Home | Speech
Speech
Speeches

Hotuba ya Shukrani kwa Wabunge kabla ya Mkutano wa Ishirini wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Kuvunjwa na Mheshimiwa Rais, Ukumbi wa Bunge, Dodoma, 15 Julai 2010...

Hotuba ya Mheshimiwa Mizengo P. Pinda (Mb) Waziri Mkuu Wakati wa Kufungua Kongamano la Vijana wa Vyuo Vikuu vya Dodoma katika Ukumbi wa African Dreams – Dodoma, tarehe 25 Juni 2010...

More Speeches
Recently Documents

kk Quotes

kama Bunge, lakini mmoja mmoja kama watumishi wa umma, tunao wajibu mkubwa sana wa kuishi na kutenda kwa mfano. Tujiepushe na tamaa zinazoweza kuliingizia Taifa hili hasara kubwa.

Kauli ya Waziri Mkuu kuhitimisha mjadala wa Richmond,
Mkutano wa 18 wa Bunge, Februari 10, 2010
More Quotes
Videos
Photo Gallery

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mtaifa, Ban Ki-Moon (katikati) akihutubia katika Mkutano Mkuu wa Shirika la Mawasiliano la Kimataifa (ITU) jijini Geneva Oktoba 6, 2009. Kulia ni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na kushoto ni Katibu Mkuu wa ITU, Dr, Hamadoun Toure
More Photos
Documents and Publications


mgPrint friendly version mg Email this page
HOTUBA YA MHESHIMIWA MIZENGO P. PINDA (MB.), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI WA KUFUNGUA MASHINDANO YA MICHEZO YA SHULE ZA SEKONDARI TANZANIA (UMISSETA) KIBAHA
TAREHE 20 JUNI 2010
 
 
Mheshimiwa Profesa Jumanne A. Maghembe, (Mb.),
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi;
Mheshimiwa Hajat Amina Mrisho, Mkuu wa Mkoa wa Pwani;
Ndugu Viongozi mbalimbali;
Wakuu wa Shule na Walimu;
Wanamichezo;
Ndugu Wananchi; na
Wapenda Michezo Wote.
 
Napenda kuchukua fursa hii kukushukuru Mheshimiwa Waziri, na Viongozi wenzako katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa kunialika kufungua Mashindano haya ya Umoja wa Michezo ya Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA).
 
Nimeupokea mwaliko huu kwa furaha kwa vile umenipa fursa ya pekee kuwaona na kuzungumza na hadhara hii ya Wanafunzi Wanamichezo na Walimu wao. Aidha, nitumie fursa hii kuupongeza Uongozi wa Mkoa wa Pwani, Mkurugenzi wa Shirika la Elimu Kibaha, Wafanyakazi wote na Wananchi kwa ujumla kwa mapokezi mazuri mliyonipa tangu kuwasili hapa. Nimefurahia pia maandalizi mazuri ya mazingira kwa ajili ya mashindano haya. Ahsanteni sana!
 
Ndugu Viongozi na Vijana Wanamichezo,
Leo tumebahatika kujumuika hapa kupitia Utamaduni wa Michezo. Kwa utaratibu huu, ni dhahiri kwamba tunapata nafasi ya kujenga Umoja wa Kitaifa wa Wanamichezo kupitia Michezo hii ya UMISSETA kuanzia ngazi ya Vijana wetu wa Shule za Sekondari. Ni kweli kwamba Michezo ni Burudani, lakini kwa sasa kutokana na mabadiliko ya Mazingira ya Kisiasa, Kiuchumi na Kijamii, Michezo ni Kipaumbele katika kutoa pia Ajira kwa Vijana wetu, kukuza Biashara na kujenga jamii bora yenye maelewano. Kwa mfano, Nchi za wenzetu za Ulaya na Marekani, Nigeria, Togo, Ivory Coast, Cameroon zinatumia kikamilifu nafasi hii ya Michezo kujitangaza Kisiasa na Kiuchumi.
 
Ndugu Wanamichezo,
Uzoefu unaonyesha kuwa kuendesha Mashindano haya kunahitaji gharama kubwa. Nimedokezwa kwamba hadi sasa ni Shule za Sekondari pekee ndiyo wanaofanya Mashindano ya Michezo mbalimbali. Ngazi nyingine za Elimu hazifanyi Mashindano haya, kutokana na sababu ya ufinyu wa Bajeti. Tungependa kwa Bajeti hiyo hiyo inayopatikana uangaliwe uwezekano wa kufanya Mashindano kama haya katika Shule za Msingi, Vyuo vya Ualimu na Vyuo vingine vya Mafunzo.
 
Pamoja na Serikali kuendelea kuongeza Bajeti kwa ajili ya Michezo ni vizuri pia kuendelea kutafuta vyanzo vingine vya kupata fedha kwa ajili ya shughuli hii. Kwa mfano, miaka ya 1980 kulikuwa na Mradi uliojulikana kama “Sports for All” yaani Michezo kwa Wote. Kupitia Mradi huu Nchi mbalimbali ikiwemo Norway ziliweza kufadhili Michezo kupitia Mradi huo. Ni wakati muafaka kuanza kufikiria kuanzisha Mradi kama huo kwa kuandaa  Andiko la Mradi. Inawezekana kabisa baadhi ya Wafadhili wakaonesha nia ya kuendelea Kufadhili Michezo kupitia Mradi huo, hususan kwa Wanafunzi katika Shule za Msingi na Sekondari. Kwa kutumia ubunifu huo tunaweza kupanua uwigo wa Mashindano kama haya katika ngazi nyingine za Elimu.
 
Ndugu  Wanamichezo,
Natambua kwamba ninyi ni Wanafunzi ambao mnahitaji kukuza Taaluma na Vipaji vyenu. Moja ya nafasi hizo ni Michezo.  Ili  Michezo iendelee kukua Nchini, ni lazima Ukuzaji wa Vipaji vya Michezo uanzie Mashuleni.  Ndiyo maana Michezo ni sehemu ya Mtaala wa Masomo yenu. Kama ambavyo tunawataka mfanye bidii sana katika masomo yenu, fanyeni bidii pia na kukuza Vipaji vyenu katika Michezo mbalimbali.
 
Serikali inatambua umuhimu wa Michezo katika Taifa letu na kwamba ni moja ya mambo yanayotuunganisha Watanzania wa Rika zote na wenzetu wa Afrika Mashariki, Afrika na Dunia kwa ujumla. Wale waliokwenda kwenye Mashindano ya Shule za Sekondari za Afrika Mashariki Nchini Uganda mwaka 2009, watakumbuka kuwa Rais Yoweri Kaguta Museveni wakati huo wa Michezo, alitoa Ngao kwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete, ikiwa ni ishara ya ushirikiano. Ndiyo maana Sera ya Chama Cha Mapinduzi inasisitiza juu ya umuhimu wa kuendeleza Michezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kujenga Viwanja na kutenga maeneo ya kuchezea.
 
Ndugu Wanamichezo,
Michezo inatufundisha Ushindani wa Kistaarabu, Ushindani unaozingatia Sheria na Kanuni, Ushindani unaojenga urafiki badala ya uhasama; Ushindani unaoleta Upendo badala ya Chuki na Ushindani unaoleta Amani badala ya Shari. Kwa sababu hiyo Mwanamichezo wa leo anayo nafasi ya kupata mafundisho muafaka na hazina ya uzoefu mkubwa wa Ushindani wa Kistaarabu kutoka kwenye Michezo, vitu ambavyo vinaweza kumfanya kuwa Mtanzania bora wa kesho. Mwanamichezo anakubali ama Kushindwa au Kushinda. Waswahili husema “Asiyekubali Kushindwa Si Mshindani”.
 
Wanamichezo bora ni Watu Wasikivu, wenye nidhamu na Watiifu. Ninyi Vijana ambao ndio Viongozi wa kesho wa Taifa letu mnahitaji sana kujijengea nidhamu na maadili ya hali ya juu ili muweze kuendana na hali ya maisha ya ushindani yatakayokuwa yanawakabili. Nidhamu, inamuwezesha Mtu kufanya kazi zake kwa mpangilio mzuri unaofuata Taratibu zote za kazi kwa wakati. Hii ndiyo njia ya uhakika ya kufikia malengo yoyote yale na kupata mafanikio.
 
Aidha, kwa njia ya Michezo, nidhamu Shuleni itaongezeka na matarajio yetu ni kuwa nidhamu hiyo itajitafsiri pia katika matokeo mazuri kwenye Taaluma. Matarajio ni kuwa, Wanafunzi watakuwa na mahusiano mazuri zaidi kati yao na Walimu wao na wale wote wanaopata Burudani ya Michezo. Ama tunatarajia kuwa wataendelea kuwa Watu wenye Nidhamu katika Utu Uzima wao, ili hatimaye tuwe na Taifa la Watu wenye nidhamu ya kutolewa mfano.
 
Ndugu Wanamichezo,
Tangu zama za kale Michezo ilikuwa ni sehemu ya Maisha ya Jamii. Jamii moja ilijipambanua na Jamii nyingine kutokana na ushupavu na ushujaa wake katika Michezo. Dhana hiyo ya kale bado inaendelezwa kupitia Sera ya Michezo kwa njia ya kisasa zaidi. Sera ya Maendeleo ya Michezo inayaainisha madhumuni ya Michezo wakati huu kuwa ni:
  • Kujenga na kuimarisha Afya Bora kwa wote;
  • Kujenga Tabia ya Ushirikiano, Upendo, Undugu na Uzalendo;
  • Kujenga Uhusiano, Uelewano na Mshikamano Kitaifa;
  • Kujenga Moyo wa Kishujaa na Kujihami na Kukuza Ukakamavu, Ujasiri na Kujiamini;
  • Kuburudisha;
  • Kulitambulisha na kulitangaza Taifa letu nje ya Mipaka yake; na
  • Kumjenga Mwanamichezo kuwa mtu imara Kiakili na Kiroho (kuanzia Utotoni hadi Utu Uzima).
Kwa mtiririko huu, napenda kusisitiza kuwa Shule zote, kuanzia za Awali, Msingi, Sekondari, Vyuo vyote vya Kati na Vikuu viwe na Viwanja vya Michezo mbalimbali. Hii ni njia ya kuwatambua na kuwaendeleza Vijana  wenye  Vipaji  Maalum ili hatimaye Washiriki kwenye Mashindano ya Kitaifa na Kimataifa. Aidha,  Halmashauri  zetu  za  Miji, Manispaa, Vijiji zihakikishe kuwa maeneo yaliyotengwa kwa Shughuli za Michezo yanatumika kwa shughuli hiyo. Aidha, Viwanja vilivyopo viimarishwe na vitunzwe ipasavyo.
 
Ndugu Wanamichezo,
Nitumie fursa hii pia kuwakumbusha kwamba mnapofurahia kushiriki katika Michezo hii, ni lazima mkumbuke pia kuwa furaha yenu itaweza kudumu kama mtatambua kuwa kuna mpinzani mkubwa kati yenu aitwaye Virusi vya UKIMWI na UKIMWI. Kila mmoja wenu anaelewa vya kutosha juu ya Adui huyu. Ni wajibu wangu kama Kiongozi na Mlezi wenu kuwakumbusha juu ya hatari inayowakabili msipochukua tahadhari ya kutosha. Kumbukeni UKIMWI bado unaenea kwa kasi kubwa sana hasa miongoni mwa Vijana wa Rika lenu kuliko Rika lolote jingine. Niwakumbushe kwamba kataeni kumalizwa na Ugonjwa huu. Msikubali kukatishwa masomo na msikubali kutenganishwa mapema na Familia zenu. Kwenu ninyi, njia bora pekee ni kusubiri hadi wakati muafaka wa kuwa na ndoa zenu. Wekeni bidii katika masomo, kwani muda ukifika yote yatajipanga vizuri.
 
Ndugu Wanamichezo,
Nimeelezwa kuwa baada ya Michezo hii yapo Mashindano ya Afrika ya Mashariki ambapo Nchi za Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudani ya Kusini hukutana ili kuimarisha mahusiano ya Vijana wa Shule za Sekondari katika Jumuiya ya Afrika ya Mashariki. Ni muhimu Timu zetu zijipange kushiriki. Vizuri sasa Timu hizo ziandaliwe vizuri ili zikashiriki kama Washindani na si Wasindikizaji.Kushiriki kwetu kunatujengea umahiri katika kujenga upeo wa akili za Vijana wetu na kujenga mahusiano mazuri ya Kimataifa katika Nchi za Afrika Mashariki. Nashukuru kusikia Mashirika na watu wengi wakichangia kufanikisha michezo. Nawakaribisha wengi zaidi kufanya hivyo, na hasa kuendeleza Michezo katika asasi za Elimu.
 
Ndugu Wanamichezo,
Mwisho napenda kukumbusha kuwa umahiri katika jambo lolote lile hufikiwa kwa kujifunza na kufanya mazoezi mengi, kwa bidii. Napenda kuwapongeza Walimu na Waamuzi na wote walioziandaa Timu hizi ambazo leo zinashindana hapa. Nawapongeza sana Wanamichezo wa Timu zilizoteuliwa kwa majaribio na kuwa Dira ya Mustakhabali wa Michezo ijayo Nchini. Natumaini mliteuliwa kwa kustahili na katika Michezo hii mtapata nafasi ya kuonyesha kuwa kuteuliwa kwenu hakukuwa kwa Bahati.  Onyesheni Umoja, Onyesheni Upendo, na Onyesheni “Fair Play” katika mashindano haya. Kumbukeni kwamba Michezo ni Afya, Michezo ni Furaha na Michezo ni Ajira.
 
Ndugu Wanamichezo, Wageni Waalikwa,
Baada ya kusema hayo, napenda sasa nitamke kuwa, Michezo ya 32 ya Shule za Sekondari UMISSETA 2010 imefunguliwa rasmi.
 
Ahsanteni kwa Kunisikiliza.
 

 

 

 

Help | Disclaimer | Privacy | Site Feedback
Copyrights ©2008-2010, The United Republic of Tanzania, Prime Minister All Rights Reserved
Designed and published by DataVision International (T) Ltd