MAJALIWA: TUTARUDISHA KWA WANANCHI MASHAMBA MAKUBWA YALIYOTELEKEZWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewahakikishia wananchi wa mkoa wa Manyara kwamba Serikali itanyang’anya mashamba makubwa yote ambayo hayajaendelezwa na kuyakabidhi kwao ili wayatumie kukuza uchumi wao.

Mheshimiwa Majaliwa ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM ameyasema hayo leo (Jumanne, Septemba mosi, 2020) wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye uwanja wa Kwaraa, mjini Babati, Manyara.

“Namuombea kura Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, wagombea ubunge na udiwani wa CCM ili Chama Cha Mapinduzi kipate ridhaa ya kuendelea kuongoza Tanzania na kuleta mageuzi makubwa ya kimaendeleo.”

Amewaomba wananchi wa mkoa wa Manyara na Taifa kwa ujumla kuchagua wagombea wa CCM ili kiunde Serikali makini itakayofanya kazi nzuri kwa ajili ya maendeleo ya wananchi ikiwemo kuimarisha ukusanyaji wa mapato ili kuboresha zaidi huduma za jamii kama za afya, elimu, maji na kilimo.

Waziri Mkuu amesema katika kipindi cha miaka mitano, Watanzania wakiwemo wakazi wa mkoa huo wa Manyara wamenufaika na huduma hizo, hivyo hawana budi kuendelea kukiamini Chama cha Mapinduzi na kuchagua wagombea wake ili kiweze kuboresha huduma za jamii nchini.

Akizungumzia kuhusu Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025, Mheshimiwa Majaliwa amesema msisitizo umewekwa katika masuala mbalimbali ya maendeleo ya wananchi ikiwemo uboreshwaji wa huduma za jamii.

Pia, amesema Serikali itadumisha amani na utulivu uliopo nchini, kukuza uchumi, hivyo amewasisitiza wananchi kuhakikisha wanampigia kura nyingi Rais Dkt. John Magufuli ili aweze kuendeleza kazi kubwa aliyoianza ya kuwaletea wananchi maendeleo.

Aidha Mheshimiwa Majaliwa alitumia jukwaa hilo kuvunja makundi ya wanachama wa CCM waliogombea nafasi ya ubunge na kuwaeleza wananchi kuwa Chama cha Mapinduzi kina utaratibu wakati wa mchakato wa ndani, ambapo baada ya uteuzi wa chama wanaCCM wote huungana na kuwa kitu kimoja.

-ends-