WAZIRI MKUU APIGA MARUFUKU TOZO YA UNYAUFU

*Aagiza Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Maghala asimamishwe kazi

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaagiza waendesha maghala waache kukata tozo ya upungufu wa uzito wa korosho ghafi zilizohifadhiwa ghalani (unyaufu) kwa wakulima na wanunuzi kwa kuwa tozo hiyo imeshaondolewa na suala hilo halijathibitishwa kitaalamu.

Ametoa agizo hilo leo (Jumamosi, Novemba 28, 2020) katika kikao kati yake na Wakuu wa Mikoa ya Pwani, Lindi, Mtwara na Ruvuma, Makatibu Wakuu wa Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Kilimo, Viwanda na Biashara pamoja Mrajisi wa Ushirika kilichofanyika kwenye ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Mlimwa jijini Dodoma.

Wengine waliohudhuria kikao hicho ni Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Korosho, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Maghala na Waendesha Maghala wote wa mikoa hiyo.

“Mimi niliwaita kuwaambia kuwa wasimamizi wa maghala hampaswi kukata tozo ya unyaufu iwe ni kwa wakulima au wanunuzi kwa sababu tozo hii haina uhalisia na haijathibitishwa na na vyombo husika, hakuna unyaufu unaotokea katika kipindi kifupi cha kuhifadhi korosho, hayo yote ni mawazo yenu tu,” amesema.

Waziri Mkuu amesema: “Hizi Korosho wala hazikai zaidi ya miezi mitatu kama ilivyoelekezwa kwenye kanuni hii, korosho zinazoanza kuvunwa mwezi wa kumi, mnada unaanza mwezi wa kumi uleule na baada ya hapo kuna minada ya kila wiki. Minada ipo mingi, korosho hazikai kutoka siku zinaanguka na kuokotwa mpaka kwenda kuuzwa. Unyaufu mnaoukata, unatokana na nini?”

Hivyo, Waziri Mkuu amemuagiza Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara amuondoe katika nafasi yake, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Maghala, Bw. Odilo Majengo kwa kushindwa kutekeleza maagizo ya Serikali kuhusu kusitisha tozo ya unyaufu katika zao la korosho.

“Mkurugenzi wa Bodi ya Maghala ulidharau maagizo ya Serikali na hatuwezi kuishi hivyo katika Serikali, tulikwambia uache lakini ukaendesha zoezi hili kwa sirisiri huku unasema hayo ni matamko ya kisiasa. Ni kwa nini basi, tubaki na wewe kwenye nafasi hiyo?”

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ametoa siku tano kwa waendesha maghala kuandaa taarifa kuhusu kuelezea ni kiasi gani cha korosho au fedha taslimu ambazo wamechukua kutoka kwa wanunuzi kama tozo ya unyafu kwani atatuma timu maalum kukagua kazi hiyo.

“Na ninyi waendesha maghala, naleta timu huko. Itakuja na kupita kila ghala ili kuona msimu huu wote mmechukua tozo ya unyaufu kiasi gani; kwa hiyo nawapa siku tano kila mmoja akaandae taarifa ya korosho zilizochukuliwa kutokana na unyaufu katika ghala lake, kwa maghala yaliyopo mikoa ya Pwani, Lindi, Mtwara na Ruvuma ili tuone nani amechukua tozo ya unyaufu iwe korosho au fedha taslimu na kwa kiasi gani”.

-ends-