Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria yapongeza uwekezaji uzalishaji vifaranga vya samaki kukuza uchumi.


KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Utawala , Katiba na Sheria imeipongeza Serikali kwa kutoa fedha zaidi ya Sh. Bilioni 3.5 kwa ajili ya kupanua uwekezaji katika Kituo cha Kuendeleza Ukuzaji Viumbe Maji Kingolwira mkoani Morogoro ili kiongeze uzalishaji wa vifaranga vya samaki hadi kufikia milioni moja kwa mwezi kutoka vifaranga 100,000.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Florent Kyombo alitoa pongezi hizo wakati kamati hiyo ilipotembelea Kituo hicho kilichopo katika Manispaa ya Morogoro ambapo alisema, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi imewezesha na kufanikisha uwekezaji huo mkubwa.

Alikipongeza kituo hicho kwa kuanza kuzalisha chakula cha samaki ambao ni mradi unaoweza kusaidia kuokoa fedha zilizokuwa zinatumika kununulia chakula kutoka nje ya Nchi . 

"Tunaipongeza Serikali kwa uwekezaji huu mkubwa wa Sh. Bilioni 3.5 zinazotolewa kwa awamu kwa ajili ya mradi wa uzalishaji wa vifaranga vya samaki ambavyo vinasambazwa nchini kote ili wananchi waweze kupata lishe na kukuza uchumi. Kamati yetu imeridhishwa na hatua hii ya mwanzo na kwamba mradi huu na mingine iliyopo kwenye mikoa tofauti itakapokamilika itakuwa ni yenye thamani kubwa kwa wananchi," Alisema Mhe. Kyombo.

Naye Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Mhe. Ummy Nderiananga aliwahakikishia Wabunge wa Kamati hiyo kuwa kazi ya uendelezaji wa kituo cha Kingolwira inaendelea kwa kasi na kuhakikisha malengo yanafikiwa na kuwanufaisha wananchi wengi wa mkoa wa Morogoro na nchini kwa ujumla.

"Tumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake na juhudi ambazo zimetuwezesha kuendelea kupata fedha kwa ajili ya kuendeleza mradi huu wa kuendeleza kilimo na uvuvi,"Alieleza Mhe. Ummy.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi , Profesa Riziki Shemdoe, pamoja na kupongeza kamati hiyo kufanya ziara katika Kituo hicho alisema kuna changamoto kubwa ya upatikanaji wa chakula za samaki .

"Kwa sasa kuna wadau Jijini Mwanza wana kiwanda kikubwa ambacho kinaanza kujengwa na hiki kitasaidia sana kupunguza uagiaji wa chakula cha samaki kwani hivi sasa asilimia kubwa ya chakula tunakipata kutoka nje," Alibainisha Prof. Shemdoe .

Awali, Mratibu wa programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi ( AFDP) ,Salimu Mwinjaka alisema programu hiyo ya miaka sita kuanzia 2022/2023 inafadhiliwa na Mfuko wa Kimataifa wa Kuendeleza Kilimo (IFAD) ambapo kwa Kituo cha Kingolwira limetengewa Bilioni 3.5 na zitatolewa kwa awamu.

"Mradi huu katika utekelezaji wa 2023/2024 kiasi cha Sh. Bilioni 1.8 zimetolewa kwa ajili ya utekelezaji wa kazi mbalimbali kwenye kituo hicho ikiwa ni pamoja na ujenzi wa mabwawa mapya 10 na eneo la Boma Road hadi kufikia Juni 2024,"Alisema Mratibu huyo

 

=MWISHO=