Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

KATIBU MKUU NZUNDA AWAASA VIJANA KUCHAPA KAZI KWA BIDII


KATIBU Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu, Bunge Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu Tixon Nzunda amewataka Vijana Kujenga msingi wa kupenda kufanya Kazi ili kujiletea Maendeleo na Taifa kwa ujumla.

Katibu Mkuu huyo aliyasema hayo Septemba 8, 2021 Jijini Dodoma katika ufunguzi wa Mkutano wa Vijana wa kupitia na kuthibitisha rasimu ya Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana, mkutano huo ulishirikisha Vijana 119 kutoka mikoa 22 nchini ambapo alisema Maendeleo ya Taifa yanachangiwa na sehemu kubwa ya vijana.

Alisema kupitishwa kwa sera hiyo kutasaidia ustawi wa Vijana katika kuwa na Mfumo rafiki ambayo itawawezesha kujiajiri na kuondokana na changamoto ya ajira pamoja na utegemezi kwenye familia na Taifa zima.

“Kupitia Sera ya mwaka 2007 tuliona Kuna umuhimu wa kufanya mapitio kuendana na hali ya sasa, hivyo rasimu ya sera hii imepitiwa na wadau wa maendeleo na kujadiliwa ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu pia imepitiwa mikoa takribani Mikoa 13 ikiwemo Pwani, Kigoma, Arusha, Dar es salaam, Mwanza na mingine kwa kuwa ni wajibu wa Serikali kuhakikisha kunakuwa na Mfumo rafiki itakayowaweza vijana kushiriki kwenye Nyanja mbalimbali, “alisema Katibu Mkuu.

Aliongeza kwamba kutokana na mapitio ya Sera hiyo Serikali inatarajia kuweka mikakati ya kimataifa ya dira ya Maendeleo ya mwaka 2025 na Serikali inajenga misingi imara ya kuwezesha Vijana kutekeleza mambo yao na kushiriki katika masuala ya kijamii, kiuchumi na kisiasa.

“Sera hii itajenga misingi ya Umoja, mshikamano, uadilifu na uzalendo kwa vijana kupenda nchi yao tunafahamu wakijengwa hivi watakuwa tayari kupigania Taifa lao na hawatakuwa tayari kuona taifa lao linachafuliwa,”alieleza Katibu Mkuu Nzunda.

Hata hivyo alielekeza sera hiyo kuwa ielekeze ubunifu kwa vijana kubadilisha mtazamo wa nchi pamoja na Kujenga ujumuishi ndani ya Sera katika makundi yote yakiwemo ya Watu wenye Ulemavu bila kubagua maslahi ya Vijana na Taifa. 

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Vijana kutoka kutoka Ofisi hiyo Bw. James Kajugusi alisema kuwa lengo la mkutano huo ni kupokea maoni ya Vijana na Maafisa Maendeleo ya Vijana wa mikoa kwa niaba ya Vijana nchi nzima ili kuhakikisha sera hiyo inakuwa yenye tija na sehemu ya kutatua changamoto zinazowakabili Vijana.

“Tumekutana na Vijana hawa 119 na Maafisa maendeleo ya vijana 21 kutoka mikoa 22 kwa sababu hawa ndiyo walengwa wa Rasimu hii ili ukusanye michango ya mawazo yao kabla haijapitishwa tunaelewa hivi sasa kilio kikubwa cha vijana ni ajira wengi wanahitimu tukaona wakijengewa uwezo wa kujiajiri itakuwa msaada mkubwa kwa Taifa letu na Vijana wenyewe,”alifafanua Mkurugenzi huyo.

Akitoa maoni mwakilishi wa vijana Bi. Debora Mlai kutoka Mkoani Arusha alishukuru Serikali kuwashirikisha Vijana katika uandaaji wa sera hiyo kwani inaonyesha namna gani inatambua mchango wao katika maendeleo. 

“Tunamshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea sera hii, kupitia nyanja hii itatusaidia sisi vijana kushiriki kikamilifu katika kusukuma gurudumu la maendeleo ya taifa letu” alisema Debora.

Kwa upande wake Bw. Hadson Seme aliomba Serikali iendelee kushirikisha kundi la Watu wenye Ulemavu katika mapitio ya Sera hiyo kwani itasaidia kuweka mikakati wezeshi kwa kundi hilo katika kujikwamua kiuchumi na kukabili changamoto zao.