TUONGEZE BIDII ILI TUFIKIE UCHUMI WA JUU - MAJALIWA

 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Watazania waendelee kufanya kazi kwa bidii ili nchi iendelee kukua kiuchumi na kufikia uchumi wa juu kwa kuwa tayari imekuwa ya uchumi wa kati.

“Kama ni mkulima, lima kwa bidi; mtumishi wa umma, fanya kazi kwa bidi; mlio viwandani fanyeni kazi na mamalishe nanyi pikeni sana ili mzunguko wa fedha uweze kuendelea kuwa mkubwa nchini.”

Alitoa kauli hiyo jana (Jumamosi, Julai 4, 2020) alipozindua jengo la ofisi na biashara la Mpanda Plaza lililojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) mjini Mpanda kwa gharama ya sh. bilioni 2.8.

Waziri Mkuu alisema Serikali ilipoingia madarakani pato la mwananchi kwa mwaka lilikuwa dogo na baada ya miaka mitano limeongezeka na kufikia sh. milioni mbili. Alisema ongezeko hilo, limeliwezesha Taifa kuingia katika uchumi wa kati kabla ya matarajio yaliyopendekezwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo.

“Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Tanzania ililenga kuifikisha Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati kupitia sekta ya viwanda ifikapo mwaka 2025 lakini nchi imewezeka kufikia uchumi wa kati mwaka 2020, miaka mitano kabla ya wakati uliotarajiwa,” alisema.

Baada ya kuzindua jengo hilo, Waziri Mkuu alitembelea kijiji cha Kasekese wilayani Tanganyika, mkoani Katavi ambako alizindua msimu wa ununuzi wa pamba. Waziri Mkuu alisema lengo la Serikali ni kurudisha ushirika ili uweze kuwa na tija kwa wakulima, na kuwataka viongozi wa Vyama vya Msingi (AMCOS) wawasaidie wanachama wao.

Waziri Mkuu pia aliwaagiza Maafisa Kilimo wawaelimishe viongozi wa vyama vya ushirika namna bora ya uendeshaji wa vyama hivyo ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Aliwahakikishia wananchi hao kwamba Serikali itaendelea kuwahimia maafisa ugani wafike katika maeneo yao na kuwapa elimu itakayowawezesha kujiongezea tija.

-ends-