HOTUBA YA MGENI RASMI MHE. KASSIM MAJALIWA MAJALIWA (MB) WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI WA UFUNGUZI WA MASHINDANO YA UMOJA WA MICHEZO NA TAALUMA KWA SHULE ZA MSINGI NA SEKONDARI TANZANIA KATIKA UWANJA WA CCM KIRUMBA, MWANZA, TAREHE 6 JUNI, 2018

 Mheshimiwa John V. Mongella, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza;

Mheshimiwa Selemani Said Jafo (Mb) Waziri wa Nchi, OR – TAMISEMI;

Mheshimiwa Joyce Lazaro Ndalichako (Mb), Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia;

Mheshimiwa Dr. Harrison Mwakyembe (Mb) Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo;

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – TAMISEMI;

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia;

Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo;

Mwakilishi kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar;

Mwakilishi wa Wizara ya Vijana, Utamaduni Sanaa na Michezo, Zanzibar;

Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya;

Wakurugenzi wa Wizara na Asasi mbalimbali;

Wakurugenzi wa Halmashauri;

Maafisa Elimu wa Mikoa;

Maafisa Elimu wa Halmashauri;

Viongozi wa Kampuni ya Cocacola;

Viongozi kutoka Wizara na Mashirika mbalimbali;

Waandaaji wa Mashindano;

Wakuu wa Shule;

Wanahabari;

Walimu na Wanafunzi;

Wageni Waalikwa;

Mabibi na Mabwana;

Ndugu Wanamichezo;

Habari za mchana!

Awali ya yote, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutupa nguvu na kutuwezesha sisi wote kukutana mahali hapa. Aidha, niendelee kumshukuru Mola wetu kwa kuwalinda na kuwawezesha kusafiri salama kutoka kwenye mikoa yenu na kufika mahali hapa salama.

Kwa niaba ya wanamichezo wote, nimshukuru Mkuu wa Mkoa na wananchi wote wa Mkoa wa Mwanza kwa kukubali kuwa wenyeji wa mashindano haya kwa mara ya tatu mfululizo. Tunawapongeza sana kwa maandalizi yote mliyofanya na kuwezesha michezo hii kuanza leo hii.

Nina hakika wanamichezo hawa wataendelea kuyafurahia mandhari ya hapa Mwanza, kwa kuneosha burudani mwanana, kucheza kwa nidhamu na kushirikiana nanyi kwa ukamilifu. Aidha, nawapongeza sana Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais -TAMISEMI, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo  kwa kushirikiana katika kufanikisha maandalizi ya michezo hii.

Ndugu viongozi na wanamichezo,

Niwapongeze wote mliosafiri kutoka kwenye vituo vyenu na kuja hapa Mwanza kwa ari na azma ya kuibua na kukuza vipaji vya Michezo na Taaluma kwa vijana wetu, hivyo ni vema   kuzingatia maadili ya michezo, nidhamu na taratibu tulizojiwekea wakati wote wa kuendesha michezo hii  kwa kuimarisha ushirikiano kwa wote ili kufikia lengo lililokusudiwa.

Nitumie fursa hii kipekee kuwashukuru Wazazi na Walezi wote kwa kuwaruhusu  watoto wao kushiriki michezo na kutambua kuwa michezo ni sehemu ya masomo na kukuza vipaji.  Aidha, niwapongeze walimu kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kufundisha kwa moyo na kufanyakazi kwa bidii. Nawashukuru pia wanafunzi kwa kuitikia wito wa Taifa wa kukuza michezo ambayo ni kwa ajili ya afya zenu na maendeleo binafsi na Taifa kwa ujumla. Nawasihi kuendelea kujishughulisha na michezo kwa ajili ya afya njema na kusoma kwa bidii ili muwe wataalamu wazuri mtakaolisaidia Taifa hili kusonga mbele kupitia nyanja ya elimu.

Ndugu Wanamichezo,

Kaulimbiu ya michezo ya UMISSETA na UMITASHUMTA ya mwaka  huu ni “MICHEZO, SANAA NA TAALUMA NI MSINGI WA MAENDELEO YA MWANAFUNZI  KATIKA TAIFA LETU.

Kaulimbiu hii inamtaka mwanafunzi ajihusishe na michezo na sanaa kama sehemu ya taaluma. Kupitia michezo na sanaa, wanafunzi wataonyesha vipaji vyao ambavyo vikiendelezwa vema vitawapatia manufaa ikiwemo afya njema, matokeo mazuri ya kitaaluma  na ajira pamoja na kuitangaza nchi yetu kimataifa na kuongeza fursa ya ajira kwa Watanzania.

Ndugu Viongozi na Wanamichezo,

Naomba kwa niaba yenu nichukue fursa hii kuishukuru na kuipongeza kampuni ya COCA COLA kwa uamuzi wao wa kutuunga mkono katika jitihada hizi za uendeshaji wa michezo ya UMISSETA kwa kudhamini michezo ya mpira wa miguu na kikapu kwa Shule za Sekondari. Tunathamini mchango wenu na kuwaomba muendelee kupanua wigo wa udhamini wenu katika michezo mingine.

Naishukuru pia kampuni ya AZAM kwa kujitolea kuonesha mubashara michezo ya UMITASHUMTA kwa mwaka huu 2018 katika ngazi ya Taifa katika viwanja hivi vya Butimba. Hatua hii itaipa michezo hii hadhi inayostahili, na kuwawezesha wadau mbalimbali kuviona na kuviendeleza vipaji vya wanafunzi wetu popote walipo. Utangazaji huu mubashara ni wa kihistoria kwani haijawahi kutokea tangu kuanzishwa kwa michezo hii. AZAM TV imekuwa mfano wa kuigwa kati ya vyombo vyote vya habari kwa kuwa chombo pekee cha habari kwa uamuzi huu.

Utangazaji huu mubashara utachochea ari kwa wanafunzi kuongeza bidii na kupenda michezo zaidi. Nashauri vyombo vingine vya habari kujitokeza kuvitangaza vipaji vya wanafunzi hawa kitaifa na kimataifa.

Ndugu Wanamichezo,

Michezo na Sanaa ni Ajira”. Ni dhahiri kuwa, uwepo wenu hapa Mwanza ni ushahidi wa dhati wa kuwapeni fursa ili kuuthibitishia umma dhamira mliyonayo ya kuonesha kuwa, zipo fursa nyingi za ajira endapo vipaji vya michezo na sanaa vitatumika kikamilifu. Mashindano kama haya yanatoa fursa kwenu kuonesha uwezo wenu na kuonekana kwa wadau mbalimbali  wanaoweza kuwaendeleza.

Si hivyo tu, uwepo wenu hapa unawapa fursa ya kutambua uwezo mlionao kwa ukamilifu na kuzidi kujiwekea malengo na mwelekeo wa maisha yenu ya baadaye. Ushiriki wenu kwenye mashindano haya ni sehemu tu ya kuwaandaa kuwa raia wema, wanaowajibika vyema katika masomo na kufahamu nafasi mlionayo katika jamii mnayoishi kwa maendeleo ya  Taifa kwa ujumla.

Natarajia kwamba wanafunzi waliofikia ngazi hii ya kitaifa ni wale walioonesha umahiri katika ngazi ya Shule, Kata, Wilaya na Mkoa, na wote ni wanafunzi halali wa shule. Endapo itabainika yupo mchezaji aliyeletwa kushiriki michezo hii ambaye si mwanafunzi (mamluki) naagiza hatua kali zichukuliwe dhidi ya wahusika kwa kuzingatia kanuni na sheria za mashindano haya, kwani mchujo wa wazi na sahihi wa wanafunzi wenye umahiri katika michezo hutuwezesha kupata vipaji kwa wachezaji wa umri wa chini ya miaka 17.

Ndugu Wanamichezo,

Kwa kutambua umuhimu wa kuandaliwa fursa kama hii, ni matumaini yangu mtaonesha Michezo na Sanaa yenye ushindani ulio katika viwango bora. Niwaombe wanamichezo wote kucheza na kutambua kuwa hii ni nafasi pekee ya kujenga urafiki miongoni mwenu na kutekeleza kwa vitendo azma ya Taifa ya kuimarisha umoja na mashikamano kati yenu na jamii kama ilivyoelezwa na mwanamichezo wa Marekani aliyekuwa mshiriki wa Olimpiki mwaka 1936 kuwa: “Katika michezo, kuna kujengeka kwa urafiki unaodumu na wenye thamani zaidi ya zawadi zinazotolewa”.

Ndugu Wanamichezo,

Mtakubaliana nami kuwa, michezo ni zaidi ya kucheza. Inatufundisha kutekeleza majukumu yetu katika nyanja mbalimbali kwa ushirikiano mwema bila kujali tofauti zozote tulizonazo miongoni mwetu. Aidha, michezo inatufundisha ushindani unaotuelekeza kukubali kushinda au kushindwa na kwa matokeo yoyote kuendelea kuwa wamoja. Michezo inatufundisha uvumilivu, kuvumiliana na kuendelea kuishi pamoja.  Michezo inaweza kuleta umoja mahali penye utengano wa kijamii na kusaidia jamii kurejesha amani na kuishi pamoja kama jamii au kama Taifa.

Hata hivyo, hayo yote hayawezi kutokea tu bila kuyatengeneza. Mazingira tuliyonayo sasa hayakuja tu bali yalitengenezwa. Ni wajibu wetu sasa kuwaandalia vijana hawa mazingira hayo ili Tanzania iendelee kuwa ya amani, umoja na mshikamano.

Ndugu Viongozi,

Pamoja na manufaa yatokanayo na michezo, kiwango cha michezo  nchini hakiridhishi sana. Inawezekana kuna sababu za msingi, lakini ni ukweli usiofichika kuwa, endapo Taifa linataka kujenga msingi wa kupata matokeo bora, ni lazima tuhakikishe kuwa vijana kuanzia shule za awali, msingi, sekondari na vyuo wanatengenezewa mazingira na kupewa fursa za kucheza na kushindana miongoni mwao. Mazingira mazuri ni pamoja na viwanja vyenye viwango vinavyokubalika, walimu wenye utaalamu wa michezo na vifaa.

Kutokana na hali hii, Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano  wa Tanzania kupitia shule za msingi na sekondari, itaangalia uwezekano wa kuajiri walimu waliosomea michezo ili kuendeleza vipaji vya vijana wetu.

Matokeo  mazuri yanapatikana kwa kufanya maandalizi ya kutosha na yenye tija. Je, tunaweza kujiuliza ni kwa kiasi gani sisi tumetumia fursa zilizopo kwa ukamilifu.  Wananchi na hata viongozi wengine tumejijengea utaratibu wa kulalamika kila tunapopata matokeo yasiyoridhisha bila kupima maarifa, ubunifu na jitihada iliyotumika katika maandalizi kwa kutumia fursa tulizo nazo.

Ndugu  Wanamichezo,

Nitoe maagizo kwa Mikoa na Wilaya kuhakikisha somo la haiba na michezo na stadi za kazi kwenye shule za msingi, linafundishwa kikamilifu na elimu kwa michezo (Physical Education) kwa shule za sekondari lifundishwe. Vyuo vya michezo kama kile cha Malya viendelee kuwaendeleza walimu wa michezo, maeneo ya michezo na burudani yapimwe na kutumika ipasavyo, pia kuangalia uwezekano wa kutenga fedha kwa ajili ya vitengo vya michezo kwenye ofisi za Halmashauri na Mikoa.

Ndugu Viongozi,

Zinahitajika tafiti mbalimbali pamoja na ubunifu wa jinsi ya kuendeleza michezo nchini. Navishauri vyama vya michezo na asasi za sanaa zijihusishe katika ukuzaji wa michezo shuleni, pasipo kuathiri taratibu za shule.

Yapo majukumu ya kisera ambayo tunatakiwa kusimamia utekelezaji wake. Sera ya Maendeleo ya Michezo inabainisha jukumu la msingi la Ofisi ya Rais - TAMISEMI kuwa ni kuimarisha mashindano ya michezo ya shule ili yaendelee kuchangia upatikanaji wa wachezaji bora wa Taifa.  Aidha, jukumu jingine la Ofisi ya Rais -TAMISEMI ni kuandaa mpango wa Mkoa, Wilaya au Miji na kuweka taratibu za utekelezaji kwa ajili ya kuleta maendeleo katika michezo. Nina hakika, haya na mengine mengi  yakisimamiwa kikamilifu tunaweza kuleta mabadiliko makubwa kwenye sekta ya michezo na sanaa.

Tuwajenge vijana wetu kuanzia umri mdogo, tuweke mikakati endelevu na  inayotekelezeka, tuwe wabunifu na tuziunganishe jamii na shule zetu katika utekelezaji wa shughuli zetu. Mamlaka zote zinazosimamia na kuendesha michezo na sanaa katika shule ziwajibike kikamilifu kuhakikisha mashindano haya yanakuwa endelevu ikiwa ni pamoja na kutafuta mbinu mbadala za kupata washirika  zaidi wa kugharamia michezo hii.

Mwisho, nawaasa vijana mjiepushe na vitendo vitakavyokwamisha ndoto zenu za kufanikiwa katika masomo na michezo kama vile matumizi ya dawa za kulevya, ngono, uvivu na wizi. 

Tuzidi kumwomba Mwenyezi Mungu aendelee kutupa afya njema, tukae mahali hapa kwa amani, tucheze na kumaliza michezo yetu kama ilivyopangwa na hatimaye tuweze kurejea nyumbani salama.

Kwa wale Waislamu wanaotekeleza nguzo ya tano ya Kiislamu ya kufunga mwezi mtukufu wa Ramadhani, nawapongeza na kuwatakia mfungo mwema. Wanamichezo mlio hapa ambao mmefunga Mwenyezi Mungu awajalie kumaliza mfungo salama na baraka za Mwenyezi Mungu ili kufungua njia ya mafanikio mengine ya maendeleo.

Ndugu Viongozi na Wanamichezo,

Pamoja na kuwatakia mashidano yenye tija, sasa natangaza kuwa mashindano ya UMISSETA na UMITASHUMTA kwa mwaka 2018 yamefunguliwa rasmi.

Ahsanteni kwa kunisikiliza!