Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Dkt. Jingu akutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Ujerumani Nchini.


KATIBU Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. John Jingu amesema Serikali itaendelea kushirikiana na balozi zilizopo nchini kwa ajili ya maendeleo ya Taifa kwa ujumla.

Ameyasema hayo Februari 10, 2022 wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania Mhe. Regina Hess ofisini kwake Jijini Dodoma.

Alisema lengo la kukutana na balozi huyo ni kuendelea kukuza na kulinda uhusiano uliopo kati ya Serikali ya Tanzania na Ujerumani ambazo hushirikiana katika masuala mbalimbali ya maendeleo.

“Tumefurahi sana kupata ugeni huu kama serikali kwa sababu ni njia mojawapo ya kukuza mahusiano yetu tuliyonayo tangu huko nyuma tunafahamu kwamba nchi ya Ujerumani imekuwa na mchango mkubwa katika Taifa letu kupitia sekta mbalimbali,”alisema Dkt. Jingu.

Pia alisisitiza kwamba Serikali haitasita kusimamia vyema utekelezaji wa miradi mikubwa inayoendelea kujengwa nchini kwani hutoa fursa kwa wananchi kupata fursa za ajira na kujikwamua kiuchumi na kuifanya Tanzania kuwa ya mfano katika mataifa mengine.

Kwa upande wake Balozi wa Ujerumani nchini Mhe. Regina Hess aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano wake kwa Serikali ya Ujerumani huku akipongeza juhudi za Rais wa Awamu ya Sita Mhe.Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha wananchi wake wanapata maendeleo na uboreshwaji wa miundo mbinu.

“Nitumie nafasi hii kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan anafanya mambo makubwa sana kwanza kushirikiana na sisi na ndiyo maana tuko hapa nchini pia jitihada zake za kuboresha huduma kwa wananchi zikiwemo huduma za afya, ujenzi wa madarasa, miundo mbinu ya barabara na nyinginezo,” alieleza Mhe. Balozi Hess.

Aidha Mwakilishi wa GIZ Tanzania Bwa. Richard Shaban alieleza kwamba hatua ya Serikali ya kushirikiana na mataifa mbalimbali hufungua fursa mpya kwa Taifa za kiuchumi, kijamii na kuifanya kuwa nchi yenye ustawi kwa wananchi wake pamoja na kukuza uchumi wa Taifa.

=MWISHO=