CCM PEKEE NDICHO KITAWATUMIKIA BILA UBAGUZI-MAJALIWA

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema CCM pekee ndicho chama cha siasa nchini kinachoweza kuwatumikia Watanzania wote bila ya ubaguzi wa aina yoyote.

 Mheshimiwa Majaliwa amewaomba wananchi wa Mkoa wa Arusha na Watanzania kwa ujumla kuhakikisha wanapiga kura za kutosha kwa Rais John Pombe Magufuli na wagombea wake wote katika ngazi ya ubunge na udiwani nchini.

Aliyasema hayo jana jioni (Jumatano, Septemba 2, 2020) alipozungumza na wananchi kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika katika Uwanja wa Barafu uliopo Kata ya Mto wa Mbu wilayani Monduli, Arusha wakati akimnadi mgombea ubunge wa Jimbo la Monduli, Fredrick Lowassa.

“…CCM ndicho chama pekee chenye uwezo wa kuwahudumia na kuwatumikia Watanzania wote bila ya ubaguzi wa aina yoyote, hivyo nawaomba wananchi wote wanaCCM na wa vyama vingine tuwachague wagombea wa CCM ili aweze kuwaletea maendeleo.”

Alisema wananchi wameshuhudia miradi mikubwa ya maendeleo inayotekelezwa kwenye maeneo yao na amewaomba wampe Rais Dkt. Magufuli ridhaa ya kuongoza miaka mitano mingine ili waweze kuendeleza kazi aliyoianza.

Akizungumza kuhusu miradi ya maendeleo iliyotekelezwa katika wilaya ya Monduli, Mheshimiwa Majaliwa alisema Serikali imetoa zaidi ya sh. bilioni 12 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya uchimbaji wa visima vya maji.

“Mheshimiwa Dkt. Magufuli ana mikakati mizuri inayolenga kumaliza tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo yenye changamoto hiyo nchini vikiwemo vijiji vya wilaya ya Monduli ili kuwawezesha wananchi kupata huduma hiyo.”

Waziri Mkuu alisema Serikali kupitia Kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo kichwani, itahakikisha wananchi katika maeneo yote nchini wanapata huduma ya maji safi na salama karibu na maeneo yao ya makazi.

Alisema mbali na huduma ya maji, pia Serikali imedhamiria kusambaza umeme katika vijiji vyote ambavyo bado havijaunganishiwa nishati hiyo nchini.

“Usambazaji wa umeme vijijini umefikia asilimia 80 na Tanzania ni ya kwanza Barani Afrika kusambaza umeme vijijini.”

Alisema Dkt. John Magufuli anataka kuona kila nyumba ya Mtanzania inapata umeme tena kwa gharama nafuu na ametenga fedha nyingi zitakazotosheleza kusambaza umeme katika vijiji vyote vikiwemo na wilaya ya Monduli. Gharama za kuunganishiwa umeme huo ni sh. 27,000 tu.

Pia Waziri Mkuu amesema wananchi hawatowajibika tena katika kulipia gharama za nguzo wala fomu za maombi ya kuunganishiwa umeme, kwa sababu tayari gharama hizo zote zimeshabebwa na Serikali.

-ends-