HOTUBA YA MHESHIMIWA KASSIM M. MAJALIWA (MB.), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI AKIAHIRISHA MKUTANO WA 15 WA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA TAREHE 28 JUNI 2019

 

UTANGULIZI

 

Shukrani

 

 1. Mheshimiwa Spika, awali ya yote, nitumie fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya na uzima hadi leo hii tunapohitimisha shughuli zote zilizopangwa katika Mkutano wa 15 wa Bunge lako tukufu. Kama tunavyofahamu, mkutano huu umepitia na kupitisha Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2019/2020, Mfuko wa Bunge na Mfuko wa Mahakama kama zilivyowasilishwa na kufanyiwa marekebisho kwa kuzingatia ushauri wa Waheshimiwa Wabunge.

 

 1. Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii pia kukushukuru wewe binafsi, Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wenyeviti wa Bunge na Waheshimiwa Wabunge wote kwa kushiriki kikamilifu katika mkutano huu tangu ulipoanza tarehe 2 Aprili, 2019. Niwashukuru pia Katibu wa Bunge, Watumishi wa Bunge na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ushirikiano mkubwa katika kipindi chote cha mkutano huu tangu ulipoanza hadi sasa. Waheshimiwa Wabunge, mtakubaliana nami kuwa kupitia mkutano huu, tumeweza kutekeleza kikamilifu wajibu wetu wa Kikatiba kwa kujadili na kupitisha Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2019/2020.

 

 1. Mheshimiwa Spika, Serikali itazingatia ushauri wote uliotolewa na Bunge ili kuboresha mipango na bajeti kwa manufaa ya watanzania. Aidha, baada ya kuwepo hapa Bungeni kwa vikao 55 tangu tarehe 2 Aprili 2019, nina uhakika kuwa kila mbunge hivi sasa atakuwa na fursa ya kurejea katika jimbo lake ili kuendelea kushirikiana na wananchi anaowawakilisha katika kutekeleza shughuli za maendeleo.

 

Salamu za Pole

 

 1. Mheshimiwa Spika, kwa masikitiko makubwa naungana tena na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kutoa salamu za pole kwa ndugu, jamaa na marafiki waliopoteza wapendwa wao na wengine kupata majeraha kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo tukio la mmomonyoko wa ardhi lililotokea Aprili 2019 huko Moshono, Arusha; ajali ya gari lililowaka moto mjini Iringa; ajali ya gari huko Mbalizi, Mbeya ambayo ilikatisha uhai wa Bibi harusi mtarajiwa na ndugu zake na ile ya treni iliyotokea Juni 2019, jijini Dodoma na kujeruhi watu wapatao 29.

 

 1. Mheshimiwa Spika, vilevile, nitoe pole kwa viongozi na waamini wa Kanisa Katoliki kufuatia vifo vya Maaskofu Wastaafu wa Kanisa Katoliki: Baba Askofu Mstaafu Gabriel Mmole wa Jimbo Katoliki Mtwara aliyefariki tarehe 15 Mei 2019 na Mhashamu Askofu Mstaafu Emmanuel Mapunda wa Jimbo Katoliki la Mbinga aliyefariki tarehe 16 Mei 2019. Nitoe pole pia kwa familia, ndugu na jamaa wa marehemu Dkt. Reginald Abraham Mengi aliyefariki Mei 2019. Tuendelee kumuomba Mwenyezi Mungu aziweke roho za marehemu mahala pema. Amina!

 

Pongezi

 

 1. Mheshimiwa Spika, nitoe pongezi kwa Mheshimiwa Innocent Lugha Bashungwa, Mbunge wa Karagwe kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara. Ninaamini Bunge hili tukufu litampatia ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza majukumu yake.

 

SHUGHULI ZA BUNGE

 

 • Maswali na Majibu

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika mkutano huu jumla ya maswali 472 ya msingi na mengine 1,416 ya nyongeza yaliulizwa na Waheshimiwa Wabunge na kupatiwa majibu na Serikali. Aidha, maswali ya msingi ya papo kwa papo 14 na ya nyongeza mawili yalielekezwa kwa Waziri Mkuu na kupatiwa majibu.

 

 • Miswada ya Serikali

 

 1. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Miswada ya Serikali, Bunge lako Tukufu lilipitisha kwa hatua zake zote miswada ifuatayo: -
 • Muswada wa Sheria ya Fedha za Matumizi wa Mwaka, 2019;
 • Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2019; na
 • Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na.3) wa Mwaka 2019.

 

 • Kauli za Serikali

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu, tarehe 25 Aprili 2019 Mheshimiwa Kapt. (Mst.) George Huruma Mkuchika (Mb.), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora alitoa kauli ya Serikali kuhusu upandishwaji vyeo kwa watumishi wa umma waliokasimiwa katika ikama na bajeti ya mishahara ya mwaka 2015/2016 ambayo iliahirishwa Mei 2016, ili kupisha zoezi la uhakiki wa watumishi.

 

 1. Mheshimiwa Spika, siku hiyo, pia Mheshimiwa Jenista Joackim Mhagama (Mb.), Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu alitoa kauli ya Serikali kuhusu maelekezo ya hatua zilizopaswa kuchukuliwa na tahadhari dhidi ya Kimbunga Kenneth kilichotazamiwa kutokea katika Bahari ya Hindi pamoja na mafuriko katika pwani ya mikoa ya Lindi na Mtwara.

 

 1. Mheshimiwa Spika, tarehe 24 Juni, 2019 katika mitandao ya kijamii ilisambaa video clip ikimuonesha Mheshimiwa Charles Njagua, Mbunge wa Jimbo la Starehe nchini Kenya akitoa vitisho dhidi ya wafanyabiashara wa kigeni waliopo nchini humo wakiwemo raia wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Aidha, baada ya kunipatia fursa ya kulieleza Bunge lako tukufu kuhusu msimamo wa Serikali kwenye suala hilo, nilieleza kuwa Serikali tayari ilichukua hatua kushughulikia kadhia hiyo sambamba na kukanusha kuwa huo si msimamo wa Serikali ya Kenya.

 

 1. Mheshimiwa Spika, hatua hizo zilikuwa ni pamoja na kumwita Balozi wa Kenya nchini sambamba na kuwasiliana na Balozi wetu jijini Nairobi ili kupata ufafanuzi zaidi kuhusu kauli hiyo ya kibaguzi na yenye kuhatarisha mtangamano wa watu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Wanajumuiya ya Afrika Mashariki tuna dhamana kubwa ya kulinda makubaliano katika nyanja za kiulinzi, kibiashara na kijamii licha ya kuwa kila nchi ina sheria, kanuni na taratibu zake. Kupitia ushirikiano huo, leo nchi ya Kenya ina makampuni yapatayo 509 yaliyowekeza Tanzania na Tanzania ina makampuni 196 yaliyowekeza nchini Kenya, ni budi tulinde amani yetu.

 

 1. Mheshimiwa Spika, napenda kutumia fursa hii kuliarifu Bunge lako tukufu kuwa tarehe 25 Juni 2019, Serikali jirani ya Kenya, ilitoa ufafanuzi kuhusu suala hilo na kukanusha vikali kuwa kauli hiyo ya kibaguzi ya Mheshimiwa Njagua si msimamo wa Serikali ya Kenya na hivyo, yafaa kupuuzwa. Nitumie fursa hii kuwasihi Watanzania kuendeleza amani na ukarimu wetu kwa wageni wote waliopo na wanaoingia nchini.

 

 • Kamati za Kudumu za Bunge

 

 1. Mheshimiwa Spika, wakati wa mkutano huu, Kamati za Kudumu za Bunge ziliwasilisha taarifa Bungeni kuhusu mapitio ya utekelezaji wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2018/2019 na uchambuzi wa Mpango na Bajeti kwa mwaka 2019/2020. Taarifa hizo zilisheheni maoni, ushauri na mapendekezo mbalimbali kwa Serikali. Nitumie fursa hii kuwapongeza Wenyeviti, Makamu Wenyeviti na wajumbe wote wa kamati hizo kwa kazi nzuri waliyoifanya kuanzia maandalizi ya kazi za kamati hadi kuwasilisha taarifa zao katika Bunge lako tukufu. Pia, Kamati ya Haki na Madaraka ya Bunge iliwasilisha taarifa kuhusu mashauri mbalimbali yaliyowasilishwa mbele ya Kamati hiyo.

 

MPANGO NA BAJETI YA SERIKALI KWA MWAKA 2019/2020

 

 1. Mheshimiwa Spika, mkutano huu wa 15 wa Bunge lako tukufu tunaouhitimisha leo ulikuwa mahsusi kwa ajili ya kujadili na kupitisha Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2019/2020. Waheshimiwa Wabunge, mtakubaliana nami kuwa bajeti tuliyoipitisha, inatoa mwelekeo mzuri wa utekelezaji wa ahadi mbalimbali za Serikali kwa wananchi kama zilivyoainishwa kupitia Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015 – 2020 pamoja na maelekezo ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliyoyatoa wakati akifungua rasmi Bunge la 11 tarehe 20 Novemba 2015.

 

 1. Mheshimiwa Spika, kwa upande mwingine nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa michango yenu mizuri mliyoitoa wakati wa mjadala kuhusu hoja ya Mpango na Bajeti ya Serikali. Binafsi ninaamini mapendekezo, maoni na hata ukosoaji mlioufanya haukuwa na nia nyingine zaidi ya kuboresha utendaji kazi wa Serikali katika kuhakikisha tunawaletea maendeleo wananchi.

 

 1. Mheshimiwa Spika, wakati wa majumuisho ya Hotuba za Wizara, Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri hawakuweza kujibu hoja zote zilizoibuliwa na Waheshimiwa Wabunge kutokana na ufinyu wa muda. Hivyo, Waheshimiwa Mawaziri, kama mlivyoahidi, hakikisheni mnatoa maelezo ya ufafanuzi kwa maandishi kwa zile hoja ambazo hazikujibiwa.

 

 1. Mheshimiwa Spika, tangu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aingie madarakani, amekuwa akiimarisha misingi ya kuiona Tanzania inajitegemea bila kuchoka wala kutetereka.

 

Mheshimiwa Rais amekuwa mstari wa mbele kuongoza vita ya kiuchumi dhidi ya watu na taasisi mbalimbali zisizo na nia njema dhidi ya nchi yetu. Mheshimiwa Rais amekuwa akisisitiza umuhimu wa kila Mtanzania mwenye uwezo wa kufanya kazi, afanye kazi kwa bidii, weledi na uaminifu. Mheshimiwa Rais ameendelea kukemea wizi, ubadhirifu na ufisadi wa mali na rasilimali nyinginezo za umma.

 

 1. Mheshimiwa Spika, maono na juhudi zote hizo za Mheshimiwa Rais zinajidhihirisha katika utekelezaji wa bajeti zote zilizopita. Aidha, mwelekeo wa bajeti ya Serikali kwa mwaka 2019/2020 unatoa ujumbe kwa umma wa Watanzania kwamba Serikali ya Awamu ya Tano inatekeleza dhamira yake ya dhati ya kugusa maisha ya watanzania hususan wale wanyonge kwa kuboresha mazingira ya kufanya biashara na uwekezaji. Lengo la Serikali ni kulifanya Taifa lijitegemee kuelekea uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda ifikapo mwaka 2025.

 

 1. Mheshimiwa Spika, kupitia bajeti ya mwaka 2019/2020, Serikali imejibu kilio cha Watanzania kuhusu kuweka mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji kwa kuondoa au kupunguza kodi na tozo kwamishi. Kadhalika, Serikali imesikia kilio cha Watanzania kuhusu upatikanaji wa huduma za kijamii ikiwemo maji, umeme, afya na elimu. Kwa kufanya hivyo, ninaamini azma ya Serikali ya kujenga uchumi imara na wenye kujitegemea itafikiwa.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Serikali imepanga kutumia jumla ya shilingi trilioni 33.11. Kati ya fedha hizo, shilingi trilioni 20.86 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida sawa na asilimia Aidha, Shilingi trilioni 12.25, sawa na asilimia 37 ya Bajeti yote zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.

 

 1. Mheshimiwa Spika, napenda kutumia nafasi hii kuwashukuru tena na kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge kwa kupitisha bajeti hii nzuri ya Serikali ambayo kwa sehemu kubwa imewagusa wananchi wengi hususan kwa kuondoa yale yaliyoonekana kuwa ni kikwazo katika kufanya biashara na uwekezaji.

 

 1. Mheshimiwa Spika, niendelee kuwasihi sana Watanzania wote pamoja na washirika wa maendeleo kwamba tuiunge mkono Serikali katika kutekeleza vipaumbele ilivyojiwekea kwenye bajeti ya mwaka 2019/2020 ili viweze kutoa mchango wa haraka kwa maendeleo ya nchi na ya watu.

 

 1. Mheshimiwa Spika, sote tunatambua kuwa mengi yameelezwa na ufafanuzi wa kina umetolewa na Waheshimiwa Mawaziri pamoja na Naibu Mawaziri kuhusu utekelezaji wa kazi za Serikali kwa mwaka 2018/2019 na mwelekeo wake kwa mwaka 2019/2020 wakati wakitoa ufafanuzi wa hoja mbalimbali za sekta husika. Kwa msingi huo, nami napenda nitumie japo muda mchache kutoa maelezo sambamba na kusisitiza kuhusu mwelekeo wa Serikali kwa baadhi ya maeneo.

 

 1. Mheshimiwa Spika, pamoja na mambo mengine, maeneo ambayo ningependa kuyatilia mkazo ni kilimo na umwagiliaji, biashara, uwekezaji na uwezeshaji. Maeneo mengine ni Homa ya Kidingapopo (Dengi) na mlipuko wa Ebola, udhibiti wa biashara ya madini, Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi za Kusini Mwa Afrika (SADC), masoko ya mazao ya kilimo na Uchaguzi Mkuu wa Serikali za Mitaa wa Novemba 2019, nikiamini kuwa maeneo mengi yamefafanuliwa kwa kina na Wizara mbalimbali kupitia maswali, mijadala, n.k.

 

KILIMO

 

 1. Mheshimiwa Spika, hali ya upatikanaji wa chakula nchini kwa kipindi cha mwaka 2018/2019 kilichoishia tarehe 31 Mei 2019, imeendelea kuimarika na kufikia asilimia 124. Hali hii inamaanisha kuwa utengamano na usalama wa chakula ni toshelevu kuelekea msimu wa mwaka 2019/2020.

 

 1. Mheshimiwa Spika, tangu awali, Serikali ya Awamu ya Tano imejipambanua kuendeleza mazao ya kimkakati, ya biashara na chakula nchini. Baadhi ya mazao hayo ni pamba, tumbaku, korosho, kahawa, chai, chikichi, zabibu, mahindi, mpunga, mbaazi, ufuta na alizeti. Miongoni mwa changamoto kubwa katika uzalishaji wa mazao hayo kwa sasa ni masoko. Lengo la Serikali, pamoja na mambo mengine ni kuongeza tija ya mazao hayo kwa kuhakikisha inavutia viwanda vya kuchakata na kuongeza thamani sambamba na upatikanaji wa masoko.

 

 1. Mheshimiwa Spika, pamoja na kutafuta masoko mapya, Serikali inaendelea kuhakikisha mazao ya kimkakati yanaendelea kuuzwa kwa njia ya minada ili kuleta ushindani na hivyo, kuwapatia wakulima bei nzuri na tija. Hatua nyingine ni kuweka mkazo katika uwekezaji wa viwanda vya kuchakata mazao hayo ili kuongeza thamani na wigo wa upatikanaji wa masoko.

 

Kilimo cha Umwagiliaji

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na kilimo tegemezi cha mvua hususan katika zama hizi za mabadiliko ya tabianchi, Serikali inachukua hatua mbalimbali kuboresha kilimo cha umwagiliaji. Lengo la Serikali ni kuwatoa wakulima katika kilimo cha kutegemea mvua pekee.

 

 1. Mheshimiwa Spika, hatua zilizochukuliwa hadi sasa katika kuimarisha kilimo cha umwagiliaji nchini ni kuunda upya na kubadili mfumo wa utendaji wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji. Hatua hizo, zinalenga kuiwezesha Tume hiyo kusimamia ipasavyo shughuli za umwagiliaji. Hali kadhalika, Serikali imehamisha Tume hiyo kutoka Wizara ya Maji kwenda Wizara ya Kilimo ambayo ndiyo yenye dhamana ya kuendeleza kilimo nchini.

 

 1. Mheshimiwa Spika, ili tuweze kufikia lengo la kuongeza eneo la kilimo cha umwagiliaji kutoka hekta 475,056 za sasa hadi hekta milioni moja ifikapo mwaka 2025. Wizara ya Kilimo imeelekezwa kusimamia kwa karibu na kutekeleza majukumu yake kwa weledi. Wizara ihakikishe inasimamia vema miradi midogo na mikubwa ya umwagiliaji inayoendelea sasa pamoja na miradi mipya itakayojengwa mwaka 2019/2020.

 

UWEKEZAJI, BIASHARA NA UWEZESHAJI

 

 1. Mheshimiwa Spika, kuanzia tarehe 1 Julai 2019, Serikali itaanza kutekeleza Mpango Kazi wa Utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Udhibiti wa Biashara Nchini (Blueprint). Utekelezaji wa Mpango huo unakwenda sambamba na dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kurahisisha mazingira ya kufanya biashara nchini. Dhamira hiyo, inajidhihirisha kupitia Sheria ya Fedha ya mwaka 2019 ambayo imefuta tozo kwamishi 54 zilizobainishwa katika Mpango Kazi wa kutekeleza Blueprint.

 

 1. Mheshimiwa Spika, kama mlivyosikia katika wasilisho la Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2019/2020, tozo zilizoondolewa au kupunguzwa ni pamoja na zinazosimamiwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), Wizara ya Mifugo na Uvuvi hususan kwenye Sekta ya Mifugo, Wizara ya Maliasili na Utalii na Wizara ya Maji.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kuwa utekelezaji wa Mpango kazi wa Blueprint unaleta matokeo chanya na yenye tija, Wizara ya Viwanda na Biashara ishirikiane na Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji, kusambaza Blueprint na Mpango Kazi wa Utekelezaji wake, kwa Wizara zote kwa ajili ya kusimamia utekelezaji.

 

 1. Mheshimiwa Spika, Aidha, wakati kazi hii inaendelea, Serikali itafanya ufuatiliaji wa karibu kuhusu utekelezaji wake na kutathmini iwapo malengo yaliyokusudiwa yanafikiwa na pia kuchukua hatua za haraka kurekebisha pale itakapolazimu. Aidha, nitoe wito kwa Wizara na taasisi zote zinazofanya maboresho kuchukua hatua za makusudi za kuufahamisha umma kuhusu mafanikio yaliyofikiwa.

 

 1. Mheshimiwa Spika, sambamba na hatua hizo, Serikali imeendelea kuchukua hatua stahiki kwa lengo la kuimarisha shughuli za uwekezaji na biashara nchini. Juhudi hizo zinakwenda sambamba na mikutano ya Viongozi Wakuu wa Serikali ambayo wamekuwa wakiifanya katika nyakati tofauti kwa lengo la kuibua na kutatua kero za wafanyabiashara wadogo, wa kati na wakubwa.

 

Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi

 

 1. Mheshimiwa Spika, pamoja na mambo mengine, Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2019/2020 unalenga kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia Mifuko ya Uwezeshaji sambamba na kuhakikisha wananchi wananufaika na fursa za utekelezaji wa miradi mikubwa ya kiuchumi.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ya Mwaka 2004, Serikali itaendelea kusimamia uanzishwaji wa vituo vya Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi kama kile cha wilayani Kahama, ambacho hupokea takriban wananchi 100 kwa siku na kina taasisi takriban 22 zinazotoa huduma mbalimbali kwa wajasiriamali. Huduma hizo ni pamoja na urasimishaji wa biashara, huduma za mikopo nafuu, elimu ya biashara, ufundi na teknolojia.

 

 1. Mheshimiwa Spika, lengo la Serikali ni kuhakikisha vituo hivi vinahamasisha na kuwawezesha wananchi kubaini fursa mbalimbali za kiuchumi ikiwemo kutoa elimu ya mlipa kodi, hifadhi ya jamii, uanzishwaji wa vikundi vya kifedha vya kijamii na Vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo (SACCOS) na taarifa za masoko kwa ajili ya kujiletea maendeleo. Kwa msingi huo, naielekeza mikoa na halmashauri zote nchini, zihakikishe kuwa zinaanzisha Vituo vya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kama kile cha Kahama ili kuharakisha nia ya Serikali ya kuwawezesha wananchi kiuchumi.

 

 1. Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kusisitiza kwa mara nyingine kuwa mikoa yote ambayo haijakamilisha kuandaa Mwongozo wa Uwekezaji nayo ihakikishe kuwa inakamilisha suala hilo ndani ya kipindi cha mwaka mmoja kuanzia sasa.

 

 1. Mheshimiwa Spika, Serikali hivi sasa inaratibu Mifuko 44 ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi yenye lengo la kupanua wigo wa utoaji huduma za kifedha ili kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kujikwamua na umaskini. Serikali imekusudia kuhakikisha mifuko hiyo inaboreshwa sambamba na kuongeza ufanisi ili iweze kuwafikia Watanzania wengi hususan wale wa vijijini.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha malengo hayo yanafikiwa, Serikali kupitia Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, inakamilisha Mfumo wa kupima Mifuko ya Uwezeshaji kwa Matokeo ya kiuchumi na kijamii na siyo kwa shughuli walizofanya. Serikali itaendelea kufanya tathmini ya mifuko yote ya uwezeshaji.

 

AFYA

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika eneo la afya ningependa kutoa ufafanuzi kuhusu Homa ya Dengi au Kidingapopo, tahadhari ya Ebola na Mpango wa Taifa wa Damu Salama.

 

Homa ya Dengi

 

 1. Mheshimiwa Spika, homa ya Dengi ambayo huenezwa na mbu aina ya aedes, mbu mweusi mwenye madoa meupe ya kung’aa, ambaye hupendelea kuuma hasa nyakati za asubuhi, mchana na jioni imeendelea kuwepo hapa nchini. Aidha, kuanzia mwezi Januari hadi Juni 2019 jumla ya watu 4,282 waliugua homa hiyo na kusababisha vifo vya watu wanne. Mkoa wa Dar es salaam ndiyo unaoongoza kuwa na wagonjwa wengi na vifo, ukifuatiwa na mikoa ya Arusha, Dodoma, Kagera, Kilimanjaro, Morogoro, Pwani, Singida na Tanga ambayo ina wagonjwa wengi.

 

 1. Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na wananchi imeendelea kutekeleza mikakati ya kudhibiti ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na kudhibiti mbu, kuimarisha usafi wa mazingira, ufuatiliaji, uchunguzi na tiba sahihi kwa wagonjwa.

 

 1. Mheshimiwa Spika, hatua mahsusi zinaendelea kuchukuliwa ambazo zinajumuisha kuangamiza mazalia ya mbu wapevu na viluwiluwi. Tayari lita zipatazo 60,000 za viuavidudu (biolarvicide) kutoka kiwanda cha Kibaha zimenunuliwa kwa ajili ya kuangamiza viluwiluwi katika mazalia ya mbu. Kati ya lita hizo, lita 11,400 zimesambazwa kwenye halmashauri tano za mkoa wa Dar es Salaam. Pia, (lita 48,600) zitasambazwa kwenye halmashauri za mikoa ya Geita (lita 8,092), Kagera (lita 12,308), Kigoma (lita 7,616), Lindi (lita 9,048) na Mtwara (lita 11,536).

 

 1. Mheshimiwa Spika, Serikali pia imeagiza mashine kubwa sita kwa ajili ya kupulizia mbu wapevu na dawa aina ya Acteric kwa ajili ya kunyunyizia nje. Dawa hizi zitasambazwa katika mikoa yenye mahitaji.

 

 1. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutoa elimu kwa jamii kupitia vyombo vya habari pamoja na ujumbe kwa njia ya mitandao ya kijamii kuhusu tahadhari ya kujikinga, dalili na umuhimu wa kuwahi kwenye vituo vya kutolea huduma ya afya ili kubaini vyanzo vya homa na kupata tiba.

 

 1. Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuzitaka mamlaka zote zinazohusika na usafi wa mazingira kuhakikisha kuwa maeneo yote ya makazi ya watu hayaruhusu kuzaliwa viluwiluwi vya mbu kwa kushirikiana na wananchi.

 

Ugonjwa wa Ebola

 

 1. Mheshimiwa Spika, ugonjwa wa ebola umeendelea kuwepo katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na umelipuka tena katika nchi jirani ya Uganda. Sote tunatambua kwamba upo muingiliano mkubwa wa wananchi kutoka katika nchi hizi mbili si tu kupitia mipaka ya nchi kavu, viwanja vya ndege na bandari lakini pia kupitia njia zisizo rasmi. Hivyo, katika kukabiliana na tishio la ugonjwa wa Ebola, Serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti za tahadhari.

 

 1. Mheshimiwa Spika, hatua hizo ni pamoja na kutoa taarifa ya tahadhari ya ugonjwa huo kwa wananchi wote hususan wale waliopo katika mikoa ya Dar es Salaam, Kagera, Katavi, Kigoma, Mbeya, Mwanza, Rukwa na Songwe. Serikali pamoja na kutumia vyombo vya mawasiliano imewaarifu viongozi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa lengo la kuhakikisha nchi nzima inatambua hatari iliyopo na hivyo, kuchukua tahadhari.

 

Mpango wa Taifa wa Damu Salama

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika hatua nyingine ya kuimarisha upatikanaji wa damu salama nchini kwa ajili ya wagonjwa wenye uhitaji, Serikali kupitia Mpango wa Taifa wa Damu Salama imekusanya lita 289,770 za damu salama sawa na asilimia 77 ya lengo.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Serikali itaendelea kutekeleza afua mbalimbali ili kuimarisha upatikanaji wa damu salama nchini. Baadhi ya afua hizo ni ujenzi wa vituo 12 vya damu salama katika mikoa 12 ya Arusha, Dar es salaam, Dodoma, Geita, Kagera, Kigoma, Mbeya, Morogoro, Mtwara, Mwanza, Pwani na Tabora sambamba na ukarabati katika Hospitali za Rufaa.

 

 1. Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuwashukuru wananchi wanaojitokeza kuchangia damu na kuwahamasisha wananchi washiriki katika zoezi la kuchangia damu ili kuokoa maisha ya wenye mahitaji hususan akinamama wajawazito na wahanga wa ajali.

 

MKUTANO WA 39 WA WAKUU WA NCHI NA SERIKALI WA JUMUIYA YA MAENDELEO YA KUSINI MWA AFRIKA (SADC)

 

 1. Mheshimiwa Spika, kuanzia tarehe 9 hadi 18 Agosti 2019, nchi yetu itapata heshima kubwa ya kuwa mwenyeji wa Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC). Mkutano huo utakaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere, Dar es Salaam utahudhuriwa na Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka nchi 16 wanachama wa SADC.

 

 1. Mheshimiwa Spika, kupitia Mkutano huo, Mheshimiwa Dkt. Hage Geingob, Rais wa Jamhuri ya Namibia na Mwenyekiti wa sasa wa SADC atakabidhi uenyekiti wa SADC kwa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia tarehe 17 Agosti, 2019 hadi 17 Agosti, 2020.

 

 1. Mheshimiwa Spika, maandalizi ya mkutano huo utakaofanyika chini ya kaulimbiu “Mazingira rafiki ya biashara ili kuleta maendeleo endelevu na shirikishi ya viwanda” (A conducive business environment for inclusive and sustainable industrial development) yanaendelea vizuri.

 

 1. Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kutoa wito kwa sekta binafsi hususan wanaviwanda na wafanyabiashara watumie vema maadhimisho ya awamu ya nne ya wiki ya viwanda ya SADC ambayo yatafanyika Agosti 2019, kabla Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC haujaanza. Hii ni fursa adhimu kwa wadau hao, kuonesha bidhaa na huduma mbalimbali zinazotengenezwa Tanzania ili kuvutia soko la SADC kwa kujitangaza, kujenga mtandao wa kibiashara na hivyo, kupanua wigo wa soko la bidhaa za Tanzania.

 

 1. Mheshimiwa Spika, sambamba na mkutano huo wa SADC, kutafanyika maadhimisho ya miaka 20 ya kumuenzi Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere tangu kifo chake mwaka 1999. Hayati Mwalimu Nyerere, ataendelea kukumbukwa kwa kuzindua Kituo cha Utafiti na Uhifadhi wa Nyaraka cha Kusini mwa Afrika (SARDC) wakati wa harakati za ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika.

 

 1. Mheshimiwa Spika, tukio hili ni muhimu sana kwa Taifa letu na katika kipindi cha uenyekiti wetu, tutaendelea kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa mchango wake katika Ukanda huu wa Kusini mwa Afrika. Kwa msingi huo, naomba nitumie fursa hii kuwaalika Waheshimiwa Wabunge kushiriki katika matukio haya makubwa na muhimu kwa Taifa letu. Ushiriki wenu utakuwa chachu na hamasa ya kipekee katika kufanikisha uenyekiti na uongozi wetu kwenye Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika.

 

UHIFADHI WA MAZINGIRA NA TAKA ZA PLASTIKI

 

 1. Mheshimiwa Spika, Tanzania inajivunia uwepo wa rasilimali nyingi za asili zikiwemo wanyama, milima na mbuga ambazo zimekuwa chachu ya kufanya vizuri kwa uchumi wetu. Hata hivyo, rasilimali hizi tulizonazo zinaweza kutoweka iwapo hatutachukua hatua za makusudi kuzilinda kwa maslahi ya sasa na vizazi vijavyo.

 

 1. Mheshimiwa Spika, Taarifa ya Tatu ya Hali ya Mazingira ya Nchi ya mwaka 2018 imeonesha kuwa hali ya mazingira nchini imeendelea kuwa ya kutoridhisha. Shughuli za binadamu ikiwemo ufyekaji na uchomaji wa misitu hovyo, kilimo kisicho endelevu, na utupaji wa taka hovyo ikiwemo taka za plastiki ni baadhi ya mambo yanayotishia kuangamiza mazingira asilia nchini. Kwa lugha nyingine, hili ni onyo ambalo linapaswa kuwekwa maanani na wananchi wote.

 

 1. Mheshimiwa Spika, Programu ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa (UNEP) inaonya kuwa hadi kufikia mwaka 2030 iwapo hatua za makusudi hazitachukuliwa, dunia itakuwa na mifuko mingi ya plastiki kwenye bahari, maziwa na mito kuliko samaki na viumbe hai wengine. Hii maana yake ni kwamba katika kipindi hicho kuna uwezekano mkubwa wa kuvua mifuko 400 ya plastiki na samaki wawili katika kila jaribio la uvuvi kwenye bahari, maziwa na mito.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika hatua za kukabiliana na taka za plastiki, tarehe 9 Aprili 2019, katika Mkutano wa 15 wa Bunge lako tukufu, nilitoa tamko kuwa ifikapo Juni mosi, 2019, itakuwa ni marufuku kuzalisha, kuingiza ndani ya nchi, kusafirisha nje ya nchi, kusambaza na kutumia mifuko ya plastiki. Marufuku hiyo ilihusu mifuko ya plastiki ya kubebea bidhaa inayotumika kwenye maduka makubwa; maduka madogo, vioski, sokoni na kwenye maeneo ya kuuzia vyakula kama vile chipsi, karanga, n.k.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katazo hilo halikuhusisha vifungashio vya bidhaa mbalimbali kama vile maziwa, mikate, maji, madawa na bidhaa za sekta ya kilimo na ujenzi. Serikali imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuweka utaratibu wa utekelezaji wa katazo hilo hatua kwa hatua.

 

 1. Mheshimiwa Spika, napenda kuliarifu Bunge lako tukufu kuwa utekelezaji wa agizo la Serikali la kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki limefanikiwa kwa kiasi kikubwa sana. Wananchi wameonesha mwitikio wa hali ya juu kwa kuacha kutumia mifuko ya plastiki na wameanza kutumia mifuko mbadala.
 2. Mheshimiwa Spika, takriban tani 253.71 za shehena za mifuko ya plastiki zilisalimishwa na wazalishaji na watumiaji wa mifuko hiyo kutoka maeneo mbalimbali nchini. Aidha, baadhi ya viwanda katika mikoa ya Pwani na Dar es Salaam wameanza kurejeleza shehena kubwa ya mifuko iliyosalia ili itumike kama malighafi ya kutengeneza bidhaa nyingine za plastiki.

 

 1. Mheshimiwa Spika, kwa upande mwingine katazo hili limeibua fursa nyingi za ajira katika kutengeneza mifuko mbadala, uanzishwaji wa viwanda vipya kwa ajili ya kutengeneza mifuko mbadala na kuongezeka kwa uzalishaji wa malighafi za kutenegeneza mifuko hii. Kwa mfano, kiwanda cha Mgololo katika kipindi hiki kimeongeza uzalishaji wa malighafi za kutengeneza mifuko mbadala kwa takriban asilimia 300.

 

 1. Mheshimiwa Spika, hadi sasa viwanda vilivyoanzishwa kwa ajili ya kuzalisha mifuko mbadala ni 11 ambapo viwanda 10 vipo Dar es Salaam na kimoja kipo Arusha. Viwanda hivyo vyote vina uwezo wa kuzalisha tani 1,414 kwa mwezi lakini kwa sasa vinazalisha takriban tani 651 kwa mwezi. Hata hivyo, uzalishaji wa sasa hautoshelezi mahitaji ya nchi nzima.

 

 1. Mheshimiwa Spika, kutokana na mahitaji makubwa ya mifuko mbadala, Serikali kupitia SIDO imeanzisha mafunzo maalumu ya utengenezaji mifuko hiyo kwa wajasiriamali wadogo. Hadi sasa mafunzo haya yametolewa kwa wajasiriamali 369 katika mikoa ya Dar es Salaam, Kagera, Arusha na Manyara.

 

 1. Mheshimiwa Spika, SIDO pia imejipanga kutoa elimu hiyo kwa nchi nzima. Sambamba na hilo, taasisi za utafiti ikiwemo SIDO yenyewe zimehamasishwa kubuni au kunakili na kuboresha teknolojia zilizopo na hivyo, kuzizalisha kwa wingi kwa kuzingatia viwango vya ubora. Nitoe wito kwa Watanzania kuendelea kuchangamkia fursa hii ya kutengeneza mifuko mbadala kwa vile mahitaji ni makubwa na soko lake ni kubwa hapa nchini.

MADINI

 1. Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na utoroshwaji wa madini, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuanzisha Ofisi za Maafisa Madini Wakazi katika kila migodi mikubwa na ya kati ili kusimamia na kuwasilisha taarifa za uzalishaji wa kila siku pamoja na kudhibiti mianya ya utoroshaji wa madini.

 

 1. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa maeneo ya viwanja vya ndege na mipakani wamewekwa wasimamizi kuhakikisha madini yanayopitishwa yana vibali husika. Serikali imeanzisha masoko ya madini ili kutatua changamoto ya ukosefu wa masoko kwa wachimbaji wadogo.

 

 1. Mheshimiwa Spika, kutokana na jitihada hizo za kudhibiti utoroshaji wa madini na kuweka mazingira wezeshi kwenye masoko ya madini yaliyoanzishwa katika mikoa mbalimbali nchini, Serikali imefanikiwa kukusanya maduhuli ya jumla ya shilingi bilioni 304 kuanzia Julai 2018 hadi Mei 2019. Kiasi hicho ni sawa na asilimia 98 ya lengo la makusanyo ya shilingi bilioni 310 ya maduhuli ya madini kwa mwaka 2018/2019.

 

 1. Mheshimiwa Spika, uanzishwaji wa masoko ya madini, umeleta hamasa kubwa kwa wachimbaji wadogo kuuza madini yao katika masoko yanayotambulika. Tangu kuanza kwa masoko ya madini Machi 2019 hadi Mei 2019, kiasi cha madini ya dhahabu kilichoripotiwa kuuzwa katika masoko hayo ni kilogramu 969 na gramu 32 yenye thamani ya shilingi bilioni 80.21.

 

 1. Mheshimiwa Spika, hatua hii ni mafanikio makubwa. Kwa mantiki hiyo, nitoe wito kwa wachimbaji na wafanyabishara wanaofanya shughuli zao kinyume cha sheria na taratibu za nchi, waache mara moja. Kwa kufanya hivyo, tutakuwa wazalendo na hivyo kuifanya rasilimali hii tuliyojaliwa iwe na manufaa kwa Watanzania wote. Vilevile, natoa wito kwa mikoa yote nchini kutangaza maeneo ambayo masoko ya madini yameanzishwa ili wanunuzi na wauzaji waweze kuyafikia kwa urahisi.

 

Uchenjuaji Madini

 

 1. Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuimarisha shughuli za uchenjuaji na kuongeza thamani ya madini hususan yale ya vito ili zifanyike nchini. Serikali kupitia Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini (SMMRP), inajenga vituo vitatu vya kisasa vya uchenjuaji madini ya dhahabu katika maeneo ya Lwamgasa–Geita, Itumbi–Chunya na Katente–Bukombe. Miradi hiyo yote, itagharimu shilingi bilioni 4.8. Hadi sasa, mradi wa Lwamgasa umekamilika kwa asilimia 100, mradi wa Katente umekamilika kwa asilimia 75 na mradi wa Itumbi umekamilika kwa asilimia 55.

 

 1. Mheshimiwa Spika, ili vituo hivi viwe na tija pamoja na kufikia malengo yaliyokusudiwa, Serikali imekubaliana na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kuhusu namna bora ya uendeshaji na usimamizi wa vituo hivi ikiwa ni pamoja na kutoza gharama nafuu kwa wachimbaji wadogo watakaopeleka dhahabu yao kwa ajili ya uchenjuaji.

 

UTALII

 

 1. Mheshimiwa Spika, sekta ya utalii nchini imeendelea kutoa mchango mkubwa katika Pato la Taifa na fedha za kigeni sambamba na kutoa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kwa watanzania. Ukuaji wa sekta hiyo unadhihirishwa na ongezeko la watalii kutoka watalii milioni 1.3 mwaka 2017 hadi kufikia watalii milioni 1.5 mwaka 2018. Kadhalika, mapato yatokanayo na utalii yaliongezeka kutoka dola za Marekani bilioni 2.2 mwaka 2017 hadi kufika dola za Marekani bilioni 2.6 mwaka 2018.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika miezi ya hivi karibuni nchi yetu imepokea watalii wengi kutoka nchi za Israel, China, India na Urusi. Katika juhudi za kutangaza na kuvutia watalii nchini, Aprili 2019 nilipata fursa ya kuwaaga watalii 274 kutoka Israel wakiwa ni sehemu ya watalii wapatao 1,000 waliotembelea nchi yetu kwa kipindi hicho. Kadhalika, Mei 2019 tulipokea na kuwakaribisha nchini watalii wapatao 300 kutoka China ambao ni sehemu ya Mpango wa Watalii 10,000 wanaotarajiwa kutembelea Tanzania kutoka China.

 

 1. Mheshimiwa Spika, ongezeko hilo la watalii limeongeza umaarufu wa Tanzania kimataifa hususan sifa zetu za usalama, amani, ukarimu na kupenda wageni. Vilevile, ujio wa watalii hao umefungua soko la ajira hususan kwa waendesha huduma za watalii, mahoteli na hata kwa wananchi mmoja mmoja kwa kuuza vitu mbalimbali.

 

 1. Mheshimiwa Spika, kuimarika kwa shughuli za utalii nchini kunakwenda sambamba na kuongezeka kwa umaarufu wa hifadhi zetu kimataifa. Mathalan, tarehe 13 Juni 2019, mtandao maarufu wa shughuli za utalii (safaribookings.com) ulitoa taarifa yake ambayo ilionesha kuwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti imeibuka hifadhi bora kwa ajili safari barani Afrika. Serengeti ilipata alama 4.9 kati ya alama 5.0 huku ikizipiku Mala Mala Game Reserve ya Afrika Kusini na Hifadhi ya Taifa ya Mana Pools ya Zimbabwe ambazo zilishika nafasi ya pili na tatu mtawalia.

 

 1. Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii, Bodi ya Utalii, Balozi za Tanzania na wadau wote wa utalii hasa wale wa sekta binafsi kwa ushirikiano na juhudi zao katika kufanikisha mipango ya Serikali ya kuiinua sekta ya utalii. Nitoe rai kwa wadu wote kwamba ongezeni nguvu katika kutumia fursa ya uwepo wa masoko mapya yanayoibukia ya China, India, Israel na Urusi.

 

 1. Mheshimiwa Spika, kipekee, niungane na Dkt. Hamisi Kigwangala (Mb.), Waziri wa Maliasili na Utalii kumpongeza kijana wa Kiingereza Braydon Bent ambaye amekuwa akiitangaza vyema Tanzania kupitia video fupi hususan kwenye mitandao ya kijamii. Nampongeza sana Braydon kwa kutuunga mkono na namkaribisha sana Tanzania.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha malengo ya Serikali ya kuongeza idadi ya watalii kutoka milioni 1.1 mwaka 2015 hadi milioni 2.0 mwaka 2020 yanafikiwa, Serikali ya Awamu ya Tano inayo pia mikakati thabiti ya kuviendeleza vivutio vya utalii vilivyopo Kanda ya Kusini. Vivutio hivyo, vinajumuisha maeneo ya kihistoria ya Kalenga na Isimila (Iringa), kumbukumbu za vita ya majimaji (Kilwa na Songea), Kimondo cha Mbozi (Songwe), Maporomoko ya Kalambo (Rukwa), Ziwa Ngozi (Mbeya), fukwe nzuri zilizoko Msimbati na Msanga Mkuu (Mtwara), Kela Beach na Mitema (Lindi), Saadani – Bagamoyo na Matema Beach (Ziwa Nyasa).

 

 1. Mheshimiwa Spika, mpango mwingine ni kuendeleza utalii wa fukwe, utalii wa mikutano, utalii wa meli, utalii wa majini, utalii wa michezo, utalii wa utamaduni na kuimarisha shughuli mpya za utalii katika maeneo ya hifadhi. Shughuli hizo zitajumuisha safari za kutembea kwa miguu hifadhini, safari za puto (Hot Air Balloon), utalii wa Canopy walkway na safari za mitumbwi kwenye hifadhi za maji kama vile Rubondo.

 

 1. Mheshimiwa Spika, lengo la Serikali ni kuchochea ujio wa watalii wengi wa kimataifa nchini sambamba na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika ukuaji wa uchumi na ustawi wa wananchi. Nitoe wito kwa Wizara ya Maliasili na Utalii ihakikishe inasimamia utekelezaji wa Mkakati wa Kuendeleza Maeneo ya Malikale ili rasilimali hizo zitumike kiutalii na kuongeza mchango katika pato la Taifa.

 

 1. Mheshimiwa Spika, jitihada na mafanikio niliyoyaeleza katika sekta ya utalii ni maelekezo mahsusi kutoka kwa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yaliyolenga kuimarisha shughuli za utalii nchini. Kama mnavyofahamu, tulianza na upatikanaji wa ndege mpya, uboreshaji wa viwanja vya ndege, huduma za hoteli, barabara, kuanzisha chaneli maalumu ya utalii (yaani Tanzania Safari Channel) na miundombinu mingine muhimu katika kukuza utalii.

 

UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA

 

 1. Mheshimiwa Spika, Novemba 2019 tutakuwa na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Uchaguzi huu ni sehemu muhimu katika kuimarisha utawala bora na demokrasia ambayo imeendelea kunawiri nchini. Mengi kuhusu maandalizi na masuala muhimu kuhusu uchaguzi huu niliyaeleza wakati wa hotuba yangu ya Aprili 2019, nikitoa mwelekeo wa Serikali kwa mwaka 2019. Kadhalika, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI pia ametoa ufafanuzi mzuri wakati akiwasilisha hotuba yake.

 

 1. Mheshimiwa Spika, tumeendelea kutumia mbio za mwenge kuhamasisha wananchi kushiriki uchaguzi huo kupitia kaulimbiu “Maji ni haki ya kila mtu, tutunze vyanzo vyake na tukumbuke kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa” kwa lengo la kuhamasisha wananchi wengi zaidi kushiriki uchaguzi huo. Napenda kutumia fursa hii kutoa wito kwa wadau mbalimbali na wananchi kwa ujumla hususan wale wenye sifa wajitokeze kwa wingi kujiandikisha na kupiga kura ili waweze kutumia haki yao ya kidemokrasia ya kuchagua au kuchaguliwa katika uchaguzi huo.

 

 1. Mheshimiwa Spika, jambo muhimu zaidi ni kuwa wale wenye nia ya kugombea ni lazima wajue majukumu wanayoomba yanahitaji umakini mkubwa na uchapaji kazi. Serikali imewekeza miradi mingi kote nchini. Hivyo, kunahitajika watu walio tayari kuhakikisha wanasimamia miradi hiyo ili itoe matokeo yanayokusudiwa. Katika hatua nyingine, Serikali itaendelea kuhakikisha uwepo wa mazingira salama na tulivu kwa kipindi chote cha uchaguzi.

 

Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura

 

 1. Mheshimiwa Spika, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba 2019, Tume ya Taifa ya Uchaguzi inakamilisha maandalizi ya uborehaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Uboreshaji huo, unatarajiwa kuanza tarehe 18 Julai, 2019 katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro ambapo litafanyika kwa muda wa siku 7 kwa kila kituo na kuendelea hadi tarehe 5 Machi, 2020 litakapohitimishwa katika mkoa wa Dar es Salaam.

 

 1. Mheshimiwa Spika, uboreshaji huo hautahusisha wapigakura walioandikishwa mwaka 2015 isipokuwa utawahusu wapigakura wapya waliotimiza umri wa miaka 18 na kuendelea au watakaotimiza umri huo ifikapo siku ya Uchaguzi Mkuu ujao. Kundi lingine litakalohusika na zoezi hili ni wale watakaoboresha taarifa zao, kama vile waliohama Jimbo au Kata na kuhamia katika maeneo mengine ya kiuchaguzi, waliopoteza au kuharibika kwa kadi zao za kupigia kura, watakaorekebisha taarifa zao pamoja na kuwaondoa wapigakura waliopoteza sifa kama vile kufariki.

 

 1. Mheshimiwa Spika, napenda kutoa wito kwa wananchi wote wenye sifa watumie fursa hii kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kuboresha taarifa zao katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ili kutimiza haki yao ya Kikatiba hasa katika awamu hii ya kwanza badala ya kusubiri awamu ya pili ili kuondoa uwezekano wa kukosa fursa hiyo ikitokea mtu kapata dharura.

 

USHIRIKI WA TAIFA STARS AFCON 2019

 

 1. Mheshimiwa Spika, sote tunafahamu kwamba timu yetu ya Taifa ya Mpira wa Miguu, Taifa Stars, ipo Misri kushiriki mashindano ya AFCON 2019, kuwania ubingwa wa Afrika. Timu yetu ilianza kampeni hiyo Jumapili tarehe 23 mwezi huu dhidi ya timu ya Taifa ya Senegal. Matokeo ya mchezo huo wote mnayajua kwamba Senegal ilitushinda kwa mabao mawili bila. Pia, tarehe 25 Juni, 2019 tulipoteza mchezo wa pili dhidi ya Kenya kwa mabao 3 – 2.

 

Ndugu Watanzania, sote tunajua historia yetu katika michezo ya kimataifa kuwa matokeo yetu bado siyo mazuri. Hata hivyo, tumeanza kuona jitihada za vilabu, shirikisho la soka na Wizara kupitia Baraza la Michezo tukiimarisha michezo nchini.

 

 1. Mheshimiwa Spika, pamoja na matokeo hayo, Taifa Stars wanastahili pongezi kwa kujitahidi kuwadhibiti Senegal licha ya kupoteza kwa magoli mawili, na pia kwa kuonyesha ubora wa mchezo dhidi ya Kenya licha ya kupoteza pia. Hata hivyo, nampongeza sana mlinda mlango Aishi Manula kwa kazi nzuri, uwezo mzuri aliouonesha wa kuzuia mashambulizi mengi ya hatari, hakika anastahili kupongezwa. Anastahili sifa. Baada ya michezo hiyo kumalizika, Watanzania tuungane pamoja kuwapokea wachezaji siku watakaporudi ili tujipange tena.

 

 1. Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kukupongeza Mheshimiwa Spika kwa uhamasishaji mkubwa uliofanya kupitia Bunge na hata kudiriki kuambatana na Waheshimiwa Wabunge zaidi ya 70 kwenda Misri kuungana na Watanzania wengine kuwatia moyo wachezaji wetu. Aidha, nawapongeza vijana wetu wanaounda Taifa Stars kwa kupambana na kusimama kidete kwa heshima ya nchi.

 

 1. Mheshimiwa Spika, nitoe wito kwa Wizara na taasisi zake, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), wachezaji, benchi la ufundi na wadau wote wa mpira wa miguu nchini, tutumie matokeo haya kujifunza, kujitathmini na tuje na mipango bora zaidi ya kuendeleza soka hususan kwa kuwekeza kwenye soka la vijana na walimu.

 

HITIMISHO

 

 1. Mheshimiwa Spika, nihitimishe hotuba yangu kwa kurejea maneno ya Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambaye katika hotuba yake aliyoitoa tarehe 2 Februari 1967 alisema: ninamnukuu

 

Kila mtu anahitaji maendeleo, lakini si kila mmoja anaelewa na kukubali hitaji muhimu la maendeleo. Hitaji muhimu la maendeleo ni kufanya kazi kwa juhudi”. Mwisho wa kunukuu.

 

 1. Mheshimiwa Spika, narudia kuwakumbusha viongozi na watendaji wote wa Serikali kuanzia ngazi ya kijiji, kata, tarafa, wilaya, mkoa hadi Wizara kuwa ili kufikia lengo na dhamira ya Serikali katika kutekeleza Mpango na Bajeti ya Serikali 2019/2020 kwa ufanisi hatunabudi kuzingatia yafuatayo:

 

Mosi;           kuwajibika ipasavyo na kudumisha nidhamu katika utekelezaji wa majukumu yetu ya kuwahudumia wananchi;

 

Pili;           kuendelea kuwasisitizia wananchi wote kushiriki ipasavyo katika ulinzi wa miundombinu inayojengwa kwa gharama kubwa na Serikali ikiwa na lengo la kuboresha shughuli za kiuchumi na ustawi wa watu;

 

Tatu;           Mamlaka husika zishirikiane na wadau wengine katika kudhibiti uharibifu wa mazingira kwa kukomesha ukataji hovyo wa misitu, uchafuzi wa bahari, mito na maziwa na taka za plastiki ili kulinda mazingira asilia; na

 

Nne;            Mamlaka za Serikali ziimarishe ushirikiano na wananchi katika kampeni za kutokomeza magonjwa ya mlipuko kama Dengi na Ebola;

 

 1. Mheshimiwa Spika, kupitia Mpango na Bajeti ya Serikali 2019/2020, Serikali itaendelea kuweka mazingira rahisi ya ufanyaji biashara kwa kutoa unafuu katika sekta za kilimo, uvuvi, mifugo na shughuli nyingine jumuishi. Aidha, nyote mtakubaliana nami kuwa suala la kuwahudumia Watanzania, kuwaletea maendeleo, pamoja na kuhakikisha nchi yetu inafikia uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda, mafanikio yake hayamo katika mikono ya Serikali pekee. Kwa msingi huo, kila mmoja wetu anao wajibu wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za kujiletea maendeleo.

 

 1. Mheshimiwa Spika, niwatakie safari njema Waheshimiwa Wabunge wanaporejea majimboni kwao kushirikiana na wananchi kutekeleza Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2019/2020. Vilevile, niwashukuru watendaji wa Serikali kwa kufanikisha shughuli zilizopangwa na Bunge lako tukufu kwa weledi, uadilifu na ufanisi mkubwa.

 

 1. Mheshimiwa Spika, pia, niwashukuru wanahabari  kwa uchambuzi wao wa hoja zilizokuwa zikiendelea bungeni na kufikisha habari hizo kwa wananchi. Kadhalika, nivishukuru vyombo vya ulinzi na usalama, madereva na wahudumu waliotuhudumia wakati wote tukiwa hapa bungeni. Nawashukuruni sana!

 

 1. Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo napenda kutoa hoja kuwa Bunge lako tukufu sasa liahirishwe hadi Jumanne, tarehe 3 Septemba, 2019 saa 3:00 asubuhi litakapokutana tena katika ukumbi huu.

 

 1. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.