HOTUBA YA MHESHIMIWA MIZENGO P. PINDA (MB) WAZIRI MKUU WAKATI WA KUFUNGUA KONGAMANO LA VIJANA WA VYUO VIKUU VYA DODOMA KATIKA UKUMBI WA AFRICAN DREAM – DODOMA, TAREHE 25 JUNI 2010
Ndugu Mwenyekiti wa Kongamano;
Waheshimiwa Mawaziri;
Waheshimiwa Wabunge;
Jumuiya ya Wanafunzi wa Vyuo Vikuu;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana.
Utangulizi:
Kama ilivyo ada, naomba tumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa Afya Njema na uhai uliotuwezesha kukutana hapa katika Kongamano la Vijana wa Vyuo Vikuu vya Dodoma. Nawakaribisha nyote mlioalikwa kwenye Kongamano hili.
Kwa njia ya pekee kabisa, niwasilishe kwenu nyote na hasa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu vya Dodoma SALAAM kutoka kwa Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wanafunzi mliokusanyika hapa mnafahamu kuwa mlikuwa mmemwomba Mheshimiwa Rais kuja kuwafungulia Kongamano hili. Kutokana na majukumu mengine ya Kitaifa, Mheshimiwa Rais ameshindwa kuwa nanyi hapa. Hata hivyo, kutokana na umuhimu wa Kongamano hili, Mheshimiwa Rais amenichagua kumwakilisha katika ufunguzi huu.
Ndugu Mwenyekiti,
Mheshimiwa Rais alipopata mwaliko wenu alikubali na aliposhindwa kuhudhuria alinituma kumwakilisha kwa sababu kuu zifuatazo:
Moja: Kupata fursa ya pekee ya kukutana na kuongea na Vijana wetu wa Vyuo Vikuu walioko hapa Dodoma na kwingineko Nchini na kuwahamasisha kupenda kuweka nguvu zao pamoja kwenye masomo na katika kuchangia mawazo kuhusu Maendeleo ya Nchi yetu.
Pili: Sisi kama Viongozi katika Serikali, tunao wajibu mkubwa wa kuandaa mazingira bora ya kuwasaidia Vijana wetu katika ngazi zote za elimu kuanzia Elimu ya Msingi, Sekondari, Vyuo na Vyuo Vikuu kutimiza malengo yao kimasomo. Lengo ni kuwawezesha kujitegemea, kukabiliana na mazingira magumu ya Maisha na kushindana katika Soko la Ajira na nafasi ya kujua mazingira ya Dunia tunayoishi leo;
Tatu: Kuwahamasisha Watanzania wa rika zote kupenda kusoma hadi kupata Elimu ya Juu ambayo inawasaidia kuchanganua masuala mbalimbali miongoni mwa Jamii; na
Nne: Kuwawezesha Vijana wote kushiriki katika shughuli za Taifa za Uchumi, Jamii, Utamaduni na Siasa.
Ndugu Wajumbe,
Mkusanyiko huu unatoa hamasa na uhusiano mzuri na muhimu katika kujenga umoja, upendo na mshikamano sio kwa Vijana wa Vyuo Vikuu tu pekee yao bali kwa Jamii ya Watanzania wote kwa ujumla.
Nitumie fursa hii basi kuwapongeza wote waliobuni kuwepo kwa Kongamano hili. Vilevile, nawapongeza wale wote walioshiriki katika kufanikisha kuwepo kwa Kongamano hili. Pongezi za pekee nazitoa kwa Kamati ya Maandalizi ambayo imefanya kazi kubwa kuhakikisha Kongamano hili linafanyika. Hii ni ishara kwamba Vijana wana uwezo mkubwa wa kubuni, kupanga na kufanikisha mambo. Hii inathibitisha kuwa Nchi yetu ina Vijana makini ambao wameiva tayari kwa majukumu ya Kiuongozi.
Umuhimu wa Elimu
Ndugu Wajumbe,
Mustakabali wa Maendeleo ya Taifa lolote yanategemea sana elimu iliyojengeka kwa Wananchi wake. Kongamano hili limekuja wakati muafaka ambapo Taifa pamoja na Vipaumbele vingine linaelekeza nguvu zake zote katika Elimu. Vilevile, Kongamano hili ni muhimu sana kwa maendeleo ya Elimu hapa Nchini, kwani litazidi kutoa mwanga kwa Changamoto zinazotukabili katika kufikia malengo tuliyojiwekea ya kuboresha Elimu katika ngazi zote.
Ni kweli kwamba wengi wa Wananchi wetu wanatambua umuhimu wa elimu katika Jamii ya sasa. Ni kwa kutambua hivyo, ndio maana ninyi mmeweza kubuni kuwepo kwa Kongamano hili na kukusanyika hapa kujadili mada mbalimbali ambazo kwa ujumla wake zinaonyesha umuhimu wa maendeleo ya Elimu na Maendeleo ya Nchi yetu kwa ujumla. Aidha, mmekusanyika hapa kuonyesha umuhimu wa Vijana katika uundaji na utekelezaji wa Sera mbalimbali za Kitaifa, Kikanda na Kimataifa ili kuleta maendeleo yenye tija kwa Jamii nzima.
Ndugu Wajumbe,
Mjadala utakaofanyika kwa siku mbili zijazo pamoja na mambo mengine, utatuwezesha kupata mawazo ambayo ninaamini yatarutubisha na kuanzisha Ari Mpya kwa wale Watanzania wachache ambao bado hawajaweka mkazo wa kutosha katika Elimu kama msingi wa Maendeleo. Mategemeo yangu ni kwamba Kongamano hili litajaribu kuchokoza mawazo kutoka kwa Washiriki ili kupata mbinu za kusisitiza umuhimu wa Elimu katika kuleta maendeleo pamoja na kusisitiza umuhimu wa Vijana kushiriki katika uzalishaji, Uongozi na Ustawi wa Jamii.
Lengo ni kushirikisha Vijana kwa pamoja katika upatikanaji wa mambo mengine yanayohusu Elimu kwa ajili ya kujenga Jamii iliyoelimika na hivyo kuleta maendeleo Nchini.
Umuhimu wa Vijana katika Maendeleo ya Nchi
Ndugu Wajumbe,
Serikali inatambua umuhimu wa Vijana wasomi katika Maendeleo ya Taifa. Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika kuzungumzia umuhimu wa Elimu kwa Vijana aliwahi kusema:
“Njia bora ya kujenga Taifa imara ni kuwekeza katika Elimu kwa Vijana wetu…………”
Kwa maana hiyo, maendeleo ya Nchi miongoni mwa Jamii yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na kiwango cha Uwekezaji katika Elimu. Ni vema Jamii iwekeze kwa kiwango kikubwa katika Sekta ya Elimu ili kujikwamua na Umaskini. Kuwekeza katika Elimu ni mkakati wa muda mrefu unaohitaji dhamira, subira, uvumilivu, kujinyima, kujitolea na kwamba matokeo yake huonekana baada ya muda mrefu wa uwekezaji.
Aidha, Mwandishi wa Vitabu, Mashairi na Mwanasiasa wa Kiingereza, Joseph Addison alisema na namnukuu kwa Kiingereza:
“Education is a companion which no misfortune can depress, no crime can destroy, no enemy can alienate, no despotism can enslave. …….. It guides virtue and it gives at once grace …. Without it, what is man? A splendid slave, a reasoning savage”. Mwisho wa kunukuu.
Ukweli ni kwamba, Elimu ndiyo utajiri usioweza kuibiwa au kuharibika kirahisi. Mtu akipata elimu anakuwa amepata rasilimali ya maisha.
Juhudi za Serikali katika Elimu
Ndugu Wajumbe,
Serikali kwa kushirikiana na Sekta Binafsi imefanya juhudi kubwa ya kuendeleza elimu Nchini kwenye ngazi zote. Hii ni kuanzia Elimu ya Chekechea, Msingi, Sekondari na Elimu ya Juu. Katika Elimu ya Juu, hadi sasa Tanzania ina Vyuo Vikuu 33, ambapo 21 kati ya hivyo ni Vyuo Vikuu Binafsi ambavyo hadi Juni 2009 vilikuwa vimedahili Wanafunzi 95,525. Idadi hii ni Asilimia 57 ya Wanafunzi 166,310 waliokuwa katika Vyuo Vikuu Nchini. Takwimu za Mwaka 2010 zinatarajiwa kuwa ni za juu zaidi.
Kwa kutambua umuhimu wa Elimu, Serikali ya Awamu ya Nne imekuwa ikitoa kipaumbele kwa Sekta ya Elimu ili kuwezesha Vijana wengi kupata Elimu kuanzia ngazi ya Shule za msingi hadi Vyuo Vikuu. Kwa mfano, katika Bajeti ya Serikali, Elimu imepewa kipaumbele katika miaka mitano iliyopita ikilinganishwa na Sekta nyingine kama ifuatavyo:
Mwaka 2006/2007
Shilingi Bilioni Asilimia
Elimu 891.2 18.4
Miundombinu 497.8 10.3
Afya 427.4 8.8
Nishati 220.2 4.5
Kilimo 195.5 4.0
Maji 189.9 3.9
Mwaka 2007/2008
Shilingi Bilioni Asilimia
Elimu 1,086 17.9
Miundombinu 777.2 12.8
Afya 589.9 9.7
Kilimo 379.0 6.2
Nishati 354.0 5.8
Maji 309.1 5.1
Mwaka 2008/2009
Shilingi Bilioni Asilimia
Elimu 1,430.4 19.8
Miundombinu 973.3 13.5
Afya 803.8 11.1
Kilimo 513.0 7.1
Nishati 378.8 5.2
Maji 231.6 3.2
Mwaka 2009/2010
Shilingi Bilioni Asilimia
Elimu 1,743.9 18.3
Miundombinu 1,096.6 11.5
Afya 963.0 10.4
Kilimo 669.9 7.0
Maji 347.3 3.6
Nishati 285.5 3.0
Mwaka 2010/2011
Shilingi Bilioni Asilimia
Elimu 2,045.3 17.6
Miundombinu 1,503.1 13.0
Afya 1,205.9 10.4
Kilimo 903.8 7.8
Maji 397.6 3.4
Nishati 327.2 2.8
Takwimu hizi zinaonyesha kuwa tangu mwaka 2006/2007 Sekta ya Elimu imekuwa ikitengewa sehemu kubwa ya Bajeti ya Serikali ya zaidi ya Asilimia 17 kila mwaka. Hii inaonyesha kuwa Serikali imedhamiria kuimarisha Sekta ya Elimu Nchini ili Vijana wengi wa Tanzania waweze kuelimika na kuweza kupambana na umaskini.
Aidha, Tanzania ni moja ya Nchi chache Duniani zenye kutoa Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu. Kutokana na ukweli huo, idadi ya Wanafunzi wanaopata Mikopo Nchini imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka sambamba na kiwango cha mikopo inayotolewa. Wanafunzi waliopata Mikopo kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita ni kama ifuatavyo:
Mwaka 2005/2006 Wanafunzi 42,729 Shilingi Bilioni 56.1
Mwaka 2006/2007 Wanafunzi 47,554 Shilingi Bilioni 76.1
Mwaka 2007/2008 Wanafunzi 55,687 Shilingi Bilioni 122.5
Mwaka 2008/2009 Wanafunzi 58,798 Shilingi Bilioni 139.7
Mwaka 2009/2010 Wanafunzi 69,560 Shilingi Bilioni 197.3
Ndugu Wajumbe,
Ni dhahiri kwamba, Serikali imejitahidi kubuni na kutekeleza mipango mbalimbali ya Elimu kwa kushirikiana na Wadau wa Elimu zikiwemo Taasisi za Kimataifa, Wabia katika Maendeleo na Wananchi kwa jumla kwa lengo la kutoa Elimu Bora kwa Watu wote. Changamoto kubwa iliyopo katika Sekta ya Elimu ni kuinua kiwango cha ubora wa Elimu kinachotolewa, kuboresha mazingira ya utoaji Elimu, kuongeza udahili wa Wanafunzi katika ngazi zote za Elimu kwa kuzingatia usawa wa Kijinsia katika upatikanaji wake. Aidha, Sekta ya Elimu bado inakabiliwa na Changamoto mbalimbali zikiwemo uhaba wa Walimu, Maabara, Nyumba za Walimu, Hosteli na upungufu wa vifaa vya kujifunzia.
Ili kukabiliana na changamoto hizo, katika kipindi cha Bajeti ya mwaka 2010/2011, Serikali itaongeza ajira ya Walimu wapya katika Shule za Msingi na Sekondari. Vilevile, itaongeza vifaa vya kujifunzia na ujenzi wa Maabara na kuimarisha Miundombinu ya Elimu katika ngazi zote.
Maandalizi ya Vijana kama Nguvukazi ya Taifa
Ndugu Wajumbe,
Tumekusanyika hapa leo tukijua umuhimu Vijana katika Taifa. Vijana ni nguvu kazi ya Taifa letu. Ninyi ni Vijana wasomi, Vijana ambao katika muda wa miaka mitatu ijayo wote mtakuwa mmefuzu katika masomo yenu. Kwa maana hiyo, inatarajiwa kuwa ninyi ndiyo mtakuwa Wataalam na Washauri wa Viongozi wa Nchi hii katika kipindi cha miaka kati ya 30 na 40 ijayo. Aidha, ninyi ndio Viongozi watarajiwa wa Nchi hii. Mnachokifanya hapa katika Vyuo Vikuu vya UDOM, St. John’s, Mipango na CBE ni kujenga uwezo na utaalam ili kuweza kumudu majukumu yenu kama Wataalam, Washauri na Wachapa kazi katika siku zijazo. Ninyi ndiyo “Think Tank” ya kutoa mwelekeo wa Nchi yetu kwa miaka hiyo 30 hadi 40 ijayo. Napenda kutumia fursa hii kuwakumbusha umuhimu wa kutumia fursa hiyo mliyonayo katika Vyuo Vikuu kujiandaa vizuri ili muwe Wachapa Kazi wazuri wenye kutoa ushauri mzuri kwa mustakabali wa Nchi yetu.
Ninakumbuka wakati wa Mkutano wa World Economic Forum, uliofanyika Mwezi Mei 2010 pale Dar es Salaam, kulikuwepo pia na Mkutano wa Vijana kutoka Ulimwenguni kote uliojulikana kama The Young Global Leaders Forum chini ya Mtoto wa Mfalme wa Jordan H. M. Queen Rania Al Abdullah ambao ulitumika kama jukwaa la Vijana kujiandaa kwa ajili ya kuwa Viongozi wa baadaye. Mkutano ule hautofautiani sana na ubunifu wenu wa kukutana leo katika Kongamano hili. Mnachokifanya ni sawa kabisa na hilo la Young Global Leadership Forum. Hili ni jambo zuri ambalo linatoa matumaini kwa ninyi Vijana wetu kujiandaa na jinsi mtakavyotumikia Nchi yenu kwa siku zijazo.
Ndugu Wajumbe,
Kiko kipindi kimoja katika moja ya Vituo vya Television kinaitwa “Ze Komedi”. Wale rafiki zangu wana sehemu wanacheza wanaiita “Enzi za Mwalimu”. Sisi tuliosoma zamani huwa kila wakati tunaangalia sehemu hiyo kuona hivi leo wanasema nini. “Enzi za Mwalimu”, Kwanza tulianza na masharti ya kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kabla ya kwenda Chuo Kikuu. Jeshini kule tulifanya kazi zote zikiwemo za Kilimo, Ujenzi na kazi za kutoa huduma mbalimbali za Elimu kwa waliokuwa Walimu na Afya kwa waliokuwa Waganga na Wauguzi. Lakini kubwa zaidi, kipindi hiki cha JKT kilitumika katika kujenga umoja, upendo na mshikamano kwa Vijana wote na kwa jinsia zote. Pamoja na kwamba JKT hapakuwa na malipo, ilikuwa sehemu ya kujenga uzalendo wa Vijana kuipenda Nchi yao. Baada ya JKT tulijiunga na Chuo Kikuu ambapo tulipata Elimu Chuo Kikuu bure lakini kwa Mkataba kwamba tutaifanyia kazi Serikali kwa mshahara utakaopangwa na Serikali kwa miaka mitano. Aidha, ilikuwa ni sehemu ya masharti kwamba tuna wajibu wa kuwafanyia Wananchi kazi kwa kipindi hicho kama sehemu ya kutambua rasilimali zilizotumika kwa njia ya kuleta maendeleo Nchini. Wakati tunasoma tulijiandaa vizuri tukijua fika kwamba tuna wajibu wa kufanya na kurejesha kitu kwa Nchi yetu. Kwa hiyo, wengi wetu tulifanya kazi kwa moyo wote kuiletea Nchi yetu maendeleo.
Kulikuwa na maneno ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambayo wengi wetu tuliyajua kwa kuyakariri kichwani kuhusu fursa ya kupata elimu wakati huo na naomba ninukuu kwa Kiingereza alisema:
“Those who receive this privilege therefore, have a duty to repay the sacrifice which others have made. They are like the man who has been given all the food available in a starving village in order that he might have strength to bring supplies back from a distant place. If he takes this food and does not bring help to his brothers, he is a traitor. Similarly, if any of the young men and women who are given an education by the people of this Republic adopt attitudes of superiority, or fail to use their knowledge to help the development of this country, then they are betraying our union” Mwisho wa kunukuu.
Vijana mliopo katika Vyuo Vikuu, mnayo nafasi na wajibu wa kujiandaa vizuri katika kulitumikia Taifa lenu katika siku zijazo. Rasilimali zilizopo na zinazotumika katika kutoa elimu sasa, ni deni la kiwajibu kwenu kwa Watanzania wa kizazi kilichotangulia na kizazi kitakachokuja nyuma. Leo mnajadili umuhimu wenu katika maendeleo ya Taifa hili. Maana yake ni kwamba mnatambua umuhimu wenu wa kuwepo Vyuoni sasa na majukumu yaliyopo mbele yenu baada ya kukamilisha mafunzo yenu. Ni dhahiri kwamba kuna wajibu wa kufanya baada ya kumaliza masomo. Hatutarajii kuona Watu ambao wanamaliza kusoma na kupata Shahada zao, wakaamua kukaa tu baada ya kuhitimu, bila ya kuchangia chochote kwa Uchumi wa Taifa. Tunachotegemea Wanafunzi walioko Vyuoni watajiandaa vizuri ili wawe tayari kuchang |