MAJALIWA APITA BILA KUPINGWA JIMBO LA RUANGWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa leo Agosti 25, 2020 ametangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kupitia msimamizi wa Uchaguzi Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa kupita bila kupingwa katika nafasi ya Ubunge wa Jimbo la Ruangwa.

Akitangaza matokeo hayo kwenye viwanja vya Ofisi ya Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Frank Chonya amesema mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mheshimiwa Majaliwa ndiye pekee aliyekidhi vigezo vilivyowekwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi na kumfanya apite bila kupingwa.

Akizungumza baada ya kutangazwa kuwa amepita bila kupingwa, Mheshimiwa Majaliwa amesema anawashukuru wanaCCM, viongozi na wanachama wa vyama rafiki na wana Ruangwa kwa ujumla kwa heshima waliyompatia na kumwezesha kupita bila kupingwa.

“Sisi wanaRuangwa wote bila kujali siasa zetu tunajua tulikotoka na wilaya hii tunajua changamoto tulizonazo kwenye wilaya hii lakini tunajua hatua tuliyoifikia sasa hivi na kauli zenu zilikuwa zinaangalia tunakokwenda na uwezekano wa kutatua changamoto huko mbele na ndiyo kwa sababu basi mwakilishi huyu tumpe nafasi nyingine tena aendelee.”

Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ameahidi kuwa ataendelea kuwa mtumishi wa wanaRuangwa, kuendelea kuwa mhudumu wao, kuwa mwakilishi wao katika maeneo mbalimbali na ataendelea kuwasemea.

“Ahadi yangu ni kuwatumikia wote bila kujali vyama vyenu vya siasa, makabila yenu, maeneo mnayotoka wala uwezo wenu.  Ninyi wote nawaona kuwa ni wazazi wangu, mama zangu, baba zangu, kaka zangu, dada zangu lakini pia wadogo zangu”.

Pia Waziri Mkuu amesema kuwa Ruangwa imepata heshima kubwa kutoka kwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli ya kumsaidia kazi ambayo pia iliwezesha kutatua matatizo mbalimbali katika wilaya ya Ruangwa.

-ends-