Home | Speech
Speech
Speeches

Hotuba ya Shukrani kwa Wabunge kabla ya Mkutano wa Ishirini wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Kuvunjwa na Mheshimiwa Rais, Ukumbi wa Bunge, Dodoma, 15 Julai 2010...

Hotuba ya Mheshimiwa Mizengo P. Pinda (Mb) Waziri Mkuu Wakati wa Kufungua Kongamano la Vijana wa Vyuo Vikuu vya Dodoma katika Ukumbi wa African Dreams – Dodoma, tarehe 25 Juni 2010...

More Speeches
Recently Documents

kk Quotes

kama Bunge, lakini mmoja mmoja kama watumishi wa umma, tunao wajibu mkubwa sana wa kuishi na kutenda kwa mfano. Tujiepushe na tamaa zinazoweza kuliingizia Taifa hili hasara kubwa.

Kauli ya Waziri Mkuu kuhitimisha mjadala wa Richmond,
Mkutano wa 18 wa Bunge, Februari 10, 2010
More Quotes
Videos
Photo Gallery

vietnam
More Photos
Documents and Publications


mgPrint friendly version mg Email this page

Hotuba  ya  Mheshimiwa  Mizengo  Peter  Pinda (mb), Waziri Mkuu, kuhusu mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya matumizi ya fedha ya ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge ya mwaka 2010/2011

UTANGULIZI


1.    Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba kutokana na Taarifa iliyowasilishwa ndani ya Bunge lako Tukufu na Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala, iliyochambua Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge lako sasa lipokee na kujadili Taarifa ya Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali kwa Mwaka 2010/2011. Aidha, naliomba Bunge lako Tukufu likubali kupitisha Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2010/2011.

2.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2009/2010, kumekuwepo na matukio mbalimbali ambayo yamewagusa Watanzania. Waheshimiwa Wabunge watakumbuka kuwa ni katika kipindi hiki Bunge lilipata Msiba wa aliyekuwa Mbunge wa Ruangwa, Marehemu Sigifrid Seleman Ng’itu, aliyefariki Dunia  tarehe 2 Novemba 2009. Aidha, Nchi yetu ilipata  Msiba  mkubwa   wa  kuondokewa  na  Mzee  wetu,
Mheshimiwa Rashidi Mfaume Kawawa, Waziri Mkuu Mstaafu na Makamu wa Pili wa Rais aliyefariki Dunia tarehe 31 Desemba 2009. Matukio mengine ni Ajali za Barabarani na Mafuriko yaliyosababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali za Wananchi wengi. Tunamwomba Mwenyezi Mungu awaponye haraka Majeruhi wote na Aziweke Roho za Marehemu Mahali Pema Peponi. Amina!

3.    Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wamepata fursa ya  kujadili  Taarifa  ya  Hali ya Uchumi  wa  Taifa kwa mwaka 2009 na Mpango na Bajeti ya Serikali  kwa  Mwaka  2010/2011. Napenda kutoa pongezi za  dhati   kwa  Mheshimiwa  Mustafa  Haidi  Mkulo  (Mb.),
Waziri wa Fedha na Uchumi kwa Hotuba nzuri na ufafanuzi fasaha wa hoja mbalimbali zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge wakati wa kujadili Hotuba hiyo. Vilevile, napenda kuwapongeza na kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa kuzijadili kwa kina Hotuba hizo na hatimaye kupitisha Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2010/2011. Serikali inathamini ushauri mlioutoa na itauzingatia wakati wa utekelezaji wa Mpango na Bajeti hiyo.

4.    Mheshimiwa Spika, nawashukuru Wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge kwa michango na ushauri waliotoa wakati wa kupitia Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara, Mikoa, Wakala, Idara za Serikali Zinazojitegemea na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Kipekee, nitumie nafasi hii  kuwashukuru Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala chini ya Uenyekiti  wa Mheshimiwa  George  Malima  Lubeleje, Mbunge wa Mpwapwa, kwa mchango wao mkubwa wakati wa uchambuzi wa Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Bunge. Maoni na Ushauri wao umesaidia sana kuboresha Makadirio ya Bajeti ninayowasilisha leo.

5.    Mheshimiwa Spika, Bunge lako Tukufu limepitisha Bajeti ya Serikali ambayo inakamilisha utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2005. Hivyo, katika Hotuba yangu, nitaelezea kwa Muhtasari baadhi ya Mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Nne kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita. Katika kipindi hicho, Serikali ilitekeleza kazi zake kwa kuzingatia Ahadi zilizopo katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, MKUKUTA na Malengo ya Milenia. Kwa ujumla, Serikali imepata mafanikio makubwa ambayo matokeo yake yanajidhihirisha katika Ukuaji Uchumi, Kuimarika kwa Huduma za Kiuchumi na Kijamii na Utawala Bora. Nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wake makini na kusimamia vizuri Serikali na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005. Aidha, nawashukuru Wananchi wote kwa kutekeleza Ilani hiyo kwa mafanikio.
HALI YA SIASA

6.    Mheshimiwa Spika, hali ya Siasa Nchini ni shwari. Nchi yetu imekuwa mfano bora wa kuendesha Mfumo wa Vyama vingi vya Siasa kwani tumeendelea kukosoana na kupingana bila kupigana. Jambo hilo limeifanya Nchi yetu iendelee  kuwa na amani na kuwezesha Watu wetu kufanya  kazi za kujiletea maendeleo. Hali hii imeiletea Nchi yetu heshima kubwa Kikanda na Kimataifa. Natoa wito  tuendelee  kudumisha  utamaduni  na  sifa  hizo njema ili tuweze kuendelea kuwa Nchi ya amani na utulivu. Tunapoelekea  kwenye  Uchaguzi  Mkuu  wa Oktoba 2010, tuendelee kutumia majukwaa yetu vizuri, tutumie lugha zenye staha na kuzingatia maadili na heshima ya Mtanzania.

Vyama vya Siasa

7.    Mheshimiwa Spika, katika kukuza Demokrasia na kusimamia  Siasa za Vyama vingi Nchini, Ofisi ya Msajili wa  Vyama vya Siasa imetoa usajili wa kudumu kwa Vyama vya Siasa 18 Nchini. Vyama viwili vya Siasa vya National Coalition for Democratic Movement (NCDM) na Chama Cha Jamii (CCJ)  vimepata  usajili wa muda. Aidha, Vyama vya Peoples Democratic Movement (PDM) na Democratic National Congress vilifutiwa Usajili baada ya kushindwa kutimiza masharti ya Usajili wa kudumu. Kanuni za Maadili ya Vyama zimetungwa na Vyama vyote vya Siasa vimekubaliana kuzifuata na kuziheshimu. Aidha, ili kuiwezesha Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kutoa huduma zake karibu zaidi na Wadau wake, Ofisi tatu mpya za Kanda za Mwanza, Arusha na Mbeya zimefunguliwa. Vilevile, Serikali imepanua wigo wa Vyama vya Siasa vinavyopata ruzuku kwa kujumuisha vile vyenye Madiwani. Kwa sasa Vyama vinavyopata Ruzuku ni CCM, CHADEMA, CUF na UDP. Vingine ni TLP, NCCR-MAGEUZI, PPT-Maendeleo na CHAUSTA.

8.    Mheshimiwa Spika, Sheria mpya ya Gharama za Uchaguzi ya mwaka 2010 inayoweka udhibiti na ukomo wa matumizi ya fedha wakati wa kura za maoni na Kampeni za Uchaguzi imepitishwa na Bunge lako Tukufu mwezi Aprili 2010. Dhana kubwa katika Sheria hiyo ni Kudhibiti Rushwa katika Siasa ili kupata Viongozi ambao wamechaguliwa kwa ridhaa ya Wananchi pasipo Rushwa. Nichukue nafasi hii kuwapongeza Wananchi kwa kushiriki kutoa mawazo yaliyowezesha kutungwa kwa Sheria hiyo yenye umuhimu wa pekee katika kuimarisha Demokrasia na kuweka uwanja sawa wa ushindani.

9.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2010/2011, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa itaendelea kutoa Elimu kwa Umma kuhusu Sheria ya Gharama za Uchaguzi, kukagua shughuli na uhai wa Vyama vya Siasa na kukagua Taarifa zitakazotolewa na Wagombea pamoja na Vyama vya Siasa kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu.

Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Mwaka 2009

10.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2009/2010, Serikali ilifanikisha Uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika ngazi ya Kitongoji, Kijiji na Mtaa uliofanyika mwezi Oktoba 2009. Katika uchaguzi huo, Chama cha Mapinduzi (CCM) kiliongoza kwa Asilimia 92, kikifuatiwa na CUF Asilimia 4 na CHADEMA Asilimia 3. Vyama  vingine vilivyoshiriki ni CHAUSTA, NCCR-MAGEUZI, TLP, UMD, UPDP, UDP, PPT-MAENDELEO, SAU, DP, NLD na NRA ambavyo kwa pamoja vilipata Asilimia Moja. Nichukue fursa hii kukipongeza kwa dhati Chama Cha Mapinduzi kwa kupata ushindi mkubwa. Aidha, navishukuru Vyama vyote vilivyoshiriki katika Uchaguzi huo na kwa utulivu walioonyesha  wakati  wote  wa  Kampeni  na  Uchaguzi.
Uchaguzi  Mkuu  wa  Mwaka  2010

11.    Mheshimiwa Spika, Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba, 2010 ni wa Nne tangu kuanzishwa kwa Mfumo wa Vyama vingi vya Siasa Nchini. Hatua mbalimbali zimechukuliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi katika kufanikisha Maandalizi ya Uchaguzi huo. Hatua hizo ni pamoja na kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, kutoa Elimu ya Mpiga Kura na kufanyika kwa marekebisho ya Sheria ya Uchaguzi. Hatua nyingine zilizochukuliwa ni kugawa Majimbo Saba ya Uchaguzi ambayo ni Ukonga, Tunduru, Singida Kusini, Kasulu Mashariki, Bukombe, Maswa na Nkasi. Vilevile, Kata mpya 808 zimeanzishwa na zitahusishwa katika Uchaguzi Mkuu ujao. Natoa wito kwa Viongozi na Wadau wote kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi wakati wote wa zoezi zima la Uchaguzi Mkuu wa Mwaka huu. Wote tunalo jukumu la kuhakikisha kwamba Uchaguzi unafanyika kwa hali ya amani na utulivu na kila mwenye sifa ajitokeze kupiga kura.

MUUNGANO

12.    Mheshimiwa Spika,  katika kipindi cha mwaka 2005 – 2010, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeimarisha na kuondoa baadhi ya vikwazo katika utekelezaji wa mambo yanayohusu Muungano. Vikao vinne (4) vya Kamati ya pamoja  ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzíbar vilifanyika chini ya Uenyekiti wa Makamu wa Rais Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein. Katika Vikao hivyo, hoja tisa (9) zilijadiliwa na kati ya hizo, hoja mbili (2) zilipatiwa ufumbuzi na kuondolewa katika orodha ya Kero za Muungano. Hoja saba (7) zinaendelea kufanyiwa kazi. Aidha, jumla ya Vikao 75 vya ushirikiano wa Serikali mbili kwa masuala yasiyo ya Muungano vilifanyika.

13.    Mheshimiwa Spika, katika jitihada za kuimarisha Muungano, miradi ya pamoja ya maendeleo imetekelezwa katika pande zote mbili za Muungano. Miradi hiyo ni TASAF, MACEMP, PADEP na SELF, pamoja na  uimarishaji na ukarabati wa njia ya umeme kutoka Dar es Salaam hadi Fumba – Zanzibar. Vilevile, utekelezaji wa mradi wa umeme kutoka Pangani kwenda Pemba ulikamilika na kuzinduliwa tarehe 3 Juni 2010 na Mheshimiwa Dkt. Aman Abeid Karume, Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Aidha, maandalizi ya ujenzi wa barabara tano (5) za Pemba yanafanyika chini ya ufadhili wa Millenium Challenge Corporation (MCC).  Serikali pia, imekamilisha Awamu ya Kwanza ya ujenzi wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Dar es Salaam na inaendelea na ujenzi wa Ofisi na Makazi ya Makamu wa Rais Tunguu – Zanzibar. Aidha, Ujenzi wa Ofisi Ndogo ya Bunge, Tawi la Benki Kuu na Ofisi ya Uhamiaji – Zanzibar umekamilika.

14.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2010/2011, Vikao vya  Kamati  ya  pamoja ya Serikali ya Jamhuri ya Mungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar vitaendelea kufanyika na kutekeleza miradi ya pamoja ya maendeleo ya pande zote za Muungano. Aidha,

Wizara zisizo za Muungano zitahimizwa kukutana mara kwa mara kujadili masuala ya Sera na kubadilishana uzoefu ili kuimarisha Muungano wetu.

Bunge

15.    Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha kuanzia Desemba 2005 hadi Juni 2010, Bunge limefanya Mikutano 20 yenye Vikao zaidi ya 340. Katika Mikutano hiyo, Miswada ya Sheria 93 ilipitishwa na Maazimio 49 kuridhiwa. Vilevile, Maswali ya Msingi 3,411 na ya Nyongeza 5,129 ya Waheshimiwa Wabunge yamejibiwa na Serikali. Hoja mbalimbali za Kamati za Kudumu za Bunge pamoja na hoja Binafsi za Wabunge ziliwasilishwa na kujadiliwa. Aidha, Waziri Mkuu alijibu  Maswali ya Msingi 270 kwa utaratibu wa Maswali ya Papo kwa Papo. Bunge letu liliandaa kwa mafanikio makubwa Mkutano wa 55 wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola uliofanyika Arusha kuanzia tarehe 29 Septemba hadi 5 Oktoba 2009. Mkutano huo ambao ulikuwa na Kaulimbiu ya “Kukabiliana na Changamoto Mbalimbali Zinazoikabili Dunia” uliiletea Nchi yetu sifa na kujulikana Duniani.
 
16.    Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kukushukuru wewe binafsi kwa kuongoza Bunge hili kwa Kasi na Viwango vya hali ya juu pamoja na umakini mkubwa. Aidha, nawashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa kutimiza wajibu wao wa Kikatiba wa kutunga Sheria na kuishauri Serikali. Nawashukuru pia kwa michango yao ambayo imesaidia kuboresha utendaji wa Serikali na kuimarisha utoaji wa huduma kwa Wananchi. Nawatakieni wote kila la kheri katika Uchaguzi Mkuu ujao ili sote turudi tena Bungeni tuendelee kuwatumikia Wananchi.

HALI YA UCHUMI

17.    Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2005 hadi 2008, Uchumi umeendelea kuimarika na Pato la Taifa lilikua kwa Wastani wa Asilimia 7.2 kwa mwaka. Mwaka 2009, Pato la Taifa lilikua kwa Asilimia 6.0 ikilinganishwa na Asilimia 7.4 mwaka 2008. Kushuka kwa ukuaji wa Uchumi kunatokana na athari za Mtikisiko wa Uchumi Duniani pamoja na ukame ulioikumba Nchi yetu kwa misimu miwili mfululizo. Pia, katika kipindi hicho, Mfumuko wa Bei ulipanda kutoka Wastani wa Asilimia 5 mwaka 2005 hadi 12.2 Desemba 2009. Hali hii ilitokana na kuongezeka kwa bei ya mafuta katika Soko la Dunia na ukame mkubwa uliotokea katika maeneo mengi Nchini na kusababisha ukosefu wa chakula na hivyo bei zake kupanda. Hata hivyo, kutokana na juhudi zilizochukuliwa na Serikali, Mfumuko wa Bei umeanza kupungua hadi kufikia Asilimia 7.9 mwezi Mei 2010. Serikali itaendelea kuandaa na kusimamia Sera za Uchumi, Mapato na Matumizi ya Serikali ili kujenga Uchumi imara na endelevu.

SENSA YA WATU NA MAKAZI MWAKA 2012

18.    Mheshimiwa Spika, Tanzania kama zilivyo Nchi nyingi Duniani hufanya Sensa ya Watu na Makazi kila baada ya miaka kumi. Sensa nyingine itafanyika mwezi Agosti 2012. Ili kufanikisha zoezi hili mwezi Mei 2010, Serikali ilitoa Waraka kuhusu kuundwa kwa Kamati mbalimbali  za  Sensa  kuanzia  ngazi  ya  Wilaya, Mkoa hadi  Taifa.  Napenda  kuchukua fursa hii kusisitiza kwamba Kamati  za Sensa katika ngazi zote ziundwe na zianze  mara  moja  utekelezaji  wa  majukumu yake. Aidha, kila Kiongozi na Mtendaji ahakikishe kuwa anazungumzia  umuhimu  wa  Sensa  kila anapopata nafasi ya  Mkutano au mkusanyiko wowote wa kikazi.    Vilevile, kila Mwananchi afahamu kwamba Sensa ya Watu na Makazi ni zoezi la Kitaifa linalohitaji ushirikiano mkubwa, hivyo kila mmoja awe ni mhamasishaji ili zoezi hilo lifanikiwe.

MAZINGIRA WEZESHI YA BIASHARA NA UWEKEZAJI

19.    Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha 2005 - 2010, Serikali imeweka Mazingira Wezeshi ya Biashara na Uwekezaji ili kuimarisha ushiriki na ushindani wa Sekta Binafsi. Lengo ni  kuhakikisha  kuwa  Sekta  Binafsi  inakua na  kuhimili  ushindani  katika  Masoko  ya  Ndani  na  Nje.

Katika kufikia azma hiyo, Serikali ilitekeleza Programu na Mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara Tanzania na Mradi wa Kuimarisha Ushindani wa Sekta Binafsi. Aidha, Serikali imeboresha Mifumo ya Kitaasisi na Kisheria kwa lengo la kuimarisha Uwekezaji, ikiwa ni pamoja na kuundwa kwa Kitengo Maalum cha kushughulikia Malalamiko ya Wawekezaji.

20.    Mheshimiwa Spika, pamoja na kuweka Mazingira Wezeshi ya Biashara Nchini, bado tunahitaji kuchukua hatua zaidi. Taarifa ya Wepesi wa Kufanya Biashara inayochapishwa kila mwaka na Benki ya Dunia, inaonyesha kuwa Tanzania ilishuka kutoka nafasi ya 126 kati ya Nchi 178 mwaka 2008, hadi 131 kati ya Nchi 183 mwaka 2010. Ili kukabiliana na hali hii, Serikali inatekeleza Mpango Kazi wa Kuboresha Mazingira Wezeshaji ya Uwekezaji na Biashara katika maeneo ya Usajili wa Biashara na Kampuni; Usajili wa Rasilimali na Ajira ya Wafanyakazi. Maeneo mengine ni Upatikanaji wa Mikopo; Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara; Vibali vya Ujenzi; Ulinzi kwa Wawekezaji; Ulipaji Kodi; Urahisi wa Kuendesha Biashara ya Ndani na ya Nje; na Masuala ya Utawala Bora. Napenda kusisitiza kuwa Wahusika wote katika utekelezaji wa shughuli zilizoainishwa katika Mpango huo wawajibike ipasavyo ili kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji Nchini.

21.      Mheshimiwa Spika, Serikali imekamilisha Sera ya Ubia baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi. Sera hiyo imeweka bayana mfumo na taratibu za ushirikiano baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi. Lengo ni kuwezesha Sekta Binafsi kuchangia zaidi katika kutoa huduma za Kiuchumi na Kijamii kwa viwango bora na gharama nafuu. Serikali pia imeendelea kuwa na Mawasiliano ya karibu na ya mara kwa mara na Wadau wa Sekta Binafsi kupitia Baraza la Taifa la Biashara. Serikali inakamilisha mapendekezo ya Muswada wa Sheria ya Ubia baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi na inatarajia kuyawasilisha katika Mkutano huu wa Bunge la Bajeti.

22.    Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2005 – 2010, jitihada za kuvutia uwekezaji wa ndani na nje ya Nchi, zimekuwa na mafanikio mbalimbali. Kituo cha Uwekezaji kilisajili Miradi 3,458 yenye thamani ya Dola za Kimarekani Milioni 22,704. Kati ya Miradi hiyo, Miradi 1,768 ni ya Watanzania, 833 ya Wageni na 857 ni ya Ubia kati ya Watanzania na Wageni. Miradi hiyo kwa pamoja inatarajiwa kuchangia upatikanaji wa Ajira mpya 407,737 kwa Watanzania katika Sekta mbalimbali.

KILIMO, MIFUGO, UVUVI NA USHIRIKA

Kilimo

23.    Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuimarisha Sekta ya Kilimo chini ya Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo katika maeneo ya kugharamia Ruzuku ya Mbolea, Mbegu Bora, Miche na Madawa. Maeneo mengine ni kusimamia utoaji wa Mikopo kupitia Mfuko wa Pembejeo za Kilimo; kuongeza uzalishaji na usambazaji wa Mbegu Bora; kuimarisha huduma za Ugani, Utafiti na Mafunzo ya Kilimo; kudhibiti Visumbufu vya mimea na mazao na kuendeleza matumizi ya Zana Bora za Kilimo.

24.    Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikiongeza Ruzuku ya Pembejeo za Kilimo ili kuhakikisha kwamba Wakulima wanazipata kwa bei nafuu na kwa wakati unaotakiwa. Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Serikali iliongeza fedha kwa ajili ya ruzuku ya pembejeo za Kilimo kwa Asilimia 1,361 kutoka Shilingi Bilioni 7.5 mwaka 2005/2006 hadi Shilingi Bilioni 109.6 mwaka 2009/2010. Kutokana na ongezeko hilo, matumizi ya Mbolea yameongezeka kwa Asilimia 244 kutoka Tani 77,557 mwaka 2005/2006 hadi Tani 267,076 mwaka 2009/2010. Vilevile, katika kipindi hicho matumizi ya majembe ya kukokotwa na ng’ombe yameongezeka kutoka 585,240 hadi 819,360 sawa na ongezeko la Asilimia 40.

25.    Mheshimiwa Spika, kwa upande wa ununuzi wa Zana za Kilimo, hadi mwezi Mei 2010, jumla ya Matrekta Makubwa 518 na Matrekta Madogo 162 yamekopeshwa kupitia Mfuko wa Pembejeo za Kilimo. Katika mwaka 2009/2010 pekee, Mamlaka za Serikali za Mitaa zimenunua Matrekta Madogo 2,154 na makubwa 53. Kutokana na juhudi hizo, tija imeongezeka katika uzalishaji wa baadhi ya mazao. Kwa mfano, uzalishaji wa mahindi umeongezeka kutoka wastani wa Tani 1.5 kwa Hekta mwaka 2005/2006 hadi Tani 3.8 kwa Hekta mwaka 2008/2009. Pia, uzalishaji wa Mpunga uliongezeka kutoka Tani  1.8  kwa  Hekta  hadi  wastani  wa  Tani 5 kwa Hekta.

Nazikumbusha Mamlaka za Serikali za Mitaa kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa Matrekta kila mwaka. Aidha, Serikali imekamilisha taratibu za kupata Mkopo wa Dola za Kimarekani Milioni 40 kutoka Serikali ya India kwa ajili ya ununuzi wa Zana za Kilimo. Meli ya kwanza yenye shehena ya Zana hizo itawasili Nchini mwezi Julai 2010.

26.    Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio hayo, Sekta ya Kilimo imeendelea kukabiliwa na changamoto mbalimbali kama Ukame, Uwekezaji mdogo kwenye Miundombinu, hasa katika Kilimo cha Umwagiliaji, Usindikaji na Masoko. Ili kukabiliana na changamoto hizo Serikali ilizindua Azma ya KILIMO KWANZA ambayo ni hatua thabiti ya kuleta Mapinduzi ya Kijani kwa kushirikisha Sekta Binafsi. Katika kutekeleza Azma hiyo, Wadau wameelimishwa lengo na madhumuni ya KILIMO KWANZA. Aidha, Serikali imetoa Shilingi Bilioni 20 kwa ajili ya kuanzisha Dirisha Maalum la Mikopo ya Kilimo katika Benki ya Rasilimali Tanzania na inaendelea na matayarisho ya kuanzisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo. Nawahimiza Waheshimiwa Wabunge kuelezea Azma ya KILIMO KWANZA popote mtakapokutana na Wananchi kama kichocheo cha kuongeza uzalishaji katika Kilimo na kupunguza umaskini.

27.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2010/2011, Serikali itaongeza upatikanaji wa Pembejeo na Zana za Kilimo ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya Chakula na Biashara. Aidha, itaimarisha Utafiti, Mafunzo na Huduma za Ugani kwenye Kilimo. Vilevile, usimamizi na uwajibikaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa ambao ni watekelezaji wa Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo kupitia Sera ya Kupeleka Madaraka kwa Wananchi utaimarishwa.

Kilimo cha Umwagiliaji

28.    Mheshimiwa Spika, Kilimo cha Umwagiliaji kinawawezesha Wakulima wengi kulima na kuvuna hata mara  mbili  kwa  mwaka  kutegemea aina ya mazao. Aidha, kinawezesha kulima mazao mengine yenye Soko na bei nzuri hasa kipindi cha ukame. Kutokana na hali hiyo, katika kipindi cha kuanzia mwaka 2005 hadi Machi 2010, Serikali ilichukua hatua mbalimbali za kuendeleza Kilimo cha Umwagiliaji. Hatua hizo ni pamoja na kuandaa Sera ya Umwagiliaji, ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya Skimu  za Umwagiliaji 244 na Mabwawa 24, kutoa mafunzo kwa Wakulima na Wataalamu katika maeneo ya matumizi bora ya Maji, utunzaji wa miundombinu na Teknolojia mbalimbali za Umwagiliaji. Aidha, miongozo ya Uibuaji wa Miradi ya Umwagiliaji katika Mipango ya Maendeleo ya Kilimo ya Wilaya ilikamilishwa na kuanza kutumika.

29.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2010/2011, Serikali itajenga Skimu mbalimbali za Umwagiliaji kwa Wakulima Wadogo na wa Kati ili kuongeza uzalishaji na ufanisi wa matumizi ya Maji. Aidha, itakamilisha uandaaji wa Mkakati na Sheria ya Umwagiliaji ili kutekeleza Sera Mpya ya Umwagiliaji.

Mifugo

30.    Mheshimiwa Spika, Sekta ya Mifugo ina fursa kubwa katika kukuza Uchumi na kupunguza umaskini. Kwa kutambua umuhimu huo, Serikali imeanzisha Mpango wa kutoa Ruzuku ya Chanjo na Dawa za Kuogesha Mifugo ili kuongeza uzalishaji wenye tija na mapato kwa Wafugaji. Kati ya Mwaka 2006 hadi 2009, jumla ya Lita 887,992 za Dawa ya kuogesha Mifugo zenye thamani ya Shilingi Bilioni 13.5 zilinunuliwa na kusambazwa kwenye Mikoa yote, ambapo Wafugaji walizinunua kwa Asilimia 60 ya bei ya Soko baada ya Serikali kutoa Ruzuku ya Asilimia 40.  Aidha, Bunge lako Tukufu lilipitisha Sheria ya Utambuzi, Usajili na Ufuatiliaji wa Mifugo ya Mwaka 2010, na Sheria ya Maeneo ya Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo ya Mwaka 2010. Kupitishwa kwa Sheria hizo kutaimarisha usimamizi wa Sekta ya Mifugo hasa katika biashara ya mifugo na mazao yake. Aidha, zitasaidia kupunguza tatizo la migogoro kati ya Wafugaji na Watumiaji wengine wa ardhi.

31.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2010/2011, Serikali itatoa kipaumbele katika kutekeleza Mpango wa Taifa wa Matumizi Bora ya Ardhi ili kubainisha maeneo ya Ufugaji na matumizi mengine ya ardhi. Vilevile, itaimarisha Utafiti na miundombinu ya Mifugo ikiwemo Majosho, Malambo, Mabwawa, Minada, Vituo vya Afya ya Mifugo na Machinjio. Aidha, Serikali itaanza kufanya maandalizi ya Sensa ya Mifugo itakayofanyika mwaka 2012 ili kupata takwimu sahihi za Mifugo Nchini.

Uvuvi

32.    Mheshimiwa Spika, Sekta ya Uvuvi inatoa mchango mkubwa katika kuwapatia Wananchi ajira, lishe, kipato, na kuingizia Nchi fedha za kigeni. Kati ya mwaka 2006 – 2009, jumla ya Tani Milioni Moja za Samaki zenye thamani ya Shilingi Bilioni 783 zilivunwa. Hata hivyo, usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi bado unakabiliwa na tatizo sugu la Uvuvi  Haramu unaoendeshwa na baadhi ya Wavuvi pasipo kuzingatia  Sheria  na  Kanuni  zilizopo. Kutokana na  hali hiyo, Serikali imeendesha zoezi la kupiga vita Uvuvi  Haramu  pamoja  na kuwaelimisha Wananchi kuhusu athari za Uvuvi Haramu.  Natoa wito kwa Viongozi na Watendaji katika ngazi zote za Serikali na Wadau wa Uvuvi  wahusike kikamilifu  katika  kudhibiti  uvuvi na biashara haramu ya Samaki. Aidha, Elimu ya Uvuvi endelevu itolewe  kwa Wavuvi, Wawekezaji na Wadau wengine.

Katika kipindi cha mwaka 2010/2011, Serikali itasimamia uvunaji endelevu wa rasilimali za Uvuvi katika maeneo yote ya maji hapa Nchini ili kuongeza mapato yatokanayo na Sekta ya Uvuvi.

Ushirika

33.    Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2005 hadi 2010, Serikali imetekeleza Programu Kabambe ya Mageuzi na Modenaizesheni ya Ushirika. Programu hii imeweka mazingira mazuri ya kuwa na Vyama vya Ushirika vinavyoendeshwa kibiashara. Idadi ya Vyama vya Ushirika imeongezeka  kutoka  5,730 mwaka  2005/2006 hadi 9,510
Desemba 2009, na Wanachama kutoka 291,368 hadi 795,482 katika kipindi hicho, sawa na ongezeko la Asilimia 173. Akiba na Amana za Wanachama zimeongezeka kutoka Shilingi Bilioni 65.7 mwaka 2005 hadi Shilingi Bilioni 385.5 mwaka 2009. Aidha, mikopo iliyotolewa kwa Wanachama kupitia Vyama vya Akiba na Mikopo kwa ajili ya shughuli za Kilimo, Ufugaji, Usafirishaji, Ujenzi na Biashara iliongezeka kutoka Shilingi Bilioni 54.1 hadi Shilingi Bilioni 463.4. Katika mwaka 2010/2011, Serikali itaendelea kuvijengea uwezo Vyama vya Ushirika ili viwe endelevu na vyenye nguvu kiuchumi.

Programu ya Uendelezaji wa Mifumo ya Masoko ya Mazao ya Kilimo
34.    Mheshimiwa Spika, Programu ya Uendelezaji wa Mifumo ya Masoko ya Mazao ya Kilimo ilikamilisha rasmi utekelezaji wa shughuli zake katika Wilaya 30 za Mikoa Minane tarehe 31 Desemba, 2009. Mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kuvijengea uwezo Vikundi 1,202 vyenye Kaya 43,000 za Wakulima, Wasindikaji wa Mazao ya Kilimo na Wafanyabiashara Wadogo; na kuviunganisha na masoko. Programu pia, imehamasisha na kuanzisha matumizi ya Mfumo wa Stakabadhi za Mazao Ghalani katika Halmashauri za Wilaya Tisa za Babati, Hanang, Mbarali, Mbeya Vijijini, Sumbawanga Vijijini, Kyela, Ileje, Mufindi na Mbozi.

35.     Mheshimiwa Spika, kuanzishwa kwa Mfumo huo kumewezesha bei ya mazao yaliyohifadhiwa ghalani kupanda kwa zaidi ya mara mbili wakati wa kuuza. Mfumo wa Stakabadhi ya Mazao Ghalani pia umewawezesha Wakulima katika Kaya zaidi ya 7,000 kujipatia mikopo yenye thamani ya Shilingi Bilioni 12.5. Vilevile, Programu imewezesha ukarabati wa Miundombinu ya Masoko Vijijini zikiwemo barabara zenye urefu wa Kilomita 957.3 katika Wilaya 30 na Masoko ya kisasa 24 kwenye Wilaya 24 kwa ushirikiano na Halmashauri husika.

Programu ya Huduma za Kifedha Vijijini

36.    Mheshimiwa Spika, Programu ya Huduma za Kifedha Vijijini imeboresha usimamizi na uendeshaji wa Asasi Ndogo za Kifedha 276 na kuimarisha Mifumo ya Kifedha Vijijini kwa kutoa mafunzo mbalimbali kwa Wanachama, Viongozi na Watendaji wa Asasi hizo. Mafunzo yalitolewa kwa Wanakamati 828 wa Kamati za Usimamizi na Maafisa Ushirika 51 kutoka Wilaya 22 na Mikoa 7 ambako Programu inatekelezwa. Aidha, Programu imeimarisha  Benki  ya Wananchi Mufindi, Benki ya Ushirika   Kilimanjaro   na  Benki   ya   Wananchi  Mwanga. Vilevile, uanzishwaji wa Benki za Wananchi Kyela na Mbeya Vijijini upo kwenye hatua za awali na Benki ya Wananchi Njombe imepatiwa Leseni.

37.    Mheshimiwa Spika, Miradi hii imeonyesha mafanikio makubwa  katika kuchangia juhudi za Serikali Kupambana na Umaskini. Mafanikio hayo yameibua chachu ya Wananchi  wa  Mikoa  mingine kuomba kufikishiwa huduma  za  Miradi  hii.  Serikali  imezingatia  maombi  hayo  na  imeanzisha  mchakato wa kuendeleza shughuli za miradi hii katika Wilaya zote za Tanzania Bara  na  Tanzania Zanzibar. Wabia  wa Maendeleo kama vile  Shirika  la Kilimo  la Umoja  wa Mataifa (IFAD),

Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) na Alliance for Green Revolution in Africa (AGRA) wameonyesha nia ya kutoa fedha kwa ajili ya upanuzi wa shughuli za Miradi hii. Hatua za mwanzo za kuangalia jinsi Miradi hii itakavyoendelezwa zimeshaanza ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa fedha za uendeshaji. Hadi sasa warsha za Kikanda na Kitaifa zimefanyika na Taarifa ya Andiko la kina imekamilika. Mradi huo mpya utajulikana kama Marketing Infrastructure, Value Addition and Rural Finance Support Programme na utekelezaji wake utakuwa wa miaka mitano na unatarajiwa kuanza rasmi mwezi Julai, 2011.

ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI


Ardhi

38.    Mheshimiwa Spika, Ardhi ni msingi wa Uchumi wa Taifa lolote Duniani. Hata hivyo, ili ardhi iweze kutumiwa na makundi yote katika jamii, inahitaji mpango mzuri. Kwa kuzingatia ukweli huo, Serikali imeandaa Mpango wa Taifa wa Matumizi Bora ya Ardhi wa Miaka 20 kuanzia mwaka 2009 hadi 2029. Mpango huo unalenga kutenga ardhi katika ngazi ya Taifa, Wilaya na Kijiji kwa kuwashirikisha Wadau. Programu 12 za Utekelezaji wa Mpango huo zilitayarishwa na jumla ya Vijiji 516 viliandaliwa Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa 64. Pamoja na hatua hizo, Serikali bado inakabiliwa na changamoto ya kupima ardhi yote Nchini na kuitayarishia Ramani ikiwa ni pamoja na kupima mashamba kwa kila Mkulima. Ili kukabiliana na tatizo hilo, Serikali imeanza kuweka alama za msingi za upimaji ardhi na utayarishaji Ramani ambazo zitawezesha kuharakisha upimaji wa ardhi na kuandaa Ramani kwa gharama nafuu.

39.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2010/2011, Serikali itatekeleza Programu  za Mpango wa Kitaifa wa Matumizi  Bora  ya  Ardhi  katika  Wilaya  na Vijiji mbalimbali Nchini. Mkazo utawekwa kwenye upimaji wa mashamba ya Wakulima; ardhi kwa ajili ya Wawekezaji na kuweka mipaka kati ya Vijiji na Hifadhi za Wanyamapori, Misitu na Vijiji vyenye migogoro ya ardhi.  Kazi hizi zitafanyika sambamba na utoaji wa Elimu kwa Umma kuhusu Sera, Sheria na Matumizi Bora ya Ardhi.

Maendeleo ya Makazi

40.    Mheshimiwa Spika, Makazi bora ni moja ya vipaumbele vya Serikali katika kuondoa umaskini. Hivyo, Serikali imehamasisha wananchi kujenga nyumba bora kwa kutumia vifaa na teknolojia rahisi za ujenzi. Aidha, kwa kuzingatia mazingira halisi ya Mijini na kasi ya ukuaji wa Miji, Sheria ya Miliki ya Sehemu za Jengo Na.16 ya mwaka 2008  (The  Unit  Titles  Act  No. 16  of  2008)  imetungwa. Sheria hiyo inawezesha mwananchi kupata Hatimiliki ya sehemu ya jengo. Hii itawezesha kipande kimoja cha Ardhi hasa Mijini kuwanufaisha Wananchi wengi, na kuongeza Soko la Nyumba na  Mapato ya Serikali. Vilevile, Sheria ya Mikopo ya Nyumba Na. 17 ya Mwaka 2008 (The Mortgage Financing Act No. 17 of 2008) imetungwa ili kuondoa tatizo la kupata Mikopo ya ujenzi na ununuzi wa Nyumba. Serikali pia, imetekeleza Programu ya Kurasimisha Makazi yaliyojengwa bila kupimwa kwa kutambua Miliki za Nyumba 290,000 katika Miji ya Dar es Salaam, Mwanza, Dodoma, Tanga na Moshi.  Wamiliki wamepewa Leseni za Makazi ambazo wameanza kuzitumia kuombea Mikopo katika Taasisi za Fedha.

41.    Mheshimiwa Spika, kutokuwepo kwa mfumo wa Kiutawala kuhusu uendelezaji wa Nyumba katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kumedumaza maendeleo ya ujenzi katika ngazi hizo. Uendelezaji wa Nyumba umebaki kuwa ni jukumu la mtu mmoja mmoja bila Uratibu, Miongozo na Udhibiti wa Mamlaka husika. Ili kukabiliana na tatizo hilo, Serikali inakusudia kuanzisha Idara ya Nyumba katika ngazi za Halmashauri. Katika mwaka 2010/2011, Serikali itahimiza uanzishwaji wa Vyama vya Ushirika wa Ujenzi wa Nyumba Nchini na kuvutia Makampuni Binafsi kuwekeza kwenye ujenzi wa Makazi Bora na Viwanda vya kutengeneza vifaa vya ujenzi.

MAWASILIANO

42.    Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza azma ya kuifanya Tanzania kuwa kiungo Kikuu cha Mawasiliano Kikanda na Kimataifa, Serikali inaendelea na Ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano. Mkongo huo hivi sasa umeunganishwa na Mikongo ya Kimataifa ya Baharini ya SEACOM na EASSy. Nchi za Rwanda na Uganda pia zimeunganishwa na Mkongo huo. Aidha, Mkongo huo umeunganishwa kwenye Mikoa 13 ambayo ni Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Iringa, Dodoma, Singida, Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Tanga, Shinyanga, Mwanza  na Kagera. Kuunganishwa huko kumewezesha Mawasiliano ya Simu na Intaneti kuwa mazuri zaidi na gharama za Mawasiliano zimepungua. Aidha, katika mwaka 2009, Serikali ilianzisha Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote kwa lengo la kufikisha Mawasiliano katika maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara hasa Vijijini. Huduma za Mawasiliano zitakazoshughulikiwa na Mfuko huo ni pamoja na Simu za Viganjani, Intaneti na Radio za Jamii. Katika mwaka 2010/2011, Serikali itaanza ujenzi wa Awamu ya Pili ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.

VIWANDA NA BIASHARA

43.    Mheshimiwa Spika, Serikali imekamilisha ujenzi wa eneo la Viwanda vya kuzalisha bidhaa kwa ajili ya kuuza nje na kuweka miundombinu yote muhimu katika eneo la Benjamin William Mkapa Special Economic Zone lililopo Mabibo Jijini Dar es Salaam. Eneo hili lilizinduliwa rasmi na Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 17 Mei 2010. Tayari Wawekezaji 24 wamewasilisha maombi ya kuwekeza katika eneo hilo ambapo Wawekezaji watano (5) wamepewa Leseni za Uwekezaji na kuanza kufunga mitambo ya uzalishaji. Aidha, Serikali kupitia SIDO ilitoa mafunzo kwa Wajasiriamali katika Mikoa ya Tanga, Kigoma, Lindi na Mtwara ili kuendeleza usindikaji wa mazao mbalimbali ya Kilimo. Changamoto tuliyonayo ni kuzalisha bidhaa bora zinazokidhi Viwango vya Kimataifa. Natoa rai kwa Wenye Viwanda Nchini kuzalisha kwa kuzingatia Ubora na Viwango vya Kimataifa ili kuhimili ushindani wa Masoko ya Nje na ndani na kuiongezea Serikali fedha za kigeni.
 
44.    Mheshimiwa  Spika,  mauzo  ya  bidhaa  nje ya Nchi  yaliongezeka  kwa   Asilimia  84.4  kutoka  Dola  za Kimarekani  Milioni  1,679  mwaka  2005 hadi Dola za Kimarekani Milioni 3,096 mwaka 2009. Hayo ni mafanikio yanayotokana na fursa za Masoko za Kikanda kama Afrika Mashariki na SADC na za Masoko ya Upendeleo Maalum (Preferential Market Access). Nawahimiza Wafanyabiashara kutumia fursa hizo vizuri ili kuongeza mauzo ya bidhaa zetu nje. Katika mwaka 2010/2011, Elimu ya Ujasiriamali itatolewa kikamilifu ili  kuongeza ushiriki wa Wajasiriamali Wadogo katika kukuza Uchumi. Aidha, Serikali itaimarisha uhusiano wa Kikanda na Kimataifa katika biashara ili kuongeza wigo wa Masoko ya bidhaa zinazozalishwa hapa Nchini.

UJENZI NA UCHUKUZI

Barabara Kuu na za Mikoa

45.    Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Serikali  imepiga  hatua  katika kufanikisha lengo la kuwa na mtandao mzuri wa Babarara za Lami na zinazopitika  wakati  wote  wa  mwaka  ili kurahisisha usafiri na usafirishaji. Serikali ya Awamu ya Nne imekamilisha  Miradi  ya ujenzi wa Barabara zilizoanzishwa na Serikali ya Awamu ya Tatu. Miradi hiyo ni: Tinde – Mwanza/Shinyanga Border (km 96), Nzega – Tinde - Isaka (km 73), Singida - Shelui (km 109),  Mbwemkuru – Nangurukuru - Mingoyo (km 190), Mkuranga – Kibiti (km 60), Tarekea – Rongai – Kamwanga (km 32), Kyamyorwa – Buzirayombo – Geita (km 220) na Dodoma – Manyoni – Singida (Km 245) isipokuwa kipande cha Kilomita 20 kutoka Mkiwa hadi Manyoni.

46.    Mheshimiwa Spika, sambamba na kazi ya kukamilisha ujenzi wa barabara hizo, Serikali ya Awamu ya Nne ilianzisha Miradi mipya 27  ya ujenzi wa Barabara za Lami  zenye urefu wa Kilomita 1,745. Kati ya Barabara hizo, jumla ya Kilomita  212 zimekamilika na nyingine zipo katika hatua mbalimbali za ujenzi. Katika mwaka 2010/2011, Serikali itaendeleza ujenzi wa Barabara zote zinazoendelea na ujenzi pamoja na kukamilisha mchakato wa kutafuta Wakandarasi wa Miradi mipya.

Barabara Vijijini na Mijini

47.    Mheshimiwa Spika, fedha zinazopelekwa kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa zote Nchini kwa ajili ya matengenezo ya Barabara za Vijijini na Mijini zimeongezeka kwa Asilimia 264 kutoka Shilingi Bilioni 23.4 mwaka 2005/2006 hadi Shilingi Bilioni 85.5 Mwaka 2009/2010. Ongezeko hilo limewezesha Barabara zenye hali nzuri kuongezeka kutoka Kilomita 12,623 mwaka 2005 hadi Kilomita 29,298 mwaka 2009. Hili ni ongezeko la Kilomita 16,675, sawa na Asilimia 132. Kutokana na ongezeko hilo la fedha katika Mfuko wa Barabara kiasi kinachopelekwa kwenye  Mamlaka  za  Serikali za Mitaa pia kimeongezeka na hivyo Mtandao wa Barabara nyingi umeimarishwa. Barabara nyingi Vijijini zimeweza kufanyiwa matengenezo ya Muda Maalum na yale ya Kawaida kila mwaka.

48.    Mheshimiwa Spika, pamoja na jitihada hizo, changamoto kubwa inayokabili Sekta ya Barabara Nchini ni kuongezeka kwa kasi kwa gharama za ujenzi ikilinganishwa na uwezo mdogo wa kifedha wa Serikali Kuu na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Kutokana na hali hiyo, ni vyema Mamlaka zote zinazohusika zihakikishe kwamba fedha kidogo zinazopatikana kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu zinatumika kwa uangalifu mkubwa ili kupata thamani halisi ya fedha za Kodi za Wananchi.

Madaraja

49.    Mheshimiwa Spika, tangu mwaka 2005 hadi sasa, Serikali imekamilisha ujenzi wa Madaraja makubwa na ya kati zaidi ya 284 katika Barabara Kuu na za Mikoa. Nafurahi kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa moja ya Madaraja muhimu yaliyokamilika ni ujenzi wa Daraja la Umoja lenye urefu wa Mita 720 ambalo linaunganisha Tanzania na Msumbiji. Daraja hilo ambalo limefunguliwa kwa  pamoja  na  Wakuu  wa Nchi za Tanzania na Msumbiji  tarehe  12  Mei 2010, litakuwa kichocheo muhimu cha kukuza biashara, kuvutia uwekezaji na kuimarisha  uhusiano  baina   ya  Nchi  yetu  na  Msumbiji. Ni imani yangu kuwa Watanzania na hasa Wananchi wa Mikoa ya Kusini watachangamkia fursa nyingi za kiuchumi na kijamii zinazotokana na kukamilika kwa kiunganishi hicho muhimu. Serikali itakamilisha miundombinu mingine muhimu katika eneo hilo la daraja ili kuwawezesha Wananchi wa Nchi hizi mbili kufanya biashara na kutembeleana bila vikwazo.

Usafiri wa Reli

50.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2009/2010, Serikali  ilikamilisha  Upembuzi  Yakinifu  wa  ujenzi  wa Reli   ya  Isaka-Kigali-Musongati  na   Isaka-Dar es Salaam. Kazi nyingine zilizokamilika katika Reli ya Kati ni utandikaji wa Reli na Mataruma mapya kati ya Malongwe na Itigi (Kilomita 47) na kukamilisha ununuzi wa Mashine Tano za Kunyanyulia Vitu Vizito. Aidha, kufuatia utendaji mbovu wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), Serikali imeamua kununua Hisa zote (Asilimia 51) za Kampuni ya RITES ya India na kuchukua jukumu la kuendesha TRL kwa muda wakati akitafutwa Mwendeshaji mpya. 

51.    Mheshimiwa Spika, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa, kazi ya ukarabati wa Miundombinu ya Reli ya Kati  iliyoharibiwa  na mafuriko katika Mikoa ya Morogoro na  Dodoma  imekamilika. Mwishoni  mwa mwezi Mei 2010, Treni ya Mizigo ilianza kufanya majaribio ya kusafirisha mizigo kuanzia Dar es Salaam kwenda Mwanza na Kigoma. Napenda kuwashukuru kwa dhati Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Wahandisi wa Wizara ya Miundombinu na Kampuni ya TRL kwa kazi nzuri waliyofanya ya kurejesha miundombinu hiyo katika hali ya kawaida kwa muda mfupi. Katika mwaka 2010/2011, Serikali itaendelea kusimamia Kampuni ya TRL ili kuhakikisha kuwa inaboresha huduma zake na kukarabati Kilomita 150 za Reli Kati ya Dodoma na Tabora.

Viwanja vya Ndege

52.    Mheshimiwa Spika, Serikali imeimarisha na kuboresha huduma za Viwanja vya Ndege Nchini. Kiwanja cha Kimataifa cha Julius Nyerere kimefanyiwa ukarabati kwa kujenga barabara za kuruka na kutua Ndege  na  Viungio vyake. Aidha, kazi ya kuweka Mitambo  ya  kisasa ya ukaguzi wa Abiria na Mizigo katika  Viwanja vya Ndege vya Julius Nyerere, Mwanza na Arusha imekamilika. Kazi za Usanifu wa Awali wa Viwanja vya Ndege vya Tabora, Bukoba, Shinyanga, Arusha,  Sumbawanga  na  Kigoma  kwa  ajili ya kujengwa   kwa  kiwango  cha  Lami  zimekamilika.  Katika mwaka 2010/2011, ujenzi wa Viwanja vya Ndege vya Bukoba, Kigoma na Tabora kwa kiwango cha Lami utaanza kwa mkopo wa Benki ya Dunia. Aidha, Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Wakimbizi (UNHCR) itajenga Uwanja wa Ndege wa Mpanda kwa kiwango  cha  Lami ili kukuza Utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Katavi.

Huduma za Bandari


53.    Mheshimiwa Spika, Serikali imeimarisha huduma zinazotolewa  na  Mamlaka ya Bandari kwa kuanzisha Vituo  8  vya  kuhifadhi  Makasha  nje  ya  Bandari  ya  Dar es Salaam pamoja na kuboresha Mfumo na Taratibu za uondoshaji wa mizigo Bandarini. Aidha, Mamlaka ya Bandari imeandaa Mpango Kabambe wa Kuendeleza Bandari na tayari kazi ya upanuzi wa maeneo ya kuhudumia mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam, Mtwara na Tanga imeanza. Katika mwaka 2010/2011, Mamlaka ya Bandari itaanza kazi ya ujenzi wa Vituo vipya vya kuhudumia Makasha katika Gati Namba 13 na 14 katika Bandari ya Dar es Salaam. Pia, Serikali itajenga Magati katika Bandari za Mafia, Kasanga na Pangani pamoja na kujenga Magati Matano (5) ya Karema, Kalya, Kirando, Lagosa na Kibirizi katika Ziwa Tanganyika.

MALIASILI


54.      Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2005 hadi 2010, Serikali iliweka mikakati imara ya kuhakikisha kwamba Maliasili tulizonazo za Misitu na Wanyamapori zinahifadhiwa na kuwanufaisha Wananchi. Halmashauri zenye maeneo ya hifadhi ziliendelea kupata mgao wa Asilimia 25 ya Mapato yatokanayo na Uwindaji wa Kitalii na kugharamia Mipango mbalimbali ya maendeleo inayoibuliwa na Jamii. Aidha, katika kipindi hicho, TANAPA imetoa Shilingi Bilioni 5.8 kugharamia Mipango ya Maendeleo  ya  Wananchi katika  maeneo  mbalimbali. Vilevile, Serikali imejenga uwezo wa Wafugaji Nyuki kwa kutoa mafunzo na mbinu za Ufugaji Bora wa Nyuki na kuwawezesha kupata vifaa vya kisasa vya Ufugaji Nyuki. Uimarishaji wa Sekta Ndogo ya Nyuki umezingatia ukweli kwamba, Urinaji wa Asali ni moja ya shughuli muhimu za kuongeza kipato na kupunguza Umaskini miongoni mwa Wananchi wetu.

55.     Mheshimiwa Spika, ili kulinda ubora wa Asali inayozalishwa Nchini, Viongozi wa Mikoa yote ambayo ina Wananchi wengi wanaojishughulisha na Ufugaji wa Nyuki wachukue hatua ya kutenga maeneo maalum kwa ajili ya Ufugaji wa Nyuki. Aidha, Kilimo cha Tumbaku katika maeneo ya Wafugaji Nyuki kisiruhusiwe ili kulinda ubora wa Asali yetu katika Masoko ya Kimataifa. Katika mwaka 2010/2011, Serikali itaimarisha usimamizi na matumizi endelevu ya Misitu na Wanyamapori. Aidha, juhudi zaidi zitaongezwa kwenye kutoa mafunzo ya Ufugaji Nyuki na utafutaji wa Masoko ya uhakika ya Asali na Nta inayozalishwa Nchini.

UTALII

56.    Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na Wadau imetangaza Utalii wa Tanzania kwa njia mbalimbali ikiwemo matumizi ya Vyombo vya Habari vya Kimataifa, Ofisi zetu za Ubalozi, safari na ziara mbalimbali za Viongozi na kupitia Makongamano ya Kimataifa. Watalii kutoka Masoko mapya ya Nchi za Asia zikiwemo China, Japan, Singapore, India na Urusi wameongezeka kutoka Watalii 23,542 mwaka 2006 hadi 32,973 mwaka 2008. Kwa ujumla, idadi ya Watalii waliotembelea Tanzania iliongezeka kutoka 612,754 mwaka 2005 hadi 770,376 mwaka 2008.  Hata hivyo, idadi ya Watalii kwa mwaka 2009 ilipungua na kufikia 714,367 kutokana na athari za Mdororo wa Uchumi Duniani. Mapato yatokanayo na biashara ya utalii yaliongezeka kutoka Shilingi Bilioni 948.6 mwaka 2005 hadi Bilioni 1,610 mwaka 2008.

57.    Mheshimiwa Spika, tunavyo Vivutio vingi vinavyoweza kutuingizia mapato na kuinua Uchumi wetu. Hivyo, hatuna budi kuelekeza nguvu zetu zaidi katika kuimarisha Sekta hii muhimu ya Utalii kwa kuitangaza kwa nguvu zaidi na kuimarisha huduma kwa Watalii wetu. Natoa wito kwa kila mmoja katika nafasi yake ajione ana wajibu wa kuitangaza Nchi yetu kila inapotokea nafasi. Katika mwaka 2010/2011, Serikali itaainisha na kutangaza Vivutio vya Utalii Ndani na Nje ya Nchi pamoja na kuhamasisha Uwekezaji kwenye maeneo mapya ya Utalii.  Aidha, itaimarisha miundombinu katika Vituo na  maeneo ya Rasilimali za Kale.

NISHATI NA MADINI

Nishati

58.    Mheshimiwa Spika, Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005 iliweka malengo ya kufikisha Umeme katika Miji Mikuu ya Wilaya mbalimbali; kuongeza kasi ya kupeleka Umeme Vijijini kupitia Mfuko wa Nishati Vijijini; na kuvutia Uwekezaji wa Sekta Binafsi katika uzalishaji na usambazaji wa Umeme.  Katika kipindi hicho, Umeme umefikishwa katika Makao Makuu ya Wilaya Tisa za Serengeti, Ukerewe, Mbinga, Simanjiro, Uyui, Ludewa, Mkinga, Kilolo na Bahi.  Aidha, Sheria ya Umeme ya mwaka 2008 ilitungwa. Sheria hiyo inaruhusu ushiriki wa Sekta Binafsi katika kuzalisha na kusambaza Umeme.

59.    Mheshimiwa Spika, ili kupunguza tatizo la upatikanaji wa umeme, Serikali ilikamilisha ujenzi wa Mtambo wa kuzalisha Umeme unaotumia Gesi Asilia wenye uwezo wa kuzalisha MW 45 katika eneo la Tegeta, Dar es Salaam.  Aidha, ilinunua na kufunga Mashine tano za kufua Umeme wa MW 6.25 kwa ajili ya Mji wa Kigoma – Ujiji.  Serikali pia inakamilisha usambazaji wa Umeme wa Gesi Asilia kutoka Mnazi Bay kwenda katika Mikoa ya Mtwara na Lindi.

60.    Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio hayo niliyoyataja, upatikanaji wa Nishati ya uhakika umekuwa ni moja ya changamoto kubwa zinazotukabili. Kukosekana kwa Nishati ya uhakika na kwa bei ya ushindani kunaathiri Uwekezaji na Mazingira ya Ufanyaji Biashara kwa ujumla. Taarifa ya Wepesi wa Kufanya Biashara Tanzania ya mwaka 2010 inaonyesha kwamba, Wazalishaji na Wafanyabiashara wengi Wadogo na wa Kati wanalalamika kuhusu upatikanaji wa Nishati ya uhakika kama moja ya kikwazo kikubwa katika shughuli zao. Changamoto hiyo ni lazima itafutiwe ufumbuzi wa kudumu  ili kuhakikisha kwamba uzalishaji wa bidhaa unaongezeka katika viwanda vyetu. 

61.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2010/2011, Serikali itajenga Mitambo ya kufua Umeme wa MW 100 Ubungo, Dar es Salaam na MW 60 Jijini Mwanza. Vilevile, itayapatia Umeme Makao Makuu ya Wilaya Nane za Namtumbo, Loliondo, Longido, Nkasi, Bukombe, Kishapu, Kasulu na Kibondo. Serikali pia, itatekeleza miradi ya kupeleka Umeme Vijijini na kuimarisha miundombinu ya mifumo ya usafirishaji wa umeme.

Madini

62.    Mheshimiwa Spika, Serikali ilikamilisha na kupitisha Sera Mpya ya Madini ya mwaka 2009 na Sheria ya Madini ambayo ilipitishwa na Bunge lako Tukufu mwezi Aprili 2010. Sheria hiyo mpya, pamoja na mambo mengine, imeweka bayana namna ambavyo Serikali na Wananchi watashiriki  katika shughuli za Madini. Serikali pia, ilianzisha Wakala wa Ukaguzi wa Madini ambao utawajibika  kukagua Madini yatakayouzwa nje ya Nchi. Uzoefu uliopatikana katika kipindi kifupi tangu kuanzishwa kwa Wakala huo na kuanza kukagua dhahabu umeonyesha kwamba, tuna uwezo wa kufanya kazi hiyo na Serikali inaokoa fedha nyingi kutokana na utaratibu huo. Natoa wito kwa Watanzania kutumia fursa ya Sheria mpya ya Madini ili washiriki kikamilifu kwenye biashara ya Uchimbaji Madini.

63.    Mheshimiwa Spika, Serikali imetenga maeneo kwa ajili ya Wachimbaji Wadogo wa Madini Nchini ili wafanye shughuli zao kwa uhakika na usalama. Aidha, Serikali imetenga  Shilingi  Bilioni  Moja kama kianzio cha Mfuko wa Kuwaendeleza Wachimbaji Wadogo na kuanzisha Kitengo maalum cha kuwaendeleza Wachimbaji hao. Vilevile, Wachimbaji Wadogo wamepewa mafunzo juu ya Utunzaji wa Mazingira, Afya na Usalama katika maeneo yao ya kazi.  Pamoja na hatua hizo, bado kuna tatizo la Wachimbaji Wadogo kutozingatia Taratibu za Kisheria na hivyo kuwepo uvamizi wa maeneo, ajali za Migodini, uharibifu wa mazingira na migogoro kwenye Migodi. Natoa wito kwa Wachimbaji Wadogo kufanya shughuli zao kwa kufuata Sheria, Taratibu na Kanuni za Usalama Migodini ili kuzuia ajali na migogoro isiyo ya lazima. Katika mwaka 2010/2011, Serikali itaimarisha Wakala wa Ukaguzi wa Madini  kwa kuupatia Watumishi Mahiri na vitendea kazi vya kisasa. Aidha, itatoa Elimu kwa Wachimbaji Wadogo na kufanya kaguzi katika Migodi yao.

MAJI

64.    Mheshimiwa Spika,  katika  kuimarisha  usimamizi  na uendelezaji wa Rasilimali za Maji Nchini, Serikali imeandaa na kupitisha Mkakati na Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji. Aidha, Sheria Na. 11 ya Usimamizi wa Rasilimali  za  Maji, na Sheria Na. 12 ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira za mwaka 2009 zilitungwa. Kwa mujibu wa Sheria hizo, Mamlaka za Serikali za Mitaa na Bodi za Maji za Mabonde zimepewa jukumu la kusajili Vyombo vya Watumiaji Maji. Hatua hiyo imesaidia kuharakisha uandikishaji Kisheria wa Vyombo hivyo na  kupanua wigo katika kusimamia huduma ya Maji na kutunza  rasilimali za Maji kwa njia endelevu. Aidha, Serikali imejenga na kukarabati miradi ya Maji na kuchimba Visima virefu na vifupi. Kutokana na hatua hizo, upatikanaji wa Maji Vijijini umeongezeka kutoka Asilimia 57.1 mwaka 2007 hadi 61 Desemba 2009 na Maji Mijini kutoka Asilimia 78 hadi 84 kwa kipindi hicho. Vilevile, upatikanaji wa Maji katika Jiji la Dar es Salaam umeongezeka kutoka Asilimia 50 mwaka 2005 hadi 68 mwaka 2009.

65.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2010/2011, Serikali  itaendelea  kutekeleza  Programu ya Maendeleo ya  Sekta ya  Maji  kwa lengo  la  kuboresha  usimamizi wa  Rasilimali  za  Maji na kuongeza upatikanaji  wa  huduma  ya Maji Vijijini na Mijini. Serikali itaandaa na kutekeleza Mipango Shirikishi ya Usimamizi na Uendelezaji wa Rasilimali za Maji katika Mabonde yote ya Maji. Aidha, itaimarisha Maabara za Maji na kujenga Miradi mipya ya Maji. Natoa wito kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa zihamasishe uvunaji wa Maji ya Mvua kwa kutumia Teknolojia Nyepesi na rahisi ya kukinga na kutunza Maji. Aidha, ziweke Sheria Ndogo kwa ajili ya Taasisi na Kaya kuvuna maji ya mvua kwenye mapaa ya nyumba na zisimamiwe kikamilifu.

ELIMU

66.    Mheshimiwa Spika,  Serikali imeongeza kasi ya uandikishaji wa  Wanafunzi na kuimarisha miundombinu ya Elimu katika Shule za Awali, Msingi, Sekondari na Vyuo vya Ufundi Stadi. Kutokana na jitihada hizo, katika kipindi cha mwaka 2005 hadi 2009, uandikishaji katika Shule za Msingi umeongezeka kutoka Wanafunzi 6,499,581 hadi kufikia 8,441,553; sawa na ongezeko la Asilimia 30. Uandikishaji  wa Wanafunzi wa Kidato cha Kwanza  kwa Shule za Sekondari za Serikali uliongezeka kutoka Wanafunzi 134,963 hadi 477,554 sawa na ongezeko la Asilimia 254.  Vilevile, idadi ya Wanafunzi wanaoingia Kidato cha Tano iliongezeka kutoka Wanafunzi 9,710 hadi 33,169 sawa na ongezeko la Asilimia 242. Kwa upande wa mafunzo ya Ufundi Stadi, idadi ya Wanafunzi wote iliongezeka kutoka 78,586 hadi 114,295.

67.    Mheshimiwa Spika, Serikali imepiga hatua kubwa katika kupanua Elimu ya Juu kwa kushirikiana na Sekta Binafsi. Miongoni mwa mafanikio ya hatua hizo ni kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Dodoma pamoja na Vyuo Vikuu Vishiriki vya Elimu vya Dar es Salaam na Mkwawa. Pia, Sekta Binafsi imepanua na kuanzisha Vyuo mbalimbali. Kutokana na juhudi hizo, idadi ya Vyuo Vikuu na Vyuo Vikuu Vishiriki vya Umma na Binafsi vimeongezeka kutoka 26 mwaka 2005/2006 hadi 32 mwaka 2009/2010. Aidha, Udahili wa Wanafunzi wanaojiunga na Vyuo vya Elimu ya Juu umeongezeka kutoka Wanafunzi 40,719 mwaka 2005/06 hadi 117,068 mwaka   2009/2010,  sawa  na  ongezeko  la  Asilimia  188.

Ongezeko hili limetokana na Serikali kuongeza Mikopo ya Elimu ya Juu kutoka Wanafunzi 42,726 mwaka 2005/2006 hadi 69,442 mwaka 2009/2010.

68.     Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuyapongeza Madhehebu mbalimbali ya Dini na Sekta Binafsi kwa kuitikia wito wa Serikali wa kuongeza fursa za Wanafunzi wengi kupata Elimu ya Juu Nchini. Kipekee nampongeza Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kusimamia kikamilifu utekelezaji wa Ahadi ya Serikali ya Awamu ya Nne ya kuanzisha  Chuo  Kikuu  cha  Dodoma.  Chuo hiki ambacho ni cha kihistoria na kikubwa hapa Nchini kitakapokamilika kinatarajiwa kuchukua Wanafunzi 40,000. Hadi sasa Chuo hiki kimedahili Wanafunzi 15,121. Kuanzishwa kwa Chuo hiki ni kielelezo kuwa Watanzania tukidhamiria tunaweza kujiletea maendeleo wenyewe.

69.    Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio hayo, Sekta ya Elimu bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo uhaba wa Walimu, Maabara, Nyumba za Walimu, Hosteli, upungufu wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia pamoja na ufaulu mdogo wa masomo ya Hisabati, Sayansi na Kiingereza. Changamoto nyingine ni mazingira magumu ya kazi katika baadhi ya maeneo ya Vijijini na uchakavu wa miundombinu katika Shule za Sekondari za Bweni, Vyuo vya Ualimu na Vyuo Vikuu.

70.    Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na changamoto hizo katika kipindi cha mwaka 2010/2011, Serikali itaongeza ajira ya Walimu wapya katika Shule za Msingi wapatao 14,800 na Sekondari Walimu 11,140. Vilevile, itaongeza vifaa vya kufundishia na kujifunzia na ujenzi wa Maabara za Masomo ya Sayansi na Lugha. Aidha, Serikali itatoa mafunzo Kazini kwa Walimu wa Masomo ya Sayansi, Hisabati na Kiingereza, kuimarisha Vituo vya Walimu na kuimarisha miundombinu ya Elimu katika ngazi zote.

AFYA NA USTAWI WA JAMII

Afya

71.    Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza Sera ya Afya ya mwaka 2007 inayolenga kuimarisha Huduma za Kinga na Tiba. Serikali ilielekeza jitihada zake katika kuzuia na kudhibiti Magonjwa mbalimbali ikiwemo Malaria ambayo inasababisha Vifo vya Watanzania wengi. Hadi sasa, Serikali imesambaza Vyandarua Milioni 3.8 vyenye Viuatilifu kwa Wanawake Wajawazito na Vyandarua Milioni 1.3 kwa Watoto Wachanga. Aidha, Vyandarua Milioni 5.6 viligawanywa kwa kila Kaya yenye Watoto wa umri chini ya miaka mitano bila malipo.  Vilevile, Serikali ilinunua na kusambaza Dawa Mseto ya Malaria kwa Vituo vyote vya Tiba vya Umma vipatavyo 5,000.

72.    Mheshimiwa Spika, Serikali imeimarisha mfumo wa utoaji wa huduma za Afya kwa kuendelea kuongeza Vituo vya Kutolea Huduma za Afya Nchini. Katika kipindi cha miaka mitano, Hospitali za Mikoa zimeongezeka kutoka 17 hadi 21, Vituo vya Afya vimeongezeka kutoka 382 hadi 468 na Zahanati zimeongezeka kutoka 3,292 hadi 4,559 ikiwa ni pamoja na kuimarika kwa huduma za chanjo. Ongezeko hilo limesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza vifo vya Watoto Wadogo. Aidha, ujenzi wa Hospitali ya Magonjwa ya Moyo Muhimbili umeanza, na inategemewa kukamilika mwezi Mei 2011. Hospitali hiyo itakapokamilika itapunguza idadi ya Wagonjwa wa Moyo wanaopelekwa nje ya Nchi kwa matibabu.

73.    Mheshimiwa Spika, pamoja na juhudi hizo, Sekta ya Afya inakabiliwa na upungufu wa Watumishi wa Afya.  Upungufu huo umeathiri zaidi maeneo ya Vijijini ikilinganishwa na Mijini. Katika kukabiliana na upungufu huo, Serikali imeandaa Mikakati ya kuendelea kuongeza Wataalamu ambayo ni pamoja na kuanzishwa kwa mafunzo ya masafa na kuongeza fedha za  kugharamia mafunzo ya utarajali na uzamili.  Hatua hii itaongeza Wahitimu wa Vyuo Vikuu na Vyuo vya Uuguzi na Sayansi Shirikishi za Afya hapa Nchini kutoka 4,900 mwaka 2010 na kufikia 22,540 mwaka 2015. Katika mwaka 2010/2011, Serikali itajenga Vituo zaidi vya kutolea Huduma za Afya na kutoa Dawa na vifaa vya Tiba.

Watu Wenye Ulemavu na Wazee

74.    Mheshimiwa Spika, Serikali imeridhia Mkataba wa Kimataifa kuhusu Haki  kwa Watu Wenye Ulemavu na kutunga Sheria Jumuishi ya Watu wenye Ulemavu na Wasiojiweza  Nchini. Hatua hizo zimeweka mfumo mzuri wa kusimamia na kutoa huduma kwa Watu Wenye Ulemavu. Serikali pia, imefanya  utafiti kuhusu idadi ya Watu  Wenye Ulemavu  kwa lengo la kupata takwimu sahihi na  kubaini mahitaji yao ili waweze kuhudumiwa kwa urahisi zaidi. Vilevile, imegharamia mahitaji muhimu katika baadhi  ya Shule  za Wanafunzi wenye Ulemavu wa Ngozi. Aidha, Serikali imeanzisha utaratibu wa kila Hospitali na Vituo vya Afya  kuwa na Kliniki pamoja na watoa huduma Maalum  kwa ajili ya kuhudumia Wazee. Vilevile, kuanzia mwaka 2010/2011, Serikali imeamua kusamehe Kodi ya Majengo kwenye nyumba wanazoishi Wazee wenye umri wa zaidi ya Miaka 60 ambao uwezo wao kiuchumi ni mdogo kuweza kulipa Kodi hiyo.

MAENDELEO YA WANAWAKE NA WATOTO

Wanawake

75.    Mheshimiwa Spika, Serikali imetekeleza kwa dhati dhamira ya kuongeza uwakilishi wa Wanawake katika ngazi mbalimbali za maamuzi kuelekea uwiano wa Asilimia 50 kwa 50. Idadi ya Wanawake katika ngazi mbalimbali za maamuzi imeongezeka kutoka wastani wa Asilimia 26 mwaka 2005 hadi Asilimia 31 mwaka 2009. Aidha, Serikali ilianzisha Benki ya Wanawake Tanzania ambayo inalenga kuwapatia Wanawake mikopo yenye masharti nafuu. Hadi sasa, zaidi ya Akaunti 9,902 zimefunguliwa na kiasi cha Shilingi Milioni 135 zimekopeshwa kwa Wajasiriamali wa Jinsia zote. Serikali pia, ilitoa mikopo yenye thamani ya Shilingi Milioni 928 kwa Vikundi vya Wanawake katika Mamlaka za Serikali za Mitaa. Katika mwaka 2010/2011, Serikali itahamasisha Jamii na Taasisi mbalimbali kununua hisa za Benki ya Wanawake na kusimamia Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake.

Watoto

76.    Mheshimiwa Spika, Serikali imeandaa Sera Mpya ya Maendeleo ya Mtoto Tanzania ya mwaka 2008 inayotoa Mwongozo wa Haki za Mtoto. Aidha, Serikali imeratibu na kuwezesha kuundwa kwa Mabaraza ya Watoto ambayo hadi sasa yameanzishwa katika Mikoa 15 ya Tanzania Bara na katika Wilaya 87. Uanzishwaji wa Mabaraza hayo ni njia mojawapo ya ushirikishwaji wa Watoto katika kutoa mawazo yao kuhusu Haki zao na Wajibu wao katika ujenzi wa Taifa. Vilevile, Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009 ambayo inajumuisha Sheria nyingi za Watoto zilizokuwepo awali ilitungwa. Sheria hiyo imetilia mkazo kuhusu Maendeleo, Ulinzi na Haki za Watoto. 

HABARI NA UTAMADUNI

Habari

77.    Mheshimiwa Spika, Sekta ya Habari ina umuhimu mkubwa katika kuiunganisha Jamii na kuleta maendeleo Nchini. Kwa sababu hiyo, Serikali imeimarisha na kuendeleza uhuru wa kupata, kutoa na kusambaza Habari Nchini ili ziweze kuwafikia Wananchi wote. Serikali kwa kushirikiana  na Wadau mbalimbali imepanua uhuru na wigo  wa Kupashana Habari kwa kiwango kikubwa. Kutokana na  jitihada  hizo,  kumekuwepo  na  ongezeko la Magazeti na   Majarida,  Vituo   vya  Redio,  Televisheni  na  Mitandao. Ninapenda kuchukua nafasi hii kuwakumbusha Wamiliki na Wahariri wa Vyombo vyote vya Habari kuandika na kutangaza habari zilizo sahihi na zinazoelimisha Wananchi kuhusu masuala muhimu ya maendeleo.

Lugha ya Kiswahili

78.    Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuimarisha Lugha ya Kiswahili kama kielelezo cha Utamaduni wetu. Moja ya kielelezo hicho ni  kuanzishwa kwa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Kiswahili  sasa  ni  mojawapo  ya  Lugha  rasmi  ya Jumuiya  ya   Afrika   Mashariki   na  Umoja   wa   Afrika. Kwa mantiki hii, ninachukua nafasi hii kusisitiza umuhimu wa matumizi ya Lugha ya Kiswahili katika shughuli rasmi za Serikali. Vilevile, nahimiza Taasisi za Elimu Nchini ziweke mkazo katika kufundisha Kiswahili Sanifu ili Watanzania waweze kunufaika na fursa nyingi za ajira ya Kiswahili za ndani na nje. Katika mwaka 2010/2011, Serikali itaendeleza mazungumzo ya kukiwezesha Kiswahili kuwa mojawapo ya Lugha rasmi za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC). 

ULINZI NA USALAMA

79.    Mheshimiwa Spika, Serikali imeimarisha Jeshi la Ulinzi kwa kulipatia vifaa na Mafunzo. Hatua hiyo imelenga kuimarisha utendaji na kuwapatia mbinu za kisasa za Kivita. Jeshi letu limeweza kushiriki katika Operesheni za Kulinda Amani huko Darfur-Sudan na Lebanon. Vilevile, Serikali imeboresha Makambi na Makazi ya Askari wa Jeshi la Wananchi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa kujenga jumla ya nyumba mpya za makazi 336. Aidha, ukarabati wa Mabwalo, Mabweni, Ofisi, Madarasa, Hospitali na Miundombinu ya Maji Safi na Taka, Umeme na Mawasiliano umefanyika katika Makambi mbalimbali ya Jeshi Nchini.

80.    Mheshimiwa Spika, ili kutekeleza ahadi ya Serikali ya kurejesha Jeshi la Kujenga Taifa, ukarabati wa miundombinu umefanyika katika Makambi 12 yenye uwezo wa kuchukua Vijana 7,110 kwa wakati mmoja. Makambi mawili ya Kanembwa na Masange yenye uwezo wa kuchukua Vijana 2,000 yanaendelea kukarabatiwa. Katika mwaka 2010/2011, Serikali itayaongezea uwezo wa utendaji kivita Majeshi ya Ulinzi kwa kuyanunulia vifaa na Zana za Kisasa, kukarabati Miundombinu na Mitambo ya Vituo vya Utafiti, Viwanda na Karakana za Kijeshi. Mwelekeo huo utahusu

 

 

 

 

Help | Disclaimer | Privacy | Site Feedback
Copyrights ©2008-2010, The United Republic of Tanzania, Prime Minister All Rights Reserved
Designed and published by DataVision International (T) Ltd