SERIKALI ITAENDELEA KUTOA ELIMU MSINGI BILA ADA- MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendeleza mpango wake wa utoaji wa elimu msingi bila ada ili kuhakikisha kila mtoto wa Kitanzania aliyefikia umri wa kwenda shule anapata elimu bila kikwazo chochote.

“Serikali ya Chama cha Mapinduzi imekuwa ikitumia takriban shilingi bilioni 24 kila mwezi kugharamia utoaji wa elimu msingi bila ada na kwamba jambo hilo ni endelevu na   litaboreshwa kwa lengo la kuhakikisha kila mtoto wa Kitanzania anapata elimu bila kikwazo.”

Mheshimiwa Majaliwa ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa ya CCM aliyasema hayo jana jioni (Jumanne, Septemba mosi, 2020) wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye uwanja wa Kwaraa, mjini Babati, Manyara.

Waziri Mkuu ambaye alikuwa mkoani Manyara kumuombea kura Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli na wagombea ubunge na udiwani wa CCM, alisema suala la utoaji elimu msingi bila ada ni miongoni mwa vipaumbele vya Serikali ya Chama cha Mapinduzi.

Alisema ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2020-2025 inasisitiza uimarishwaji wa mfumo wa elimu ili uweze kuzalisha wataalam mahiri zaidi wenye uwezo katika sayansi, teknolojia, ufundi na nyanja nyingine ambao wanaweza kujiajiri na kuajirika mahali popote duniani.

Waziri Mkuu alisema ilani hiyo pia imeweka msisitizo katika upatikanaji wa huduma bora za afya, maji na umeme, hivyo aliwaomba wananchi wa mkoa wa Manyara na Taifa kwa ujumla waichague CCM ili iendelee kuleta maendeleo katika maeneo yao.

Waziri Mkuu alisema katika kipindi cha miaka mitano Watanzania wakiwemo wakazi wa mkoa huo, wamenufaika kutokana na miradi mbalimbali ya kimkakati ambayo imejengwa nchini ikiwemo ya miundombinu, afya, elimu, maji na umeme.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi wa mkoa huo waliahidi kuwachagua wagombea wa CCM akiwemo mgombea wa nafasi ya urais, Dkt John Pombe Magufuli kwa kuwa amefanya mambo mengi ya maendeleo nchini ukiwemo mkoa wao.

-ends-