Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Majaliwa: Serikali inaendelea kuboresha sekta ya elimu


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ipo makini na inaendelea kuboresha sekta mbalimbali nchini ikiwemo ya elimu ili kuweka mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia.

Pia, Mheshimiwa Majaliwa amewaagiza Maofisa Elimu wahakikishe wanatenga muda na kwenda katika shule kwa ajili ya kuzungumza na walimu na wanafunzi na kusikiliza kero zao na kushirikiana nao kuzitafutia ufumbuzi badala ya kusubiri ziara za viongozi wa Kitaifa.

Ameyasema hayo leo (Jumamosi, Novemba 27, 2021) wakati akizungumza na walimu, watumishi wa shule na wanafunzi wa shule ya Sekondari ya Wasichana ya Kayuki baada ya kukagua na kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa madarasa manne shuleni hapo akiwa katika ziara ya kikazi wilayani Rungwe, Mbeya.

“Mheshimiwa Rais Samia ametoa fedha nyingi katika sekta ya elimu ili kuhakikisha shule za msingi na sekondari, vyuo vya elimu ya juu na ya kati vinaboreshwa, hivyo tumieni vizuri miundombinu hii kwa kusoma kwa bidii na mtimize ndoto zenu.”

Kadhalika, Waziri Mkuu ameiagiza Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ihakikishe shule hiyo kongwe inaingizwa katika mpango wa kukarabatiwa kwa kuwa baadhi ya majengo yake ni chakavu. “Pamoja na Serikali kuendelea kuboresha maslahi ya walimu naelekeza shule hii ikarabatiwe.”

Naye, Mkuu wa shule hiyo Mwalimu Bertha Sarufu amemshukuru Mheshimiwa Rais Samia kwa kuwapatia jumla ya shilingi milioni 80 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa. Shule hiyo ya Sekondari ya Wasichana Kayuki ni ya kidato cha kwanza hadi cha sita na ina jumla ya wanafunzi 1,282.

Pia, Mheshimiwa Majaliwa amekagua na kuweka jiwe la msingi kwenye mradi wa ujenzi wa maktaba na chumba cha TEHAMA katika chuo cha Ualimu Tukuyu, ambapo amewasisitiza viongozi wote wasimamie vizuri miradi inayotekelezwa katika maeneo yao ili iweze kutoa matokeo chanya.

Mheshimiwa Majaliwa amewataka watumishi wa umma nchini watimize majukumu yao na washughulikie matatizo ya Watanzania ipasavyo.“Tushughulike na matatizo ya wananchi, Wakuu wa Mikoa na Wilaya hakikisheni miradi yote inayotekelezwa, inakamilika kwa wakati na kwa viwango.”

Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Mheshimiwa Rais Samia amesisitiza kila mtumishi wa umma kuwatendea haki Watanzania ikiwa ni pamoja na kuwahudumia katika sekta zote. “Hili ni jukumu letu, tunapaswa kuwa wawajibikaji, tufanye kazi na ziwe za matokeo chanya”

Kwa upande wake, Mshauri Elekezi wa mradi huo kutoka Chuo cha Ufundi Arusha Mhandisi Saidi Shaushi amesema ujenzi wa jengo hilo la maktaba ambao kwa sasa umefikia asilimia 70 unagharimu shilingi milioni 346. Mradi huo unatekelezwa kupitia mfumo wa force account.

Naye, Mkuu wa chuo hicho amesema kukamilika kwa ujenzi wa mradi huo pamoja na ukarabati wa maabara tatu za kemia, baiolojia, fizikia na upanuzi wa chumba cha darasa la TEHAMA kutaboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia kwa kiwango kikubwa katika kuandaa walimu bora wa stashahada katika masomo ya sayansi na TEHAMA.