Wasifu
Mh. Rashid Mfaume Kawawa
Waziri Mkuu MstaafuHuyu alikuwa ni Waziri Mkuu wa pili wa Serikali ya Tanganyika akipokea nafasi hiyo kutoka kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Maisha Yake
Mheshimiwa Rashid Mfaume Kawawa alizaliwa tarehe 27 Februari, 1926 katika kijiji cha Matepwende, Wilaya ya Namtumbo, mkoani Ruvuma. Alianza elimu ya msingi katika Shule ya Tunduru Mjini huko Lindi mwaka 1935. Aliendelea na Elimu ya Kati (Middle School) Dar es Salaam Central School mwaka 1942 hadi 1947 kabla ya kwenda Shule ya Tabora Boys kati ya mwaka 1951 na 1956 kuendelea na masomo yake.
Uongozi
Kabla ya kuingia katika harakati za kupigania Uhuru, Mzee Kawawa alikuwa ni miongoni mwa waanzilishi wa Shirikisho la Wafanyakazi mwaka 1955 ambapo alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa kwanza. Ni katika nafasi hii ndipo alianza kushiriki kwa nguvu zaidi katika harakati za kupigania Uhuru wa Tanganyika akihamasisha wafanyakazi. Kabla ya hapo alikuwa ni Katibu Mkuu wa Shirikisho la Wafanyakazi wa Serikali (TLF). Februari 1956, Mzee Kawawa aliacha kazi yake ya Shirikisho la Wafanyakazi kwa vile alikuwa mwajiriwa wa Serikali kitu ambacho kilimkataza kujihusisha na siasa na akaamua kuingia katika harakati za kudai Uhuru kupitia TANU. Alikuwa Mjumbe wa Kamati Kuu 24 ya TANU mwaka 1957 na Makamu wa Rais wa TANU mwaka 1960. Tarehe 22 Januari, 1962 aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa Pili wa Tanganyika wakati Mwalimu Nyerere alipoamua kwenda mikoani kujenga chama na kufanya shughuli za kisiasa. Alishika wadhifa huo hadi tarehe 8 Desemba, 1962. Aliteuliwa tena kushika wadhifa huo tarehe 2 Machi, 1972 hadi tarehe 13 Februari, 1977 ambapo nafasi yake ilichukuliwa na Mheshimiwa Edward Moringe Sokoine.
Mtiririko wa nyadhifa alizowahi kushika ni kama ifuatavyo:
• Mwaka 1960 Mzee Rashid Mfaume Kawawa aliteuliwa kuwa Waziri wa Serikali za Mitaa na Nyumba kwenye Serikali ya Madaraka iliyoundwa na Rais wa TANU.
• Mwaka 1962 mwezi Januari, Mzee Rashid Mfaume Kawawa alichukua wadhifa wa Waziri Mkuu wakati huo alikuwa Waziri asiyekuwa na Wizara Maalum baaada ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kujiuzulu wadhifa huo ili aende kuimarisha TANU.
• Mwezi Desemba, 1962 Mzee Rashid Mfaume Kawawa aliteuliwa kuwa Makamu wa Rais baada ya nchi kuwa Jamhuri chini ya Rais Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
• Baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964, Mzee Rashid Mfaume Kawawa aliteuliwa kuwa Makamu wa Pili wa Rais na pia 25 alikuwa na dhamana ya Waziri wa Ulinzi. Alitoa mchango mkubwa katika kuanzishwa kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika kipindi hicho na kujenga misingi imara ya Jeshi hilo. Aidha, alianzisha pia Jeshi la Kujenga Taifa.
• Mwaka 1972, Mzee Rashid Mfaume Kawawa aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wadhifa alioendelea nao hadi mwaka 1977 alipoteuliwa tena kuwa Waziri wa Ulinzi.
• Pamoja na majukumu haya Mzee Rashid Mfaume Kawawa aliwahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Nachingwea na baadaye Liwale kati ya mwaka 1965 – 1985.
• Katika siasa amewahi kushika nafasi mbalimbali ikiwemo ile ya Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi mwaka 1980 na Makamu Mwenyekiti wa CCM mwaka 1982 na amekuwa Mjumbe wa kudumu wa Kamati Kuu ya CCM.
Mauti
Mzee Kawawa alifariki dunia Alhamisi ya tarehe 31 Desemba, 2009 saa 3.20 asubuhi akiwa na umri wa miaka 83 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili. Ijumaa, Januari mosi 2010, kuanzia saa 7 mchana wakazi wa Jiji la Dar es Salaam walipata nafasi ya kutoa heshima za mwisho katika Viwanja vya Karimjee na alizikwa Jumamosi, tarehe 2 Januari 2010, saa 7 mchana katika makazi yake kwenye kijiji cha Madale, eneo la Wazo Hill, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Anavyokumbukwa:
• Kusimamia mpango wa kugawa madaraka kwa Waafrika (Africanizations).
• Kusimamia uanzishwaji wa Vijiji vya Ujamaa maarufu kama “Operesheni Vijiji” mwaka 1975. Hii ilikuwa hatua mojawapo ya utekelezaji wa Azimio la Arusha.
• Kuanzisha Maduka ya Vijiji ambayo yalilenga kutoa bidhaa kwa wananchi kwa ukaribu zaidi.
• Alikuwa maarufu kwa jina la ‘Simba wa Vita’ kwa sababu alikuwa haogopi kutekeleza maamuzi mazito.
• Alikuwa Kamanda wa Vijana wa Chama cha TANU na baadaye CCM.