mmuya alipotembelea Maonesho hayo ya 21 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Afrika Mashariki maarufu kama Nguvu Kazi au Jua Kali yanayoendelea katika Viwanja vya Rock City Mall Jijini Mwanza hii leo Desemba 11, 2021.
Alieleza kuwa, Wajasiramali wengi wamekuwa wakibuni bidhaa nzuri, lakini zinashindwa kununuliwa au kupata mafanikio kutokana na kushindwa kutafuta misingi ya kuzitangaza bidhaa hizo, hivyo aliwasihi wajasiriamali walioshiriki na kutembelea maonesho hayo kutangaza bidhaa wanazozalisha na kutafuta masoko ya bidhaa hizo ndani na nje ya nchi.
“Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amekuwa akiwajali wajasiriamali na aliridhia Maonesho haya yaweze kufanyika hapa nchini ili kuwawezesha kupata fursa ya kutangaza bidhaa zao, kubadilishana taarifa, kukuza ujuzi, kukuza masoko ya bidhaa na kukuza teknolojia ya utengenezaji wa bidhaa pamoja na kuongeza fursa za ajira za staha nchini, hivyo ni vyema wajasiriamali wakatumia fursa ya maonesho haya kujitangaza kwa wingi,” alisema Mmuya
Aliongeza kuwa, Serikali kwa kutambua umuhimu wa maonesho hayo inategemea kuwa Wajasiriamali walioshiriki wanakuwa wabunifu na kutengeneza bidhaa zenye ubora wa kiwango cha juu ili waweza kuleta ushindani katika soko la afrika mashariki ambalo lina idadi kubwa ya watu na kuhakikisha bidhaa hizo ziweze kuuzika na kukuza pato la Taifa.
Aidha, Naibu Katibu Mkuu huyo alitoa wito kwa Halmashauri zote nchini kuhakikisha zinaendelea kuwawezesha Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu kupitia mikopo ya asilimia 10 yaani 4% kwa Wanawake, 4% Vijana na 2% Wenye Ulemavu ili waweze kuzalisha ajira zaidi na kuanzisha viwanda vidogovodogo na vya kati vitakavyowasaidia kuzalisha bidhaa zenye ubora wa hali ya juu.
Naye, Mjasiriamali kutoka kikundi cha Moro Batiki, Bi. Elieth Mkaanga ameishukuru Serikali kwa kutambua mchango wa Wajasiriamali na alipongeza kuanzishwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo imewasaidia wajasiriamali katika nchi hizo wanachama kujitathmini na kuwapatia fursa ya kutimiza malengo yao na malengo ya kuanzishwa kwa maonesho hayo ya nguvu kazi au jua kali.
MWISHO