Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Kamati Yapongeza Juhudi za Serikali Uboreshwaji Huduma za Afya


Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Afya na Masuala ya UKIMWI Mhe. Dkt. Lembulung Lukumay ameipongeza Serikali kwa kuwekeza fedha katika ujenzi wa miundombinu ya sekta ya afya pamoja na uboreshaji wa upatikanaji vifaa tiba.

Dkt. Lukumay ametoa pongezi hizo leo Jijini Dodoma wakati akipokea taarifa ya Muundo na Majukumu ya Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) iliyo chini Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu.

 “Serikali imeongeza idadi ya madaktari wabobezi katika jitihada za kuboresha huduma za afya ikiwemo kuweka utaratibu mzuri wa kuendelea kuwezesha afua za UKIMWI kwa kutegemea fedha zetu za ndani ili kuendeleza upatikanaji wa dawa,” alieleza Dkt. Lukumay.

 Aidha, amebainisha kuwa, wananchi hawana budi kuelezwa juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais, Dkt, Samia Suluhu Hassan katika uimarishaji wa huduma za afya, katika ngazi ya Zahanati, Vituo vya afya, hospitali za Wilaya na hospitali za Mikoa.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Bunge Uratibu na Wenye Ulemavu Mhe. William Lukuvi ameahidi kuendelea kushirikiana na kamati kwa ukaribu  na kufanyia kazi kwa ukamilifu ushauri na maelekezo yatakayotolewa na kamati.