Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

JKT yaanza kuitekeleza Programu ya ASDP II


Jeshi la kujenga Taifa (JKT) kupitia kikosi cha 837KJ Chita, kilichopo Wilayani Kilombero, Mkoani Morogoro kimeanza kutekeleza kwa vitendo Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) kwa kuanza ujenzi wa skimu ya umwagiliaji ambayo kwa awamu ya kwanza skimu hiyo itakuwa na urefu wa Km 2.3, ambayo hivi karibuni Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Venance Mabeyo ameweka jiwe la msingi la kuizindua.

Programu ya ASDP II inayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, malengo yake ni kuleta mageuzi katika sekta ya kilimo (kilimo, mifugo na uvuvi) kupitia maeneo makuu manne ikiwemo eneo la Usimamizi Endelevu wa Matumizi ya Maji na Ardhi ambalo moja ya kipaumbele cha uwekezaji ni kuendeleza miundo mbinu ya umwagiliaji.

Akiongea mara baada ya kufanya ziara kwenye Kikosi cha Jeshi 837KJ Chita, tarehe 21 Oktoba, 2020, Wilayani Kilombero lengo likiwa ni kufuatilia utekelezaji wa Programu hiyo kwa wadau wa Programu ya ASDP II, Mratibu wa Programu ya ASDP II Ofisi ya Waziri Mkuu, Dkt. Salim Nandonde, amefafanua kuwa ujenzi wa skimu hiyo utasaidia Programu kulifikia lengo la Kitaifa kwa miaka mitano la kuwa na eneo la umwagiliaji la hekta milioni moja na laki mbili.

“Jeshi la kujenga Taifa ni mdau muhimu katika utekelezaji wa Programu ya ASDP II, na kwa kikosi hiki cha 837 KJ Chita, kuanza ujenzi huu wa skimu ya umwagiliaji itasaidia kuongeza eneo linalohitajika la kilimo cha umwagiliaji nchini ambapo kwa sasa eneo lililopo la kilimo cha umwagiliaji ni takribani hekta laki sita na alfu tisini na nne tu.

Ameongeza kuwa mradi huo pia umezingatia kuongeza thamani ya zao la mpunga kwa kuanza ujenzi wa ghala la kuhifadhi mpunga sambamba na kuwa na mpango wa kujenga kiwanda cha kusindika mpunga huo ambapo hatua hiyo inaongeza wigo wa Kikosi hicho kuwekeza kwenye eneo kuu la tatu la Programu ya ASDPII ambalo ni kukuza Biashara na Kuongeza Thamani.

Kwa upande wake Afisa Utawala wa Kikosi cha 837 KJ Chita, Kapteni Nyakohanda Rusuhi ameeleza kuwa ujenzi wa skimu hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Programu ya ASDP II pamoja na mipango ya JKT inayosimamiwa na Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa, Meja Jenerali Charles Mbuge, ambapo Programu hiyo inawataka wadau wake kufanya mageuzi kwenye sekta ya kilimo kwa kulima kilimo chenye tija.

“Awali wakati tunategemea kilimo cha mvua tulikuwa tunavuna gunia sita kwa hekari moja, lakini baada ya kukamilisha ujenzi wa skimu hii tunatarajia kuvuna takribani ya gunia 35 kwa hekari moja. Tukifanikiwa kupata mavuno haya tutakuwa tumezalisha chakula cha kutosha lakini pia tutakuwa tumefanikiwa kutekeleza maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli aliyelitaka Jeshi la kujenga Taifa kujilisha.” Amesisitiza Rusuhi.

Kwa upande wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Kanda ya juu Kusini -Mbeya, ambao wanashirikiana na JKT kujenga skimu hiyo, Mhandisi Elibariki Mwendo ameeleza kuwa tayari wameanza kuboresha miundombinu ya umwagiliaji kwa kuanza na ujenzi wa awali wa ekari 2,500 kati ya ekari 12,000 zinazolengwa kujengwa.

Mhandisi Mwendo ameongeza kuwa ujenzi wa skimu hiyo utakuwa na ujenzi wa mifereji katika mito mitatu tofauti, ujenzi wa mifereji mikuu mama mitatu yenye urefu wa mita 1,716 pamoja na vivushamaji kupita kwenye reli ya TAZARA, pia ujenzi wa mabanio matatu, mifereji midogo ya kutoa maji shamba ipo 155, matuta mawili ya kuzuia mafuriko yenye kina cha wastani wa mita mbili.

Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) ilizinduliwa rasmi mwaka 2018 na inaratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu ambapo inatekelezwa na wadau wakuu wa tatu ambao ni Serikali, Sekta Binafsi na Washirika wa maendeleo.

Malengo makuu ya Programu ya ASDP II ni kuleta mageuzi katika sekta ya kilimo (kilimo, mifugo na uvuvi) ili kuongeza uzalishaji na tija, kukifanya kilimo kiwe cha kibiashara zaidi na kuongeza pato la wakulima wadogo kwa ajili ya kuboresha maisha yao, usalama wa chakula na lishe.

Mbali na maeneo makuu ya ASDPII ambayo Kikosi cha JKT Chita kimeanza kutekeleza maeneo mengine ni Kuongeza Tija na Faida kwa lengo la kuongeza uzalishaji wenye tija hasa kwenye mazao ya kipaumbele; na Kuweka Mazingira Wezeshi ya Kuendeleza Sekta ya kilimo kwa kuwezesha uratibu, ufuatiliaji na kufanya tathmini ya sekta ikiwa ni pamoja na kuimarisha taasisi na kuweka mazingira wezeshi ya uratibu. Ni wazi kuwa Jeshi la Kujenga Taifa lipo kwenye nafasi kubwa ya kutekeleza Programu ya ASDPII kwenye maeneo yote makuu ya Programu hiyo.