WAZIRI MKUU AZINDUA BANDARI YA KABWE

 

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amezindua bandari ya Kabwe iliyojengwa na kampuni ya Kitanzania ya Sumry’s Enterprises kwa thamani ya sh. bilioni saba.

Ujenzi huo wa bandari ya Kabwe yenye ukubwa wa mita za mraba 10,864, unalenga kuongeza tija katika shughuli za bandari kwenye mwambao wa Ziwa Tanganyika na kupanua fursa za kibiashara.

Waziri Mkuu amezindua bandari hiyo leo (Jumapili, Julai 5, 2020) wakati akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Rukwa. Bandari hiyo imejengwa Kata ya Kabwe, wilayani Nkasi, Rukwa.

Waziri Mkuu ameipongeza kampuni ya Sumry’s Enterprises kwa kujenga vizuri mradi huo. “Rais wetu Dkt. Magufuli amesema Watanzania tunaweza na huyo mkandarasi amedhirisha hilo. Hizi ni jitihada zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli za kuhakikisha maendeleleo yanawafikia wananchi wote.”

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwasisitiza wananchi washirikiane na Serikali kulinda miundombinu ya mradi huo ili iweze kudumu. “Hatuna historia mbaya hapa, endeleeni kudumisha uaminifu ili bandari hii iwe ni mahali salama kwa abiria na mizigo. Bandari hii itaongeza fursa kibiashara kati yetu na nchi jirani.”

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Dkt. Baraka Mdima amesema mradi huo utakuwa chachu ya kukuza uchumi na kuboresha usafiri. “Mradi huu wa bandari utaboresha usafiri wa majini kwa wananchi waishio kandokando ya Ziwa Tanganyika hususani wilaya ya Nkasi na katika kata ya Kabwe na vijiji vinavyoizunguka.”

Amesema mradi umehusisha ujenzi wa gati la kupaki meli lenye uwezo wa kuhudumia meli kubwa za kubeba abiria na mizigo zenye urefu hadi mita 75 na miundombinu mingine ya bandari kama jengo la kupumzikia abiria, majengo ya ofisi, nyumba za kuishi watumishi na eneo la mgahawa.

-ends-