WAZIRI MKUU AWAONYA WAKAZI WA MISHAMO NA KATUMBA

*Awataka wasiwe madalali wa kuingiza wahamiaji haramu nchini

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wananchi wanaoishi kwenye makazi ya Mishamo na Katumba wawe waadilifu na wasitumike kama madalali wa kuingiza wahamiaji haramu nchini. 

Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema mkoa wa Katavi umekithiri kwa kuwa na wahamiaji haramu wengi, hivyo amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Juma Homera ashughulikie tatizo hilo.

Ametoa agizo hilo leo (Jumamosi, Julai 4, 2020) alipozindua jengo la ofisi na biashara la Mpanda Plaza lililojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) mjini Mpanda kwa gharama ya sh bilioni 2.8.

“Katavi imetulia lakini haijatengamaa kwa sababu ni kati ya mikoa yenye idadi kubwa ya wahamiaji haramu nchini ambao njia yao wanayotumia kuingilia Katavi, ni makazi ya Katumba na Mishamo.”

Waziri Mkuu amesema Tanzania haijazuia watu wa mataifa mengine kuingia nchini ila inawataka wafuate taratibu zilizowekwa na si kuingia kwa kutumia njia za panya.

Amesema ana majina ya watu zaidi ya 2,000 walioingia Tanzania kwa njia za panya na wamejiingiza katika maeneo mbalimbali, amewataka warudi kwao na wafuate taratibu kabla ya kuja tena nchini.

Akizungumzia kuhusu ujenzi wa jengo la Mpanda Plaza, Waziri Mkuu amelipongeza Shirika la Nyumba la Taifa kwa uwekezaji huo ambao utaliwezesha shirika hilo kujiongezea kipato.

Kadhalika, Waziri Mkuu amelielekeza shirika hilo likajenge majengo ya makazi katika wilaya mpya ili kuwawezesha watumishi na wananchi kuishi kwenye makazi bora.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Dkt. Maulidi Banyani amesema uzinduzi wa jengo hilo la ghorofa tano ni muendelezo wa miradi iliyowekezwa na NHC kwa gharama ya sh. bilioni 7.2 mkoani Katavi.

Dkt. Banyani amesema miradi mingine iliyowekezwa na NHC mkoani Katavi ni pamoja na ujenzi wa nyumba 70 katka eneo la Ilembo na nyumba 24 katika mji wa Inyonga, Mlele.

“Tumejenga nyumba tano za Wakuu wa Idara katika Halmashauri ya Wilaya ya Mlele, nyumba 24 za walimu katika shule ya msingi Kakuni na nyumba sita shule ya Kibaoni katika Halmashauri ya Mpimbwe.”

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, alisema miongoni mwa changamoto zilizokuwa zinaukabili mkoa huo ni majangili ambapo waliendesha operesheni na kufanikiwa kukamata silaha 100.

Alisema kwa sasa wananchi wanaendelea kufanya kazi na kwamba ukusanyaji wa mapato umeongeza kutoka asilimia 76 mwaka 2019 hadi kufikia asilimia 97 mwaka huu.

Mkuu huyo wa mkoa ameongeza kuwa mbali na kuboresha ukusanyaji wa mapato, pia wameimarisha upatikanaji huduma za afya hususani kwa mama na mtoto.

-ends-