Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Majaliwa: Barabara ya Lami Katavi-Tabora kufungua fursa za kiuchumi


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami kutoka Tabora hadi Katavi utafungua fursa za kiuchumi kwa wananchi wa mikoa hiyo.

Amesema kuwa ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa Kilomita 335.8 ambao tayari umekamilika kwa asilimia themanini 80% na itagharimu Shilingi Bilioni 450.8 pia itakuwa ni kiunganishi cha biashara na usafirishaji wa mizigo kutoka Tanzania kwenda nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Burundi.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Agosti 27, 2021) alipokuwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo katika Wilaya ya Mpanda Mkoani Katavi, Amesema ujenzi wa mradi huo umeenda sambamba na uboreshaji wa miundombinu mingine ya usafirishaji ikiwemo bandari na reli.

“Leo tunaifungua Katavi, tunaufungua Mkoa huu kwa fursa, Ujenzi wa Bandari ya Karema ambayo itakamilika mwezi wa tatu mwakani, na bandari hiyo ni kubwa kuliko zote katika eneo la ziwa Tanganyika ukiondoa ya kibirizi Kigoma na ina uwezo wa kuhifadhi makontena zaidi ya elfu moja na miatano (1500) kwa wakati mmoja, Wafanyabiashara wa Tanzania wajipange kufanya Biashara na nchi jirani”

Aidha, Waziri Mkuu amesema tayari Rais Samia Suluhu Hassan, amesaini mkataba wa ujenzi wa meli kubwa mbili kwenye ziwa Tanganyika ambayo meli ya kwanza itabeba abiria na mizigo na nyingine itakuwa ni ya mizigo tu, itafanya kazi kutoka Kibirizi, Sibwisi, Karema na Bandari za nchi jirani huku mipango ya uboreshaji wa reli ikiwa tayari imekamilika.

Mradi huo umeajiri jumla ya wafanyakazi 2000 na kati ya wafanyakazi hao asilimia tisini na sita ni Wazawa wakiwemo wataalam wa kawaida na asilimia nne ni wataalam kutoka nje ya Tanzania.

“Nataka nitoe tahadhari kwa TANROADS, kwa kazi niliyoiona katika eneo lilobaki la asilimia 20 na bado miezi miwili ni lazima wajiridhishe kuhakikisha kazi iliyobaki inafanywa vizuri, kila hatua lazima iwekwe kwa ukamilifu na kwa thamani sababu eneo lililobaki ni kubwa hivyo nendeni mkasimamie lakini mjiridhishe na viwango.”

Akiwa katika eneo la Koga na kukagua ujenzi wa daraja Majaliwa Amesema ni vyema TANROADS Wakaandaa kanzi data ya kuwatambua wakandarasi wa kitanzania wanaofanya kazi katika miradi mikubwa ya ujenzi ikiwemo ujenzi wa madaraja ili waweze kujifunza na kupata utaalam kutoka kwa wakandarasi wa nje ili baadae kazi hizo za ujenzi zifanywe na vijana wa kitanzania.

-End-