Habari
Vitendo vya kihalifu katika Maziwa na Bahari kuu nchini Kudhibitiwa
Serikali ya Tanzania kupitia Ofisi ya waziri Mkuu kwa kushirikiana serikali ya Japan na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), wamezindua mpango wa Kukabiliana na Vitendo vya Kiuhalifu katika Maziwa na Bahari nchini. Mradi huo utaimarisha juhudi za kupambana na vitendo vya kihalifu hususani; uvuvi haramu, uhamiaji haramu, usafirishwaji wa nyara za serikali pamoja na upitishwaji wa madawa ya Kulevya.
Akiongea wakati wa kuuzindua Mradi huo Jijini Dodoma, leo tarehe 12 Februari 2021, Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu), Bi. Dorothy Mwaluko, amefafanua kuwa mpangoi huo utatekelezwa kwa kipindi cha mwaka mmoja, lengo lake ni kuimarisha usalama katika maziwa na bahari na utanufaisha wavuvi kwa kuwapa elimu ya njia bora za uvuvi na kujenga miundombinu ya kisasa ya kukausha samaki.
“Serikali inakusudia kutekeleza mpango huu kwa ufanisi kwa kuhakikisha wadau wa mradi huu wananufaika na utekelezaji wake. Kupitia mradi huu serikali itaweza kununua boti ili kuimarisha doria katika bahari na hivyo kuweza kupunguza vitendo vya kihalifu. Ni matarajio yangu mpango kazi huu utakidhi mahitaji tulionayo ya kuainisha mfumo wa kitaasisi, makundi ya wadau na wajibu wao katika kupambana na uhalifu katika maziwa na bahari.” Amesisitiza Mwaluko
Awali akiongea katika uzinduzi huo; Mwakilishi kutoka Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Bi. Christine Musisi, ameeleza kuwa wanaamini Maendeleo ya Uchumi na ustawi wa watu hauwezi kupatikana bila kuwa na ulinzi imara katika maziwa na bahari pamoja na uboreshwaji wa maisha ya watu wanaoishi katika maeneo ya maziwa na bahari. Ameongeza kuwa Kupitia mpango huo wataiwezesha serikali ya Tanzania kufanikisha malengo yake ya kuimarisha uchumi wa bluu.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah ameeleza kuwa mpango huo ni muhimu kwa nchi kwa kuwa utajikita katika kupambana na uvuvi haramu ambao umekuwa ukisabbisha uharibifu wa rasilimali katika Bahari. Ameongeza kuwa kwa sasa nchini asilimia 30 hadi 40 ya samaki wanaovuliwa na wavuvu wadogo wadogo wanaharibika, hivyo ujio wa mpango huo utakuwa ni mkombozi kwa wavuvi kwa kuboresha miundo mbinu ya kukausha samaki ambayo itawezesha kuongeza thamani samaki na kupata soko la kikanda.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya mambo ya ndani, Christopher Kadio, ameongeza kuwa mpango huo utaisiadia wizara hiyo katika uwezo wa kudhibiti vitendo vya kiuhalifu hususan kwenye meneo ya ufukwe wa bahari na maziwa. Amesisitiza kuwa utekelezaji wa mpango huo utawezesha katika kuimarisha uchumi wa nchi na ustawi wa jamii.
Utekelezaji wa mpango huo utasimamiwa na Kamati ya Usimamizi ambayo pamoja na kusimamia jukumu la utekelzaji wa Mradi huo, kamati itakuwa na jukumu la kuidhinisha mpango kazi na taarifa ya utekelezaji. Mwenyekiti wa Kamati hiyo ni Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu). Wajumbe wengine wa Kamati hiyo ni Makatibu wakuu wa Wizara ya TAMISEMI, Ofisi ya Makamu wa Rais, Feddha na Mipango; Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Mambo ya ndani, Maliasili na Utaliina Ujenzi na Uchukuzi.
ENDS-