HOTUBA YA MHESHIMIWA KASSIM M. MAJALIWA (MB.), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWENYE MAADHIMISHO YA MIAKA 25 YA MTANDAO WA VIKUNDI VYA WAKULIMA TANZANIA (MVIWATA) UWANJA WA JAMHURI MJINI MOROGORO TAREHE 3 OKTOBA 2018.

Ndugu Abdul Gea - Mwenyekiti wa MVIWATA;

Ndugu Bashiru Ally - Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi;

Mhe. Innocent Kalogeris – Mwenyekiti wa CCM;

Mhe. Charles Tizeba (Mb) - Waziri wa Kilimo;

Mhe. Steven Kebwe - Mkuu wa Mkoa wa Morogoro;

Mhe. Omari Mgumba (Mb);

Mhe. Angelina Mabula (Mb) Naibu Waziri Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi;

Mstahiki Meya Pascal Kihanga - Manispaa ya Morogoro;

Katibu Mkuu – Wizara ya Kilimo;

Waheshimiwa Wabunge;

Mhe. Flolence Mattli – Balozi wa Uswizi nchini Tanzania;

Ndg. Fred Kafeero - Mwakilishi FAO;

Ndg. Stephen Ruvugu – Mkurugenzi Mtendaji wa MVIWATA;

Mhe. Stephen Mashishanga – Mkuu wa Mkoa Mstaafu na mlezi wa MVIWATA;

Wenyeviti wa Halmashauri na Madiwani;

Wajumbe wa Bodi – MVIWATA;

Ndugu Wageni Waalikwa;

Ndugu Wanachama na Watumishi wa MVIWATA;

Mabibi na Mabwana;

Ndugu Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa uongozi wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) kwa kunialika niwe mgeni rasmi katika maadhimisho haya ya Miaka 25 ya MVIWATA. Binafsi nimepokea kwa heshima kubwa mwaliko huu wa kushiriki nanyi kwenye tukio hili la kihistoria ambalo linawaleta pamoja wakulima wadogo wanachama wa MVIWATA wasiopungua 2,400 wakiwakilisha wakulima wenzao kutoka mikoa yote ya Tanzania. Uwepo wa wanachama wenu na shamrashamra ninazoziona kwangu ni uthibitisho wa wazi kwamba hii kweli ni taasisi ya wakulima.

Kabla sijaendelea nitumie fursa hii kuwasilisha kwenu salaam za Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye anawasalimu sana na anawapongeza kwa kuwa na wazo la kuanzisha mtandao huu.

Ndugu Mwenyekiti,

Nitumie pia fursa hii kutoa pongezi zangu za dhati kwa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania, yaani MVIWATA kwa kuadhimisha miaka 25 tangu taasisi yenu ianzishwe. Hongereni sana. Sina budi kukiri kwamba uhai wa miaka 25 kwa taasisi si haba kwani kuna taasisi nyingi ambazo zilianza kama ninyi na zikaishia njiani na sasa zimebaki kuwa ni historia. Nioneshe faraja yangu baada ya kutembelea mabanda na kuona kazi nzuri ya wakulima wadogo.

MCHANGO WA WAKULIMA WADOGO

Ndugu Mwenyekiti,

Nimefika hapa kujumuika nanyi ikiwa ni kutambua na kuenzi umuhimu wa wakulima wadogo na mchango wenu mkubwa katika uchumi wa Taifa letu. Naomba nichukue dakika chache kuwakumbusha Watanzania kwa ujumla kuhusu umuhimu wa wakulima wadogo katika taifa letu.

Mchango wa wakulima wadogo katika Taifa letu ni wa kihistoria. Harakati za kupigania uhuru wa nchi yetu kwa kiasi kikubwa zilifanikishwa na tabaka la wakulima na wafanyakazi ikizingatiwa kwamba katika kipindi hicho nchi yetu ilikuwa na idadi ndogo tu ya wasomi. Mchango wa wakulima kupitia vyama vyao vya ushirika katika mapambano ya kupigania uhuru unajulikana na upo katika vitabu vya historia ya nchi yetu. Kama tabaka la wakulima na wafanyakazi lisingeunga mkono harakati za mapambano ya kupigania uhuru wa nchi yetu chini ya uongozi wa waasisi wa taifa letu, hususan Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, basi huenda tungechelewa sana kupata uhuru.

Vilevile, kwa miaka yote tangu uhuru wa nchi yetu, wakulima wamekuwa ni wachangiaji wakubwa wa pato la Taifa letu na kwa wakati fulani mchango huo ulikuwa unakaribia asilimia 70 ya pato la Taifa na asilimia 50 ya fedha za kigeni. Hata kama kwa sasa mchango wa kilimo katika pato la Taifa kimahesabu umepungua, ukweli ni kwamba nguvu kazi kubwa ni wakulima wadogo na hilo pekee linadhihirisha umuhimu wao katika Taifa letu.

Kwa upande mwingine, wakulima wadogo ndiyo wanaolilisha Taifa letu kwa kutambua kwamba takribani asilimia 90 ya chakula tunachokula kinazalishwa na wakulima wadogo. Mchango huu wa Wakulima wadogo ndiyo ambao umewezesha taifa letu kujitosheleza kwa chakula na hata kuuza nje ya nchi mazao ya kilimo. Kwa kutambua mchango huo, niliamua tena bila kusita kujumuika nanyi kuadhimisha miaka 25 ya taasisi yenu ya MVIWATA mara tu nilipopokea mwaliko wenu.

Ndugu Mwenyekiti,

Nimefurahishwa sana na tukio hili. Kwa upande wangu, ninaona kwamba ni jukwaa sahihi kwa Serikali kulitumia kwa lengo la kupata maoni na kero za wakulima.

Hivyo, nitoe rai kwa viongozi na watendaji wa Serikali kujenga utamaduni wa kuhudhuria tukio hili la kila mwaka la MVIWATA ili kukutana na kuzungumza na wakulima kuhusu mahitaji, malalamiko, maoni na ushauri wao.

MCHANGO WA WAKULIMA WADOGO

Ndugu Mwenyekiti,

Tangu kuasisiwa kwake, tarehe 5 Februari 1977, Chama cha Mapinduzi hadi leo hii kimeendelea kutambua na kuheshimu mchango wa wakulima wadogo nchini. Waasisi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), chini ya uongozi wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wanadhihirisha hilo pale walipoamua kuweka nembo ya jembe na nyundo kama ishara ya kuthamini na kutambua mchango wa makundi ya wakulima na wafanyakazi katika ujenzi wa Chama Cha Mapinduzi na Taifa kwa ujumla.

CCM kupitia Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015–2020, itaendelea kuisimamia Serikali kutekeleza Awamu ya Pili ya Programu ya Kuendeleza Kilimo nchini yaani Agricultural Sector Development Programme Phase Two – ASDP II (ASDP II) ili kukifanya kilimo kuwa cha kisasa na cha kibiashara; chenye tija na ambacho mazao yake yatakuwa yameongezewa thamani.

JUHUDI ZA SERIKALI KUBORESHA KILIMO

Ndugu Mwenyekiti,

Tunafahamu kwamba wakulima mna changamoto nyingi zikiwemo za kisera, kirasilimali na kiutendaji hususan kwenye masuala ya ardhi, masoko, mitaji na hata kero za tozo na ushuru. Kwa upande wake, Serikali inatekeleza mipango mbalimbali kwa lengo la kutatua kero zinazowakabili sambamba na kuwawezesha wakulima wadogo kufikia malengo yao ya kujikwamua kiuchumi kupitia kilimo. Mpango tunaoendelea nao ni kuhakikisha kuwa mazao yanalimwa kitaalam, kuyahudumia kwa kusambaza pembejeo na kutafuta masoko yake.

Tarehe 14 Juni 2018, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alizindua Awamu ya Pili ya Programu ya Kuendeleza Kilimo hapa nchini (ASDP II). Aidha, katika hotuba yake ya uzinduzi Mheshimiwa Rais aliweka wazi kuwa namnukuu:

“…mageuzi makubwa ya kiuchumi yaliyotokea kwenye mataifa mengi duniani, yalianzia kwenye sekta ya kilimo. Mifano ya nchi za mwanzo kupata maendeleo, kama vile Uingereza, Marekani, Japan imetufundisha hivyo. Na vilevile nchi zilizoendelea hivi karibuni, kama vile Vietnam, Brazil, India na China zimetufundisha kuwa mageuzi kwenye sekta hii ya kilimo ni chachu na kichocheo muhimu cha kuleta mageuzi ya kiuchumi.” Mwisho wa kunukuu”.

Ndugu Mwenyekiti,

Maelezo hayo ya Mheshimiwa Rais yanadhihirishwa na azma yake ya dhati ya kuhakikisha sekta ya kilimo inapewa kipaumbele stahiki ili iweze kuleta tija kwa wakulima wenyewe na nchi yetu kwa ujumla. Aidha, katika kutekeleza hilo, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha sekta ya kilimo ikiwemo kutoa mikopo kwa wakulima wadogo; kuondoa baadhi ya tozo zenye kufifisha uzalishaji; kuweka mipango mizuri ya matumizi bora ya ardhi na kutafuta masoko pamoja na kuongeza thamani kwenye mazao ya kilimo ili kumuongezea tija mkulima.

Ndugu Mwenyekiti,

Serikali katika kipindi cha Agosti 2015 hadi Septemba 2018, kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo nchini (TADB) imefanikiwa kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 56.45 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya kilimo katika mikoa 13 hapa nchini. Mikopo hiyo imewanufaisha wakulima wadogo zaidi ya 527,000 waliopo kwenye mnyororo wa thamani wa mazao ya kahawa, karafuu, mahindi, mboga mboga na mazao mengine mengi kama ilivyoainishwa kwenye Awamu ya Pili ya Proramu ya Kuendeleza Kilimo nchini (ASDP II). Hivyo, suala la mikopo linafanywa na mabenki yote TADB, NMB, CRDB, TIB.

Ndugu Mwenyekiti,

Chama cha Ushirika Skimu ya Mombo Korogwe ni mfano mzuri wa wanufaika wa mikopo ya TADB. Chama hicho kilikopa pembejeo katika benki yetu ya TADB, baadaye walikopa trekta, baadaye walikopa tena mashine ya kuvuna mpunga na sasa wamejenga ghala na wapo katika hatua za mwisho kupata mashine ya pili ya kukoboa. Kutokana na mkopo wa TADB wameweza kuongeza uzalishaji mara dufu kutoka tani 1.9 mpaka tani sita kwa ekari moja. Sasa Benki hii inaratibu mpango wa kuwawezesha wakulima wadogo wadogo wa zao la michikichi. Mikopo inakuwa rahisi kuipata kama mtajiunga kwenye ushirika (vikundi).

Ndugu Mwenyekiti,

Niwasihi ndugu zangu wakulima wadogo, kuimarisha ushirika na kuutumia ipasavyo kupata mikopo yenye tija kutoka Benki yetu ya Maendeleo ya Kilimo. Aidha, nitumie fursa hii pia kukemea baadhi ya Vyama vya Ushirika na AMCOS ambavyo vimekuwa vikipewa mikopo lakini vinasahau jukumu la kulipa deni kwa wakati na hivyo, kuharibu dhana nzima ya Ushirika kwa mageuzi ya kilimo na viwanda.

Ndugu Mwenyekiti,

Serikali imeendelea kufuta na mahala pengine kupunguza kwa kiwango kikubwa tozo mbalimbali zilizokuwa zikimkandamiza mkulima. Mathalan, katika zao la kahawa jumla ya tozo zipatazo 17 zimefutwa zikiwemo ada ya leseni ya kuuza nje ya nchi kahawa ya kijani kwa kampuni na vyama vya ushirika kiwango cha dola za Marekani 1,000 (sh. milioni 2.1).

Nyingine ni makato ya asilimia 0.75 ya bei ya kahawa mnadani kwa ajili ya kugharamia shughuli za utafiti wa kahawa; ada ya leseni ya ghala la kahawa kwa kampuni na vyama vya ushirika kiwango cha dola za Marekani 500 (sawa na shilingi milioni 1.05); ada ya leseni ya Premium Coffee kwa kampuni kiwango cha dola za Marekani 1,000 na kupunguza kwa asilimia 50 makato ya asilimia 0.75 ya bei ya kahawa mnadani.

Ndugu Mwenyekiti,

Licha ya ukweli kwamba tozo nyingi katika kilimo zimefutwa, Serikali bado inaendelea na zoezi la uchambuzi wa tozo ili kubaini zile ambazo bado zinaathiri wakulima hususan wadogo. Zoezi hili endelevu lina lengo la kuhakikisha wakulima wadogo wananufaika na kilimo chao.

Ndugu Mwenyekiti,

Katika kutatua migogoro ya ardhi kati ya wafugaji na wakulima, Serikali imeandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi ya kilimo kwa kuendelea kupima mashamba ya wakulima na kutoa hatimiliki za kimila kwa wakulima wadogo kwa lengo la kuondoa migogoro ya matumizi ya ardhi lakini pia kuwawezesha wakulima hao wadogo kutumia hati hizo kama dhamana kupata mikopo katika taasisi za kifedha.

Hadi sasa, tayari Serikali imeanzisha Mabaraza 97 ya Ardhi na Nyumba ambapo mpango ni kuwa na mabaraza ya aina hiyo kwa kila Wilaya ili kukabiliana na changamoto za kijiografia na wingi wa migogoro.

Ndugu Mwenyekiti,

Katika suala zima la matumizi ya ardhi naomba niwarejeshe kidogo katika Azimio la Arusha ambalo bado ni msingi wa mfumo wetu wa kijamii na kiuchumi. Azimio hilo liliweka ardhi mikononi mwa umma na kufuatiwa na Sera ya Ardhi ya mwaka 1995 ambayo inatamka wazi kwamba ardhi ni mali ya umma na kila Mtanzania awe mwanamke au mwanaume ana haki ya kutumia na kumiliki ardhi.

Ni kwa kutambua hilo, Serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeamua kufuta hati za mashamba yasiyoendelezwa ikiwa ni njia ya kuirejesha ardhi kwa walio wengi na kukomesha migogoro ya ardhi. Serikali itaendelea kuchukua hatua hiyo ya kufuta umiliki wa mashamba ambayo yanahodhiwa na watu wachache wakati wananchi wakiwa hawana ardhi kwa ajili ya uzalishaji mali.

Nitumie fursa hii kuzitaka halmashauri zote zilizo na mashamba ambayo yamefutiwa umiliki wake kuhakikisha kwamba ardhi hizo zinagawiwa mara moja kwa wananchi kwa kufuata utaratibu uliowekwa. Serikali haitasita kuwachukulia hatua maafisa wote na watendaji ambao kwa makusudi wanapindisha au wanachelewesha ugawaji wa mashamba hayo kwa maslahi yao binafsi kwani kufanya hivyo, ni kusaliti dhamira ya Serikali na kuchonganisha wananchi dhidi ya Serikali yao jambo ambalo haliwezi kuvumilika kamwe.

Ndugu Mwenyekiti,

Kwa upande mwingine, Serikali imeendelea kuwezesha upatikanaji wa masoko ya mazao ya wakulima kupitia ujenzi wa miundombinu bora ya kuhifadhia mazao ya kilimo; kuhakikisha mazao yanauzwa kwenye masoko mbalimbali ndani na nje ya nchi kwa njia ya mnada na utaratibu wa Stakabadhi ya Mazao Ghalani. Natambua tatizo la masoko kwa mazao ya mbaazi, mihogo, choroko, dengu, tangawizi na soya.

Kadhalika, Serikali inatambua kuwa soko la uhakika ni kichocheo cha uzalishaji. Hivyo, imekuwa ikikabiliana na matumizi ya vipimo visivyo sahihi, maarufu kama lumbesa, na kuhakikisha kuwa vipimo sahihi vinatumika katika uuzaji na ununuzi wa mazao ya mkulima. Ninaagiza Wakala wa Vipimo kwa kushirikiana na Halmashauri zote nchini kuhakikisha kwamba zinachukua hatua katika kudhibiti matumizi ya vipimo visivyo sahihi ambavyo kwa ujumla vinamkandamiza mkulima na kuikosesha mapato Serikali ikiwemo lumbesa na sijakuita.

Ndugu Mwenyekiti,

Katika kuboresha miundombinu ya kuhifadhi mazao ya chakula na kukabiliana na upotevu, Serikali kupitia mkopo wa masharti nafuu kutoka Serikali ya Poland, inatumia dola za Marekani milioni 55 kutekeleza mradi wa ujenzi wa maghala na vihenge vya kisasa katika maeneo nane (8) ya Dodoma, Songea, Makambako, Mbozi, Sumbawanga, Mpanda, Shinyanga na Babati.

Aidha, kiasi kilichobaki cha dola za Marekani Milioni 55 zimetumika katika mradi wa kujenga kiwanda cha matrekta ya URSUS ambayo tayari yameanza kuzalishwa na yanafanya kazi. Nitoe wito kwa wakulima wadogo, na wadau wengine wa kilimo kuchangamkia fursa hiyo ya matrekta ili kuongeza uzalishaji.

Ndugu Mwenyekiti,

Vilevile, kupitia usimamizi mzuri wa Serikali wa mifumo ya uuzaji wa mazao kwa njia ya mnada na Stakabadhi za Mazao Ghalani, wakulima wadogo wameendelea kunufaika na mifumo hiyo. Mathalan, kwa kutumia minada bei ya korosho kwa mwaka 2017/2018 iliongezeka hadi shilingi 4,100 kwa kilo ikilinganishwa na shilingi 2,700 kwa kilo mwaka 2016/2017.

Kwa upande wa zao la ufuta, kwa kutumia minada bei ya ufuta imeongezeka kutoka shilingi 1,870 mwaka 2016/2017 mpaka shilingi 3,770 mwaka 2017/2018. Hali kadhalika, kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo nchini (TADB), Serikali imeweza kutekeleza mfumo mpya wa kununua na kuuza kahawa mkoani Kagera kupitia ushirika. Mfumo huo, una tija kwani unamfanya mkulima awe na masilahi makubwa kutokana na jasho lake.

Ndugu Mwenyekiti;

Nimefarijika sana kusikia juhudi mnazofanya za kuhamasisha wakulima kujiunga na kuanzisha vyama vya kuweka na kukopa (SACCOS na VICOBA) na vyama vya ushirika vya mazao.

Hatua hiyo, inakwenda sambamba na mkakati wa Serikali wa kuimarisha vyama vya ushirika kama njia sahihi ya kuboresha soko la mazao ya wakulima. Serikali itaendelea kuwaunga mkono katika juhudi hizo kuhakikisha kuwa vyombo hivyo vinakuwa endelevu na vinachangia kumkwamua mkulima kiuchumi. Nitumie fursa hii kuhamasisha wakulima hususan wadogo wajiunge na ushirika ili waweze kuwa na nguvu ya pamoja na kunufaika na fursa mbalimbali zikiwemo mikopo.

BIMA YA AFYA KUPITIA USHIRIKA

Ndugu Mwenyekiti,

Ili kuhakikisha kuwa afya bora inafikiwa kwa wote ikiwemo wakulima wadogo, tumeanzisha matibabu kwa bima yaitwayo Ushirika Afya. Bima hii inatoa fursa kwa wakulima wadogo kutibiwa kwa gharama nafuu.

Ndugu Mwenyekiti,

Serikali itaendelea kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wakulima wadogo ikiwemo; migogoro sugu ya ardhi, uimarishaji wa miundombinu vijijini, kuongeza upatikanaji wa nishati vijijini, sambamba na upatikanaji wa huduma bora za jamii kama vile elimu, afya, maji na nyinginezo zote zikilenga kuinua maisha ya Watanzania ambao wengi wao ni wakulima wadogo tena waishio vijijini.

SHUGHULI ZA MVIWATA

Ndugu Mwenyekiti,

Nimekuwa nikifuatilia kazi mnazozifanya na nina taarifa kwamba lengo kuu la MVIWATA ni kuwaunganisha wakulima wadogo ili waweze kuweka mikakati ya pamoja ya kujiletea maendeleo. Ninapenda kuwahimiza na kuwatia moyo katika shughuli mnazozifanya za kusaidia wakulima wadogo katika nchi hii nasi kama Serikali tunawaunga mkono.

Ndugu Mwenyekiti,

Ninayo taarifa kuhusu matamko yenu hususan yale mawili ambapo tamko la kwanza lilikuwa ni kuunga mkono hatua mbalimbali tunazozichukua za kurejesha uwajibikaji serikalini; kuziba mianya ya matumizi mabaya ya fedha za umma na kukusanya kodi. Tamko la pili la kuunga mkono hatua ya Serikali ya kulinda madini yetu dhidi ya uporaji kupitia mikataba mibovu na ya kinyonyaji lililotamkwa katika uwanja huu huu wa Jamhuri.

Ndugu Mwenyekiti,

Tulifurahishwa sana na matamko yenu ambayo yalimtia moyo kiongozi wetu na kuona kwamba hayupo peke yake bali anaungwa mkono na umma wa Watanzania. Matamko yenu yalitoa ujumbe si kwa umma wa Watanzania tu bali pia kwa wale wasio na nia njema na nchi hii. Nitumie fursa hii kutambua uungaji mkono wenu mlioufanya na kuwashukuru sana.

Halikadhalika, nitoe rai kwenu kwamba pale mnapoona Serikali yenu imefanya jambo jema mjitokeze kupongeza ili kumtia moyo kiongozi wetu Mheshimiwa Rais kwa yale anayoyafanya. Vivyo hivyo, msisite kutoa ushauri kwa kutumia njia sahihi kwa yale ambayo mnaona mnahitaji kuyaboresha.

Ndugu Mwenyekiti,

Nimevutiwa kipekee na mada mliyoichagua ambayo mtaitafakari katika kongamano lenu: ”Ujenzi wa Uchumi wa Viwanda; Nini Nafasi ya Wakulima Wadogo?” kwa uhakika mada hii inaendana na kipaumbele cha Serikali ya awamu ya tano cha kufikia uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda ifikapo mwaka 2025, na maazimio yenu niyapate tuyafanyie kazi.

Tunafahamu kwamba kwa muda mrefu uchumi wa taifa letu umekuwa unategemea kilimo na kwamba takribani asilimia 70 ya nguvu kazi ni wakulima. Ni mtazamo wa serikali kwamba ili kilimo kiwe na manufaa ni lazima kiunganishwe na viwanda na huu ndiyo msingi wa kuwa na mkakati wa kujenga uchumi wa viwanda unaokwenda sambamba na Utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Programu ya Kuendeleza Kilimo nchini (ASDP II).

Ndugu Mwenyekiti,

Kwa kutambua kuwa kilimo ni uti wa mgongo, tangu awali Mwalimu Nyerere alihakikisha kwamba sekta ya kilimo inaunganishwa na viwanda vya kuchakata na kuongeza thamani ya mazao yetu ikiwemo viwanda vya nguo ambayo vilijengwa katika kila kanda ya nchi. Kwa mfano, viwanda vya tumbaku na sigara, mafuta, viatu na ngozi, usindikaji wa nyama, maturubai, magunia, viwanda vya kubangua korosho na vingine vingi vya aina hiyo.

Mwalimu Nyerere, hakuishia hapo pia alijenga viwanda kwa ajili ya vipuri kama kile cha Mang’ula na Kilimanjaro Machine Tools ili kulisha viwanda vingine. Kwa sababu ya mapungufu ya menejimenti na ubinafsi viwanda hivi vingi havipo tena. Hivyo, serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuhuisha viwanda ambavyo vitatoa fursa kwa wakulima. Aidha, tunaweka mfumo mzuri wa kuhakikisha kwamba mkulima hanyonywi wala kupunjwa na wenye viwanda.

NGUVU YA WAKULIMA WADOGO

Ndugu Mwenyekiti;

Kupitia maadhimisho haya, ninapenda kuwakumbusha nguvu na uwezo wa wakulima wadogo katika kujenga uchumi wa viwanda. Huenda mkaona ni jambo gumu au haliwezekani lakini niwakumbushe kwamba katika historia ya nchi yetu katika miaka ya 70 wakulima wadogo kupitia vyama vya ushirika waliweza kuanzisha viwanda hususani vya usindikaji wa pamba na kahawa katika kanda ya ziwa.

Kwa bahati mbaya, kutokuwepo kwa viongozi waadilifu, viwanda hivyo na vyama vingi vya ushirika vilianguka na kuwatelekeza wakulima. Hii ndiyo sababu ya Serikali ya Awamu ya Tano kuamua kuwashughulikia na kuwachukulia hatua za kisheria wale wote ambao wamehujumu vyama vya ushirika. Hivyo, ndugu wakulima mkijipanga vema kupitia vikundi vyenu na ushirika mnaweza kuanzisha na kumiliki viwanda vyenu. Msikate tamaa. Mnaweza.

Ndugu wana MVIWATA natambua kuwa ili tuendelee kufanya kazi za kilimo, hatuna budi tuwe na afya bora hivyo, ni muhimu tukaendelea kutambua afya zetu kwa kupima. Kwa sasa tuko kwenye kampeni ya kuhamasisha wananchi nchi nzima tupime afya zetu ili tutambue hali zetu na kuchukua hatua stahiki.

HITIMISHO

Ndugu Mwenyekiti,

Nimeelezwa kwamba, katika mlolongo wa shughuli za maadhimisho haya mtafanya kongamano na Mkutano Mkuu wa Wanachama. Ni matumaini yangu kwamba mtakuwa na mjadala wenye mafanikio na kwamba maazimio yenu yatatusaidia upande wa Serikali ili kuona namna bora zaidi ya kuwahudumia wakulima.

Wakati nikihitimisha hotuba yangu hii niwapongeze kwa kuweza kuitisha mikutano yenu mikuu 23 tangu msajiliwe mwaka 1995. Hii ni ishara kwamba taasisi yenu imejiwekea misingi ya uwazi na ya kidemokrasia na ndiyo maana mna ushujaa wa kuitisha mikutano hiyo kila mwaka. Ninapenda kutumia jukwaa hili kutoa wito kwa asasi zisizo za kiserikali ziige mfano huu na kuzingatia sheria katika uendeshaji wake.

Ndugu Mwenyekiti,

Kwa mara nyingine, napenda kuwashukuru sana kwa kunipa heshima hii kubwa ya kuwa mgeni rasmi katika tukio hili kubwa na la kihistoria na nitamke kwamba maadhimisho ya miaka 25 ya MVIWATA yamefunguliwa rasmi.

Ahsanteni kwa kunisikiliza.