Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Wasifu

Mh. Julius Kambarage Nyerere
Mh. Julius Kambarage Nyerere
Waziri Mkuu Mstaafu

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikuwa ni Waziri Mkuu wa Kwanza wa Serikali ya Tanganyika Huru kuanzia tarehe 9 Desemba, 1961 hadi tarehe 22 Januari, 1962 alipojiuzulu na kumwachia wadhifa huo Mheshimiwa Rashid Mfaume Kawawa ili yeye aende kuiimarisha TANU mikoani.

Maisha Yake

Julius Kambarage Nyerere alizaliwa tarehe 13 Aprili, 1922 katika Kijiji cha Butiama, Wilaya ya Musoma, Mkoa wa Mara, Tanzania. Alikuwa mmoja wa watoto 26 wa Chifu wa kabila la Wazanaki, Mzee Nyerere Burito. Alipokuwa mtoto, Nyerere alichunga mifugo ya baba yake; alipofikisha umri wa miaka 12 alianza Shule akitembea kilomita 30 hadi Musoma. Baada ya kumaliza Shule ya Msingi aliendelea kusoma Shule ya Wamisionari Wakatoliki huko Tabora.

Alipofikisha miaka 20, alibatizwa akawa Mkatoliki hadi mwisho wa maisha yake. Mapadre walibaini kipaji alichonacho wakamsaidia kusomea ualimu katika Chuo Kikuu cha Makerere, Kampala, Uganda kuanzia 1943 hadi 1945. Akiwa Makerere alianzisha Tawi la Umoja wa Wanafunzi Watanganyika na pia akajihusisha na Tawi la Tanganyika African Association (TAA). Baada ya kumaliza masomo ya ualimu alirudi Tabora akawa Mwalimu katika Shule ya Sekondari ya St. Mary´s. Mwaka 1949 alipata nafasi ya kwenda kusoma kwenye Chuo Kikuu cha Edinburgh huko Uingereza akasomea Shahada ya Uzamili ya Historia na Uchumi. Alihitimu mwaka 1952. Alikuwa Mtanzania wa kwanza kusoma katika Chuo Kikuu cha Uingereza na Mtanzania wa pili kupata shahada ya elimu ya juu nje ya Tanzania.

Ajira

Aliporejea Tanganyika kutoka masomoni, Nyerere alifundisha Historia, Kingereza na Kiswahili katika Shule ya Sekondari ya St. Francis (Dar es Salaam) ambayo kwa sasa inajulikana kama Shule ya Sekondari Pugu. Mwaka 1953 alichaguliwa kuwa Rais wa Chama cha Tanganyika African Association (TAA), Chama ambacho alikisaidia kukijenga alipokuwa mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Makerere. Mwaka 1954 alikibadilisha Chama cha TAA kuwa Chama cha Tanganyika African National Union (TANU) ambacho kilikuwa cha kisiasa zaidi kuliko cha TAA.

Katika kipindi cha mwaka mmoja, Chama cha TANU tayari kilikuwa chama cha siasa kinachoongoza Tanganyika. Uwezo wa Mwalimu Nyerere uliwashtua viongozi wa kikoloni na kumlazimisha achague kufanya kazi ya siasa au abaki na kazi ya ualimu. Nyerere alisikika akisema kuwa alikuwa mwalimu kwa kuchagua na mwanasiasa kwa bahati mbaya.

Alijiuzulu ualimu na kuzunguka nchini Tanganyika kuzungumza na watu wa kawaida na machifu ili kuleta muungano katika kupigania Uhuru. Pia alizungumza kwa niaba ya TANU katika Baraza la Udhamini na Kamati ya Nne ya Umoja wa Mataifa huko New York, Marekani. Uwezo wake wa kuunganisha watu ili wawe na umoja na mshikamano kutetea haki zao pamoja na kipaji chake cha kujenga hoja, kutetea na kuzungumza kwa ufasaha ulimwezesha kufanikisha Tanganyika kupata Uhuru bila umwagaji wa damu. Ushirikiano mzuri aliouonyesha kwa aliyekuwa Gavana wa wakati huo, Bw. Richard Turnbull ulisaidia pia kuharakisha upatikanaji wa Uhuru.

Uongozi

Tanganyika ilipata Uhuru wake tarehe 9 Desemba, 1961 na Nyerere alichaguliwa kuwa Waziri Mkuu wa Tanganyika huru. Mwaka mmoja baadaye, Nyerere alikuwa Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Tanganyika. Nyerere alikuwa kiungo muhimu katika kuleta Muungano wa Tanganyika na Zanzibar iliyounda Tanzania baada ya Mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1964 ambayo yalimtoa madarakani Sultani wa Zanzibar, Jamshid bin Abdullah.

Mnamo tarehe 5 Februari, 1977 Mwalimu Nyerere aliongoza chama cha TANU katika kuungana na chama tawala cha Zanzibar cha Afro - Shiraz Party (ASP) na kuanzisha Chama kipya kilichoitwa Chama cha Mapinduzi (CCM) akiwa Mwenyekiti wake wa kwanza. Mwalimu Nyerere aliongoza Taifa kwa miaka 23 hadi mwaka 1985 alipostaafu na kumwachia nafasi Rais wa Awamu ya pili, Mzee Ali Hassan Mwinyi. Yeye alibaki kuwa Mwenyekiti wa CCM hadi mwaka 1990 alipostaafu licha ya kuwa aliendelea kuwa na heshima kubwa katika nyanja za siasa ya Tanzania na duniani hadi kifo chake.

Mwalimu Nyerere alitumia muda mwingi kukaa kijijini kwake Butiama huku akilima shambani kwake. Pamoja na hayo, alianzisha Taasisi ya Mwalimu Nyerere Foundation mwaka 1996. Aidha, alikuwa mpatanishi wa vita vya wenyewe kwa wenyewe huko Burundi. Pia kati ya mwaka 1987 hadi 1990 alikuwa Mwenyekiti wa Tume ya Kusini (South Commission).

Mauti

Tarehe 14 Oktoba 1999, ni siku ambayo Taifa la Tanzania halitaisahau kamwe kwani Mwalimu Nyerere aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 77 katika Hospitali ya St. Thomas iliyoko jijini London, Uingereza baada ya kuugua kansa ya damu. Mwili wa Mwalimu ulipokelewa jijini Dar es Salaam tarehe 18 Oktoba, 1999 na kupelekwa nyumbani kwake Msasani. Tarehe 20 Oktoba, 1999 mwili wa Baba wa Taifa ulipelekwa Uwanja wa Taifa ili Watanzania kwa ujumla waweze kumuaga mpendwa wao. Tarehe 21 Oktoba, 1999 ilifanyika sala ya mazishi ya Kitaifa katika uwanja huo ambayo iliongozwa na Muadhama Polycarp Kardinali Pengo. Viongozi mbalimbali wa ndani na nje ya nchi walihudhuria ibada hiyo. Watu waliendelea kumuaga Baba wa Taifa Taifa usiku na mchana hadi tarehe 22 Oktoba, 1999 jioni mwili wake ulipoondolewa na kusafirishwa kwenda Musoma na hatimaye ukasafirishwa kwenda kijijini kwake Butiama kwa ajili ya mazishi. Mazishi ya Mwalimu Nyerere yalifanyika tarehe 23 Oktoba, 1999 nyumbani kwake huko Mwitongo katika kijiji cha Butiama, wilayani Musoma Vijijini, mkoani Mara.

Anavyokumbukwa:

• Mwalimu Nyerere ni kati ya viongozi wachache wa Afrika ambao wameachia madaraka kwa hiari baada ya kutawala kwa muda wa miaka 23.

• Alileta umoja, upendo, mshikamano, amani na haki Tanzania na barani Afrika.

• Alishiriki hatua mbalimbali za kupigania hadi kupata Uhuru.

• Alitokomeza ubaguzi wa rangi.

• Kabla ya kuingia kwenye siasa alikuwa ni Mwalimu. Kazi hii ndiyo ilimpatia jina maarufu la "Mwalimu."

• Alijenga umoja wa Taifa na utamaduni wa Kiafrika pamoja na kukuza lugha ya Kiswahili.

• Alitetea usalama wa Taifa katika vita dhidi ya Nduli Idd Amin.

• Alitoa mchango mkubwa kwa Vyama vya Ukombozi vya Nchi za Kusini mwa Afrika kama vile ZANU (Zimbabwe), ANC na PAC (Afrika Kusini), SWAPO (Namibia), MPLA (Angola) na FRELIMO (Msumbiji).

• Alisimamia sera za kujali utu na ubinadamu.

• Alikuwa Muasisi wa itikadi ya Ujamaa na Kujitegemea na Azimio la Arusha. Azimio hilo lilikuwa na shabaha ya kujenga nchi ya Kijamaa ambayo watu wake ni huru na wenye uwezo wa kuamua mambo yao wenyewe.

• Alikuwa Muasisi wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

• Alikuwa Muasisi wa Chama cha TANU na CCM.

• Alikuwa Muasisi wa OAU na South South Cooperation.