MAJALIWA: TUTAENDELEZA SEKTA YA VIWANDA

*Asema lengo ni kuimarisha uchumi na ajira kwa vijana

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imejipanga kuimarisha sekta ya viwanda nchini ili kukuza uchumi na kumaliza tatizo la upatikanaji wa ajira hususani kwa vijana.

Amesema sekta ya viwanda ndiyo msingi imara wa ukuaji wa uchumi na muarobaini wa tatizo la ajira kwa sababu inaajiri watu wengi wenye kada za aina mbalimbali. Pia amewataka vijana wajishughulishe na shughuli mbalimbali zitakazowapatia kipato cha halali na wasisubiri kuajiriwa tu.

Aliyasema hayo jana jioni (Jumatatu, Septemba 7, 2020) alipohutubia mkutano wa kampeni uliofanyika katika uwanja wa Polisi Tarakea, wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro wakati akimuombea kura Rais Dkt. John Pombe Magufuli na mgombea ubunge wa Jimbo la Rombo Profesa Adolf Mkenda na wagombea udiwani kupitia CCM.

Mheshimiwa Majaliwa alisema Serikali ya Awamu ya Tano imehamasisha wawekezaji kujenga viwanda nchini lengo likiwa ni kukuza uchumi wa Taifa na wananchi kwa ujumla kwa sababu viwanda vinatoa ajira kwa watu wengi kupitia sekta mbalimbali ikiwemo ya kilimo, usafirishaji.

Alisema wananchi wanatakiwa kumchagua Rais Dkt. Magufuli ili aendelee kusimamia mikakati ya kukuza uchumi kupitia sekta ya viwanda ambayo aliianzisha. “Wana-Tarakea mnafahamu mambo makubwa aliyofanya Rais Dkt. Magufuli katika Taifa hili. Nawaomba siku ikifika, tumpigie kura za kutosha.”

Alisema Rais Dkt. Magufuli ameliletea heshima kubwa Taifa ndani na nje ya nchi kutokana na uhodari wake katika kufanya kazi ya kuwaletea maendeleo Watanzania wote bila ya kujali itikadi zao za kisiasa, kidini wala kikabila, hivyo ni vema wakaonesha shukrani zao kwa kumchagua ili aendelee kuiongoza nchi.

Akizungumzia upatikanaji wa nishati ya umeme wilayani Rombo, Mheshimiwa Majaliwa alisema kati ya vijiji 519 vilivyopo Rombo, vijiji vyenye umeme ni 498 na 21 havina umeme. “Vijiji vyote visivyokuwa na umeme vitawekewa umeme kwani tayari mkandarasi yupo Rombo anaendelea na kazi.”

Alisema Rais Dkt. Magufuli anataka kuona kila nyumba ya Mtanzania inapata umeme tena kwa gharama nafuu na ametenga fedha nyingi zitakazotosheleza kusambaza umeme katika vijiji vyote vikiwemo na wilaya ya Rombo. Gharama za kuunganishiwa umeme huo ni sh. 27,000 tu.

Pia Waziri Mkuu amesema wananchi hawatowajibika tena kulipia gharama za nguzo wala fomu za maombi ya kuunganishiwa huduma hiyo ya umeme, kwa sababu tayari gharama hizo zote zimeshabebwa na Serikali yao.

-ends-