HOTUBA YA MHESHIMIWA KASSIM M. MAJALIWA (MB), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI WA KUHITIMISHA SHUGHULI ZA MKUTANO WA KUMI NA TISA WA BUNGE

Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujaalia afya njema na kutuwezesha kufika siku hii ya leo ambayo naiita kuwa ni siku ya kihistoria kwetu.

Nasema kuwa ni ya kihistoria kwa sababu Bunge lako Tukufu linahitimisha shughuli za Bunge la Kumi na Moja (11) la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pia tunahitimisha Mkutano wa Kumi na Tisa (19) wa Bunge ulioanza mwezi wa Aprili mwaka huu wa 2020.

Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu wa Bunge, licha ya uwepo wa ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona (COVID-19), tumeweza kukaa hapa Dodoma kwa kipindi kisichopungua miezi miwili na nusu. Aidha, katika kipindi hicho tumeweza kutekeleza majukumu yetu yote kama ilivyokuwa imepangwa.

Ama kwa hakika hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwani tunakamilisha maisha yetu ya Kibunge kwa kipindi cha miaka mitano toka Novemba 2015. Tumeshirikiana katika maeneo mengi nje na ndani ya Bunge kwa kila mmoja kutekeleza majukumu yake.

Mheshimiwa Spika, siwezi kuanza kueleza yaliyojiri kwenye majukumu yetu bila kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyeniwezesha kuwa na afya njema na kunisimamia katika kila jambo na hasa nilipokuwa natekeleza majukumu yangu binafsi na ya umma kwa kipindi chote hadi sasa. InshaAllah, yeye ndiye msimamizi wa yote.

Mheshimiwa Spika, kwa moyo mkunjufu kabisa naomba nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kitendo chake cha kuniamini na kuniteua kushika wadhifa wenye dhamana kubwa ya kumsaidia kazi ya utendaji ndani ya Serikali kwa kipindi chote cha miaka mitano.

Kwa niaba ya Familia yangu na Wana-Ruangwa wote, namshukuru sana kwa ukarimu, imani na upendo aliouonesha kwetu, Mwenyezi Mungu aendelee kumpa nguvu, ulinzi, kheri na kila lililo jema na aendelee kuliongoza Taifa hili vyema na kwa mafanikio makubwa kama ambavyo Watanzania tumeendelea kushuhudia mafanikio makubwa katika kipindi hiki cha Uongozi wake wa Awamu ya Tano.

Mheshimiwa Spika, Rais wetu ametenda mema kwa Watanzania na watamlipa mema. Ninamwombea kheri pia kwa Uchaguzi Mkuu ujao ashinde kwa ushindi wa kishindo. Amina.

Mheshimiwa Spika, ninamshukuru sana pia Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushirikiano wake mkubwa wakati wote nikitekeleza majukumu ya Waziri Mkuu. Vilevile, ninashukuru sana kwa ushirikiano mkubwa nilioupata kutoka kwa Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar pamoja na viongozi, watendaji na wananchi wote wa Zanzibar.

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii pia kukushukuru sana wewe binafsi kwa upendo uliouonesha kwangu kipindi chote cha uhai wa Bunge la Kumi na Moja (11). Kwa uzoefu ulionao katika kuendesha Bunge, umekuwa msaada sana kwangu kwa kunipa ushauri na ushirikiano wa dhati ulionifanya nijenge imani kubwa kwenye majukumu yangu ndani ya Bunge.

Mheshimiwa Spika, nami niungane na wenzangu kukutakia kheri nyingi kwenye Uchaguzi ujao, naamini Wana-Kongwa watasikiliza na kutekeleza dua zetu za kuwa upite bila kupingwa, na ukirudi hapa chukua fomu ya Uspika ili upate kura zote za ndiyo uendelee kuwa Spika wa Bunge la Kumi na Mbili (12).

Mheshimiwa Spika, sitasahau tukio la tarehe 19 Novemba, 2015 siku ambayo Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipowasilisha jina langu katika Bunge lako Tukufu na kupendekeza niwe Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru tena wewe na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwa imani mlioionesha kwa kuridhia mapendekezo ya Mheshimiwa Rais na kunipigia kura nyingi za ndiyo na mkaridhia tufanye kazi kwa pamoja katika kuwatumikia Watanzania.

Waheshimiwa Wabunge wenzangu, natambua, naheshimu na nathamini ushirikiano wa dhati mlionipa katika kipindi chote cha Bunge. Nami nawaombea na nawatakia ushindi wa kishindo kwenye Majimbo yenu ili mrudi tena hapa mwezi Novemba, 2020.

Mheshimiwa Spika, pia, nawashukuru sana Mheshimiwa Dkt. Tulia Akson, Naibu Spika, Wenyeviti wa Bunge Mheshimiwa Mtemi Andrew Chenge, Mheshimiwa Najma Murtaza Giga na Mheshimiwa Mussa Zungu Azzan ambaye mwishoni alipata uteuzi wa Mheshimiwa Rais kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira kwa kuliongoza Bunge hili kwa busara na umahiri mkubwa.

Mheshimiwa Spika, vilevile, namshukuru Mheshimiwa Mashimba Mashauri Ndaki, Mbunge wa Maswa Magharibi na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti pamoja na Wajumbe wote wa Kamati hiyo kwa mchango wao mkubwa katika kufanikisha Bajeti ya Serikali. Pia, nawashukuru Katibu wa Bunge Ndugu Stephen Kagaigai na Watumishi wote wa Bunge kwa ushirikiano mkubwa waliotupatia katika Mkutano huu na Mikutano iliyoendeshwa kipindi chote cha miaka mitano.

Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu hapa Bungeni, napenda kutambua mchango wa Mheshimiwa Jenista Joakim Mhagama (Mb), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayesimamia Sera, Uratibu, Bunge, Ajira, Kazi, Vijana na Watu wenye ulemavu. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mhagama kwa kunisaidia ipasavyo katika kutekeleza majukumu yangu sambamba na majukumu yake ya unadhimu na uratibu wa shughuli za Serikali Bungeni. Nakuombea sana kwa wananchi wa Peramiho, Maposeni, Mgazini, Mdunduwalo, wakupitishe upite bila kupingwa.

Mheshimiwa Spika, vilevile, namshukuru Mheshimiwa Angela Kairuki (Mb), Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji kwa kufuatilia na kusimamia hatua mbalimbali za kuimarisha na kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini. Mheshimiwa Waziri Kairuki amekuwa akitembelea maeneo mbalimbali na kukutana na Wawekezaji wadau wa sekta binafsi ili kusikiliza changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi. Juhudi zake hizo, zimekuwa na mchango mkubwa katika kuboresha mazingira ya biashara na kuimarisha mahusiano ya sekta binafsi na Serikali nchini. Nawe nakutakia kila la kheri huko uendako ili upate kura za kutosha.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa masuala ya maendeleo na uwezeshaji wa vijana napenda kumshukuru Mheshimiwa Anthony Peter Mavunde, Mbunge wa Dodoma Mjini, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu kwa msaada mkubwa katika kusimamia vizuri masuala ya vijana na ajira. Kadhalika, namshukuru Dada yangu Mheshimiwa Stella Ikupa Alex (Mb), Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kusimamia vema masuala na maslahi ya Watu Wenye Ulemavu.

Nawashukuru sana Waheshimiwa Mawaziri wenzangu na Naibu Mawaziri; Professor Adelardus Kilangi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali; Balozi Mhandisi John William Kijazi, Katibu Mkuu Kiongozi; Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu wakiongozwa na Bw. Tixon Tuyangine Nzunda, Andrew Wilson Massawe, na Bibi Dorothy Aidan Mwaluko kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu. Nawashukuru kwa ushirikiano wa dhati mlionipa katika kuratibu na kusimamia shughuli za Ofisi ya Waziri Mkuu. Bila kuwasahau Watendaji wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii pia kuwashukuru Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama akiwemo Jenerali Venance Mabeyo - Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama; Inspekta Jenerali wa Polisi - Simon Nyakoro Sirro; Brigedia Jenerali Suleiman Mzee -Kamishna Jenerali wa Magereza; Dkt. Anna Makakala - Kamishna Jenerali wa Uhamiaji; John William Hasunga - Kamishna Jenerali wa Zimamoto na Uokoaji; Kamishna Diwani Athumani - Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa; Brigedia Jenerali John Mbung’o - Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa; James Kaji - Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Madawa ya Kulevya.

Wakuu hao wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama wameonesha nidhamu na uzalendo mkubwa katika kuhakikisha Nchi yetu, raia wake na mali zao wanakuwa salama.

Mheshimiwa Spika, nawashukuru pia Wakuu wa Taasisi, Wakurugenzi na Watendaji wote Serikalini kwa ushirikiano mzuri walioutoa na utendaji wa pamoja wenye mafanikio makubwa. Aidha, tuendelee kutakiana mema na tuchape kazi hadi hapo utumishi wetu utakapokoma.

Mheshimiwa Spika, nimalizie salamu zangu za shukrani kwa Familia yangu ambayo inaniunga mkono, kunivumilia pale ambapo nawatumikia Watanzania na kunitia moyo siku hadi siku kwenye majukumu yangu. Bila kuwasahau Wana-Ruangwa ambao walinipigia kura bila kujali Vyama vyao na kuniwezesha kuingia Bungeni na hatimaye nikapata uteuzi wa Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa ajili ya kuwatumikia Watanzania. Nataka niwahakikishie Wana-Ruangwa kuwa bado tuko pamoja katika harakati za kuleta maendeleo. Nawashukuru sana.

Mheshimiwa Spika, nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitawashukuru wananchi na Watanzania wote kwa kuiunga mkono Serikali ya Awamu ya Tano na ushirikiano walioutoa kwa Serikali wakati wa utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo ya Taifa kwa ujumla bila kujali tofauti zao za kiitikadi au dini. Sambamba na kuonesha uzalendo, mshikamano na kudumisha amani na utulivu uliowezesha Serikali kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na weledi, kwa mujibu wa taarifa zinazotolewa na taasisi ya GLOBAL PEACE INDEX 2020 inayofuatilia masuala ya amani duniani. Tanzania ni nchi ya saba kwa amani na utulivu Afrika na   ni nchi ya kwanza kwa amani Afrika Mashariki. Naamini wananchi wataendelea kuiunga mkono Serikali yetu ili ifanye mambo makubwa zaidi katika kipindi cha pili cha Awamu ya Tano kwa amani na maendeleo yake.

Mheshimiwa Spika, baada ya salamu za shukurani nami naungana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu walionitangulia kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, Mbunge wa Iramba Magharibi kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria na Mheshimiwa Dkt. Godwin Aloyce Mollel, Mbunge wa Siha kwa kuteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Aidha, mkiwa viongozi mlioteuliwa, tambueni kuwa mnalo jukumu kubwa la kuwahudumia Watanzania, hususan katika kipindi hiki ambacho Nchi yetu imekumbwa na changamoto mbalimbali likiwemo janga la Corona.

SALAMU ZA POLE

Mheshimiwa Spika, wakati tukiendelea na Mkutano huu wa 19, Bunge lako Tukufu lilipata pigo kwa kuondokewa na Wabunge wenzetu akiwemo Mheshimiwa Mchungaji Dkt. Getrude Pangalile Rwakatare, aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum; Mheshimiwa Richard Mganga Ndassa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Sumve na Mheshimiwa Balozi Dkt. Augustine Philip Mahiga, aliyekuwa Mbunge na Waziri wa Katiba na Sheria.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi hicho pia, tuliondokewa na aliyekuwa Jaji Mkuu Mstaafu, Mheshimiwa Jaji Augustino Ramadhan. Aidha, niungane na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kuwapa pole majirani zetu, wananchi wa Burundi kwa kifo cha aliyekuwa Rais wa Nchi hiyo, Mheshimiwa Pierre Nkurunzinza. Tuendelee kumuomba Mwenyezi Mungu azipumzishe Roho za wapendwa wetu wote mahali pema. Amina.

Mheshimiwa Spika, vilevile, Taifa letu lilikumbwa na majanga mbalimbali ikiwa ni pamoja na mafuriko, COVID-19 na ajali za barabarani ambazo zilisababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali. Napenda kutoa salamu za pole kwa ndugu, jamaa na marafiki waliopoteza wapendwa wao na wengine kupata majeraha kutokana na matukio hayo. Tumuombe Mwenyezi Mungu aziweke Roho za marehemu mahali pema na waliopata majeraha awajalie nafuu na kupona mapema. Amina.

MAFANIKIO YA SERIKALI YA AWAMU YA TANO

Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee kabisa nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutokana na fikra na uongozi makini katika ujenzi wa Taifa letu. Ni dhahiri kuwa maono yake katika kuongoza na kusimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015 - 2020 na mipango ya Serikali, zimeleta mafanikio makubwa ambayo hivi sasa wote tunayaona.

Mheshimiwa Spika, nyote mtakubaliana nami kwamba Mheshimiwa Rais na Makamu wake Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanawafikia Watanzania, wanawasikiliza na kutatua kero zao. Lengo la ziara hizo, pamoja na mambo mengine lilikuwa ni kusimamia utekelezaji wa maelekezo ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015 ikiwemo kukagua miradi ya maendeleo; kuzungumza na watumishi na kuwafahamisha kuhusu falsafa ya Serikali ya awamu ya tano ya Hapa Kazi Tu.

Mheshimiwa Spika, ziara hizo zimesaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha utendaji wa watumishi wa umma. Hivi sasa, wananchi wanapokwenda katika ofisi za umma wanapokewa, wanasikilizwa na kuhudumiwa vizuri. Aidha, usimamizi wa miradi ya maendeleo umeimarika sambamba na kuakisi thamani halisi ya fedha katika utekelezaji wa miradi hiyo. Hapa Bungeni ninawashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa maoni, ushauri na ushirikiano ambao mmekuwa mkiutoa wakati wa ufuatiliaji wa shughuli za maendeleo sambamba na kuisimamia Serikali yetu.

Mambo mengi ya kujivunia yamefanywa na tumekuwa tukiyaeleza katika maeneo mengi kupitia mikutano ya hadhara, vyombo vya habari, nyaraka mbalimbali, uwepo wa miradi mingi ya kimkakati hadi kwa wananchi wa kawaida.

Nitaeleza majukumu na miradi michache tena kwa kifupi ili kuwakumbusha nini Serikali imefanya katika kipindi hiki cha miaka mitano.

 

 • Marekebisho ya nidhamu kwa utumishi wa umma na uwajibikaji Serikalini ili kuwezesha Watumishi kutambua majukumu yao na kuwatumikia Watanzania.

 

 • Mapambano dhidi ya rushwa ndani ya Serikali na nje ya Serikali ili kulinda mali na fedha za umma. Hatua hii ni endelevu, lengo ni kung’oa mizizi ya rushwa nchini.

 

 • Kuimarisha vyombo vya ulinzi na usalama, mhimili wa Bunge na Mahakama. Matakwa yetu ni kuhakikisha kuwa nchi inabaki salama na mihimili ifanye kazi yake.

 

 • Mapambano dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya ili kujihakikishia kuwa tunakuwa na Taifa lenye nguvukazi inayofanya kazi. Mapambano bado yanaendelea. Tutapambana na wazalishaji, wasambazaji, wauzaji na watumiaji wa dawa za kulevya.

 

 • Utambuzi wa watumishi hewa waliokuwa wanalipwa fedha wakiwa hawapo. Katika zoezi hili tumepata mafanikio makubwa na kuokoa shilingi Bilioni 19.83 kwa kuwaondoa kwenye mfumo wa malipo watumishi hewa 19,708 na wenye vyeti vya kugushi 15,411.

 

 • Ukusanyaji wa mapato ili kuwezesha Serikali kujenga miradi na kutoa huduma muhimu. Ukusanyaji wa mapato umeongezeka kutoka wastani wa shilingi Bilioni 800 kwa mwezi mwaka 2015 hadi wastani wa shilingi trilioni 1.5 kwa mwezi katika kipindi cha Julai 2019 hadi Aprili 2020.

 

 • Kuimarisha uwekezaji kwa kujenga viwanda. Hadi Aprili 2020 jumla ya viwanda vipya 8,477 vikiwemo vidogo, vya kati na vikubwa vimeanzishwa katika maeneo mbalimbali nchini na hivyo kuwezesha ongezeko la ajira viwandani za viwandani zipatazo 482,601.

 

 • Kuimarisha kilimo na masoko. Tumeimarisha kilimo cha mazao makuu, kama vile, Korosho, Pamba, Chai, Tumbaku, Kahawa, Michikichi na Mkonge pamoja na mazao ya chakula ili kuwa na uhakika wa usalama wa chakula.

 

 • Kuimarisha ushirika wa kilimo na upatikanaji wa pembejeo pamoja na huduma za ugani ili kuwafanya wakulima kuzalisha kwa tija.

 

 • Marekebisho ya Sheria ya madini yamefanyika sambamba na kuanzisha masoko ya madini 28 na vituo 12 vya ununuzi wa madini katika maeneo ya uchimbaji na hivyo kuongeza makusanyo ya Serikali, kupungua biashara haramu na utoroshaji madini kwenda nje. Mwezi Machi hadi Septemba, 2019 jumla ya kilo za dhahabu 4,680.28 zenye thamani ya shilingi bilioni 432.49 zimezalishwa na Serikali kukusanya shilingi bilioni 30.27.

 

 • Kuhamishia Makao Makuu Dodoma ambapo tayari Watumishi wapatao 15,361 wamehamia Dodoma na sasa fursa za uwekezaji zimeongezeka katika Jiji la Dodoma.

 

 • Kuboresha miundombinu na taaluma Sekta ya Elimu kwa ngazi zote kuanzia awali hadi Elimu ya Juu ikiwemo ujenzi na ukarabati wa madarasa, maktaba, maabara, nyumba za walimu, mabweni na ukarabati wa shule kongwe ili kuziongezea uwezo wa kupokea wanafunzi wengi zaidi.

 

 • Sera ya Elimu bila Ada ambayo inatumia zaidi ya Shilingi Bilioni 20.8 kila mwezi kwa ajili ya fidia ya ada, posho ya madaraka kwa walimu wakuu, wakuu wa shule na waratibu kata kila mwezi toka 2016 na tutaendelea. Hii imesaidia kuongeza uandikishaji na mahudhurio shuleni.

 

 • Kuimarisha huduma za afya kwa kujenga Zahanati, Vituo vya Afya, kujenga Hospitali za Wilaya, Mikoa, Kanda na za Kitaifa, huduma za Madawa na Vifaa Tiba. Tumejenga Zahanati 1,198 Vituo vya Afya 487, Hospitali za Wilaya 71, Hospitali za Rufaa za Mikoa 10, na Hospitali za Kanda 03 za Kusini – Mtwara, Magharibi – Tabora na Kanda ya Ziwa - Burigi.

 

 • Ujenzi wa miradi ya maji Vijijini na Mijini tumefikia asilimia 84 Mijini na asilimia 1 Vijijini.

 

 • Ufufuaji wa Shirika la Ndege kwa kununua ndege kumi na moja (11) ambazo zinatoa huduma mikoa yote yenye Viwanja vya Ndege na nje ya nchi.

 

 • Ujenzi na ukarabati wa Viwanja vya Ndege kwenye mikoa isiyo na Viwanja vya Ndege unaendelea.

 

 • Ununuzi wa Rada nne mpya za kuongoza Ndege za kiraia zilizo Mwanza, Mbeya, Dar-es-Salaam na Kilimanjaro.

 

 • Ujenzi wa mradi mkubwa wa kufua umeme (Mwalimu Nyerere Dam) utakaozalisha Mg 2115 kwa sasa umefikia asilimia 40. Ujenzi una gharama ya Shilingi Trilioni 6.5

 

 • Usambazaji wa umeme Vijijini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) tumefikia Vijiji kwa asilimia 80% ambapo hadi Aprili 2020 shilingi trilioni 2.27 zimetumika na kufanikisha jumla ya vijiji 9,112 kati ya 12,268 vya Tanzania Bara kuunganishwa na umeme kutoka vijiji 2,118 mwaka 2015.

 

 • Ujenzi wa Mradi wa Reli ya Kimataifa (SGR) wa Kilomita 300 Dar-es-Salaam–Morogoro. Mradi umefikia asilimia 78. Kipande cha Morogoro hadi Makutupora Kilomita 422 mradi umefikia asilimia 30 ya kazi. Lengo ni kukamilisha mradi huu ifikapo Juni 2021 kwa gharama ya Shilingi Trilioni 7.5.

 

 • Ujenzi wa Barabara kwa kiwango cha lami zikiwemo barabara kuu, barabara za mikoa na za wilaya zenye thamani ya zaidi ya Shilingi Trilioni 7.6. Pia serikali inaendelea kujenga barabara ya njia nne kutoka kutoka Kimara hadi Kibaha (km 19.2)

 

 • Ujenzi wa madaraja: ujenzi wa daraja la juu la Mfugale (Dar-es- Salaam), daraja la Furahisha (Mwanza) na daraja la Magufuli (mto Kilombero) umekamilika; ujenzi wa barabara ya pete (Ubungo interchange) umefikia asilimia 77 kwa shilingi bilioni 247; Aidha, ujenzi unaendelea kwa daraja la New Selander (Dar- es-Salaam) kwa shilingi Bilioni 270. Daraja la Kigongo- Busisi shilingi Bilioni 699.2

 

 • Ujenzi wa Bandari, uboreshaji na upanuzi wa Bandari za Tanga, Dar-es-Salaam na Mtwara kwa Shilingi zaidi ya Trilioni 1.2. Pia, ujenzi wa Bandari ya Kigoma na Kalema umeshatengewa fedha.

 

 • Ujenzi wa Meli mpya yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo katika Ziwa Victoria na ujenzi wa chelezo; ukarabati wa meli ya MV Victoria na MV Butiama ambapo katika kipindi cha mwaka 2015/16 hadi Aprili, 2020 jumla ya shilingi bilioni 111.7 zimetumika.

 

Vile vile, Serikali imekamilisha ujenzi wa meli moja mpya yenye uwezo wa kubeba abiria 200 na tani 200 za mizigo katika Ziwa Nyasa; na ukarabati wa meli ya mafuta ya MT Sangara katika Ziwa Tanganyika.

 

 • Ujenzi wa Vivuko vya MV Kigamboni, MV Pangani, Kigongo -Busisi, MV Sengerema na Nyamisati.

 

 • Urejeshaji na usimamizi wa mali za Ushirika zilizokuwa zimechukuliwa kinyume na utaratibu, kama vile, NYANZA, SHIRECU, KNCU, Mamlaka ya Mkonge Tanzania, n.k.

 

 • Kusimamia maboresho kwenye Sekta ya Uvuvi na Mifugo kwa kuvua na kufuga kisasa, kujenga viwanda na masoko yake.

 

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Chama cha Mapinduzi kupitia Bunge lako Tukufu katika kipindi cha miaka minne imeidhinisha jumla ya shilingi trilioni 33.1 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kote nchini ikiwemo miradi ya kimkakati niliyoitaja hivi punde

MVUA KUBWA ZILIZONYESHA NCHINI

Mheshimiwa Spika, baadhi ya maeneo ya Nchi yetu yalikumbwa na mafuriko kufuatia mvua nyingi zilizonyesha nchini. Mafuriko hayo yalisababisha madhara mbalimbali ikiwemo uharibifu wa miundombinu, mali na vifo. Serikali imeendelea kuchukua hatua za kurejesha hali ya miundombinu iliyoharibika na zoezi hilo ni endelevu.

Mheshimiwa Spika, mvua nyingi tulizopata msimu huu zimeleta neema ya mavuno lakini pia katika baadhi ya maeneo mazao yameharibika. Hivyo, niendelee kusisitiza kauli ya Waziri wa Kilimo wakati akiwasilisha Hoja ya Wizara yake kuwa hali ya chakula nchini imeendelea kuimarika. Kwa msingi huo, hatutarajii kuwa na upungufu wowote wa chakula kwa msimu ujao. Muhimu kwetu ni kuongeza umakini wa matumizi kwa kuweka akiba ya chakula ili kitosheleze mahitaji ya familia hadi msimu ujao.

MAPAMBANO DHIDI YA HOMA KALI YA MAPAFU COVID 19

Mheshimiwa Spika, mwezi Machi, 2020, baada ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kutangaza kuwa COVID 19 ni janga la dunia, ambako nchi nyingi duniani zilipata maambukizi makubwa, Tanzania tulitangaza kisa cha kwanza tarehe 15 Machi, 2020.

Nchi nyingi duniani zikiwemo nchi za Bara la Afrika ugonjwa huu ulianza kuingia. Kila nchi ilichukua hatua kadhaa za kudhibiti maambukizi zikiwemo watu kutotoka ndani ya nyumba zao “Lockdown”, kuzuia mikusanyiko kwa kufunga mashule, vyuo, michezo, aina zote za usafiri wa ndani na nje, maeneo ya Ibada na shughuli za uzalishaji maeneo ya kazi, viwanda, n.k. vilifungwa.

Tanzania nasi tulianza kuchukua hatua kadhaa ili kukabiliana na maambukizi kwa kuunda Kamati 3 za ngazi ya Mawaziri, Watendaji na Wataalam wa Afya kwa lengo la kufanya tathmini ya hatua za kuchukua ili kupunguza maambukizi na kulinda anguko la kiuchumi.

Hatua zilizochukuliwa ni kupunguza misongamano kwa kufunga shule, vyuo, mikutano, kunawa maji, matumizi ya vitakasa mikono na kuvaa barakoa.

Mheshimiwa Spika, siku ya tarehe 22 Machi, 2020 Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwa Jijini Dodoma na tarehe 03 Mei, 2020 akiwa Chato aliwataka Watanzania kuwa watulivu waondoe hofu ya ugonjwa huu na ni ugonjwa kama magonjwa mengine, kama vile Malaria, UKIMWI, Kifua Kikuu, n.k. na kuwataka Watanzania kuchukua tahadhari na kuendelea na shughuli za uzalishaji mali, kufanya kazi ofisini, viwandani, mashambani na kutofunga nyumba za Ibada.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais alihutubia tena Taifa tarehe 16 Aprili, 2020 kwa kutoa maelekezo na kusisitiza yafuatayo:

Mosi:           Aliwasihi Watanzania kuondoa hofu kwa kuwa Mungu yupo nasi na hivyo, waendelee kuchapa kazi ili kunusuru uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla na kuzingatia kanuni za afya.

 

Pili:             Watanzania watumie siku tatu kumuomba na kumlilia Mwenyezi Mungu kwani Mungu yu pamoja nasi na atatusikia huku akiendelea kusimamia kauli yake ya kuwataka Watanzania wafanye kazi kwa bidii na kumtegemea Mungu bila kujali kauli za kebehi na ukosoaji kutoka pande mbalimbali za dunia;

 

Tatu:           Alihimiza Watanzania kumtegemea Mwenyezi Mungu na kwamba Mwenyezi Mungu pekee ndiye atakayetuvusha na kutuepusha na janga hili;

 

Nne:            Aliwahimiza Watanzania kutopuuza umuhimu wa tiba mbadala katika mapambano dhidi ya COVID-19. Kauli hii, imekuwa chachu katika kuimarisha tafiti za dawa za asili ambazo zimekuwa na mchango mkubwa katika kupambana na maradhi mbalimbali ikiwemo COVID-19; na

 

Tano:          Tarehe 20 Mei, 2020 akiwa Singida, aliwaomba Watanzania watumie siku tatu kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa maajabu aliyoyafanya kwa Taifa letu kwa kutuepusha kusambaa kwa virusi vya COVID-19.

Mheshimiwa Spika, hali iliyoko sasa, ni kuwa maambukizi yamepungua na wagonjwa wamepungua hospitalini. Kama kuna anayestahili sifa ni Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa msimamo wake usiotetereka na maono ya mbali aliyokuwa nayo yamekuwa chachu katika kupunguza maambukizi ya COVID-19 na kulinda uchumi wa Nchi. Mheshimiwa Rais ameifanya Tanzania kuwa ya kupigiwa mfano duniani kwa namna alivyoshughulikia ugonjwa huu.

Mheshimiwa Spika, pongezi maalum kwa Viongozi wa dini kwa namna walivyoshirikiana na waumini katika mapambano ya ugonjwa wa COVID-19. Wakati wote Viongozi hao wamekuwa wakiwapatia waumini (Watanzania) faraja pia na wagonjwa kwamba Mwenyezi Mungu atawaponya. Hatua hizo zimekuwa mhimili mkubwa wa upendo, umoja, mshikamano na ujasiri miongoni mwa Watanzania. Tunawashukuru sana.

Mheshimiwa Spika, taarifa iliyotolewa na Taasisi ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (Organisation for Economic Cooperation and Development - OECD) inabashiri kuwa kitendo cha kuwafungia watu ndani yaani Lockdown kumesababisha vifo kwa njaa na kusinyaa kwa uchumi wa nchi zilizoendelea kwa asilimia 2 kila mwezi.

Mheshimiwa Spika, hivi sasa, nchi nyingi zinakubaliana kuwa “Lockdown” si hatua sahihi ya kukabiliana na COVID-19. Vilevile, kisayansi inakadiriwa kuwa nchi ambazo ziliwafungia watu wake na mipaka yake zipo katika hatari ya kukumbwa na madhara makubwa ya ugonjwa huo pindi utakapotokea mlipuko wa pili na hata wa tatu.

Mheshimiwa Spika, kwa mantiki hiyo, mtizamo na hatua zilizochukuliwa na Tanzania katika kupambana na COVID-19 zinaonesha upekee tulionao kama nchi. Serikali, inayo kila sababu ya kuwapongeza Watanzania ambao si tu walipokea maelekezo ya Serikali lakini pia walifanya hivyo kwa uaminifu mkubwa na kwa hiari yao wenyewe bila kushurutishwa na mamlaka yoyote ya nchi.

Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuwashukuru wataalamu wetu wa afya kwa kuwahudumia wagonjwa wa COVID19. Wataalamu wetu hao, walitekeleza majukumu yao bila kujali hatari ya virusi hivyo kwa maisha yao na wapendwa wao. Vievile, naishukuru sekta binafsi, mtu mmoja mmoja na wadau wote ambao waliitikia wito wa Serikali kwa kutoa michango ya hali na mali katika kufanikisha vita dhidi ya COVID19 nchini. Kipekee, niwashukuru wamiliki wa viwanda ambao waliitikia wito wa Mheshimiwa Rais na kuanza kuzalisha vifaa kinga hapa nchini badala ya kuagiza nje waende kufanya hivyo.

Mheshimiwa Spika, ni matumaini yetu kwamba zile nchi zilizoondoa vizuizi sasa zinalo somo la kujifunza kutoka Tanzania. Aidha, suala la kudhibiti maambukizi ya COVID 19 litaendelea kuwa kipaumbele cha Serikali kwa sasa sambamba na malengo ya muda mrefu ya kumaliza ugonjwa huo hususan katika kipindi hiki ambacho Shirika la Afya Duniani (WHO) nalo limebainisha kwamba COVID 19 si gonjwa la kuondoka mara moja. Hivyo, watu na dunia kwa ujumla hatuna budi kujifunza namna ya kuishi na virusi hivyo kama ilivyo kwa UKIMWI na virusi vingine, huku tukifanya kazi ili kujiletea maendeleo.

Mheshimiwa Spika, tarehe 9 Juni Bunge lako Tukufu lilipitisha Azimio la kumpongeza na kumuunga mkono Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna alivyomudu kuivusha nchi katika janga la COVID-19. Waswahili husema mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni. Katika hili, nami naomba niseme kidogo kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa hotuba zake zote zilizohusu ugonjwa huu ambapo alihimiza masuala muhimu kwa Watanzania katika kukabiliana na janga hili na zilitibu hofu kubwa iliyokuwa imetanda kwa Watanzania.

Mheshimiwa Spika, leo tunaona idadi ya wagonjwa wanaougua inapungua sana. Kwa mfano, taarifa ya leo, Jumatatu tarehe 15 Juni, 2020 kutoka katika Vituo vya kutolea huduma na Hospitali za Serikali na Binafsi nchini, inaonesha kuwa tuna wagonjwa 75 katika Mikoa 12 na Mikoa 14 haina wagonjwa ikiwemo Mkoa wa Dodoma, Geita, Kagera, Katavi, Kigoma, Lindi, Mara, Manyara, Pwani, Rukwa, Ruvuma, Simiyu, Songwe na Tabora. Pamoja na mwenendo huu, ninawaomba wananchi wote kuendelea kuchukua tahadhari zote za kiafya na miongozo inayotolewa na Serikali.

Nampongeza sana Mheshimiwa Ummy Mwalimu (Mb), kwa kazi kubwa aliyoifanya usiku na mchana kuhakikisha kuwa maambukizi yanapungua kwa kasi. Tumshukuru Mwenyezi Mungu kwa hatua tuliyofikia. Pia, nawashukuru Katibu Mkuu, Mganga Mkuu wa Serikali na Watendaji wote wa Wizara ya Afya kwa usimamizi wa tatizo hili na naamini mnaendelea vema. Hongereni sana.

SHUGHULI ZILIZOTEKELEZWA KATIKA BUNGE LA 11 (2015–2020)

Mheshimiwa Spika, wakati Bunge la 11 likielekea kuhitimisha shughuli zake, limefanikiwa kutekeleza masuala mbalimbali ikiwemo kujibu maswali na hoja zilizowasilishwa na Waheshimiwa Wabunge; kujadili na kupitisha Miswada ya Serikali; Maazimio mbalimbali yenye kuhusisha Mikataba na Itifaki za Kikanda na Kimataifa; kupokea kauli za Serikali kuhusu ufafanuzi wa mambo mbalimbali pamoja na kuunda Tume kwa ajili ya kufuatilia masuala muhimu yenye maslahi mapana kwa Taifa letu.

Maswali na Majibu

Mheshimiwa Spika, katika kipindi chote cha Bunge la 11 linaloelekea kuhitimisha uhai wake tarehe 16 Juni, 2020 jumla ya maswali ya msingi 3,962 yameulizwa na Waheshimiwa Wabunge na kujibiwa na Serikali. Aidha, maswali ya nyongeza 9,563 yameulizwa kutokana na maswali ya msingi na kujibiwa na Serikali. Vilevile, jumla ya maswali 178 ya kawaida na ya nyongeza 162 yameulizwa na Wabunge na kujibiwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu kupitia utaratibu wa maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Spika, kupitia Mkutano huu wa Kumi na Tisa, jumla ya maswali 471 ya msingi na mengine 69 ya nyongeza yaliulizwa na Waheshimiwa Wabunge na kupatiwa majibu na Serikali.

Miswada, Maazimio ya Bunge na Kauli za Serikali

Mheshimiwa Spika, hadi sasa Serikali imewasilisha jumla ya Miswada 60 ya Sheria ambayo imejadiliwa na kupitishwa na Bunge la 11 wakati Sheria 159 zimefanyiwa marekebisho. Vilevile, jumla ya Maazimio 38 ya Bunge yamejadiliwa na kuridhiwa na Bunge.  Pia,

Kauli 20 za Serikali zimetolewa ikiwa ni ufafanuzi wa masuala mbalimbali yaliyowasilishwa na Mawaziri. Aidha, Kamati Maalumu 4 za Bunge zimeundwa katika Bunge la 11 kwa ajili ya uchunguzi wa masuala mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu, Bunge lako Tukufu lilipitisha kwa hatua zake zote Miswada ya sheria sita ambayo ni:

 

 • (i) Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na.2) wa Mwaka 2020;

 

 • (ii) Muswada wa Sheria ya Afya ya Mimea wa Mwaka 2020;

 

 • (iii) Muswada wa Sheria ya Kusimamia na Kuendeleza Uvuvi wa Bahari Kuu wa Mwaka 2020;

 

 • (iv) Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na.3) wa Mwaka 2020;

 

 • (v) Muswa wa Sheria ya Fedha za Matumizi wa Mwaka 2020; na

 

 • (vi) Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2020.

 

Maazimio ya Serikali

Mheshimiwa Spika, vilevile, Serikali iliwasilisha katika Mkutano huu Maazimio matano ya Bunge. Maazimio hayo yaliyoridhiwa na Bunge ni kama ifuatavyo:

 • (i) Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa Utoaji Mafunzo na Vyeti vya Wafanyakazi wa Meli za Uvuvi wa Mwaka 1995 F;

 

 • (ii) Azimio la Bunge la kuitaka Serikali Kutobadili Uamuzi wa Jiji la Dodoma kuwa Makao Makuu ya Nchi na Shughuli za Serikali;

 

 • (iii) Azimio la Bunge la Kumpongeza Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa Mafanikio ya Bunge la Kumi na Moja;

 

 • (iv) Azimio la Bunge la Kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa namna alivyoliongoza Taifa katika Mapambano Dhidi ya Janga la Ugonjwa wa Corona (COVID-19);

 

 • (v) Azimio la Bunge Kuhusu Marekebisho ya Kanuni za Kudumu za Bunge.

Kamati za Kudumu za Bunge

Mheshimiwa Spika, wakati wa Mkutano huu, Kamati za Kudumu za Bunge 15 ziliwasilisha Bungeni taarifa za mwaka za kazi. Taarifa hizo zilisheheni uchambuzi wa kina, maoni, ushauri na mapendekezo mbalimbali kwa Serikali. Nitumie fursa hii kuwapongeza Wenyeviti, Makamu Wenyeviti na wajumbe wote wa Kamati hizo kwa kazi nzuri waliyoifanya kuanzia maandalizi ya kazi za Kamati hadi kuwasilisha taarifa zao katika Bunge lako Tukufu.

UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI YA SERIKALI KWA MWAKA 2020/2021

Mheshimiwa Spika, leo hii tarehe 15 Juni, 2020 Waheshimiwa Wabunge 304 kati ya Wabunge 371 wamepitisha kwa kishindo Bajeti ya Serikali ya mwaka 2020/2021 ya jumla ya shilingi trilioni 34.88. Kati ya fedha hizo, shilingi trilioni 21.98 ni za matumizi ya kawaida na shilingi trilioni 12.90 ni za miradi ya maendeleo sawa na asilimia 37 ya bajeti yote.

Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kuungana na Waheshimiwa Wabunge kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), Waziri wa Fedha na Mipango, kwa kuwasilisha kwa umahiri mkubwa Hotuba ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2019 na Mpango wa Maendeleo na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2020/2021 na kuhitimisha hoja hiyo. Ninawapongeza pia Mheshimiwa Dkt. Kijaji, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango;   Katibu Mkuu; Naibu Makatibu Wakuu na Watendaji wa Wizara kwa kufanya kazi kwa ushirikiano. Matunda tunayaona.

Mheshimiwa Spika, kipekee niwashukuru na kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yao ambayo imesheheni maoni na ushauri mzuri kwa Serikali wakati wa kujadili makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara mbalimbali kwa mwaka 2020/2021 pamoja na mjadala kuhusu Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2019 na Mpango wa Maendeleo na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2020/2021. Nalishukuru Bunge lako Tukufu kwa kupitisha Bajeti ya Serikali ya mwaka ujao wa fedha kwa kura nyingi za ndiyo.

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi shupavu wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imejipanga vizuri kutekeleza mipango yote iliyowekwa katika Mpango wa Maendeleo na Bajeti ya mwaka 2020/2021. Nitoe rai kwa Waheshimiwa Wabunge na Madiwani kuendelea kushirikiana na Serikali katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu.  Aidha, natoa wito kwa sekta binafsi, wadau wa maendeleo na wananchi wote kuendelea kutoa ushirikiano katika utekelezaji wa mpango na bajeti ya Serikali kwa mwaka ujao wa fedha.

Mheshimiwa Spika, sambamba na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu, utekelezaji wa kazi za Serikali utaendelea. Hivyo, Watumishi wote wa Umma wanashauriwa kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uaminifu na kutoa huduma bora kwa wananchi kwa ufanisi na tija wakati wote. Aidha, katika kufanikisha utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2020/2021, napenda kutoa msisitizo katika maeneo yafuatayo:

Kwanza:     Serikali itaendelea kutekeleza Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2020/2021 kwa kuzingatia athari na changamoto za ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya Corona;

Pili:             Serikali itakamilisha mchakato wa shughuli zilizobaki za maandalizi ya uchaguzi mkuu wa ubunge, urais na udiwani na kuiwezesha Tume ya Taifa ya Uchaguzi kusimamia kikamilifu shughuli zote za uchaguzi huo kwa uhuru na haki;

 

Tatu:           Serikali itatoa msukumo wa kipekee katika kukamilisha miradi ya kipaumbele na miradi ya kimkakati inayoendelea kutekelezwa na Serikali ya awamu ya tano ili wananchi waendelee kupata huduma bora;

 

Nne:             Serikali itashirikiana na sekta binafsi kuleta mageuzi kwa kutekeleza kwa kasi mpango wa kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini (yaani Blue Print for Business Environment). Lengo ni kuhakikisha shughuli za uchumi na biashara zinashamiri na kuchangia kuondoa umaskini nchini; na

 

Tano:           Serikali itaendelea kuboresha huduma za jamii pamoja na kuhakikisha kwamba ulinzi na usalama unaimarishwa.

 

UCHAGUZI MKUU WA MWAKA 2020

Mheshimiwa Spika, Tume ya Taifa ya Uchaguzi inaendelea vema na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020. Hivi sasa, pamoja na mambo mengine Tume imekamilisha matakwa ya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi ya kufanya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mara mbili kati ya Uchaguzi Mkuu mmoja na mwingine.

Mheshimiwa Spika, zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura wa awamu ya kwanza lilianza rasmi tarehe 18 Julai, 2019 na kukamilika tarehe 23 Februari, 2020 kwa Nchi nzima wakati awamu ya pili ilianza tarehe 17 Aprili, 2020 na kukamilika tarehe 05 Mei, 2020.

Mheshimiwa Spika, takwimu za awamu ya kwanza na ya pili, zinaonesha kuwa wapiga kura wapya walioandikishwa ni 7,326,552, wapiga kura walioboresha taarifa zao ni 3,548,846 na wapiga kura 30,487 wamepoteza sifa. Hadi sasa jumla ya Wapiga Kura halali kwa mwaka 2020 ni 29,804,992 ikilinganishwa na Wapiga Kura 23,161,440 wa mwaka 2015.

Mheshimiwa Spika, Tume inaendelea na uchambuzi wa taarifa za Wapiga Kura waliojiandikisha na baada ya zoezi hilo kukamilika, Daftari la mwisho litakalotumika katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 litaandaliwa na kuwekwa wazi.

Mheshimiwa Spika, niwasihi viongozi na wanachama wa vyama vyote vya siasa na wananchi kwa ujumla kuendelea kulinda amani yetu na kuendeleza mshikamano katika kipindi hiki na wakati wa uchaguzi mkuu. Natoa wito kwa Viongozi wa Vyama vya Siasa na Wadau wengine wa uchaguzi kuzingatia Katiba, Sheria, Kanuni na miongozo iliyopo katika uendeshaji wa shughuli za uchaguzi.

MICHEZO

Mheshimiwa Spika, kwa miaka hii mitano tunaendelea kuonesha upekee wa Mheshimiwa Rais wetu mbali ya kazi kubwa ya ujenzi wa miradi ya huduma za jamii, pia Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli amehamasisha masuala ya kijamii ikiwemo michezo.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais ni mwanamichezo na msanii ambaye amekuwa hasiti kuonesha kipaji chake cha matumizi ya ala ya ngoma. Aidha, wote ni mashahidi kila awapo palipo na wasanii wanaotoa burudani ya ngoma huwa lazima akaungane nao na kuonesha umahiri wake kwa kupiga ngoma. Naye anaingia kwenye orodha ya washiriki waliochomoza kuwa maarufu kwa kumudu kutumia ala hiyo kwa kipindi hiki cha miaka mitano.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa michezo na burudani tunao Watanzania waliofanya vizuri kwenye eneo hilo katika kipindi cha miaka mitano. Ikumbukwe kuwa ninaowazungumzia hapa ni baadhi ya wanamichezo na wasanii waliolibeba Taifa letu na kupeperusha vema bendera ya Taifa nje ya Nchi.

Mheshimiwa Spika, kwenye michezo ya riadha ni muhimu tukampongeza kijana wetu Alphonce Felix Simbu aliyetuletea medali ya fedha na kupeperusha vyema bendera ya Taifa kwenye mashindano ya mbio ndefu ya majeshi ya Dunia yaliyofanyika nchini China. Wanamichezo wengine waliochomoza nje ya nchi ni pamoja na Mwanamasumbwi Hassan Mwakinyo aliyemtwanga Sam Eggington wa Uingereza kwa knock out katika Raundi ya 2 na kupeperusha Bendera ya Taifa huko Uingereza.

Mheshimiwa Spika, eneo la sanaa na burudani hususan muziki wa Bongo Flavour limekuwa na mchango mkubwa katika kuitangaza nchi yetu. Natumia fursa hii kuwapongeza vijana wetu ambao ni wasanii wa muziki wa Bongo Flavour akiwemo Naseeb Abdul Juma maarufu kama Diamond Platnumz (Simba) pamoja na Rajabu Abdul Kahali maarufu kama Harmonize (Konde boy–Tembo). Tumekuwa tunashuhudia mapokezi wanayopata huko nje na wakitumbuiza muziki wetu na kupeperusha Bendera yetu kwenye mataifa mbalimbali. Wako wengine wengi kama Vanessa Mdee, Raymond Mwakyusa (Rayvanny), Ali Kiba (King Kiba), n.k.

Mheshimiwa Spika, mchezo wa soka nao licha ya kuwa ndio mchezo unaoongoza kwa wapenzi hapa nchini pia umetoa vijana wengi nje wanaoiletea sifa nchi yetu. Kwa upande huu wa soka, sote tumpongeze kijana wetu Mbwana Samata anayelitangaza Taifa letu katika ligi kuu ya Soka nchini Uingereza kwenye Timu ya Aston Villa. Tunawapongeza sana wachezaji wetu kama Simon Msuva, Hassan Kessy, Abdi Banda, Kelvin John, n.k. ambao wanatangaza Taifa letu nje ya nchi. Ni matarajio yetu wapo watakaofuata nyayo zao ili kuliletea sifa Taifa letu.

Soka la Vijana nalo limeendelea kuimarika ambapo Timu za Soka za Vijana wa umri wa miaka 17 na 20 na Timu ya Wanawake – Twiga Stars, zimefanya vizuri katika michezo ya kimataifa na kuleta makombe hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, Taifa Stars nayo katika kipindi cha miaka 39 imeweza kucheza AFCON mara ya pili katika kipindi cha miaka mitano hii.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki cha miaka mitano, tumeshuhudia Klabu kongwe ikipeperusha Bendera ya Taifa nje ya nchi na ikitutoa kimasomaso katika medani za soka la kimataifa kwa kuweka historia ya Taifa letu kwa kucheza hatua ya robo fainali ya Mabingwa wa Afrika baada ya kufuzu hatua ngumu ya makundi nayo si nyingine bali ni SIMBA SPORTS CLUB, Klabu ambayo inakaribia kutangaza ubingwa wa Tanzania kwa Ligi ya ndani kwa mara ya tatu mfululizo ikiwa haijakamilisha michezo 9.

Mheshimiwa Spika, kama inaweza kutangaza ubingwa ikiwa haijamaliza michezo yote hiyo nini faida ya mkuki. Mheshimiwa Spika, ili kuonesha ubora wa Timu mchezaji anayeongoza kwa kufunga magoli mengi ni Medie Kagere aliyefunga magoli 19 kutoka SIMBA SPORTS CLUB na wachezaji wanaofuatia kwa magoli mengi ni Reliants Lusajo wa Namungo FC magoli 11; Yusuph Mhilu wa Kagera Sugar magoli 11; Bigirimana Bleiz wa Namungo FC magoli 10 na Paul Nonga wa Lipuli FC magoli 10. Hatua hii haiwezi kufikiwa na Timu yoyote kwa kuwa mikuki mingi ni butu. Mkuki wenye ncha kali uko SIMBA SPORTS CLUB.

HITIMISHO

Mheshimiwa Spika, nihitimishe hotuba yangu kwa kumshukuru tena Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wake makini uliolipatia Taifa letu mafanikio makubwa katika kipindi kifupi cha miaka mitano. Watanzania wanakuhitaji kuliongoza Taifa hili. Nitoe wito kwa Watanzania kujitokeza kwa wingi ili tumpigie kura za kutosha.

Mheshimiwa Spika, naomba kwa mara nyingine niwashukuru sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Mheshimiwa Dkt. Ali Mohammed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kusimamia vema utekelezaji wa Ilani ya CCM.

Mheshimiwa Spika, vilevile, namshukuru sana Mheshimiwa Balozi Seif Ali Idd, Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa ushirikiano ambao amekuwa akinipatia wakati wote wa kutekeleza majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Spika, narudia tena kukushukuru na kukutakia afya njema. Namshukuru pia Mheshimiwa Prof. Ibrahimu Juma, Jaji Mkuu wa Tanzania kwa ubunifu wake wa kuendesha shughuli za Mahakama kwa njia ya mtandao katika kipindi cha ugonjwa wa COVID-19. Namshukuru pia Mheshimiwa Dkt. Eliezer Feleshi, Jaji Kiongozi, Waheshimiwa Majaji wote, Mahakimu na watendaji wote wa mhimili wa Mahakama kwa kazi nzuri ya kuwahudumia Watanzania.

Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuwashukuru tena Mawaziri na Naibu Mawaziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Makatibu Wakuu pamoja na Wakurugenzi, Wakuu wa Taasisi zilizopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Wafanyakazi wote kwa ushirikiano mkubwa wanaonipatia katika kutekeleza majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Spika, napenda pia kuwashukuru washirika wa maendeleo zikiwemo Nchi rafiki, Taasisi na Mashirika ya Kimataifa, madhehebu ya dini na mashirika yasiyo ya kiserikali, kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kujenga uchumi wa viwanda na kuiletea Nchi yetu maendeleo. Ninawashukuru pia, Viongozi wote wa dini na wanahabari wote kwa ushirikiano mkubwa waliouonesha kwa Serikali katika kipindi chote cha miaka mitano. Mchango wao umekuwa muhimu katika kuiwezesha nchi yetu kupiga hatua kubwa kimaendeleo kulingana na mipango tuliyojiwekea.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki cha miaka mitano tumekuwa karibu sana na kupata ushirikiano mkubwa kutoka kwa viongozi wa Chama cha Mapinduzi katika ngazi zote. Hivyo, Mheshimiwa Philip Mangula, Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa pamoja na Dkt. Bashiru Ally, Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi; nawashukuru sana Viongozi wangu wa CCM kwa kusimamia ipasavyo utekelezaji wa Ilani ya Chama chetu.

Mheshimiwa Spika, kabla sijafika mwisho, niwashukuru tena Waheshimiwa Wabunge kwa ushirikiano wao mkubwa katika kuishauri Serikali. Pia ninawashukuru Watumishi wote wa Bunge kwa huduma nzuri na msaada ambao wamekuwa wakitupatia kipindi chote tulichokuwa hapa Bungeni. Aidha, ninawashukuru Watendaji wote wa Serikali na Taasisi mbalimbali kwa kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi, umahiri na ufanisi mkubwa na hivyo kufanikisha utekelezaji wa shughuli zilizopangwa na Bunge bila kuwasahau Wanahabari kwa uchambuzi na kuuhabarisha umma na Madereva wote walituhudumia wakati wote wa shughuli za Bunge

Mheshimiwa Spika,kipekee, nitumie nafasi hii kuishukuru tena familia yangu ambayo imeweza kunivumilia wakati mwingi nilipokuwa nikitekeleza majukumu yangu ya kitaifa. Namshukuru sana mke wangu Mary Majaliwa na watoto wangu kwa kuniombea, na kunitia moyo wakati wote ninapokuwa nikitekeleza majukumu yangu.

Mheshimiwa Spika, katika utekelezaji wa majukumu ya Waziri Mkuu inawezekana kabisa kwa namna moja au nyingine niliwakwaza baadhi ya viongozi na watendaji, lakini yote ni katika kutekeleza majukumu ya Waziri Mkuu. Imani yangu ni kwamba tutaendelea kulijenga taifa kwa pamoja hususan katika kipindi hiki tunachoelekea kwenye kinyang’anyiro cha Uchaguzi Mkuu.

Mheshimiwa Spika, mwisho wa Bunge hili, ndiyo kiashiria cha Bunge lijalo. Hivyo, nawaaga wote kwa kuamini kuwa wale waliofanya vema katika kipindi hiki wataaminiwa tena na wananchi na kurejea kwenye Bunge lijalo. Hivyo, tuombeane heri ili kila mmoja wetu atakayechukua fomu za kugombea tena apate ushindi na fursa ya kuwatumikia wananchi.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.