AFRIKA NI MDAU MUHIMU KWA MAENDELEO YA UCHUMI WA DUNIA - PUTIN

RAIS wa Urusi, Vladimir Putin amefungua Kongamano la Biashara baina ya Urusi na Afrika (Russia-Africa Business Forum) na kusema kuwa bara la Afrika ni mdau muhimu katika maendeleo ya uchumi wa dunia na ni kivutio kikubwa kwa wafanyabiashara wa Urusi.

Ameyasema hayo leo (Jumatano, Oktoba 23, 2019) wakati akihutubia mkutano huo uliofanyika kwenye ukumbi wa Kituo cha Olympic Park katika mji wa Sochi, Urusi. Rais Putin amesema takwimu zilizotolewa na watalaamu wa masuala ya uchumi zinaonyesha kwamba pato la Afrika (GDP) litafikia dola trilioni 29 ifikapo mwaka 2050.

Amesema biashara kati ya Urusi na Afrika imeongezeka maradufu katika kipindi cha miaka mitano iliyopita na kufikia dola za Marekani bilioni 20. Amesema nchi yake inaunga mkono wazo la kuanzishwa eneo huru la biashara barani Afrika ukiwa ni mkakati wa Umoja wa Afrika (AU) na kwamba itatoa ushirikiano ili kufanikisha wazo hilo.

Kadhalika, Rais Putin ameongeza kuwa nchi yake inatekeleza kwa vitendo mpango wa kuzifutia madeni nchi za Afrika na hadi sasa imeshafuta madeni ya zaidi ya dola za Marekani bilioni 20. Amesema utoaji wa mafunzo mbalimbali ya kitaaluma ni sehemu ya utamaduni wa ushirikiano kati ya Urusi na Afrika. “Hadi katikati ya miaka ya 80, nchi yetu imejenga taasisi zipatazo 100 za mafunzo mbalimbali barani Afrika na watu 500,000 wamepata mafunzo katika taasisi hizo.”

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameshiriki mkutano huo akimwakilisha Rais John Pombe Magufuli. Pamoja naye idadi kubwa ya Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka Afrika wanahudhuria mkutano huo.

Miongozi mwa viongozi hao ni Rais Yoweli Museveni wa Uganda, Rais Paul Kagame wa Rwanda, Rais wa Misri na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, Abdel Fattah al Sissi, Rais wa Afrika ya Kusini, Cyril Ramaphosa, Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa na Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi.

Kesho (Alhamisi, Oktobba 24, 2019) Waziri Mkuu anatarajia kushiriki mkutano baina ya Urusi na Wakuu wa Nchi na Serikali wa Bara la Afrika.

-ends-