Habari
Global Fund Yaunga Mkono Serikali Kukabiliana na Magonjwa Nchini.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. John Jingu amekutana na kufanya mazungumzo na Meneja Mkaguzi kutoka Mfuko wa Kimataifa wa Kupiga Vita UKIMWI, TB na Malaria (GLOBAL FUND) Bwa. Andrew Hammond ofisini kwake Jijini Dodoma.
Dkt. Jingu amesema mazungumzo hayo yalilenga kujadili masuala mbalimbali kuhusu sekta ya afya nchini ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora ya afya katika maeneo yao.
Ameongeza kuwa serikali ya Tanzania itaendelea kushirikana na mfuko huo kwani umekuwa na mchango mkubwa katika kuwezesha vifaa tiba kama ilivyo azima ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ya kujenga miundo mbinu ya na kuboresha masuala ya tiba kwa wananchi.
Naye Meneja Mkaguzi kutoka Mfuko wa Kimataifa wa kusaidia mapambano dhidi ya UKIMWI, TB na Malaria (GLOBAL FUND) Bwa. Andrew Hammond ameishukuru Tanzania kwa kushirikiana na Mfuko huo katika kupiga vita maradhi ya Kifua Kikuu, Malaria na Ukimwi.
Ameahidi kuwa Mfuko wa Dunia utaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za kukabiliana na magonjwa hayo hapa nchini kwa kuelekeza rasilimali fedha kwa ajili ya kununua dawa pamoja na kuboresha mifumo ya utoaji huduma ya afya.