WAZIRI MKUU AMJULIA HALI MBOWE

 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa leo (Jumanne, Juni 9, 2020) amemtembelea na kumjulia hali Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe ambaye amelazwa katika hospitali ya Ntyuka, jijini Dodoma.

Waziri Mkuu amemuombea kiongozi huyo uponyaji wa haraka wa majeraha aliyoyapata baada ya kuvamiwa na watu ambao bado hawajajulikana wakati akiingia nyumbani kwake jijini Dodoma usiku wa kuamkia leo Juni 9, 2020.

“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za tukio la kuvamiwa kwa Mheshimiwa Mbowe na watu ambao bado hawajajulikana, namuomba Mwenyezi Mungu amjalie apone haraka ili aweze kurejea katika majukumu yake.”

Baadhi ya wabunge wa upinzani waliokuwepo hospitalini hapo na ambao walimpokea Waziri Mkuu ni Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya; Mbunge Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa; Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema.

-ends-