Habari
Majaliwa: Waajiri toeni ushirikiano kwa wenye ulemavu
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewatakaa waajiri wote nchini wawe tayari kuwapokea na kuwapa ushirikiano watu wenye ulemavu ili waweze kupata fursa ya kuchangia katika shughuli za ujenzi wa Taifa kama sheria ya ajira na mahusiano kazini inavyotaka.
Pia amewaagiza waajiri wote wahakikishe wanazingatia sheria namba tano (5) ya mwaka 2003 kuhusu afya na usalama mahala pa kazi kwa kusajili maeneo yao ya kazi ili mamlaka husika ikiwemo OSHA ziweze kutoa ushauri na namna ya kuwalinda wafanyakazi na uwekezaji wao.
Waziri Mkuu ametoa wito huo leo (Alhamisi, Desemba 3, 2020) kwenye sherehe za kuadhimisha miaka 60 ya kuanzishwa kwa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) zilizofanyika katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam. Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni ‘Uchumi wa Kati Endelevu Unaotokana na Mazingira Bora ya Biashara na Maendeleo ya Ujuzi Tanzania.’
Amesema anatambua umuhimu wa kujenga uchumi wenye manufaa kwa watu wote hususani watu wenye ulemavu, ikiwemo kazi nzuri inayofanywa na ATE kupitia Mradi Jumuishi kwa Wote (All Inclusive Project) kwa kushirikiana na Asasi isiyo ya Kiserikali ya CEFA kutoka Italia, CCBRT na wadau wengine unaolenga kuboresha afya na hali ya kiuchumi kwa watu wenye ulemavu katika jijiji la Dar es Salaam.
Pia, Waziri Mkuu amewaagiza waajiri wote wajali maslahi ya watumishi kwa kuwasilisha kwa wakati na kwa usahihi michango ya watumishi katika mifuko ya hifadhi ya jamii. ’’Ninazo taarifa za kuwepo waajiri ambao wanadaiwa malimbikizo ya michango na adhabu jambo ambalo husababisha mateso na usumbufu katika ulipaji wa mafao kwa watumishi wengi wanapostaafu.’’
Akizungumzia, kaulimbiu ya maadhimisho hayo, Waziri Mkuu amesema inahimiza umuhimu wa kuendeleza ujuzi katika kuimarisha uchumi wa kati,hivyo amewahamasisha waajiri wawekeze kwenye usimamizi mzuri wa rasilimali watu kama moja ya nyenzo muhimu za kukuza uchumi wa Taifa.
’’Ni vema wote tukatambua kwamba, suala la kuendeleza ujuzi ni moja ya kipaumbele kilichopo katika Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025. Pia ifahamike kuwa Serikali sasa imekamilisha awamu ya kwanza ya kutekeleza mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano na sasa ikiwa ni awamu ya pili ambayo inalenga kuongeza idadi ya watu wenye ujuzi wa kutosha kama kiungo muhimu katika ukuaji wa uchumi wetu na ustawi wa jamii nzima.’’
Waziri Mkuu amewataka waajiri wote nchini waendelee kuunga mkono juhudi za kuendeleza ujuzi kwa kuwapatia fursa vijana wanaotoka katika taasisi mbalimbali za elimu kuweza kujifunza katika maeneo yao ya kazi kwani suala hilo litasaidia kutengeneza Taifa lenye vijana wengi wenye ujuzi kwa manufaa ya nchi.
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema Serikali iko tayari kujadiliana na Sekta binafsi ili kuona Tanzania inaendelea kuwa sehemu salama zaidi ya kufanya biashara duniani. ’’Hivyo natumia fursa hii kusisitiza kwamba Serikali yetu imejipanga kikamilifu kuhakikisha inaendelea na utaratibu huo ili kukuza biashara na uwekezaji hatimaye kuongeza fursa za ajira nchini.’’
Maadhimisho hayo amehudhuriwa na Mwenyekiti wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Bibi Jayne Nyimbo, Makamu Mwenyekiti wa ATE, Bw. Felix Kagisa, Mkurugenzi Mtendaji na Afisa Mtendaji Mkuu wa ATE, Dkt. Aggrey Mlimuka, Kaimu Katibu Mkuu TUCTA, Bw. Saidi Wamba, Wajumbe wa Bodi ya ATE pamoja na wadau mbalimbali wa masuala ya ajira.
-ends-