Habari
Majaliwa: Watanzania tuwapuuze wasiolitakia mema Taifa
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amewataka Watanzania waendelee kushikamana, kudumisha amani na wapuuze kauli za chuki zinazotolewa na watu wasioitakia mema nchi kuhusu afya ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwani ni mzima wa afya.
”Tuendelee kufanya ibada na kupata mawaidha yanayohamasisha amani na utulivu. Rais Dkt. Magufuli ni mzima wa afya anaendelea na majukumu yake wakati sisi wasaidizi wake tukizunguka kuwahudumia wananchi. Leo nimezungumza naye na anawasalimia.”
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Machi 12, 2021) baada ya kushiriki sala ya Ijumaa mjini Njombe, ambapo amesisitiza kuwa Rais anafanya kazi kulingana na mpango kazi wake. Amesema wananchi wanatakiwa kushikamana na kuifanya nchi kuendelea kuwa na amani na utulivu.
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwasisitiza wananchi waendelee kuliombea Taifa na wawapuuze baadhi ya Watanzania ambao hawapo nchini na wamekuwa wakitoa kauli za chuki kwa sababu hawapendi maendeleo ya nchi na wanatamani kuona Taifa likiporomoka.
”...Tuwapuuze baadhi ya Watanzania ambao wamejawa na chuki tu, wamejawa na husda tu na wanatamani kuwachonganisha na kutaka kushuhudua Taifa hili likiporomoka.”
”Kuanzia juzi hata leo asubuhi nimeona Watanzania wenzetu wenye husda tena hawako ndani wako huko wanashawishi vyombo vya Kimataifa viseme Rais wa Tanzania anaumwa kajifungia hizo ni chuki tu, husda tu.”
”Watanzania tulieni uongozi wenu upo imara na mafanikio tunayaona, kumzushia rais ugonjwa ni chuki, wanasema atoke aende wapi? Ulishamkuta siku moja anazurura Kariakoo? Rais anampango wake wa kazi si mtu wa kuzurura.”
Waziri Mkuu amesema Rais Dkt. Magufuli anawasaidizi wake kuanzia ngazi ya Taifa hadi kijijini na kwamba anafanyakazi kulingana na mpangokazi wake, hivyo amewataka Watanzania waendelee kuwa na amani huku wakiamini Serikali yao.
-End-