MAJALIWA: FANYENI TATHMINI KABLA YA KUPIGA KURA

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema katika kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika tarehe 28 Oktoba 2020, wananchi wanatakiwa wafanye tathmini ya hali ilivyokuwa kabla na ilivyo sasa ili waweze kufanya maamuzi sahihi kwani siku zote mwenye macho haambiwi tazama.

“Kwa lugha nyingine, mkifanya tathmini yenu vizuri ninaamini kuwa mtajitokeza kwa wingi siku hiyo kumpigia kura mgombea wa CCM wa nafasi ya urais Rais Dkt. John Pombe Magufuli na Dkt. Hussein Mwinyi, Mgombea wa Urais wa Zanzibar, Wabunge na Madiwani wa CCM kwa kuwa ndiyo wagombea pekee wenye kutosha kwenye nafasi hizo.”

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumamosi, Septemba 12, 2020) wakati akifungua NMB Bima Marathon kwa mwaka 2020. “Ni muhimu kuendelea kudumisha upendo, amani, umoja na mshikamano katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu na hata baada ya uchaguzi mkuu.”

Wakati huo huo, Waziri Mkuu Serikali imewekeza shilingi milioni 75 kwa ajili ya kuongeza vitanda kwa huduma ya matibabu ya tiba kemia (chemotherapy) kutoka vitanda 40 mwaka 2014/15 hadi vitanda 100 kwa sasa.

“Hii imefanya Idadi ya wagonjwa wanaohudumiwa kwa wakati mmoja kuongezeka kutoka wagonjwa 40 hadi wagonjwa 100. Pia muda wa kusubiri tiba kemia kwa wagonjwa imepungua kutoka siku tatu hadi ndani ya masaa 24.”

Amesema sh. bilioni 11.8 zimetumika kukamilisha ujenzi wa “bunkers” na ununuzi na usimikaji wa mashine mbili mpya na za kisasa za tiba mionzi aina ya LINAC na CT simulator. “Uwekezaji huu umewezesha kupunguza rufaa za wagonjwa wa saratani kwenda nje ya nchi kutoka wagonjwa 164 mwaka 2014/2015 hadi wagonjwa 5 mwaka 2019/2020.”

Waziri Mkuu amesema idadi ya wagonjwa wanaotibiwa kwa siku imeongezeka kutoka 170 kwa siku mpaka kufikia 290 kwa siku. Wagonjwa waliotoka nchi jirani ili kupatiwa tiba waliongezeka kutoka wagonjwa 12 mwaka 2014/2015 hadi wagonjwa 53 mwaka 2019/2020. “Aidha, Serikali imeokoa shilingi bilioni 10.4. ambazo zingetumika kama wagonjwa wangepelekwa nje ya nchi.”

“Shilingi milioni 673 zimetumika kununua vyanzo vipya vya mionzi kwa mashine za mionzi ya ndani (Bachtherapy) na mashine maalum 60 za kutolea tiba kemia (infusion pumps). Vifaa hivi vimewezesha utoaji wa huduma bora za uchunguzi na mionzi.”

Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuipongeza benki ya NMB kwa kwenda sambamba na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano, inayoongozwa na Rais Dkt. Magufuli hususan kwenye kupenyeza huduma za kifedha jumuishi kwa jamii, ikiwemo kurahisisha upatikanaji wa bima kupitia mtandao wao mpana wa matawi 226 nchini.

-ends-