Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Awamu ya pili ya ujenzi wa Ofisi za Wizara mji wa Serikali yazinduliwa


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezindua wa awamu ya pili ya ujenzi wa Ofisi za Wizara katika Mji wa Serikali uliopo eneo la Mtumba jijini Dodoma na ameiagiza Wizara ya Fedha na Mipango ihakikishe kuwa fedha kwa ajili ya mradi huo zinapatikana kwa wakati na kikamilifu.

 Mheshimiwa Majaliwa ametoa agizo hilo leo (Alhamisi, Desemba 2, 2021) baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora ikiwa ishara ya uzinduzi wa awamu ya pili ya ujenzi wa Ofisi za Wizara katika Mji wa Serikali.

Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kumpongeza na kumshukuru Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuidhinisha shilingi bilioni 300 ili zitumike katika ujenzi wa Ofisi za Wizara na miundombinu mbalimbali itakayojengwa katika Mji wa Serikali na Jiji la Dodoma.

Mheshimiwa Majaliwa amesema kwamba awamu ya kwanza ya ujenzi wa ofisi 23 za Serikali ulianza tarehe 28 Novemba, 2018 na kukamilika tarehe 22 Machi, 2019 ambapo Shilingi bilioni 39.387 zilitumika kwa ajili ya awamu ya kwanza ya ujenzi huo.

“Watumishi zaidi ya 18,300 wa Serikali Kuu, Bunge, Vyombo vya Ulinzi na Usalama na baadhi ya Taasisi wamehamia Dodoma ambapo kiasi cha shilingi bilioni 162.123 kimetumika kwa ajili ya gharama za posho za uhamisho, ununuzi na usafirishaji wa vifaa, ukarabati na ujenzi wa miundombinu wezeshi ya ofisi.”

Uzinduzi wa huo wa awamu ya pili ya ujenzi wa Ofisi za Wizara na miundombinu mbalimbali zinazojengwa katika Mji wa Serikali ni miongoni mwa matukio ya maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania ambayo kitaifa yatafanyika mkoani Dar es Salaam Desemba 9, 2021.

Amesema uzinduzi huo ambao utahusisha majengo 24 ya ghorofa unalengo la kuwa na Mji wa Serikali wa kisasa utakaozingatia dhana ya Mji wa Kijani na mji rafiki ili kudhibiti gharama za kiuendeshaji za Serikali za majengo hayo ikiwemo kuzingatia matumizi ya nishati mbadala.

“Awamu ya pili ya ujenzi wa ofisi za Wizara itakwenda sambamba na ujenzi wa miundombinu muhimu ya kudumu ya maji, umeme, mawasiliano, usalama, gesi, TEHAMA, zimamoto na uokoaji, programu za upandaji miti pamoja na ujenzi wa huduma mbalimbali za kijamii.”

 “Katika utekelezaji wa agizo la Mheshimiwa Rais Samia la kuzitaka Wizara kuanza ujenzi mara moja, ninafurahi na kufarijika kuona kwamba tayari Wizara zote zimeshakamilisha taratibu za manunuzi za kuwapata wakandarasi na washauri elekezi wa ujenzi.”

“Wakandarasi mbalimbali kutoka sekta ya umma na sekta binafsi wanaendelea na shughuli za ujenzi wa ofisi zote za Wizara. Ni matumaini ya Serikali kuona kwamba wakandarasi hao watatekeleza mradi huu kwa kuzingatia weledi, muda, ubora na bajeti iliyotengwa na Serikali.”

Waziri Mkuu ameagiza ujenzi wa majengo hayo ufanyike kwa kuzingatia ramani za upangaji wa viwanja zinazotokana na Mpango kabambe wa Mji wa Serikali ili kutokinzana na mipango ya ujenzi wa miundombinu mingine inayojengwa na itakayojengwa juu na chini ya ardhi.

“Kikosi kazi kinachoratibu ujenzi huo kihakikishe kwamba ujenzi wa majengo ya Ofisi za Wizara unakwenda sambamba na ujenzi wa miundombinu mingine ya kudumu ya umeme, maji safi na maji taka, mawasiliano, TEHAMA, usalama, zimamoto na uokoaji, gesi na upandaji miti.”

Ameiagiza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Wizara ya viwanda na Biashara kuendelea kuwasiliana na wazalishaji wa ndani wa bidhaa za ujenzi ili vipangiwe utaratibu wa manunuzi mapema na hivyo, kuwezesha kuzalishwa vifaa vya kutosha vyenye ubora unaohitajika.

“Kamati Maalumu ya Makatibu Wakuu wanaosimamia ujenzi huu ihakikishe unatekelezwa kwa mujibu wa mpango kazi, ndani ya bajeti, muda, ubora, usalama, mazingira na bidhaa za kutosha za ujenzi zipatikane ikiwa ni pamoja na kutatua changamoto zinazojitokeza.”

Mbali na maagizo hayo, pia Mheshimiwa Majaliwa amekiagiza kikosi kazi kinachoratibu ujenzi wa Mji wa Serikali kwa kushirikiana na Wizara zote kuainisha mahitaji ya fedha za kukamilisha ujenzi katika mwaka ujao wa fedha wa 2022/2023 ili yatengewe fedha katika kipindi husika;

Amesema kikosi kazi kinachoratibu ujenzi huo kwa kushirikiana na Taasisi husika kikamilishe maandalizi ya ujenzi wa huduma mbalimbali za kijamii katika Mji wa Serikali ikiwemo maeneo ya kupumzikia, viwanja vya michezo, maduka ya kibiashara, vituo vya mabasi na reli.

Kwa upande wakeWaziri wa Nchi - Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama amesema ujenzi wa Ofisi za Serikali jijini Dodoma ulitumia wakandarasi wazawa na hivyo kusaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha biashara na upanuzi wa masoko ya biadhaa za ujenzi.

Waziri Jenista amsema ujenzi wa Mji wa Serikali kwa awamu ya kwanza na ya pili umesaidia kwa kiasi kikubwa katika kuchangia pato Taifa kupitia Kodi ya Ongezeko la Thamani  (VAT) kupitia ununuzi wa vifaa vya ujenzi pamoja na kutoa fursa za ajira rasmi na zisizo rasmi 1,588 kwa wananchi wa kada mbalimbali kwa Mkoa wa Dodoma na mikoa mingine.

Awali, Mheshimiwa Majaliwa aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Mji wa Serikali chenye hadhi ya daraja A, unaotarajia kugharimu kiasi cha shilingi milioni 948. Amesema amefurahishwa na ujenzi huo unaojengwa kwa mfumo wa force account.

Baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa kituo hicho, Waziri Mkuu alikagua ujenzi wa mradi wa kitega uchumi unaotekelezwa na jiji la Dodoma katika Mji wa Serikali Mtumba ikiwa ni sehemu ya matukio ya kuadhimisha miaka 60 ya uhuru wa Tanzania.

Akizungumza baada ya kukagua ujenzi huo, Mheshimiwa Majaliwa alilipongeza jiji la Dodoma kwa kutekeleza mradi huo kwa kutumia mapato ya ndani na kuyataka majiji mengine kuiga mfano. Mradi huo unajengwa kwa awamu mbili unatarajiwa kugharimu shilingi bilioni 59.3.

Awamu ya kwanza ya mradi huo inahusisha ujenzi wa jengo hoteli lenye maduka na huduma za kibenki pamoja na jengo la kumbi za mikutano ukiwemo mkubwa wenye uwezo wa kuhudumia washiriki 1000 kwa wakati mmoja na kumbi ndogo sita zenye uwezo wa kuhudumia washiriki 120 kwa wakati mmoja.

Pia, Mheshimiwa Majaliwa alikagua ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilomita 51.2 inayojengwa katika Mji wa Serikali kwa kiwango cha lami ambao unatarajiwa kugharimu shilingi bilioni 87.88 na umefikia asilimia umefikia aslimia 88. Pia Waziri Mkuu alipanda mti katika eneo litakalojengwa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

-End-