HOTUBA YA MHESHIMIWA MIZENGO P. PINDA (MB), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA ILIYOTOLEWA WAKATI WA UFUNGUZI WA MKUTANO WA TATU WA KITAIFA WA WADAU WA MAZAO YA BUSTANI, ULIOFANYIKA HOTELI YA NAURA SPRINGS, ARUSHA
TAREHE 31 MEI, 2010
Mheshimiwa Stephen Masato Wasira, (Mb.),
Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika;
Mheshimiwa Isidori Shirima,
Mkuu wa Mkoa wa Arusha;
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Arusha;
Ndugu Felix Mosha, Mwenyekiti wa Baraza la Kuendeleza Mazao ya Bustani Tanzania;
Wajumbe wa Mkutano;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana.
Napenda kutumia fursa hii kuwashukuru Wajumbe wa Baraza la Kuendeleza Mazao ya Bustani Tanzania (Horticulture Development Council of Tanzania – HODECT) kwa kunialika kuwa pamoja nanyi katika Mkutano huu wa Tatu wa Kitaifa wa Wadau wa Mazao ya Bustani Nchini. Kwa niaba ya Serikali na Watu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania napenda kuwakaribisha Wajumbe wote wa Mkutano huu muhimu katika Sekta ya Kilimo. Natambua kuwa Washiriki wengine wametoka mbali ikiwa ni pamoja na nje ya Tanzania. Nyote nawakaribisha Tanzania hususan hapa Arusha.
Mji wa Arusha ni maarufu kwa vivutio vingi vya Kitalii zikiwemo Mbuga za Wanyama zilizo karibu sana na hapa tulipo. Baadhi ya Vivutio Tanzania inavyojivunia sana ni pamoja na Mbuga ya Serengeti ambayo ni kati ya Maajabu ya Dunia, Mbuga ya Manyara, Bonde la Ngorongoro, Milima ya Meru na Kilimanjaro. Vilevile, ninaamini kuwa Wageni wetu mtafurahia hali ya hewa ya Mji huu ambao uko katikati kutoka Jiji la Cairo, Misri hadi Cape Town, Afrika ya Kusini.
Nawaomba mtumie fursa hii adimu mpatapo nafasi wakati au baada ya Mkutano huu mtembelee katika Mbuga za Wanyama kujionea Hazina kubwa iliyopo Tanzania. Vilevile, nawakaribisha kupanda Mlima Kilimanjaro. Ninaamini itakuwa kumbukumbu nzuri kwenu na isiyosahaulika kuhusu Mkutano huu.
Ndugu Washiriki,
Mkutano wa leo ni wa Tatu ukifuatia Mikutano miwili ya awali iliyofanyika mapema Mwezi Desemba 2005 na Aprili 2008 hapa Arusha. Katika Mikutano yote miwili iliyotangulia Wadau wa Mazao ya Bustani walipata nafasi ya kujadili fursa na changamoto zinazoikabili Sekta ya Mazao ya Bustani. Mazao ambayo yanajumuisha Mboga, Matunda, Viungo na Maua. Hivyo, Mikutano hii inatoa fursa kwa Wadau wote kupata nafasi ya kukutana, kubadilishana uzoefu na kushauriana nini kifanyike ili kukabiliana na changamoto hizo. Nawapongezeni wote kwa utaratibu huu mzuri mliojiwekea wa kukutana mara kwa mara kwani Wahenga walisema “Palipo na Wengi Hapaharibiki Jambo”.
Ndugu Washiriki,
Nimeelezwa kuwa katika Mkutano wenu wa Kwanza mwezi Desemba 2005, mliamua kuunda Chombo kitakachoratibu maendeleo ya Sekta hii ya Mazao ya Bustani Nchini. Aidha, kwa usahihi kabisa mlipendekeza kuhusisha Wajumbe kutoka Vyama na Taasisi zinazohudumia Sekta ya Mazao ya Bustani kwa upande mmoja na upande wa pili kuwa na Wajumbe kutoka Wizara na Taasisi za Serikali zinazohudumia Sekta hiyo. Shabaha ya kuwa na Chombo hicho ni kuhakikisha kunakuwepo na ushirikiano wa karibu kati ya Sekta Binafsi, Serikali na Wadau wengine katika Sekta hii ya Mazao ya Bustani. Huu ulikuwa ni uamuzi mzuri ambao utasaidia sana kuimarisha Sekta hii hasa kama ushirikiano huu utatumika kikamilifu. Nawapongezeni kwa uamuzi huo mzuri wa kushirikisha Wadau wote katika masuala ya Mazao ya Bustani.
Ndugu Washiriki,
Nimefurahi kusikia kwamba, Baraza la Kuendeleza Mazao ya Bustani Tanzania liliundwa na kuzinduliwa rasmi wakati wa Mkutano wa Pili wa Wadau uliofanyika Mwezi Aprili 2008. Nimefarijika zaidi kusikia kwamba Baraza hili limejumuisha Wajumbe wa Halmashauri za Wilaya. Kwa ujumla Halmashauri zetu ndizo ziko karibu na Wananchi ambao ndiyo Wadau Wakubwa wa uzalishaji wa Mazao ya Bustani. Nikiangalia kwa haraka haraka, hali ya maandalizi ya Mkutano naweza kusema kwamba, Baraza limeanza vizuri. Waswahili wanasema “Nyota Njema Huonekana Asubuhi”. Kila kitu kimepangiliwa vizuri. Aidha, Ushirikiano kati ya Serikali na Sekta Binafsi katika kuendeleza Sekta ya Mazao ya Bustani Tanzania unajitokeza bayana. Naomba nitumie nafasi hii na kwa kipekee kabisa kumpongeza Mwenyekiti wa Baraza hili pamoja na Wajumbe wote wa Baraza kwa maandalizi mazuri ya Mkutano huu.
Umuhimu wa Mazao ya Bustani
Ndugu Washiriki,
Mazao ya Bustani hususan Matunda na Mbogamboga yana umuhimu mkubwa katika Uchumi wa Taifa letu. Aidha, Mazao haya ni muhimu kwa matumizi ya Chakula kwa Watanzania wengi. Kwa mfano, zao la Ndizi ni zao muhimu siyo tu katika Mikoa ya Kagera, Kilimanjaro, Mbeya na Arusha, bali sasa zao hili limejipatia umaarufu mkubwa katika maeneo mengi na hivyo kuwa sehemu muhimu ya lishe ya Wananchi. Aidha, Mazao ya Mboga Mboga kama vile Nyanya, Mchicha, Kabichi, Mlenda, Kisamvu, Mnavu, ni mazao muhimu kwa matumizi ya mboga kwa Wananchi wengi.
Hivi leo wengi wetu tunafahamu kuwa Ugali au Wali bila mboga za majani, chakula chenye lishe hakijakamilika. Mazao ya matunda hususan Maembe, Machungwa, Mananasi, Mapesheni na Ndizi Mbivu ni sehemu muhimu na ya lazima kwa lishe ya Binadamu. Mazao haya hutoa viini vingi kwa Chakula bora na kwa bei nafuu. Pamoja na kuwa ni chanzo muhimu cha Viinilishe na Virutubisho kwa ajili ya ukuaji na kinga katika miili yetu, mazao hayo pia ni chanzo muhimu cha kipato kwa Wananchi wengi hususan wa Vijijini.
Ndugu Wajumbe,
Najua ziko tamaduni ambazo bado kuna Wenzetu ambao kula matunda au hata mboga za majani ni jambo ambalo Mtu mzima hapaswi kulifanya hadharani. Hizi ni tamaduni ambazo zimepitwa na wakati na ni fikra ambazo hazitusaidii kwa afya zetu. Hizi ni tamaduni ambazo zinatufanya tusitumie kwa ufanisi mazao tuliyonayo kwa ajili ya afya zetu na za familia zetu. Iko haja ya kuweka mikakati maalum kuhimiza Wananchi wetu kutumia Mazao yatokanayo na Bustani kama chakula muhimu katika Familia zetu.
Takwimu zilizotokana na Mkutano wa Wadau wa Mazao ya Bustani (All African Horticulture Congress) tarehe 31 Agosti 2009 Mjini Nairobi Kenya, zinaonyesha kwamba, hivi sasa kiwango cha matumizi ya matunda Nchini kiko chini kwani ni takriban Moja ya Nane tu, sawa na Asilimia 12.5 ya kiwango kilichopendekezwa na Shirika la Afya Duniani, ndicho kinachotumika. Hiki ni kiasi kidogo sana! Inapaswa kuweka jitihada za dhati katika kuwaelemisha Wananchi umuhimu wa Matumizi ya Vyakula vya Mazao ya Bustani zikiwemo Mbogamboga. Kuna msemo mzuri sana unaosema “A Fruit a Day Keeps a Doctor Away”ikiwa na maana kwamba ukila tunda kwa siku unajenga Afya njema na hutaonana na Daktari mara kwa mara kwa maradhi madogomadogo.
Mapato ya Mazao ya Bustani
Ndugu Washiriki,
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa, kuanzia miaka ya 1990, Mazao ya Mboga, Matunda na Viungo yalikuwa yakipata Soko zuri lenye uhakika wa bei nzuri katika Masoko ya Nje ya Nchi na katika Soko la Dunia. Kwa mfano, Maua mengi yaliuzwa Uholanzi, Matunda yaliuzwa Mashariki ya Kati na Mbogamboga ziliuzwa zaidi Uingereza. taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa, Mapato yanayotokana na mauzo ya Mazao ya Matunda na Mbogamboga yalifikia takriban Dola za Kimarekani Milioni 345 mwaka 2008. Vilevile, Mazao ya Bustani yameanza kupata umuhimu kama Mazao makubwa ya Biashara kwa mfano, Kahawa, Pamba, Korosho na Sukari. Hii ni taarifa nzuri kwa Wakulima wa Mazao haya ya Mbogamboga ambayo inawapa moyo waongeze bidii katika uzalishaji.
Tofauti na Mazao mengine, Mazao ya Mboga Mboga na Matunda na yanaweza kuzalishwa katika maeneo yote Nchini kwa mwaka mzima kama tukitumia Wataalam vizuri. Mengi ya mazao hayo huhitaji muda mfupi wa takriban miezi mitatu tangu kuyapanda hadi kuvuna. Aidha, aina bora za miche ya Matunda nayo huchukua Wastani wa miaka mitatu toka kupandwa hadi mavuno ya Matunda ya kwanza ikilinganishwa na Wastani wa miaka 7 hadi 9 iliyokuwa ikihitajika awali kwa zao la Maembe na Machungwa. Hivyo, mazao haya yana uwezo mkubwa wa kuwapatia Wananchi kipato cha uhakika kwa muda mfupi na hivyo kupunguza umaskini. Katika kipindi cha hivi karibuni kwa mfano, mwaka 2008/2009, Uzalishaji ulifikia Tani 560,000 za Matunda, Tani 602,000 za Mboga na Tani 6,860 za Mazao ya Viungo ambayo yote kwa ujumla yaliliingizia Taifa takriban Shilingi Bilioni 195.
Mazao ya Maua
Ndugu Mwenyekiti,
Kwa upande wa Mazao ya Maua, historia inaonyesha kwamba biashara ya Maua hapa Tanzania ilianza zamani kuanzia miaka ya 1950 kwa kuuza mbegu za Maua katika Nchi za Ulaya. Hadi miaka ya 1990, Ukuaji wa Sekta ya Maua ulifikia kati ya Asilimia 8 – 10. Takwimu zinaonyesha mauzo yalifika Wastani wa Dola za Kimarekani Milioni 160 kwa mwaka. Aidha, Watanzania takriban Milioni Mbili (2) walifaidika na biashara ya Maua. Katika miaka ya 2000 Sekta hii imekuwa na mafanikio ya jumla yafuatayo:-
(i) Kumekuwepo na ukuaji endelevu katika biashara hii. Uwekezaji mpya umefikia Asilimia 61 wakati upanuaji wa Uwekezaji wa zamani umefikia Asilimia 23;
(ii) Mazingira ya kazi yameboreshwa hususan baada ya kuongezeka kwa ushirikiano kati ya Sekta Binafsi na Sekta ya Umma;
(iii) Mapato yatokanayo na Mauzo ya Maua yameongezeka kutoka Dola za Kimarekani Milioni 1.4 mwaka 2001/2002 hadi Milioni 140 mwaka 2007/2008; na
(iv) Ajira imeongezeka kutoka Watu 12,000 mwaka 2006 hadi Watu 20,019 mwaka 2009.
Changamoto
Ndugu Washiriki,
Pamoja na uwezekano mkubwa wa uzalishaji wa Mazao ya Bustani na juhudi kubwa zinazofanywa na Wakulima Nchini, bado Kilimo cha Mazao ya Bustani kinakabiliwa na changamoto nyingi. Moja ya changamoto hizo nitija ndogo inayotokana na Kilimo kisichofuata Kanuni za Kilimo Bora hasa matumizi ya mbegu duni, matumizi yasiyo sahihi ya pembejeo na mashambulizi ya visumbufu. Huduma za Ugani ikiwa ni pamoja na uhaba wa Wagani na upatikanaji wa pembejeo nalo ni tatizo katika uzalishaji wa Mazao ya Bustani. Kwa maana hiyo, tija kiuzalishaji iko chini ikilinganishwa na fursa zilizopo.
Kwa mfano, tija kwa zao la Nyanya likizalishwa kwa kufuata Kanuni za Kilimo Bora, inaweza kumpatia Mkulima Tani 60 hadi 80 kwa Hekta. Hivi sasa, Wakulima wa Nyanya hapa Nchini Wanapata Wastani wa Tani 20 kwa Hekta ambazo ni sawa na Asilimia 25 ya uwezo wa kuzalisha. Kabichi uwezo upo wa kuzalisha Tani 40 lakini tija kwa Wakulima ni Tani 15 ambazo ni sawa na Asilimia 37.5.
Tija katika zao la Ndizi uwezo ni Tani 75 kwa Hekta lakini tunazalisha Wastani wa Tani 20 sawa na Asilimia 26.7; Machungwa uwezo ni Tani 45 Wakulima wanapata Tani 10 sawa na Asilimia 2; Mananasi uwezo ni Tani 60 lakini Wakulima wanapata Tani 20. Tunaweza kuendelea, na orodha ndefu kwa sababu bado Mazao mengi hatujafikia Wastani wa tija inayowezekana kwa kila zao tunalolizalisha. Hii ni changamoto kubwa ambayo inahitaji ushirikiano wa karibu kwa Wadau wote ili kuwawezesha Wakulima kufikia Viwango bora vya Tija kwa Mazao wanayoyazalisha.
Ndugu Washiriki,
Changamoto nyingine inayokabili Uzalishaji wa Mazao ya Bustani ni kiasi kikubwa cha Upotevu wa Mazao baada ya kuvunwa (Post Harvest Losses). Takwimu zinaonesha kwamba takriban Asilimia 30 hadi 50 ya Mazao ya Mboga na Matunda hupotea baada ya kuvuna kutokana na utunzaji mbaya, mashambulizi ya visumbufu na kukosekana kwa huduma za usindikaji, uhifadhi na Soko lenye uhakika. Viwango hivyo vya upotevu ni vikubwa ambavyo inabidi kuvitafutia ufumbuzi. Suala hili ni muhimu kufanyiwa kazi kwani likifanikiwa tutaweza kuongeza upatikanaji wa mazao mengi zaidi kwa takriban mara mbili.
Ndugu Washiriki,
Inasadikiwa kwamba Asilimia 80 ya Mazao mengi Makuu ya Biashara tunayoyazalisha yanauzwa Nje ya Nchi. Wanunuzi hao ndio wanaopanga bei za mazao hayo. Aidha, Wastani wa bei za Mazao hayo katika Soko la Dunia imekuwa ikishuka na hivyo Pato la Mkulima na Pato la Taifa kushuka. Matokeo yake, Wakulima wamekuwa wakilazimika kupunguza uzalishaji au kutafuta mazao mbadala. Yapo maeneo ambayo Wakulima wamediriki kung’oa Mazao yao na kupanda Mazao Mbadala ili kupata Soko la uhakika.
Ndugu Washiriki,
Kwa upande wa Mazao ya Maua, mtakumbuka ni hivi karibuni tu, kulitokea msukosuko wa Uchumi Duniani ambapo bei ya Mazao yanayouzwa Nje ilitetereka. Kwa Wakulima wa Maua wao pia walipata msukosuko kutokana na kufungwa kwa Viwanja vya Ndege katika Bara la Ulaya kutokana na Vumbi la Volkano kule Ireland. Kiasi cha Euro 250,000 sawa na Shilingi za Tanzania Milioni 500 zilikuwa zikipotea kila siku kutokana na kutosafirisha Mazao ya Maua kwenda kwenye Masoko ya Ulaya kama vile Uholanzi na Uingereza. Hii ni hasara kubwa! Aidha, hata baada ya Viwanja kufunguliwa, bado ule mtikisiko uliathiri masoko ya bidhaa hizi na hivyo kuathiri Mapato ya Wakulima na Wafanyabiashara. Yote haya ni matukio yanayotupa changamoto zaidi zinazokabili Sekta hii. Nitumie fursa hii kuwapongeza sana Wakulima wa Mazao ya Bustani kwa mchango wenu na wa muhimu katika Uchumi wa Taifa na kwa kutokata tamaa.Kinachotakiwa sasa ni kufanya ubunifu wa kukabiliana na Changamoto hizi.
Ndugu Washiriki,
Nimetumia mifano hii michache kuonyesha changamoto hizo ambazo zinahitaji ufumbuzi wa haraka. Nimeelezwa kwamba katika Mkutano wa mwaka 2008 suala hili lilijadiliwa na kuazimia kuandaa Mkakati wa kukabiliana na Changamoto hizi. Nimefurahi kusikia kwamba Rasimu ya Mkakati huo iliyoandaliwa kwa kushirikisha Sekta Binafsi, Wizara na Taasisi nyingine za Serikali ni moja ya Agenda itakayojadiliwa katika Mkutano huu kwa ajili ya kupata maoni ya Wadau wote. Matumaini yangu ni kwamba Wajumbe wa Mkutano huu Watatoa maoni yao kwa uwazi kuhusu Rasimu hii ili kupata mapendekezo mahsusi ambayo yatasaidia sana katika kuboresha Sekta hii ya Mazao ya Bustani.
Hatua za Kuchukua
Ndugu Mwenyekiti,
Takwimu za Ajira, Uzalishaji na Mauzo zimeonyesha kuwa Sekta hii ya Mazao ya Bustani inachangia kwa kiasi kikubwa katika Uchumi wa Taifa. Tumeona Ajira imeongezeka kutoka 12,000 mwaka 2006 hadi 20,019 mwaka 2009. Uzalishaji wa Mazao ya Bustani umeongezeka toka Tani 40,602, mwaka 2001/2002 hadi 92,250 mwaka 2007/2008 na hivyo mauzo kuongezeka kutoka Dola za Kimarekani 63,400 mwaka 2001/2002 hadi 140,340 mwaka 2007/2008. Kwa kutambua mchango wa Sekta hii katika Uchumi, kuna umuhimu wa kufanya mambo yafuatayo:
(i) Ipo haja ya kupanua ushiriki wa Wizara za Serikali katika Baraza la Sekta hii. Hivi sasa, ni Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika na Wizara ya Viwanda Biashara na Masoko pekee ambazo zina Wawakilishi ambao ni Wajumbe wa Baraza. Nashauri kuwa ni muhimu Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Wizara ya Fedha na Uchumi na Wizara ya Miundombinu ziwe na Wajumbe katika Baraza lenu ili kufanikisha malengo ya Sekta hii katika kuendeleza Mazao ya Bustani Tanzania;
(ii) Upo umuhimu wa Baraza kuandaa mapendekezo ya nini kifanyike chini ya Kaulimbiu ya KILIMO KWANZA ili kuimarisha mazingira ya uzalishaji wa Mazao ya Bustani Nchini. Mapendekezo hayo yazingatie mahitaji ya watoa huduma muhimu kama pembejeo na Wasindikaji wa Mazao ya Bustani. Serikali inaahidi itayapokea na kuyafanyia kazi mapendekezo hayo kikamilifu.
(iii) Upo umuhimu wa kuongeza kwa kasi ya kuanzisha Viwanda vya Usindikaji wa Mazao yanayozalishwa hapa Nchini ili kupunguza upotevu wa mazao. Pamoja na kwamba uwekezaji katika eneo hili unahitaji mtaji mkubwa, bado hasara inayopatikana kwa kutosindika mazao hayo kila mwaka ni kubwa zaidi. Natumaini Washiriki wa Semina hii mtapata muda mzuri wa kutoa mapendekezo ambayo yataainisha nini wajibu wa Sekta Binafsi na ule wa Serikali katika kuendeleza Sekta hii.
(iv) Ni muhimu mchango mahsusi wa Sekta Binafsi uonekane dhahiri hasa katika kuainisha Rasilimali Fedha na Rasilimali Watu zitakazoelekezwa katika Sekta hii. Ipo dhana inayoanza kujengeka kuwa Serikali itafanya kila kitu na mara nyingine Sekta Binafsi inaomba kusamehewa kodi. Dhana hii si sahihi. Ni muhimu Sekta Binafsi nayo ionyeshe jinsi itakavyochangia utekelezaji wa Kaulimbiu ya KILIMO KWANZA kwa dhati.
(v) Mamlaka za Serikali za Mitaa na Taasisi nyingine za umma ambazo kulingana na wajibu wao wanahusika na uendelezaji wa Mazao hayo zitoe kipaumbele kwa Mazao ya Bustani katika mipango yao kwa kuwa mazao haya yanatoa fursa kubwa na kwa muda mfupi kuwaongezea kipato Wananchi wengi.
(vi) Tuongeze jitihada za kuvutia Wawekezaji wa Ndani na Nje waje kuwekeza katika uzalishaji wa Kibiashara wa Mazao ya Bustani. Aidha, ni vizuri kusisitiza utaratibu wa kuanzisha Kilimo cha Mkataba (Contract Farming) baina ya Wazalishaji Wadogo wa Mboga Mboga na Wafanyabiashara wanaouza Mazao haya ili Wazalishaji Wadogo wawe na uhakika wa Soko, Bei na kuepuka upotevu wa Mazao.
Hitimisho
Ndugu Mwenyekiti, Wajumbe wote wa Mkutano, Mabibi na Mabwana,
Nimalizie kwa kuwashukuru tena wote mliojumuika hapa kwa kuonyesha nia ya kusaidia Sekta ya Mazao ya Bustani. Nawashukuru Wahisani wetu kwa kusaidia katika kufanikisha malengo yake. Sisi kama Serikali tunatambua umuhimu wa mchango wao katika kutoa elimu, maarifa na uzoefu kwa Wataalam kwa Wakulima wa Tanzania. Wito wangu kwa Wahisani wetu ni kuwaomba waendelee na moyo huo wa kujitolea. Aidha, nawaagiza Wataalam na Wakulima wanaopata fursa ya kupata mafunzo kutoka kwa Taasisi na Asasi hizo wafuatilie kwa umakini ushauri wanaopewa ili juhudi hizo zitoe matunda yanayotegemewa.
Ndugu Mwenyekiti, Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana,
Mwisho, napenda tena kuwashukuru kwa kujumuika pamoja katika Mkutano huu muhimu. Baada ya kusema hayo, sasa natamka rasmi kuwa Mkutano wa Tatu wa Kitaifa wa Wadau wa Mazao ya Bustani Nchini umefunguliwa.
Asanteni sana kwa kunisikiliza |