HOTUBA YA MHESHIMIWA KASSIM M. MAJALIWA (MB.), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWENYE UZINDUZI WA MBIO ZA MWENGE WA UHURU MKOANI GEITA TAREHE 02 APRILI, 2018

Mheshimiwa Jenista Mhagama (Mb.); Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu,

Mheshimiwa Balozi Ali Abeid Karume, Waziri wa Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo – Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,

Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri,

Mheshimiwa Eng. Robert Gabriel Luhumbi, Mkuu wa Mkoa wa Geita,

Mheshimiwa Alhaji Said Kalidushi, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita;

Makatibu Wakuu,

Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa,

Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya,

Waheshimiwa Wabunge na Wawakilishi,

Waheshimiwa Viongozi wa dini na Vyama mbalimbali vya Siasa;

Waandishi wa Habari;

Ndugu Wananchi;

Mabibi na Mabwana.

SHUKRAN NA PONGEZI

Nianze hotuba yangu kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa Rehema kwa kutufikisha siku hii ya leo tukiwa salama, wenye afya njema, upendo, umoja na mshikamano kama Taifa. Aidha, nitumie fursa hii kuupongeza uongozi wa Mkoa wa Geita na wananchi wake kwa kukubali kuwa mwenyeji wa shughuli hii ya Uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu. Nawashukuru sana kwa maandalizi mazuri mlioyafanya ya kuhakikisha mbio hizi za Mwenge kwa mwaka 2018 zinazinduliwa hapa mkoani Geita kwa kishindo. Hakika mmefanya kazi nzuri. Hongereni sana!

Vilevile, nitumie nafasi hii, kuzipongeza Wizara zetu zinazoratibu shughuli za Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kutimiza wajibu wao kikamilifu. Niwaombe muendelee kusimamia tunu hii tuliyoachiwa na waasisi wa Taifa hili, yaani Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mzee wetu Sheikh Abeid Amani Karume katika misingi ile ile ya kuimarisha Muungano wetu, amani, umoja, uzalendo, upendo, mshikamano, kuhamasisha shughuli za maendeleo katika jamii zetu na kumulika wabadhilifu wa mali za umma.

CHIMBUKO LA MWENGE WA UHURU

Ndugu Wananchi

Mwenge wa Uhuru uliasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mwaka 1961 ikiwa ni ishara ya kuwepo kwa Taifa huru la Tanganyika. Hatua hiyo ilikuwa ni utekelezaji wa ndoto yake iliyotafsiriwa kwa maneno aliyoyatamka mwaka 1958 kwa wajumbe wa Baraza la Kikoloni la Kutunga Sheria na kuyarudia tena mwaka 1959 alipohutubia kikao cha 35 cha Baraza la Umoja wa Mataifa wakati akidai Serikali ya madaraka kama Mbunge mwakilishi pekee wa Tanganyika kwa kusema, ninanukuu;

Sisi watu wa Tanganyika, tungependa kuwasha Mwenge na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro, umulike ndani na nje ya mipaka yetu, ulete matumaini pale ambapo hakuna matumaini, upendo mahali palipo na chuki na heshima palipojaa dharau.Mwisho wa kunukuu.

Falsafa hiyo ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ilikuwa ni ujumbe mzito kwa Waingereza kwamba, watu wa Tanganyika wamechoka kutawaliwa.

Siku Tanganyika ilipopata Uhuru wake, tarehe 9 Desemba, 1961, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliuwasha Mwenge wa Uhuru na akamkabidhi Luteni Alexander Ngweba Nyirenda na kikosi cha vijana wenzake wakaupandisha Mwenge wa Uhuru juu ya Mlima Kilimanjaro. Siku hiyo hiyo Mwalimu akihutubia Taifa, aliwatangazia Watanganyika, Afrika na Dunia nzima akiyarudia maneno hayo kwa kusema, nanukuu; “Sisi tumekwisha uwasha Mwenge wa Uhuru na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro, umulike ndani na nje ya mipaka yetu, ulete matumaini pale ambapo hakuna matumaini, ulete upendo mahali penye chuki na heshima mahali palipo jaa dharau”.

Ndugu Wananchi

Falsafa hii ya Mwenge wa Uhuru siyo tu inatukumbusha historia na harakati za kudai Uhuru, bali ndiyo msingi wa sera zetu za ndani na nje ya Taifa letu. Mifano ya matokeo chanya ya falsafa hii tangu Mwenge wa Uhuru ulipowashwa hadi sasa ni pamoja na; Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964 yaliondoa utawala wa Kisultani, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar Mwaka 1964 ambao ulizaa Taifa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Azimio la Arusha la Mwaka 1967 lililosisitiza Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, sera madhubuti ya nje ya kutofungamana na siasa za upande wowote, Ushiriki wa Tanzania katika Ukombozi wa nchi za Kusini mwa Bara la Afrika ambapo Tanzania ilikuwa Makao Makuu ya Kamati ya Ukombozi Kusini mwa Afrika na kuwa kichocheo kikubwa katika kuhamasisha wananchi wetu kujiletea maendeleo yao wenyewe.

Hivyo, kama Mheshimiwa Rais wetu mpendwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alivyosema mnamo tarehe 14 Oktoba, 2017 huko Zanzibar wakati akihitimisha Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka jana, busara na hekima zilizojengwa chini ya falsafa ya Mwenge wa Uhuru, hazitaachwa na kupotea. Serikali itaendelea kuienzi falsafa hii kwa vitendo na kuifanya kuwa endelevu kwa vizazi vijavyo na kwa maslahi mapana ya Watanzania, Afrika na Dunia kwa ujumla.

ELIMU KAMA UJUMBE MAALUM WA MBIO ZA MWENGE 2018

Ndugu Wananchi

Kama alivyoeleza Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Mbio za Mwenge wa Uhuru huambatana na ujumbe maalum kuhusu masuala muhimu ya Kitaifa au Kimataifa ambao Taifa hulenga wananchi waupate. Kwa mwaka huu wa 2018, tumeamua ujumbe wa Mbio za Mwenge wa Uhuru uzingatie hoja, vipaumbele na mikakati ya Serikali ya kuboresha elimu nchini kupitia kaulimbiu isemayo: “Elimu ni Ufunguo wa Maisha, Wekeza Sasa kwa Maendeleo ya nchi yetu”.

Dhamira ya Serikali kupitia kaulimbiu hii ni kuwashirikisha wananchi na wadau mbalimbali wa maendeleo kuwekeza katika elimu kama sekta muhimu ya kuzalisha rasimali watu yenye ujuzi na stadi zitakazowezesha kuchochea mapinduzi ya viwanda yatakayoifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. Aidha, tumeamua Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu ziendelee kuwakumbusha Watanzania kwamba, mapambano dhidi ya UKIMWI, Malaria, Rushwa na matumizi ya dawa za kulevya yanaendelea hadi tutakapo shinda vita hii kama Taifa.

Ndugu Wananchi

Sasa, kwa kifupi nizungumzie umuhimu wa Sekta ya Elimu katika kuongeza kiwango cha ushiriki wa wananchi katika ujenzi wa taifa letu. Elimu ni mchakato unaomwezesha mwanadamu kupata maarifa na ujuzi ambao unahitajika katika kuleta madiliko ya kimaendeleo ndani ya jamii. Elimu bora huwafanya wanaoipata kufikiri kwa makini juu ya ukweli wa mambo yaliyopo na mambo mapya. Kwa msingi huu, elimu bora ni ile inayohamasisha uendelevu wenye ufanisi katika maisha yote ya mwanadamu. Hii, inatukumbusha usemi wa wahenga wetu usemao: “Elimu ni ufunguo wa maisha”.

Ndugu Wananchi

Napenda nitumie fursa hii kuwaambia kwamba, ukitaka kuleta maendeleo ya uchumi ulio imara, ukitaka kujenga jamii inayo heshimu na kufuata misingi ya uwajibikaji na ubunifu, ukitaka kujenga taifa lenye amani na utulivu, lazima uwekeze zaidi katika elimu. Kwa hiyo, uwekezaji katika elimu haumaanishi tu kuhakikisha watoto wetu na Watanzania kwa jumla wanapata haki yao ya msingi bali ni kuweka misingi imara itakayo liwezesha Taifa na mtu binafsi kufikia hatua bora ya maisha.

Ili kuhakikisha kama Taifa tunafikia viwango bora vya elimu nchini, Serikali ya awamu ya tano inyoongozwa na Rais wetu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, imedhamiria kuboresha elimu katika ngazi zote nchini, kuanzia elimu ya awali hadi elimu ya juu. Uboreshaji huu unakwenda sambamba na ukuaji wa elimu ya ufundi na ufundi stadi tukiweka msisitizo mkubwa katika maendeleo ya sayansi, teknolojia na ubunifu. Elimu hii ndiyo itawawezesha watoto wetu kuwa mahiri katika kukabiliana na mazingira yao na ulimwengu wa soko la ajira kwa kutumia fursa zilizopo ndani na nje ya nchi yetu.

Aidha, kwa kutambua changamoto zinazowakabili wananchi, Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi ya kuhakikisha kuwa Watanzania wanapata elimu iliyo bora kwa usawa. Tumeondoa vikwazo vya kupata elimumsingi (kuanzia Elimu ya Awali hadi Kidato cha Nne) kwa kuanzisha Mpango wa Elimu bila Malipo, kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu na kuhimiza uwekezaji hasa kwenye uboreshaji wa miundombinu, rasilimali watu na vifaa vya kufundishia na kujifunzia.

Ndugu wananchi,

Kama nilivyotangulia kusema, baada ya Serikali ya awamu ya tano kuingia madarakani kumefanyika mageuzi makubwa katika sekta ya elimu kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2015 hadi mwaka huu wa 2018 kama ifuatavyo:

 • Uandikishaji wa wanafunzi wa elimu ya awali umeongezeka kutoka 917,137 hadi 1,182,466 sawa na asilimia 79.32 ya lengo. Kuhusu uandikishaji wa wanafunzi wa Darasa la Kwanza, idadi imeongezeka kutoka 1,386,592 hadi 1,653,397 sawa na asilimia 95.49 ya lengo na wanafunzi walioripoti kidato cha kwanza wameongezeka kutoka 366,396 hadi kufikia 562,266 sawa na asilimia 85.77 ya wanafunzi 655,518 waliopangwa kuingia Kidato cha Kwanza mwaka 2018.
 • Kuhusu uandaaji wa walimu, hadi sasa upo utoshelevu na ziada ya walimu wanaofundisha masomo ya Historia, Jiografia na Uraia katika Shule za Sekondari. Aidha, walimu wa masomo ya sayansi wameongezeka kutoka 14,031 mwaka 2012 hadi 19,470 mwaka 2017. Pamoja na hatua hii nzuri, bado kuna upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi na hisabati 15,854 sawa na asilimia 45.12 ikilinganishwa na mahitaji ya walimu 35,136 wa masomo hayo. Ili kukabiliana na upungufu huo, Serikali imejipanga kuandaa na kuajiri walimu wote wanaosoma masomo ya Sayansi na Hisabati. Tumeanza kufanya hivyo mwaka jana, ambapo Serikali imeajiri jumla ya walimu 3,412 wa masomo hayo.
 • Mahudhurio ya wanafunzi shuleni yamedhibitiwa ili kuhakikisha kuwa, wanafunzi wote wanaoandikishwa shuleni, wanahudhuria, wanasoma na kuhitimu ngazi husika. Eneo hili bado lina changamoto kubwa kwa baadhi ya Mikoa kuwa na kiwango kikubwa cha utoro wa wanafunzi na kuacha shule. Takwimu zilizokusanywa na Ofisi ya Rais - TAMISEMI mwezi Machi 2018, mikoa hiyo kwa upande wa utoro wa wanafunzi wa Sekondari ni Tabora (9.7%), Geita (8.1%), Mtwara (6.4%) na Shinyanga (6.3%). Kuhusu utoro wa wanafunzi wa shule za Msingi ni Mikoa ya Rukwa (3.2%), Geita (3.1%), Tabora (2.9%), Simiyu (2.0%) na Singida (1.9%). Kwa ujumla utoro wa wanafunzi wa Sekondari ni mkubwa zaidi kwa Mikoa husika kuliko shule za msingi. Nitumie nafasi hii kuikumbusha mikoa niliyoitaja kuhamasisha wananchi wakiwemo wazazi, walezi na wanafunzi wenyewe kuhusu umuhimu wa elimu na mahudhurio endelevu shuleni kwa kutumia taratibu na sheria tulizojiwekea katika maeneo yetu.
 • Serikali imeendelea kusambaza vifaa vya maabara katika shule za sekondari 1,625 ambazo awali hazikuwa na vifaa hivyo. Aidha, imeendelea kupeleka ruzuku ya uendeshaji wa shule kwa wastani wa shilingi 10,000 na 25,000/= kwa mwanafunzi kwa shule za msingi na sekondari sawia katika mwaka. Sehemu ya fedha hizo hutumika kununua vifaa vya maabara na kemikali.

Tumeendelea kuhakikisha kuwa wahitimu katika ngazi mbalimbali za elimu ni bora na wenye viwango stahiki vya kitaaluma. Kwa kutumia kigezo cha mitihani, kumekuwa na ongezeko la ufaulu kuanzia mwaka 2012 hadi 2017. Ufaulu wa mtihani ya kuhitimu elimu ya msingi umeongezeka kutoka asilimia 30.7 hadi 72.76 mwaka 2017. Ufaulu wa mtihani wa kidato cha nne umeongezeka kutoka asilimia 43.5 hadi asilimia 77.57 mwaka 2017. Aidha, waliofaulu kwa ubora (Daraja la I - III) wameongezeka kutoka asilimia 6.39 hadi 30.15 mwaka 2017. Lengo la Serikali ni kuongeza idadi ya wanaofaulu kwa ubora kufikia zaidi ya asilimia 50 ili kuliwezesha Taifa kuwa na rasilimali watu bora inayoweza kushindana katika soko la ajira na kuchangia vizuri zaidi katika maendeleo ya uchumi wa Taifa.

Serikali imeendelea kudhibiti ubora wa nje ya shule kwa kuimarisha taasisi zetu za udhibiti zilizopo na kuanzisha kamati ya udhibitii ubora wa ndani ya shule kwa ajili ya ufuatiliaji wa uwajibikaji wa walimu na wanafunzi, ili kila mmoja atambue na kutimiza wajibu wake.

Kuhusu elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa Maendeleo imeanzisha taasisi na vyuo vya ufundi takribani 560 vinavyotoa elimu ya ufundi wakati taasisi na vyuo 513 vinatoa elimu ya ufundi stadi. Taasisi na vyuo hivi vinamilikiwa na Serikali, mashirika ya watu binafsi na taasisi za kidini zilizosajiliwa na kupewa ithibati.

Kwa upande wa elimu ya juu, Watanzania wenye sifa wameendelea kuandaliwa pamoja na kuongeza vyuo vya elimu ya juu. Kwa mfano, Serikali kwa kushirikiana na wadau imeongeza vyuo vikuu kutoka kutoka kimoja mwaka 1961 hadi 67 mwaka 2018.

Ili kuhakikisha kuwa Watanzania wote wenye sifa wanapata elimu ya juu, Serikali imeweka utaratibu wa kutoa mikopo kupitia Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu. Katika mwaka wa masomo 2017/2018, jumla ya shilingi bilioni 427.55 zimetumika kama mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu 122,623 (mwaka wa kwanza 33,857 na wanaoendelea 86,766).

Ndugu wananchi,

Nitumie pia nafasi hii kuzungumzia kidogo dhana ya mpango wa “Elimumsingi bila Malipo” kwa jina maarufu “elimu bure”. Mpango huu wa Serikali umeandaliwa kwa lengo la kuhakikisha watoto wa Kitanzania wenye umri wa kwenda shule wanapata haki ya elimu ya msingi bila kikwazo cha ada na michango mingine.

Mpango huu ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 ambayo imetamka kuwa elimumsingi (Elimu ya awali hadi kidato cha nne) ni ya lazima na itatolewa bure katika shule za umma. Utekelezaji wake umefafanuliwa kwa kina kupitia Waraka wa Elimu Na.3 wa mwaka 2016 ukirejerea Waraka wa Elimu Na. 6 wa mwaka 2015. Waraka Na. 3 wa mwaka 2016 unafuta nyaraka zote zilizoelekeza utaratibu wa kutoa ada na michango mingine ya hapo awali. Hivyo, michango iliyofutwa ni pamoja na; tozo ya ada kwa mwanafunzi wa shule ya kutwa na bweni, michango mbalimbali waliyotakiwa kutoa wazazi au walezi kulingana na makubaliano yao kupitia Bodi au Kamati za shule na ada ya mitihani kwa shule za sekondari za Serikali. Hivyo, hii ndiyo tafsiri ya dhana ya “Elimu bila Malipo.”

Ndugu Wananchi

Kwa tafsiri niliyoeleza, Elimumsingi bila malipo haiondoi jukumu la mzazi au mlezi kushirikiana na Serikali kumhudumia mtoto wake kwa kumpa mahitaji ya msingi yanayomwezesha kusoma kwa ufanisi. Aidha, tafsiri niliyoieleza haiondoi jukumu la jamii la kuchangia maendeleo ya elimu katika maeneo yao na Taifa kwa ujumla. Majukumu ya mzazi au mlezi yanayobaki ni kumnunulia mtoto wake sare, vifaa vya kusomea na kujifunzia, vifaa vya malazi, nauli na kufuatilia mahudhurio na maendeleo yake ya kitaaluma.

Nimeona suala hili nilizungumze kwa undani ili tuelewane vizuri. Lengo la Serikali hapa ni kuhakikisha kuwa, kila mwanafunzi katika ngazi ya elimumsingi atasoma kwa kugharimiwa na Serikali bila mzazi au mlezi kulipa ada au michango mingine ya fedha katika shule za umma. Hivyo, naomba viongozi na watendaji katika ngazi zote msimamie vizuri utekelezaji wa dhamira nzuri ya Serikali ya kutoa elimumsingi bila malipo. Serikali itaendelea kuwachukulia hatua kali watakaotoza michango kinyume na utaratibu ulioelekezwa na Serikali. Vilevile, nawaomba wananchi na wadau wa maendeleo, tuendelee kuiunga mkono Serikali kwa kuwekeza zaidi katika elimu hasa uboreshaji wa miundombinu, upatikanaji wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia na uandaaji wa rasilimali watu katika ngazi zote za elimu hapa nchini. Kaulimbiu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu inatukumbusha kuwa, Elimu ni Ufunguo wa Maisha; Wekeza sasa kwa Maendeleo ya Taifa letu.”

VITA DHIDI YA RUSHWA

Ndugu Wananchi;

Kama nilivyokwishasema, Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu zitaendelea kuhimiza mapambano dhidi ya rushwa. Rushwa katika nchi yetu bado ipo, na inaendelea kuwa ni adui wa haki na kudhoofisha jitihada zetu za kuimarisha uchumi, kuimarisha huduma za jamii na utawala bora. Athari zinazotokana na vitendo vya rushwa si tu humuathiri kila mmoja wetu bila kujali uhusika wake katika vitendo vya rushwa, bali pia watu wa kawaida huathirika zaidi na kuendelea kubaki wanyonge katika jamii. Kutokana na hali hii, Serikali itaendelea kupambana na vitendo vya rushwa bila kuchoka mpaka jamii yetu itakapoachana na vitendo hivi vya kidhalimu.

Ndugu Wananchi,

Katika kuthibitisha kuwa rushwa bado ipo, Serikali kupitia TAKUKURU imefanya utafiti na kugundua kuwepo kwa vitendo vya rushwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa asilimia 26.2 ya miradi iliyokaguliwa kwa mwaka 2017. Hata hivyo, pamoja na kuwa wananchi wanaridhishwa na utoaji wa huduma kwa ujumla hususani katika sekta ya afya na taasisi za umma, bado Serikali ya Awamu ya Tano imechukua hatua kadhaa kwa lengo la kupunguza tatizo la rushwa kama ifuatavyo:

 • Kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Disemba, 2017, Serikali kupitia TAKUKURU, imefungua kesi mpya 428 mahakamani. Kati ya kesi hizo, tayari Serikali imeshinda kesi 53, nyingine bado zipo mahakamani zikiwemo kesi 40 za uhujumu uchumi;
 • Aidha, katika kipindi hicho cha Januari hadi Desemba 2017, TAKUKURU iliendesha operesheni mbalimbali kwenye maeneno ya ukusanyaji mapato, uzuiaji malipo hewa pamoja na kufanya kaguzi za mara kwa mara katika miradi ya maendeleo. Operesheni hizo, zimewezesha Serikali kuokoa fedha na mali za umma zenye thamani ya shilingi bilioni 59.56 kutoka katika sekta za elimu, afya, mahakama, Serikali za Mitaa, kilimo, misitu na mamlaka ya mapato.
 • Serikali imeimarisha usimamiaji na ukusanyaji wa kodi kwa kutumia mashine za kielectroniki (Electronic Fiscal Devices - EFD) kwa ajili ya kuziba mianya ya ukwepaji wa kodi ya Serikali kwa mujibu wa sheria za nchi.

Ndugu Wananchi

Napenda kuwahakikishia kuwa, Serikali yenu itaendelea kufuatilia na kubaini vitendo vyote vya rushwa hususan katika miradi ya maendeleo iliyo kwenye sekta za kipaumbele ambazo ni maji, ujenzi, afya, mawasiliano, madini, maliasili na elimu ili kuhakikisha inatekelezwa kwa ubora na ufanisi na kuzuia upotevu wa fedha za umma na ucheleweshaji wa ukamilishaji wa miradi hiyo. Aidha, nitumie fursa hii kuwaomba wananchi wote, “Tukatae rushwa - tuijenge Tanzania.”

VITA DHIDI YA VVU NA UKIMWI

Ndugu Wananchi,

Wakati tunajielekeza katika mapambano dhidi ya rushwa, hatuna budi kufahamu kwamba maambukizi ya VVU na UKIMWI yanaendelea kupunguza nguvukazi ya Taifa na ustawi wa nchi yetu kama ilivyo kwa nchi nyingine duniani. Kwa mujibu wa matokeo ya utafiti uliofanywa na “Tanzania HIV Impact Survey” (THIS) mwaka 2017, imebainika kuwa wastani wa maambukizi mapya ni asilimia 4.7 kwa watu wenye umri kati ya miaka 15 hadi 49. Aidha, imebainika kuwa, maambukizi mapya kwa watu wenye umri kati ya miaka 15 hadi 64 ni asilimia 0.2. Maambukizi haya ni sawa na watu 81,000 kwa mwaka.

Ndugu Wananchi

Lengo la kutoa takwimu hizi, si kuwatisha Watanzania bali ni kuwaonyesha hali halisi ya tatizo tulilonalo kama Taifa. Naomba niwasihi na kuwakumbusha Watanzania kuwa: “Afya yetu, ndio mtaji wetu.” Hivyo, Serikali inasisitiza kila mwanachi kwa hiari yake akapime afya yake. Vita dhidi ya VVU na UKIMWI ni vita inayohitaji dhamira ya dhati katika uwanja wa mapambano. Vita hii inahusisha tafakari ya kina ya kila mmoja wetu katika kujilinda asipate maambukizi mapya. “Mtanzania jitambue, pima afya yako sasa”

VITA DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA

Ndugu Wananchi;

Tatizo la dawa za kulevya nalo limeendelea kuisumbua dunia na kuathiri nchi nyingi zilizoendelea na zinazoendelea ikiwemo Tanzania. Kulingana na taarifa ya ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia dawa za kulevya na uhalifu (United Nations Office on Drugs and Crime - UNODC) ya mwaka 2017, inakadiriwa kuwa hadi kufikia mwaka 2015 takribani watu millioni 255 walikuwa wanatumia dawa za kulevya duniani. Kati yao, watu wapatao millioni 29.5 walikuwa tayari wameathirika kiafya kwa sababu zitokanazo na matumizi ya dawa hizo.

Tanzania ni moja ya nchi zilizoathirika na tatizo la biashara na matumizi ya dawa za kulevya kwa kiwango kikubwa ambapo bangi imeendelea kuwa ni dawa ya kulevya inayotumika zaidi hapa nchini. Watumiaji wengi wa dawa za kulevya ni vijana wenye umri wa miaka kati ya 14 hadi 15 ambao ni nguvukazi ya Taifa. Aidha, imebainika kuwa, baadhi ya watumiaji wa dawa hizo wana umri wa zaidi ya miaka 60. Hali hii si ya kufanyia mzaha hata kidogo, kwani pamoja na kuathiri nguvukazi ya Taifa, bado inawafanya watoto na vijana wetu wapoteze uelekeo katika maisha na kuwafanya wazazi wabaki na majonzi makubwa.

VITA DHIDI YA MALARIA

Ndugu Wananchi,

Nimearifiwa kuwa, Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu zitatumika kuwaelimisha wananchi kuhusu ugonjwa wa malaria. Ugonjwa wa malaria hapa nchini unawaathiri zaidi watoto wenye umri chini ya miaka mitano na wanawake wajawazito. Ingawa takwimu zinazokusanywa katika mfumo wa kutolea taarifa (District Health Information System – DHIS 2) kutoka kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini zinaonesha kuwa matukio ya malaria yamepungua kwa zaidi ya asilimia 40, kutoka wastani wa wagonjwa milioni saba mwaka 2015 hadi kufikia wagonjwa milioni nne mwaka 2017, bado tatizo lipo.

Sote tunafahamu madhara makubwa yanayosababishwa na ugonjwa wa malaria, hapa nataja baadhi tu ya madhara hayo:- Malaria hukatisha maisha na ndoto za watoto, mama wajawazito na wananchi kwa ujumla kwa kusababisha vifo vingi vya Watanzania. Vilevile, gharama za tiba ya ugonjwa huu ni kubwa kiasi kwamba huathiri uchumi wa mtu mmoja mmoja, familia na taifa kwa ujumla. Aidha, wagonjwa hushindwa kufanya kazi za uzalishaji mali na badala yake kutumia muda mwingi kujiuguza na kufuatilia matibabu.

Ndugu Wananchi,

Nawaomba wote kwa pamoja tuendelee kushirikiana na Serikali kutekeleza Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria (National Malaria Control Programme - NMCP) kwa kudhibiti mbu waenezao malaria kwa njia ya utengamano (intergration) na kufanya uchunguzi kabla ya tiba. “Shiriki kutokomeza ugonjwa wa malaria kwa manufaa ya jamii.”

HITIMISHO

Naomba sote tushirikiane kumuomba Mwenyezi Mungu awajalie afya njema na safari ya salama vijana tutakaowakabidhi jukumu la kukimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa kwa siku 195 nchi nzima ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Napenda kuwakumbusha kuwa:

 • Mnatakiwa kutekeleza jukumu hili kubwa na nyeti kitaifa kwa bidii, juhudi, nidhamu, uadilifu na weledi wa hali ya juu.
 • Kukagua na kufuatilia miradi ya maendeleo kwa kulinganisha thamani ya fedha na hali halisi ya miradi ilivyo.
 • Kuchunguza kwa umakini jinsi michango ya Mwenge ilivyotolewa na matumizi yake.
 • Mwisho, kutoa taarifa ya matokeo ya kazi yenu Serikalini bila woga wala shinikizo la mtu yeyote na sisi tutaifanyia kazi.

Baada ya kusema hayo, sasa natamka rasmi kuwa niko tayari kuzindua Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2018 kama nilivyoombwa.

Nawashukuru sana kwa kunisikiliza.