HOTUBA YA MHESHIMIWA KASSIM M. MAJALIWA, (MB.), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA KILELE CHA MAADHIMISHO YA SIKU YA UKIMWI DUNIANI, DODOMA TAREHE 01 DISEMBA, 2018

Mheshimiwa Jenista Mhagama (Mb.), Waziri wa Nchi – Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu);

Mheshimiwa Selemani Jafo (Mb), Waziri wa Nchi – Ofisi ya Rais, TAMISEMI;

Mheshimiwa Dkt. Binilith Mahenge, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma;

Mheshimiwa Faustine Ndungulile, (Mb.), Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto;

Mheshimiwa Antony Mavunde, (Mb.), Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Vijana);

Mheshimiwa Musa Sima, (Mb.), Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira);

Mheshimiwa Mnyongo, (Mb.), Naibu Waziri wa Madini;

Mheshimiwa Oscar Mukasa (Mb.), Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Kuhusu Masuala ya UKIMWI;

Waheshimiwa Wabunge wote mliopo hapa;

Mheshimiwa Petrobas Katambi, Mkuu wa Wilaya, Dodoma;

Mheshimiwa Mwanahamisi A. Mukunda, Mkuu wa Wilaya ya Bahi;

Waheshimiwa Makatibu Wakuu wote mliopo hapa;

Mhe. Jamila Yusuph, Katibu wa CCM Mkoa wa Dodoma;

Dkt. Leonard Maboko, Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania;

Prof. Devis Mwamfupe, Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma;

Kamishna Jenerali Siang’a, Kamishna Jenerali Mamlaka ya Kupambana na Dawa za Kulevya;

Makamishna wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania;

Viongozi na Watendaji Wakuu wa Serikali;

Bw. Rodriguez Alvaro, Mratibu Mkazi wa Taasisi za Umoja wa Mataifa (UN);

Dkt. Lee Zekeng, Mkurugenzi Mkazi wa Umoja wa Mataifa (UNAIDS);

Waheshimiwa Wadau wa Maendeleo Mliopo Hapa;

Bibi Leticia Mourice, Mwenyekiti wa Baraza la Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (NACOPHA),

Waheshimiwa Viongozi wa Dini na Asasi za Kiraia;

Wageni waalikwa;

Ndugu Wanahabari;

Wana Maonesho/Wasanii wote mliopo hapa;

Mabibi na Mabwana.

Ninayo furaha kubwa siku hii ya leo, kuungana nanyi wananchi wa jiji la Dodoma na Watanzania wote kwa ujumla katika kuadhimisha Siku ya UKIMWI Duniani ambayo kitaifa inafanyika jijini Dodoma, Makao Makuu ya Serikali. Aidha, nitumie fursa hii kuupongeza sana uongozi wa mkoa chini ya uongozi wake Mheshimiwa Dkt. Binilith Mahenge, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kwa kukubali kuwa mwenyeji na kufanikisha shughuli hizi za maadhimisho haya muhimu.

Vilevile, nitoe shukrani zangu kwa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania kwa uratibu wa maadhimisho haya na kwa kunialika kuwa Mgeni Rasmi ili nijumuike nanyi kuadhimisha Siku ya UKIMWI Duniani kwa mwaka 2018. Nitumie fursa hii pia kuwapongeza Wadau Wote, mlioshiriki katika maadhimisho ya mwaka huu kwa kuchangia fedha, kuchangia vifaa mbalimbali, kutoa huduma na kuonesha shughuli zenu hapa uwanjani kwa muda wa wiki nzima.

Nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mama Leticia Mourice kupita kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa Baraza la Taifa la Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (VVU).

Ndugu Wananchi,

Nimevutiwa mno na mabanda ya maonesho niliyotembelea muda mchache uliopita. Nilichojifunza kupitia wadau hao wa maonesho ni utayari wao katika kufanyakazi ya kudhibiti UKIMWI nchini tena kwa weledi mkubwa na tija, tena ni vijana. Miongoni mwa mambo niliyoyashuhudia kupitia mabanda hayo ni pamoja na huduma za elimu, uhamasishaji na upimaji wa VVU na magonjwa mengine yakiwepo yale sugu na yasiyoambukiza pamoja na burudani za wasanii. Mambo yote haya ama kwa hakika yamenogesha sana maadhimisho haya. Hongereni nyote, kwa kulifanya tukio hili kuwa lenye kutia fora!

Kipekee, nimefurahishwa na kuwepo kwa KIJIJI CHA VIJANA katika maadhimisho ya mwaka huu. Kwani kama wengi wetu tunavyofahamu, asilimia 40 ya maambukizi mapya ya VVU katika nchi yetu hutokea kwa vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 24. Hivyo, uamuzi wa kuwepo kwa shughuli zinazolenga vijana zenye kuhusisha upimaji wa VVU, elimu ya ujasiriamali, afya ya uzazi, stadi za maisha na nyinginezo, ni uamuzi wa busara sana na hatupaswi kuubeza. Uamuzi wa namna hii ni muhimu sana katika kunusuru kundi hili linalokabiliwa na changamoto nyingi.

MADHUMUNI YA SIKU YA UKIMWI DUNIANI

Ndugu Wananchi,

Naomba sasa nitumie fursa hii kwa uchache kabisa kukumbusha kuhusu madhumuni ya tukio hili muhimu la leo. Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani hutoa fursa ya kutathmini hali halisi na kutoa mwelekeo kuhusu udhibiti wa UKIMWI.

Kadhalika, maadhimisho haya husaidia katika kubaini changamoto, mafanikio na hivyo, kuja na mikakati mbalimbali katika kupambana na maambukizi ya VVU pamoja na UKIMWI. Siku hii hutoa fursa kote Duniani kutafakari kwa mara nyingine kuhusu tulipotoka, tulipo na tunapokwenda katika mapambano dhidi ya UKIMWI kwenye jamii zetu.

Halikadhalika, maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani hutumika kuwakumbuka kwa huzuni maelfu ya wenzetu waliopoteza maisha na kuwa wahanga wa mwanzo wa kuenea kwa VVU na UKIMWI wakati ambapo hapakuwepo na huduma stahiki za matibabu. Vilevile, siku hii ni muhimu katika kukumbushana kuwajali maelfu ya watoto yatima ambao wazazi wao wamefariki kwa UKIMWI.

Kwa upande mwingine, maadhimisho haya ya Siku ya UKIMWI Duniani hutumika kuikumbusha jamii hususan inayotuzunguka kuendelea kujikinga dhidi ya maambukizi ya VVU. Aidha, tuendelee kuwakumbusha Wanaoishi na VVU (WAVIU) kuendelea kutumia dawa za kufubaza makali ya VVU (ARV) bila kuacha. Kwa msingi huo, ni vema tukaendelea kutumia fursa hii kuikumbusha jamii kutowanyanyapaa au kuwabagua WAVIU bali tuwajali na tuwafariji, bila kusahau kuwatia moyo wale wote wanaowahudumia.

Ndugu Wananchi,                                                                                                                             

Kitaifa, tumekuwa tukiadhimisha siku hii kila mwaka katika mikoa mbalimbali ya nchi yetu ambapo mwaka huu tunafanya hivyo hapa jijini Dodoma. Vilevile, tumekuwa tukitoa maelekezo kupitia Ofisi ya Rais - TAMISEMI kwamba maadhimisho haya yafanyike kote nchini katika ngazi ya mikoa na Halmashauri husika.

Ni matarajio yangu kuwa agizo hili limepewa uzito unaostahili. Hivyo basi, natoa maelekezo kwa kila mkoa kuandaa taarifa ya namna walivyoadhimisha tukio hili kwa uratibu wa Ofisi ya Rais TAMISEMI ikishirikiana na TACAIDS nami nipatiwe mrejesho kabla ya mwisho wa mwaka 2018.

KAULIMBIU YA MAADHIMISHO YA SIKU YA UKIMWI DUNIANI 2018

Ndugu Wananchi,

Kaulimbiu ya maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani mwaka huu kwa Taifa letu inasema: PIMA, JITAMBUE, ISHI. Kaulimbiu hii inalenga kutoa msukumo wa upimaji wa hiari wa VVU baada ya ushauri nasaha pamoja kuanza kutumia dawa za kufubaza VVU (ARVs) mapema kwa watakaogundulika kuwa na maambukizi ya VVU.

Kwa wale mnaokumbuka, kaulimbiu hii ni mwendelezo wa kampeni ya FURAHA YANGU niliyoizindua mimi wenyewe mwezi Juni mwaka huu 2018 hapahapa katika Uwanja wa Jamhuri, Jijini Dodoma. Nilizindua na kukubali kuwa kinara wa kampeni hiyo kwa lengo la kuhamasisha upimaji wa VVU kwa Watanzania na kuanza matumizi ya dawa za kufubaza (ARV) mapema kwa wale watakaogundulika kuwa na VVU. Aidha, kaulimbiu hii inakwenda sambamba na kaulimbiu ya kimataifa ya maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani isemayo TAMBUA HALI YAKO (KNOW YOUR STATUS).

Kama kaulimbiu inavyosema, kipaumbele cha maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani kwa mwaka huu ni kuhamasisha upimaji wa VVU kwa hiari na kuanza kutumia mapema dawa za kufubaza VVU (ARVs). Kama nilivyosema wakati wa uzinduzi wa kampeni ya FURAHA YANGU mwezi Juni mwaka huu, utafiti wa nne uliofanyika katika ngazi ya kaya kuanzia Oktoba 2016 hadi Agosti 2017, ulibainisha kuwa asilimia 52.2 tu ya watu wanaoishi na VVU (WAVIU) nchini ndiyo walikuwa wakijua hali zao za maambukizi.

Kama mtakavyoona, kiwango hicho cha watu kujitokeza kupima VVU bado si chenye kuridhisha, hususan, kwa wanaume, ambao ni asilimia 45 tu ndiyo waliojitokeza kupima. Hivyo, kwa mara nyingine, nikiwa kinara wa Kampeni ya Upimaji wa VVU nchini, natoa wito kwa watu wote, hususan wanaume, tujitokeze kwa wingi tena kwa hiari kupima VVU kwenye vituo vya upimaji kote nchini na kuanza dawa kwa haraka mara tu mtu anapogundulika kuwa na maambukizi ya VVU.

KAMPENI ZA UHAMASISHAJI

Ndugu wananchi,

Juni mwaka huu, wakati nikizindua kampeni ya FURAHA YANGU, niliagiza mikoa yote ifanye uzinduzi wa kampeni hiyo kwenye ngazi za mikoa na hata wilaya. Aidha, niliagiza TACAIDS itoe taarifa za maendeleo ya kampeni hiyo leo katika maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani.

Kufuatia maelekezo hayo, nimearifiwa hapa kuwa mikoa yote ya Tanzania bara imefanya uzinduzi wa kampeni hii. Nawapongeza sana Wakuu wa Mikoa kwa utekelezaji wa agizo hilo. Ni imani yangu kuwa upimaji huu utakuwa ni endelevu katika mikoa yote nchini, kwani bado hatujashinda vita hii dhidi ya VVU na UKIMWI.

Kama mlivyosikia, takwimu zinaonesha kuwa wakati wa uzinduzi wa kampeni ya FURAHA YANGU katika mikoa yote ya Tanzania Bara, jumla ya wananchi 262,114 walijitokeza kupima VVU, wakiwemo wanawake 136,389 na wanaume 125,725. Natoa wito kwa Mikoa na Wilaya zote kuwa kampeni hii iwe endelevu. Viongozi katika ngazi mbalimbali tuungane kwenye uhamasishaji wa jambo hili kwani vita dhidi ya VVU na UKIMWI inahitaji dhamira ya dhati na tafakuri ya kina katika kujilinda dhidi ya maambukizi mapya.

FAIDA ZA KUTAMBUA HALI ZETU ZA AFYA

Ndugu Wananchi,

Kaulimbiu ya maadhimisho haya ya Siku ya UKIMWI Duniani ambayo ni PIMA, JITAMBUE, ISHI, inalenga kuhamasisha Upimaji wa hiari wa VVU na kuunganishwa kwenye huduma ya ARV kwa wanaokutwa na maambukizi. Aidha, ni vema tukatambua kuwa kuna faida nyingi za kupima na kutambua hali ya afya zetu. Kwa mfano, kama ukigundulika kuwa na maambukizi ya VVU, basi hatua inayofuata ni kuunganishwa kwenye huduma ya dawa mapema.

Kwa kufanya hivyo, tutawezesha afya kuimarika kwa kufubaza VVU na kuongeza kinga ya mwili hususan dhidi ya magonjwa nyemelezi. Vilevile, matumizi sahihi ya dawa za ARV kwa mama wajawazito, wanaogundulika kuwa na maambukizi ya VVU humkinga pia mtoto dhidi ya maambukizi ya VVU. Kwa upande mwingine, mtu akipima na kujua kuwa hana maambukizi ya VVU, inamsaidia kuchukua tahadhari na kuacha tabia hatarishi zinazoweza kuchangia apate maambukizi ya VVU. Kupitia kampeni yetu inayowataka kila mmoja kupima kujua afya yako tumeanza kupata mafanikio.

 1. Kampeni ilikuwa inahamasisha wanaume kupima; na
 2. Wenye maambukizi kuanza kutumia dawa.

MKAKATI WA NNE WA TAIFA WA KUDHIBITI UKIMWI 2018/19 -2022/23

Ndugu Wananchi,

Sambamba na maadhimisho haya ya Siku ya Ukimwi Duniani kwa mwaka 2018, leo pia nitazindua MKAKATI WA NNE WA TAIFA WA KUDHIBITI UKIMWI 2018/19 - 2022/23. Matayarisho ya Mkakati huu yamezingatia mambo yafuatayo:

 1. Matokeo ya Mapitio ya Mkakati wa Tatu wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI 2013/14 – 2017/18;
 2. Matokeo ya Utafiti wa Viashiria vya UKIMWI Tanzania wa 2016/17;
 3. Jitihada mpya zinazojitokeza sambamba na matumizi ya teknolojia mpya;
 4. Dhamira za kitaifa, kikanda na kimataifa za kuharakisha mwitikio wa VVU na UKIMWI ili kufikia malengo ya 90-90-90 (yaani TISINI TATU) ifikapo mwaka 2020 na hatua za kuelekea kutokomeza UKIMWI ifikapo mwaka 2030; na
 5. Dhamira ya Tanzania katika utekelezaji wa Azimio la Umoja wa Mataifa kuhusu VVU na UKIMWI la mwaka 2015, Malengo ya Umoja wa Mataifa ya Maendeleo Endelevu 2030 na Ajenda 2063 ya Umoja wa Afrika.

Mkakati huu pia umewianisha na kupanga programu mbalimbali zinazosaidia mwitikio wa Taifa zikiwemo afua zinazotekelezwa kupitia Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa UKIMWI (PEPFAR), Mfuko wa Dunia wa kudhibiti UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria (Global Fund) na jitihada nyingine za makubaliano ya ushirikiano baina ya nchi mbalimbali.

Ndugu Wananchi,

Matokeo yanayotegemewa kutokana na utekelezaji wa Mkakati wa Nne wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI ifikapo 2023 ni pamoja na yafuatayo:

 1. Kupungua kwa maambukizi mapya ya VVU kwa asilimia 75 ifikapo mwaka 2020 na asilimia 85 ifikapo mwaka 2023;
 2. Kupungua kwa maambukizi mapya ya VVU miongoni mwa watoto kwa chini ya asilimia tano ifikapo mwaka 2023 na chini ya asilimia mbili ifikapo mwaka 2030;
 3. Kupungua kwa vifo vinavyohusiana na UKIMWI kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2020 na asilimia 70 ifikapo mwaka 2023; na
 4. Kupunguza unyanyapaa na ubaguzi ifikapo 2023 na kuelekea kutokomeza kabisa ifikapo mwaka 2030.

Aidha, katika kuhakikisha tunapata matokeo mazuri ya utekelezaji wa mkakati huu, tunapaswa kuimarisha mawasiliano na uratibu miongoni mwa wadau wote sambamba na kufuata na kutekeleza vipaumbele vilivyoainishwa. Hivyo, natoa rai kwa wadau wa kitaifa na kimataifa kuendelea kuunga mkono utekelezaji wa mkakati huu kwa hali na mali kwa kushirikiana na Serikali.

CHANGAMOTO YA BAJETI KATIKA VITA DHIDI YA UKIMWI

Ndugu Wananchi,

Serikali inatambua changamoto kubwa ya kuedelea kupungua kwa rasilimali fedha katika vita dhidi ya UKIMWI na utegemezi mkubwa wa wafadhili kwa takriban asilimia 93. Katika kukabiliana na hali hiyo ya utegemezi, Serikali imeanzisha Mfuko wa Udhamini wa UKIMWI (AIDS Trust Fund). Lengo ni kuongeza rasilimali za ndani kwa ajili ya kuboresha huduma za UKIMWI zinazotolewa.

Mfuko huu ulizinduliwa tarehe kama ya leo mwaka 2016. Serikali kama mchangiaji mkubwa wa mfuko huu itaendelea na jitihada za kuuwezesha mfuko huu ufikie malengo yake yaliyo kusudiwa ya kuwa na chanzo cha fedha endelevu cha kugharamia mwitikio wa Taifa dhidi ya UKIMWI na kupunguza utegemezi wa wafadhili. Kwa kufanya hivyo, tutamudu kuongeza uwajibikaji wa Serikali na sekta binafsi katika kutoa fedha za kutosha kwa ajili ya programu za UKIMWI na hatimaye kuokoa maisha ya Watanzania.

 Ndugu Wananchi,

Katika kutunisha mfuko huu, Serikali na wadau wameanza kuchangia fedha ambapo hadi kufikia Novemba 2018 tayari shilingi bilioni 2.45 zilikuwa zimekusanywa. Kati ya fedha hizo shilingi bilioni 2.07 ni fedha za Serikalini na shilingi milioni 375 ni michango ya wananchi kupitia harambee, matembezi ya hiari na namba za simu.

Naomba nitoe wito kwa wadau wa ndani na nje kwamba endeleeni kutoa michango yenu kwa nia ya njema ya kuokoa maisha ya Watanzania wenzetu. Aidha, kwa mara nyingine tena, naiagiza Bodi ya Mfuko kusimamia uendeshaji wake kwa misingi ya utawala bora. Aidha, hakikisheni kuwa mfuko huo unatumika kwa malengo yaliyokusudiwa. Wananchi wote pia mnayo fursa ya kuchangia mfuko huu kupitia namba simu 0684 90 90 90 kwa mfumo wa wa miamala ya fedha ya AIRTELMONEY.

 Tunapoendesha Kampeni hii hatuwezi kuacha kuhamasisha jamii hasa vijana kuachana na matumizi ya dawa za kulevya ambazo zinachangia maambukizi. Ukitumia hupoteza ufahamu na uelewa hivyo hujihusisha na matendo (ngono, sindano n.k).

HITIMISHO

Ndugu Wananchi,

Napenda kuwahakikishia kuwa Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, itaendelea kutekeleza na kuboresha huduma za upimaji wa Virusi Vya UKIMWI, kuzuia kabisa maambukizi ya kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, matibabu ya magonjwa nyemelezi pamoja na kupiga vita unyanyapaa wa aina zote kwa WAVIU.

Mwisho, nitumie tena fursa hii kuishukuru Jumuiya ya Kimataifa ikiwemo Serikali ya Marekani, Ujerumani, Canada, Denmark, Shirika la Kazi Duniani (ILO), Mfuko wa Dunia (GF), Umoja wa Mataifa (UN) na wadau wengine kwa ufadhili wao mkubwa wa rasilimali fedha na msaada wa kiufundi wanayoitoa katika kufanikisha vita dhidi ya UKIMWI.

Pia natambua mchango wa sekta binafsi, asasi za kiraia, mashirika ya dini na makampuni mbalimbali katika kuitikia wito huu. Baada ya maelezo haya, niko tayari kuzindua mkakati mpya wa kudhibiti UKIMWI ukiwa na kaulimbiu ileile ya PIMA, JITAMBUE, ISHI.

Asanteni sana kwa kunisikiliza.

Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania