WAZIRI MKUU AWATAKA WATANZANIA WALINDE AMANI

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Watanzania waendelee kudumisha amani na utulivu uliopo nchini kwa kuishi kwa umoja na upendo ili kujiletea maendeleo kuanzia mtu binafsi hadi jamii nzima kwa ujumla.

Ametoa wito huo leo (Ijumaa, Novemba 08, 2019) wakati akitoa salamu kwa waumini wa dini ya Kiislamu aliposhiriki sala ya Ijumaa kwenye msikiti wa Nunge jijini Dodoma.

“Waislamu wenzangu pamoja na jamii nzima hatuna budi kuendelea kutunza amani iliyopo kwa maombi, hasa kwa kuwaombea viongozi wetu wa kitaifa kuongoza nchi kwa hekima na busara katika kuimarisha umoja na upendo uliopo nchini.”

Waziri Mkuu alieleza kuwa ni muhimu jamii ikatambua mchango wa dini katika Taifa kwa kuzingatia kuwa ndicho chombo chenye nguvu kuleta misingi myema kupitia mawaidha na mafundisho yanatolewa kwa makundi yote hususan kundi la vijana ambalo linategemewa katika nguvu kazi ya Taifa.

Alisema dini zina mchango mkubwa katika kuimarisha uwepo wa amani ambayo inatoa fursa kwa jamii kushiriki vema kwenye shughuli za uzalishaji mali za kila siku, hivyo jamii haina budi kuzingatia yale wanayofundishwa katika dini zao ili kudumisha umoja, mshikamano na upendo.

“Tuendelee kuungana pamoja bila kujali tofauti za imani zetu na hii itasaidia kuwa na maendeleo endelevu na kuendelea kuwaombea viongozi wote nchini wawe na afya njema.”

Aidha pamoja na hayo aliliasa kundi la vijana ambalo ni nguvu kazi ya Taifa, liendelee kutumia nafasi zao kwa kujishughulisha kwa bidii katika kazi za uzalishaji na kuondokana na makundi yasiyofaa.

Kwa upande wake, mtoa hutba katika ibada hiyo, Ustaadh Salim Omari alimshukuru Waziri Mkuu na akatumia nafasi hiyo kuwakumbusha Watanzania waendelee kufanya kazi kwa bidii ili waondokane na magenge ya mitaani yanayoshiriki katika mambo maovu ikiwemo uhalifu unaohatarisha amani na utulivu.

“Vijana lazima mfanye kazi kwa bidii na muendelee kumtumikia Mungu anayewapa uhai bila kusahau ibada; na hii itasaidia kuondokana na makundi ya machokoraa ambao tunaamini wangejifunza masuala ya elimu ya Mungu ingetusaidia tuwe na Taifa lenye viongozi wazuri wa kesho,” alisisitiza Ustaadh Omari.

Waziri Mkuu alisema anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika sherehe za maulid ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W) kwa niaba ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Pombe Magufuli zitakazofanyika kitaifa mkoani Mwanza Novemba 9, mwaka huu.

Aidha, alisema kwa mkoa wa Dodoma, wanatarajia kuadhimisha kwa kuwa na maandamano yatakayoanzia katika viwanja vya Nyerere Squere hadi msikiti wa Gadaffi.

-ends-