WANA-RUANGWA TUMCHAGUE MAGUFULI - MAJALIWA

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewasihi wananchi wa Jimbo la Ruangwa wampigie kura Rais Dkt. John Pombe Magufuli ili aendelee kujenga na kuimarisha huduma mbalimbali za jamii nchini.

Akizungumza wakati alipozindua kampeni za CCM katika jimbo la Ruangwa kwenye kijiji cha Chinongwe leo (Ijumaa, Septemba 11, 2020) Mheshimiwa Majaliwa amesema maendeleo makubwa yaliyofanyika nchini katika kipindi cha kwanza cha utawala wa Rais Dtk. Magufuli kwa kiwango kikubwa yamebuniwa na kusimamiwa kwa karibu na Rais mwenyewe.

Amesema kwa kuwa bado ipo miradi mingi mikubwa iliyoanzishwa na Rais Dkt. Magufuli inayohitaji kukamilishwa, ni vema Watanzania wakampigia kura za kishindo zitakazompa nafasi ya kuliongoza Taifa kwa kipindi cha pili ili aweze kumalizia miradi hiyo na kuanzisha mingine mingi kama ilivyoonyeshwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020-2025.

Aliitaja miradi inayotekelezwa ni ya ujenzi wa Bwawa la Kufua Umeme wa Maji la Nyerere, Reli ya Kiwango cha Kimataifa ya SGR, ujenzi na uboreshaji wa huduma za afya kama vile ujenzi wa vituo vya afya, hospitali za wilaya, mikoa na rufaa pamoja na ujenzi wa miradi ya maji kuwa ni baadhi ya miradi ambayo inamfanya Rais Magufuli astahili kupewa kipindi kingine cha kuiongoza nchi.

Akizungumzia mipango ya Serikali ya kuongeza ajira kwa Watanzania, Mheshimiwa Majaliwa amesema msukumo mkubwa uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kuhamasisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kujenga viwanda vidodo, vya kati na vikubwa ni moja ya mikakati ya makusudi ya kuongeza ajira kwa Watanzania.

“Kiwanda cha samani na kiwanda cha kubangua korosho vinavyojengwa katika kijiji cha Namkonjera wilayani Ruangwa ni moja ya juhudi zinazolenga kuwapatia ajira wananchi wa wilaya hii na Watanzania kwa ujumla.”

Kuhusu utolewaji wa vitambulisho vya wajasiriamali nchini, Mheshimiwa Majaliwa amevitaja vitambulisho hivyo kuwa ni chanzo kingine cha ajira hasa kwa vijana ambao hapo awali walibugudhiwa kwa kuonekana kuwa hawana uhalali wa kufanya biashara katika baadhi ya maeneo hasa ya katikati ya miji na majiji.

Mheshimiwa Majaliwa amesema bugudha kwa vijana hao hivi sasa imekwisha na  sasa wanafanya biashara zao  ambazo ni ajira halali inayotambuliwa na Serikali  ambayo inayowapa kipato cha kuendesha maisha yao na familia zao .

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa aliwashukuru wana-Ruangwa wanachama wa vyama vyote vya siasa kwa kumpitisha bila kupingwa katika jimbo hilo.

Naye mgombea ubunge wa Jimbo la Ndanda, Bw. Cecil Mwambe alipopewa nafasi ya kuzungumza, alisema Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020-2025 imegusa maisha ya wananchi wa Ruangwa kwani imezungumzia maboresho ya zao la korosho pamoja masoko yake.

Bw. Mwambe amewaomba wana-Ruangwa wamchague Rais Dkt. Magufuli na madiwani wa CCM kwani Ilani ya CCM imezingatia maslahi yao hasa kilicho cha mazao ya biashara na chakula.

Mbuge Mstaafu wa Viti Maalum, Bi. Riziki Lulida aliyerejea CCM kutoka Chama cha Wananchi (CUF), aliwaomba wana-Ruangwa wamuunge mkono Rais Dkt. Magufuli kwa kumpa kura nyingi kwani kawafanyia mengi na makubwa wana-Lindi.

-ends-