Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Majaliwa: SEKOMU kamilisheni mahitaji ya TCU


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameutaka uongozi mpya wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Mashariki inayomiliki Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Sebastian Kolowa (SEKOMU) ukamilishe mahitaji ambayo yataiwezesha Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) ikiruhusu chuo hicho kiendelee na udahili.

Ametoa wito huo leo (Jumamosi, Januari 16, 2021) wakati alipokutana na Askofu Mteule wa Dayosisi hiyo, Mchungaji Dkt. Msafiri Mbilu pamoja na viongozi wengine wapya waliochaguliwa. Kikao hicho kimefanyika Ofisi ya Waziri Mkuu, Mlimwa, Dodoma.

Waziri Mkuu amefikia hatua hiyo baada ya Askofu Dkt. Mbilu kuiomba Serikali iusaidie uongozi wa Dayosisi hiyo kukiwezesha chuo hicho kifunguliwe na kuruhusiwa kufanya udahili. Mwaka 2018, TCU ilikisitishia chuo hicho kufanya masomo na udahili wa wanafunzi katika ngazi zote za masomo baada ya kubainika kuwa hakina vigezo.

“Kamilisheni mahitaji yatakayokifanya chuo chenu kiweze kuendelea kufanya udahili. Taarifa niliyonayo ni kwamba, TCU walishakuja kukutana nanyi na kufanya ukaguzi, walitoa mahitaji kadhaa ambayo mnapaswa kuyakamilisha na nimesikia mmeridhia na kazi hiyo inaendelea.”

Mbali na maagizo hayo, pia Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwashukuru viongozi wa dini nchini kutokana na mchango mkubwa wanaoendelea kuutoa kwa Taifa. “Viongozi wa dini ni watu muhimu sana, nchi imetulia na ina amani, hivyo kuwa kimbilio kwa waliokosa amani makwao.”

Awali, Askofu Dkt. Mbilu alimweleza Waziri Mkuu kwamba Chuo Kikuu cha SEKOMU kimezuiliwa kufanya udahili kutokana na changamoto mbalimbali za kimfumo wa ndani ya Dayosisi na ndani ya chuo ikiwa ni pamoja na kuwa na viongozi wanaokaimu kwa muda mrefu jambo ambalo kwa sasa tayari limeshapatiwa ufumbuzi.

Alitaja changamoto nyingine kuwa ni madeni makubwa yakiwemo ya mishahara ya watumishi, ambapo tayari uongozi umeshaanza kulipa malimbikizo hayo na wameweka mipango ya kumaliza kulipa madeni hayo. Pia, kiongozi huyo alisema chuo kimeshapata waalimu wa kutosha kwa ajili ya kufundisha wanafunzi mara kitakapofunguliwa.

Askofu Dkt. Mbilu alisema kabla ya kufungiwa, Chuo Kikuu cha SEKOMU kilikuwa kinatoa elimu katika nyanja mbalimbali ikiwemo elimu maalumu ya kuwahudumia watu wenye ulemavu katika ngazi ya shahada na shahada ya uzamili, hivyo kimetoa wataalamu wengi.

-Ends-