BIASHARA KATI YA TANZANIA NA URUSI IRATIBIWE-MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwwa ameutaka ubalozi wa Tanzania nchini Urusi uratibu mipango ya wafanyabiashara wa Urusi wanaokusudia kuja kuwekeza nchini kwa kuwaunganisha na taasisi na wizara husika ili waweze kuwekeza mitaji yao kwa kuzingatia maslahi ya Taifa.

Ametoa agizo hilo jana (Alhamisi, Oktoba 24, 2019) baada ya kugundua uwepo wa wafanyabiashara wengi wa Urusi wenye nia ya kuja Tanzania kuangalia maeneo ya kuwekeza na kutafuta wafanyabiashara wa Kitanzania watakaoungana nao kwenye uwekezaji wanaokusudia kuufanya.

“Tayari miadi imekwishawekwa ya kuwakaribisha wawekezaji wa Urusi waje Tanzania kutokana ushawishi wangu pamoja na ushawishi wa wafanyabiashara wa Tanzania. Nisingependa wafanyabiashara hao wasumbuliwe au kukatishwa tamaa katika kutimiza nia yao hiyo,” Waziri Mkuu alisisitiza.

Alisema mkutano baina ya Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka Mataifa ya Afrika na Urusi uliomalizika jana, Oktoba 24, 2019 ulilenga kujenga uhusiano mzuri zaidi katika nyanja mbalimbali hususani za kiuchumi.

Akizungumza baada kumalizika mkutano huo kwenye ukumbi wa Olympic Park wa Sochi, Urusi, Waziri Mkuu alisema Urusi imeutumia mkutano huo kueleza bayana maeneo ambayo wako tayari kushirikiana na Afrika katika kuwekeza kwa faida ya pande zote mbili.

Waziri Mkuu aliyataja maeneo hayo kuwa ni pamoja na uuzaji wa zana za kilimo kama vile matrekta, sekta ya mafuta na gesi pamoja na madini, ujenzi wa miundombinu hasa reli, masuala ya elimu hasa utoaji wa nafasi za mafunzo nchini humo.

Alisema kwa upande wake, Tanzania imejinadi vizuri kwani alifanya mazungumzo na viongozi wa makampuni ya Kirusi zaidi ya nane ili kuyashawishi yawekeze nchini na yote yalikubali kuja Tanzania mapema iwezekanavyo.

“Viongozi wa makapuni yote niliyopata nafasi ya kuzungumza nao wamesema wako tayari kuja nchini ili waweze kufanya mazungumzo na Serikali pamoja na wafanyabiashara wazalendo ambao wako tayari kuungana na wafanyabiashara hao kuwekeza nchini Tanzania.”

Waziri Mkuu alisema viongozi hao walimueleza maeneo ambayo wao wanaamini kuwa wanafanya vizuri na wangependa kupata kibali cha kuwekeza Tanzania baada ya mazungumzo yao na Serikali. Pia walieleza ni kwa namna gani Taifa litanufaika na uwekezaji wao.

Alisema, tayari wafanyabiashara binafsi 18 wa Tanzania walijitokeza kushiriki mkutano huo na walifanya kazi kubwa na nzuri ya kuwahabarisha wenzao wa Urusi kuhusu mazingira mazuri ya kuwekeza yaliyopo nchini hasa baada ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kuondoa kero, kanuni na taratibu zilizokuwa zikiyafanya mazingira ya uwekezaji yawe magumu.

Awali, akizungumza kwenye mkutano baina ya Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka mataifa ya Afrika na Urusi, Waziri Mkuu alisema kwa sasa Tanzania ni nchi sahihi kwa uwekezaji kwa wanaotaka kuwekeza barani Afrika kwani imedhamiria kukuza uchumi wake na kufikia wa kati ifikapo 2025 kwa kupitia sekta ya viwanda. Pia ni nchi yenye amani na utulivu.

“Nchi yetu imejaliwa kuwa na maliasili nyingi ambazo vilevile ni malighafi kwa viwanda kama vile mazao ya kilimo, misitu, bahari, maziwa, madini na mbuga za wanyama ambazo ni kivutio cha watalii,” alifafanua Waziri Mkuu.

Leo (Ijumaa, Oktoba 25, 2019), Mheshimiwa Majaliwa ataondoka nchini Urusi kwenda Azerbaijan ambako pia atamwakilisha Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwenye mkutano wa siku mbili wa nchi zisizofungamana na upande wowote.

-ends-