Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Kamati za Usimamizi wa Maafa zatakiwa kuchukua Hatua Kutokana na Utabiri wa Kimbunga 'JOBO'-Waziri Mhagama


HATUA ZA KUCHUKUA KWA KAMATI ZA USIMAMIZI WA MAAFA NA SEKTA MBALIMBALI KUTOKANA NA UTABIRI WA KIMBUNGA ‘JOBO’

 

Kwa mujibu wa Sheria ya Menejimenti ya Maafa namba 7 ya mwaka 2015, Ofisi ya Waziri Mkuu ina jukumu la kuratibu shughuli za maafa kwa kuhakikisha Wizara, Idara, Taasisi, Mamlaka za Mikoa na Serikali za Mitaa pamoja na asasi zote zisizo za kiserikali zinashiriki kikamilifu katika kuzuia, kupunguza madhara na kujiandaa kukabiliana na kurejesha hali.

Hivyo, Kufuatia taarifa ya Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini ya terehe 24 Aprili, 2021, kuna uwezekano wa Kimbunga kutokea katika maeneo ya pwani ya nchi yetu katika mikoa ya Pwani (ikiwemo kisiwa cha Mafia), Lindi, Mtwara, Dar es Salaam, Tanga siku ya Jumapili tarehe 25 Aprili, 2021.

 

Imeelezwa kwamba,  Kimbunga hicho kilichopewa jina la ‘Jobo’  kwa leo tarehe 24 Aprili, 2021, kipo umbali wa kilomita 200 mashariki mwa kisiwa cha Mafia. Kimbunga hicho kimepungua nguvu kwa haraka baada ya kuingia katika mazingira yenye mzunguko wa upepo kinzani. Hivyo, “Jobo” kwa sasa ni kimbunga hafifu kinachosafiri kwa kasi ya kilometa 18 kwa saa baharini. Kutokana na hali hiyo, kasi ya upepo katika kitovu cha kimbunga kwa sasa imepungua kwa kiwango kikubwa hadi kufikia kilometa 60 kwa saa.

 

Aidha, kinatarajiwa kuingia nchi kavu siku ya Jumapili tarehe 25 Aprili, 2021, katika eneo la Pwani ya Dar es Salaam na Mafia na baadae kupungua nguvu. Kwa leo kimbunga hafifu “Jobo” kinaendelea kusogea katika eneo la pwani ya Lindi na Dar es Salaam kikitarajiwa kuwa na kasi ya upepo wa wastani wa kilometa 40 hadi 50 kwa saa.

 

Taarifa za kitaalam zinaonesha uwepo wa vipindi vya upepo mkali unaofikia kilometa 50 hadi 60 kwa saa, pia  kunatarajiwa kuwepo kwa  mawimbi makubwa baharini pamoja na ongezeko la mvua kwa maeneo ya ukanda wa Pwani. Aidha, uwepo wa kimbunga ‘Jobo’ unatarajiwa kuendelea kutawala na kuathiri mifumo ya hali ya hewa hapa nchini na kusababisha ongezeko la vipindi vya mvua kwa maeneo mengine yaliyo mbali na ukanda wa pwani (ikiwemo ukanda wa Ziwa Victoria).

 

Hali hii inatarajiwa kuleta athari mbalimbli ikiwa ni pamoja na vipindi vya mvua zinazoweza kusababisha mafuriko na upepo mkali utakaopelekea madhara ya maisha, uharibifu wa makazi, mali, mazao mashambani, miundombinu na mazingira.  Pia, shughuli za usafirishaji kwa njia ya anga, kwenye maji na nchi kavu zitaathirika hasa kwa mikoa husika kutokana na hali mbaya ya hewa iliyotabiriwa.

 

Kufuatia utabiri huo, Ofisi ya Waziri Mkuu inatoa maelekezo kwa Kamati za Usimamizi wa Maafa za Mikoa, Wilaya, Kata na Vijiji katika mikoa husika nchini, ambazo ndizo zenye jukumu kubwa la kusimamia menejimenti ya maafa, kuchukua hatua mara moja za Kujiandaa,  Kupunguza,  Kukabili na Kurejesha hali endapo maafa yatatokea.

 

Ili kutekeleza agizo hili kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Maafa namba 7 ya Mwaka 2015, ninaziagiza Kamati za Usimamizi wa maafa ziwajibike kutekeleza mambo yafuatayo; katika mikoa ya Pwani (ikiwemo kisiwa cha Mafia), Lindi, Mtwara,  na Dar es Salaam:-

 

  1. Wananchi washauriwe kuhakikisha paa za nyumba zipo imara, kupunguza matawi ya miti iliyopo karibu na nyumba, kufunga milango na madirisha muda wote, kuondoa vitu vinavyoweza kupeperushwa katika makazi na kuzima vifaa vyote vya umeme na gesi. Aidha, washauriwe kuwa na akiba ya chakula cha kutosha ili kuepuka safari zisizo za lazima.
  2. Kamati zishirikiane na mamlaka husika kuwashauri Wananchi wasimamishe shughuli mbalimbali zinazofanywa kandokando na ndani ya Bahari ya Hindi hususani uvuvi, biashara ndogondogo, usafirishaji wa majini na anga katika kipindi hicho kilichotabiriwa kuwa hatarishi ili kuepusha athari zinazoweza kujitokeza.
  3. Kamati ziendelee kutoa tahadhari katika mitaa mbalimbali ya mikoa hiyo juu ya uwepo wa hali hiyo hatarishi pamoja na hatua muhimu za kuchukuliwa ili kupunguza madhara ya kimbunga hicho endapo kitatokea.
  4. Kamati zishirikiane na wadau wa maafa katika kufuatilia hali hii kwa ukaribu na kujiandaa kwa pamoja katika kukabili maafa  kwa  kutoa misaada mbalimbali ya kibinadamu endapo itahitajika.

 

Nachukua fursa hii kutambua hatua mbalimbali ambazo zimekua zikichukuliwa na viongozi, Kamati za Maafa na wataalamu katika sekta mbalimbali kwa kushirikiana na wanachi katika kukabiliana na Maafa.  Pamoja na kazi nzuri ambayo inaendelea kufanyika, naelekeza hatua stahiki ziendelee kuchukuliwa kuhakikisha tunakuwa na hali ya utayari ili kupunguza madhara ya kimbunga na mafuriko yaliyotabiriwa.

 

Vilevile, Wananchi wote wanaelekezwa kuchukua hatua kwa kuwa suala la kushughulikia maafa kisheria ni la kila mmoja wetu kwa nafasi yake.  Hivyo, kila mwanachi anapaswa kushiriki kikamilifu katika jitihada za kuzuia, kupunguza madhara, kukabili na kurejesha hali endapo maafa yatatokea.

Kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Serikali itaendelea kuchukua hatua za kuhakikisha maisha na mali za wananchi zinakuwa salama kutokana na majanga yaliyotabiriwa.  Hivyo, wananchi wote mnaombwa kufuatilia na kuchukua hatua kutokana na taarifa na tahadhari za mara kwa mara zinazoendelea kutolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa.

 

Imetolewa na 

Mhe.Jenista  J. Mhagama (Mb)

WAZIRI WA NCHI OFISI YA WAZIRI MKUU

(SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WATU WENYE ULEMAVU)