Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Majaliwa kupeleka timu maalum kuchunguza uharibifu wa miundombinu ya reli kiwanda cha Kilua


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema atapeleka timu maalum kwa ajili ya kuchunguza uharibifu wa reli iliyojengwa na Serikali kwenye kiwanda cha kuzalisha Nondo cha Kilua kilichopo Mlandizi Mkoani Pwani.

 Amesema kuwa Serikali iliamua kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa reli katika kiwanda hicho ili kurahisisha usafirishaji wa nondo kutoka kiwandani hapo kwenda katika maeneo mbalimbali nchini kupitia reli ya kati.

Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo leo (Jumatatu Novemba 15, 2021) wakati alipotembelea kiwanda cha kuzalisha nondo cha Kilua kilichopo Mlandizi Mkoani Pwani.

“Kampuni yenyewe ndiyo iliyoandika barua kuomba reli na Serikali ilitenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa reli kwenye kiwanda hiki, lakini mmeamua kuiua na kuijengea zege na vyuma vingine mmechukua”

Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan itaendelea kuwaunga mkono wawekezaji ili kuhakikisha wanafaidika kutokana na shughuli zao za uwekezaji hapa nchini.

Aidha, Waziri Mkuu amewataka Watanzania wanaofanya kazi katika viwanda mbalimbali nchini wawe mabalozi wazuri ili kuisaidia Serikali kutimiza malengo ya kutatua changamoto ya ajira kupitia sekta hiyo. “fanyeni kazi, ninyi ni mabalozi wazuri kwenye hili wasaidieni wawekezaji watimize malengo yao.”

Pia, Mheshimiwa Majaliwa amewataka wanasheria katika kiwanda cha Kilua kutanguliza uzalendo pale wanapotekeleza majukumu yao. “Wasaidieni kujua kwenye sheria suala gani lipoje, saidieni kuhakikisha sheria zinatekelezwa ipasavyo  na yeyote awe wa Mtanzania au mgeni msiegemee upande mmoja.”