Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Dkt. Mwigulu: waliopora mali ya wananchi warudishe wenyewe


WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema watu wote waliopora mali za wenzao ikiwemo ardhi warudishe wenyewe kabla hawajafikiwa na mkono wa Serikali.

Pia, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu amesisitiza kuwa hakuna sababu ya wananchi kukaa kimya pale wanapoonewa bali watoe taarifa kwani hakuna mbabe mbele ya Serikali.

Ameyasema hayo leo Januari 06, 2026 jijini Dar es Salaam katika Kongamano la Mwaka la Wamachinga na Madereva Pikipiki na Bajaji za kubeba abiria.

Amesema Watanzania wote wana haki sawa, hivyo hakuna mtu mwenye ruhusa ya kuchukua mali au kitu chochote cha mtu mwingine, atakayebainika achukuliwe hatua.

Waziri Mkuu ameyasema hayo baada ya kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa wananchi katika maeneo mbalimbali wakidai kuchukuliwa mali zao ikiwemo ardhi.

Akizungumza kuhusu hoja zilizowasilishwa na wamachinga na waendesha pikipiki na bajaji, Waziri Mkuu amesema amezipokea na kwamba Serikali itazifanyia kazi.

Kadhalika, Mheshimiwa Dkt Mwigulu amesema Serikali inathamini sana mchango unaotolewa na makundi hayo katika maendeleo ya Taifa, itaendelea kushirikiana nao.

Pia, Waziri Mkuu ametoa wito kwa madereva hao wa bajaji na pikipiki za kubeba abiria wahakikishe wanakuwa makini wawapo barabara na wajiepushe na ajali zinazosababishwa na uzembe.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Shirikisho la Umoja wa Machinga Tanzania, Ernest Masanja ameishukuru Serikali kwa ushirikiano inaowapatia ikiwemo mikopo.

Pia, kiongozi huyo ameiomba Serikali kuhakikisha inapokamilisha maeneo ya kufanyia biashara yakiwemo masoko wamachinga ndiyo wapewe kipaumbele.

Naye, Mwenyekiti wa Shirikisho la Bajaji na Pikipiki Taifa, Said Chunja ameiomba Serikali iingilie kati suala la mikataba kwani linawaumiza sana.

“Masharti tunayopewa inatuumiza sana, kwa sababu hata kama mtu unaumwa na zimebaki siku chache umalize unaporwa chombo, tunaiomba Serikali itusaidie.”