HOTUBA YA MHESHIMIWA KASSIM M. MAJALIWA WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI AKIPOKEA MAANDAMANO YAAMANI YA SHIRIKISHO LA VYAMA VYA WAFANYAKAZI TANZANIA (TUCTA) YA KUMPONGEZA MHESHIMIWA RAIS DKT. JOHN POMBE MAGUFULI KWA KULIPATIA UFUMBUZI SUALA LA KIKOKOTOO CHA PENSHENI KATIKA MIFUKO YA HIFADHI YA JAMII KWENYE VIWANJA VYA NYERERE SQUARE, DODOMA,TAREHE 7 JANUARI, 2019.

Makamu wa Rais wa TUCTA,Mh. Sulle

Mheshimiwa Jenista Mhagama, (Mb.) Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye ulemevu,

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA)-Dkt. Yahya Msigwa,

Waheshimiwa Wenyeviti wa Vyama vya Wafanyakazi Tanzania

Kamati ya Utendaji Taifa ya TUCTA

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Mahenge

Waheshimiwa Maibu Mawaziri- Mh. Anthony Mavunde (NW-OWM(Mb)), Mh. Stella Ikupa (NW-OWM), Makati Wakuu wa Wizara mbalimbali

Katibu wa Bunge, Bw. Kigaigai

Waheshimiwa Wabunge,

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma,

Wakuu wa Taasisi Mbalimbali, 

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma na Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya,

Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi Nchini,

Waandishi wa Habari, 

Wafanyakazi wote, 

Mabibi na Mabwana.

Heri ya Mwaka Mpya 2019!

MSHIKAMANOOOO!!!!

SOLIDARITY…….

SHUKRANI NA PONGEZI

Awali ya yote, napenda kutumia fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa kutujalia kuuona mwaka huu mpya wa 2019 tukiwa wazima na wenye Afya njema.

Nitumie nafasi hii kutoa shukrani zangu za dhati kwenu kwa kunialika kupokea maandamano haya ya amani yanayokusudia kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kulipatia ufumbuzi suala la kikokotoo cha pensheni katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.Niwapongeze pia wafanyakazi wote mliojitokeza kushiriki.

Kabla sijaendelea napenda nitumie nafasi hii kuwasilisha kwenu salamu za upendo kutoka kwa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Samia Hassan Suluhu, Makamu wa Rais wote kwa pamoja wamenituma niwasalimu na kuwapongeza na wanawashukuru kwa kutambua jitihada zao kwa wafanyakazi.

Kwa msingi huo kwanza, napenda kuwapongeza kwa uamuzi wenu wa busara unaonesha moyo wa shukrani kwa Rais wetu na serikali yenu sikivu ya Awamu ya Tano. Pili, Nawahakikishia kuwa salam na pongezi zenu nitazifikisha kwa Mheshimiwa Rais, Serikali imefurahishwa mno na mshikamano mnaouonesha. 

Serikali ipo tayari wakati wote kuyapatia ufumbuzi matatizo ya wafanyakazi ikiwa ni pamoja na kuboresha mishahara na maslahi yenu. Wito wa Serikali ni kuwa wafanyakazi watekeleze majukumu yao kwa uadilifu,weledi na kujituma ikiwa ndio chachu ya kufikia malengo na ustawi wa nchi yetu

Napenda pia kuwapongeza wafanyakazi wote nchini kwa kuwa watulivu na kuendelea kutekeleza wajibu ipasavyo wakati suala hili linaendelea kufanyiwa kazi ngazi mbalimbali. Huu ndio uzalendo wa kweli wa kuipenda nchi yako.

LENGO LA SERIKALI KATIKA KUFANYA MABADILIKO YA SEKTA YA HIFADHI YA JAMII

Ndugu wafanyakazi,

Kama mnavyofahamu tarehe 31 Januari, 2018 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha Muswada wa Sheria wa kuunganishwa kwa Mifuko minne ya PPF; PSPF; LAPF na GEPF kuwa Mfuko mmoja na kuifanyia marekebisho Sheria ya NSSF ili iweze kuhudumia sekta binafsi. Sheria hiyo ilitiwa saini na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 8 Februari, 2018 na kuanza kutumika tarehe 31 Julai, 2018.  

 Ndugu watumishi wenzangu,

Hatua hii ya uunganishwaji wa Mifuko ililenga kukidhi kilio chenu cha muda mrefu kuhusu kuunganisha Mifuko ya Pensheni ili kupunguza gharama za uendeshaji wa mifuko, kuondoa ushindani usio na tija baina ya Mifuko ya pensheni ambayo kimsingi ilikuwa inatoa mafao yanayofanana, kupunguza migongano baina ya Mifuko inayotoa huduma kwa watumishi wenye masharti yanayofanana, na muhimu zaidi kuboresha mafao ya wanachama wa mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

Kwa kuwa haya yalikuwa ni matakwa yenu na mmeeleza katika risala yenu kuwa mlishirikishwa katika kila hatua,sina shaka kwamba sasa mnatambua jinsi ambavyo Rais wetu na Serikali ya Awamu ya Tano inatambua mchango wenu, inatambua kazi mnazofanya na inawathamini sana wafanyakazi wa Tanzania na Serikali iko nanyi haitowaangusha.

Kama mlivyosema, sheria hiyo inampa waziri mwenye dhamana na Hifadhi ya Jamii kutengeneza kanuni na katika kufanya hivyo anapaswa kuwashirikisha wadau. Katika Risala yenu mmekiri kuwa wakati wa mjadala mlitofautiana mawazo juu ya mapendekezo ya kitokotoo kipya. Kwa kujali maslahi ya wafanyakazi wa Tanzania Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli alitoa uamuzi kuwa vikokotoo vilivyokuwa vikitumika awali virejeshwe na tuwe na kipindi cha mpito cha miaka mitano wakati mchakato unaendelea wa kuyafanyia kazi haya ili kuwanufaisha wafanyakazi.

Nawaomba sana mkubali kushirikiana na mamlaka husika katika kupata muafaka wa jambo hili kwa siku za usoni kwa kujadiliana kwa nia njema ili kupata kikokotoo sahihi kitakachotumika kuanzia baada ya majadiliano hayo Serikali itaendelea kuwashirikisha katika kila hatua.

MAOMBI YA TUCTA

Katika Risala yenu mmeeleza maombi yenu kwa Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli. Hata hivyo baadhi ya maombi hayo yamekwisha jibiwa kwenye maelekezo ya Mheshimiwa Rais katika kikao cha tarehe 28 Desemba, 2018. Mathalani suala la kikokotoo cha mafao kwenye Mfuko wa NSSF ambapo uamuzi wa Mheshimiwa Rais ndio umewafanya leo wafanyakazi tuungane pamoja.

Serikali imeendelea kulipa stahili za watumishi wa umma kwa wakati  na kulipa madeni hatua kwa hatua.

Kati ya Julai 2018 hadi Septemba 2018, Serikali imelipa shilingi bilioni 184.9 za madai mbalimbali ya watumishi.

Kati ya kiasi hicho Serikali imelipa shilingi bilioni 49 kwa ajili ya malimbikizo ya mishahara kwa watumishi 28,214 ambayo yanajumuisha shilingi bilioni 19.2 za walimu 16,214.

Serikali inaendelea na utafiti wa tathmini ya kazi katika Wizara na Taasisi mbalimbali ili kupanga vizuri mishahara na motisha kwa watumishi wa umma.

Ndugu Wafanyakazi, 

Kuhusu suala la kupandisha mishahara, madaraja na maslahi ya wafanyakazi kwa ujumla Mheshimiwa Rais alishatoa maelekezo na Serikali inayafanyia kazi maelekezo yake madara yameanza kwa baadhi ya kada. Suala la mishahara linafanaendelea kufanyiwa kazi. Suala la kulipa madeni mbalimbali tunaendelea kulipa.

Kuhusu ombi la lenu kuwa ofisi yangu ishirikishe wadau ipasavyo katika kipindi cha mpito kwenye zoezi la mapitio ya kikokotoo, niwaahidi kuwa kama ambavyo tumekuwa tukifanya siku zote ofisi ya Waziri Mkuu itawashirikisha katika hatua zote na  kusimamia kwa makini utaratibu huu ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Mheshimiwa Rais. Aidha, niwahakikishie kuwa maoni na maombi yenu yote uliyoyatoa hapa Serikali imeyapokea na tutayafanyia kazi kikamilifu.

HITIMISHO

Napenda kuwashukuru kwa kunialika na kushirikiana nanyi. Maombi yote yaliyomo kwenye risala yatafanyiwa kazi kama mlivyoomba na sina shaka kwa ushirikiano mwema ambao umekuwepo kila hoja itapatiwa ufumbuzi.

Narudia kuwakumbusha wafanyakazi wenzagu kuwa tutekeleze wajibu wetu katika maeneo yetu ya kazi. Sisi ndio chachu ya maendeleo na sisi ndio watekelezaji wa shughuli za maendeleo nchini.

Nawatakieni mwaka wenye neema na Baraka tele.

HERI YA MWAKA HUU MPYA WA 2019.

Ahsanteni kwa kunisikiliza

MSHIKAMANOOOO!!!!