MAJALIWA: MSIKATISHWE TAMAA BEI YA MAZAO KUSHUKA

*Awataka wakulima waendelee na kilimo katika kipindi hiki cha mpito    

 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wakulima wa mazao ya biashara wakiwemo wa ufuta waendelee na kilimo na kwamba tatizo la kushuka bei lililotokea kwenye msimu huu, lisiwakatishe tamaa kwani litakwisha.

Amesema Serikali inaendelea kulifanyia kazi suala hilo na kwamba bei ya mazao nchini itaimarika baada ya kuongezeka kwa ujenzi wa viwanda vya kuchakata mazao nchini, ambapo wakulima watakuwa na masoko na uhakika na pia nchi itauza bidhaa zitokanazo na mazao hayo na si malighafi.

Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo jana jioni (Jumatano, Juni 24, 2020) wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Kata ya Nachingwea wilayani Ruangwa, mkoani Lindi na akawasihi wakulima wasiache kulima.

“Kushuka kwa bei ya ufuta kusiwakatishe tamaa na kuwafanya muache kulima kwa sababu bei haijashuka kwa zao hilo tu bali na mazao mengine kama chai, tumbaku, kahawa na chai. Hali hii imetokana na mlipuko wa ugonjwa wa COVID-19 ambao umeikumba dunia.”

Waziri Mkuu ambaye yuko Ruangwa kwenye ziara ya kikazi, aliongeza kuwa Serikali inatarajia kwamba kadri ugonjwa wa COVID-19 unavyoendelea kupungua katika mataifa mbalimbali duniani, bei ya mazao nayo itaimarika, hivyo wakulima waendelee kuwa na subira katika kipindi hiki ambacho ni cha mpito.

Alisema moja ya msisitizo wa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli ni kuboresha sekta ya kilimo ili iweze kujitosheleza kwa chakula. “Suala la bei ya mazao linapangwa na wanunuzi Serikali inasimamia tu.”

Pia, Waziri Mkuu ameendelea kuwashukuru wananchi wa wilaya hiyo kwa ushirikiano mkubwa waliompatia katika kipindi chote cha miaka mitano na amewasisitiza waendelee na ushirikiano huo kwa ajili ya maendeleo ya wilaya yao na Taifa kwa ujumla.

-ends-