OFISI YA WAZIRI MKUU YAKIDHI VIWANGO VYA OSHA

MAMLAKA ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) imetoa cheti kwa Ofisi ya Binafsi ya Waziri Mkuu baada ya kufanyia ukaguzi katika maeneo yote ya ofisi hiyo na kuonesha kuwa yamekidhi viwango.

Cheti hicho kimetolewa jana jioni (Jumamosi, Februari mosi, 2020) na Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda na kupokelewa na Katibu wa Waziri Mkuu, Bw. Raymond Gowelle.

Akikabidhi cheti hicho, Bi Khadija aliipongeza Ofisi hiyo kwa kuonesha mfano wa utekelezaji wa sheria, ambapo amezishauri ofisi nyingine za umma ziige mfano huo.

“Ofisi Binafsi ya Waziri Mkuu wameonesha mfano wa kuigwa kwa utekelezaji wa sheria, kwani walituita tukaja kufanya ukaguzi na tukatoa maelekezo ya namna ya kuboresha baadhi ya maeneo na tayari wamerekebisha.”

Alisema baada ya kutekeleza maelekezo hayo, suala lililokuwa limebakia ni upimaji wa afya kwa wafanyakazi pamoja na kutoa mafunzo ya huduma ya kwanza ambayo yalifanyika jana.

Mtendaji huo alisema ni muhimu kwa ofisi zote kuzingatia sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi kwa kuwa hakuna aliye juu ya sheria.

Baada ya kukamilisha zoezi la upimaji wa afya na mafunzo ya OSHA, pia watumishi wa Ofisi Binafsi ya Waziri Mkuu walikumbushwa namna bora ya kufanya kazi kwa uadilifu. Mafunzo yalitolewa na watalaamu kutoka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Watumishi hao waliushukuru uongozi wa ofisi kwa kuandaa zoezi la upimaji wa afya ambalo lilikuwa na mwitikio mkubwa, mafunzo ya huduma ya kwanza pamoja na kukumbushwa kuhusu uadilifu na matumizi ya madaraka na ofisi kwa manufaa ya umma.

 -ends-