Habari
Majaliwa: TPA hakikisheni meli za MV Njombe na MV Ruvuma zinafanya kazi
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) ihakikishe meli za mizigo na abiria za MV Ruvuma na MV Njombe zinaanza kazi ya kutoa huduma mara moja.
“Kutaneni na wafanyabiashara wakubwa mfanye nao mazungumzo ili kuona namna meli hizo zitakavyofanyakazi ya kusafirisha mizigo yao nchini pamoja na nchi jirani ya Malawi.”
Ametoa maagizo hayo leo (Jumatatu, Agosti 2, 2021) alipotembelea Bandari ya Itungi wilayani Kyela mkoani Mbeya na kukuta meli hizo zimeegeshwa bandarini hapo.
“Sisi tunafursa ya kuwa na maziwa na mafundi wa kampuni ambazo zinatengeneza hata boti lakini hatuzitumii kwa hiyo TPA lazima iwe na wabunifu watakaowezesha wananchi kunufaika.”
“Meli zimekaa hapo kwa kushindwa kwenda kubeba makaa ya mawe kwa kushindwa kukubaliana bei nyie mnataka shilingi ngapi na zinapokaa hapo mnapoteza shilingi ngapi.”
Waziri Mkuu amesema mamlaka hiyo imeshindwa kufanya hesabu kuona gharama za uendeshaji wa kwenda kubeba makaa ya mawe kwa kuanzia na faida ndogo kuliko kuziegesha tu.
Pia, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ifuatilie kwa karibu utendaji wa mamlaka hiyo pamoja na bandari zake ili kuhakikisha mabadiliko yaliyofanyika yanakuwa na tija.
Amesema Serikali imetumia fedha nyingi katika ujenzi wa meli hizo kwa lengo la kutoa huduma za kusafirisha mizigo katika ukanda wa ziwa Nyasa, hivyo ni lazima zifanyekazi iliyokusudiwa.
Amesema TPA imefanya mabadiliko na anataka kuona mabadiliko hayo yanakuwa na tija ikiwa ni pamoja na matumizi mazuri ya bandari zilizo kwenye ukanda wa ziwa Nyasa na Tanganyika.
Wakati huo huo, Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kutoa pole kwa familia ya aliyekuwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Meli ya Songoro, Mzee Songoro ayefariki hivi karibuni.
Waziri Mkuu amesema Serikali inatambua na itaendelea kuienzi kazi nzuri iliyofanywa na mkurugenzi huyo, hivyo amewasihi wanafamilia na wafanyakazi wa kampuni hiyo wamuenzi kwa kufanyakazi kwa bidii.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Uhandisi wa TPA, Dkt Baraka Mdima amesema Meli ya MV Mbeya II iliharibika baada ya kupigwa na wimbi wakati ikiwa safarini na sasa ukarabati unaendelea na umefikia asilimia 80.
-End-