Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Majaliwa: Simamieni miradi kwenye Wilaya, Halmashauri


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Wakurugenzi wa Ofisi ya Rais (TAMISEMI) wahakikishe wanasimamia na kuratibu miradi iliyoko kwenye mikoa, wilaya na Halmashauri zilikozo kwenye sekta wanazosimamia.

“Nendeni mkasimamie uratibu wa miradi kwenye mikoa, wilaya na halmashauri. Tambueni miradi iliyoko ni mingapi, mingapi iko vizuri, mingapi inasuasua kisha toeni taarifa kwa Katibu Mkuu,” alisema.

Ametoa wito huo jana (Jumanne, Mei 31, 2022) alipokutana na Waziri wa TAMISEMI, Naibu Mawaziri, Katibu Mkuu, Naibu Makatibu Wakuu pamoja na Wakurugenzi na Wakuu wa taasisi za wizara hiyo kwenye kikao alichokiitisha jijini Dodoma ili kuwakumbusha wajibu wao.

Waziri Mkuu aliwapongeza viongozi hao kwa kusimamia vizuri miradi inayotekelezwa kwa fedha zilizotolewa chini ya Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO-19 ambayo kwenye elimu ilichukua muda mfupi sana kukamilika.

“Kama tuliweza kusimamia miradi ya fecha za UVIKO-19 na kuikamilisha chini ya miezi mitatu, ni kwa nini sasa hivi tushindwe kufanya hivyo kwa miradi mingine? Kuna miradi ilianza kujengwa kabla fedha za UVIKO-19 hazijatolewa, lakini hadi sasa haijakamilika. Ni kwa nini hali iko hivyo? Mkurugenzi jiulize, ulipopewa mradi, ulipaswa kuisha lini? Waziri na Naibu Mawaziri simamieni hilo na mfanye tathmini,” alisema.

Akizungumzia mgawanyo wa majukumu kwa wakurugenzi wa wizara na wakuu wa idara, Waziri Mkuu aliwataka wakae ofisini na kutoa maamuzi ili kazi nyingine zifanyike badala ya kuweka msisitizo kwenye safari. “Kaeni ofisini na kufanya maamuzi, hizo safari wapeni wasaidizi wenu, na wakirudi wawape mrejesho,” alisisitiza.

“Katibu Mkuu na Naibu Makatibu Wakuu fuatilieni utendaji wa Wakuu wa Idara. Kuwe na utaratibu wa kuondoka, siyo mtu anatimka tu kwenda mkoani au wilayani,” alisema.

Amewahimiza waandane mipango yao ya kazi kwa kufuata Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020 ambayo imeainisha kila sekta na kutaja miradi inayotakiwa kusimamiwa kwenye mikoa, wilaya, Halmashauri na kata nchini.

“Nilishaelekeza kila mkuu wa idara apate nakala ya Ilani ya CCM na awe nayo mezani kwake. Tunatakiwa tuipitie na tuainishe mpango kazi kila mmoja kulingana na sekta yake,” alisema.

Kuhusu matumizi ya fedha za umma, Waziri Mkuu alisema kwenye maeneo mengi alikopita amebaini kuwa matumizi ya fedha siyo mazuri na akasisitiza wasimamie eneo hilo ili kupata thamani halisi ya fedha (value for money) kwenye miradi inayotekelezwa na Serikali.

Aliwataka wajiepushe na tamaa ya kutaka kuhusika kwenye manunuzi ya vifaa vya miradi hiyo. “Tuna kamati za ujenzi katika kila kata. Iweje wao wafanye manunuzi wakati kamati zipo na zinasimamia? Wakuu wa idara mjiondoe kwenye nafasi ya kutuhumiwa. Hebu cheki kanuni zenu kuhusu kamati za ujenzi na masuala ya manunuzi zinasemaje.”