Home | Speech
Speech
Speeches

Hotuba ya Shukrani kwa Wabunge kabla ya Mkutano wa Ishirini wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Kuvunjwa na Mheshimiwa Rais, Ukumbi wa Bunge, Dodoma, 15 Julai 2010...

Hotuba ya Mheshimiwa Mizengo P. Pinda (Mb) Waziri Mkuu Wakati wa Kufungua Kongamano la Vijana wa Vyuo Vikuu vya Dodoma katika Ukumbi wa African Dreams – Dodoma, tarehe 25 Juni 2010...

More Speeches
Recently Documents

kk Quotes

kama Bunge, lakini mmoja mmoja kama watumishi wa umma, tunao wajibu mkubwa sana wa kuishi na kutenda kwa mfano. Tujiepushe na tamaa zinazoweza kuliingizia Taifa hili hasara kubwa.

Kauli ya Waziri Mkuu kuhitimisha mjadala wa Richmond,
Mkutano wa 18 wa Bunge, Februari 10, 2010
More Quotes
Videos
Photo Gallery

16 of us
More Photos
Documents and Publications


mgPrint friendly version mg Email this page
HOTUBA YA MHESHIMIWA MIZENGO P. PINDA (MB), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA AKIONGOZA MATEMBEZI YA HISANI YA
ASASI YA SARATANI YA MATITI TANZANIA (TBCF)
TAREHE 25 APRILI, 2010, DAR ES SALAAM
 
Mheshimiwa Prof. David Mwakyusa, (Mb.), Waziri wa
Afya na Ustawi wa Jamii;
 
Mheshimiwa William Lukuvi, (Mb.), Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam;
 
Mheshimiwa Mama Anna Mkapa, Mlezi wa Asasi ya
Saratani ya Matiti Tanzania;
 
Mama Angela Kuzilwa, Mwenyekiti Mtendaji wa Asasi ya
Saratani ya Matiti Tanzania;
 
Dkt. Twalib Ngoma, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya
Saratani, Hospitali ya Ocean Road;
 
Wadau na Washiriki wa Matembezi haya;
 
Wageni Waalikwa;
 
Mabibi na Mabwana.
 
Nianze kwa kukushukuru wewe Mkurugenzi Mtendaji kwa kunialika kuongoza Matembezi ya Hisani ya Asasi ya Saratani ya Matiti Tanzania. Nawashukuru pia Wadau na Wananchi kwa ujumla kwa kuitikia wito wa kushiriki kwa hali na mali katika Matembezi haya. Shukrani za pekee ziwaendee Susan Komen Foundation kwa kushirikiana nasi kwa karibu katika kupambana na Saratani hapa Tanzania.
 
Ndugu Wananchi,
Taarifa zilizopo zinaonyesha kwamba mwaka 2008 matembezi kama haya yalifanyika hapa Dar es Salaam ambapo Shilingi 42,006,955 zilikusanywa. Hii imeiwezesha Asasi hii kuongeza ufanisi katika kuwahudumia Wanachama na kutoa elimu kwa jamii juu ya kutambua mazingira ya kuishi na Ugonjwa huu, hususan baada ya kupata tiba ya upasuaji hospitalini. Tumaini langu ni kwamba Matembezi haya ya leo yataongeza hamasa na uelewa wa Watanzania juu ya Asasi hii na Ugonjwa wa Saratani ya Matiti ili kujiunga  nayo na kuichangia zaidi.
 
Ujasiri wa Wagonjwa
 
Ndugu Wananchi,
Nimefarijika kuona Wagonjwa ambao kwa hali ya kawaida wangeweza kusononeka na kila mara kujisikia kwamba wao ni Wagonjwa, lakini leo wametuita kujumuika nao kufanya Matembezi haya ya Hisani. Nichukue nafasi hii kuwapongeza Wanachama wote wa Asasi hii ya Saratani ya Matiti Tanzania kwa uamuzi wa kuanzisha Chama hiki. Huu ni Ujasiri Mkubwa na faraja kwa Wagonjwa wote wa Saratani ya Matiti ambao wengine walikwishakata tamaa. Hii inadhihirisha usemi kwamba, “Kuugua Siyo Kufa”. Wanachama hawa sasa wanaweza kutoa huduma kwa Wagonjwa wenzao kwa njia ya Elimu na kuhamasishana. Nawapongeza Sana! Wito wangu kwa Wagonjwa wote wa Saratani ya Matiti ni kujiunga na Chama hiki ili kuweza kuweka nguvu za pamoja katika kupambana na Ugonjwa huu. Umoja ni Nguvu na ni faraja kubwa kwa wote wenye Saratani ya Matiti. Unapojiunga na Wenzako, unapata faraja kwa kubadilishana mawazo kuhusu Ugonjwa huu.
 
Ukubwa wa Tatizo
 
Ndugu Wananchi,
Saratani ya Matiti ni Ugonjwa ambao tiba yake ni ngumu na ya gharama kubwa. Tumeambiwa kwamba takriban Watu 40,000 hapa Tanzania wanapata Saratani kila mwaka, ambapo Asilimia 12 kati ya hao wana Saratani ya Matiti. Hii ni idadi kubwa ya Wagonjwa kwa mwaka. Takwimu zilizopo kutoka Hospitali ya Saratani – Ocean Road zinaonyesha kuwa Wanawake zaidi ya 3,000 hapa Nchini wanapata Ugonjwa huu kila mwaka ambapo ni Asilimia 10 tu ndio wanaofika Hospitali kwa matibabu na wengi wao wakiwa wamechelewa. Leo hii, tunaambiwa kila baada ya Sekunde 68 kuna Mwanamke mmoja anayekufa Duniani kutokana na Ugonjwa wa Saratani ya Matiti. 
 
Tumesikia pia taarifa za kusikitisha kwamba kati ya Wanachama Waanzilishi 215 wa Asasi ya Saratani ya Matiti Tanzania, hivi sasa wamebaki 118 tu. Wengine 107, sawa na Asilimia 49.8 wamefariki katika kipindi kifupi tangu Chama hiki kuanzishwa. Takwimu hizi pamoja na kusikitisha, zinaonyesha pia kwamba kuna umuhimu wa kuwa na mipango dhabiti ya kufanya uchunguzi mapema wa ugonjwa huu hatari, hususan kwa Wanawake hasa wenye umri kuanzia miaka 40 na kuendelea. Nitumie fursa hii kuwapongeza kwa dhati Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania (Medical Women Association of Tanzania – MEWATA) kwa kuwa mstari wa mbele katika kutoa Elimu ya kutambua Saratani ya Matiti kupima na kutibu. Juhudi zao zinaonekana. Tunawashukuru kwa kazi nzuri.
 
Changamoto
 
Ndugu Washiriki,
Tunazo Changamoto kubwa mbele yetu kuhusu Ugonjwa wa Saratani ya Matiti:
 
Kwanza: Ni jinsi tunavyojipanga katika kupambana na Ugonjwa huu. Kwa mfano, kwa bahati nzuri kwa sasa tunayo Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii; Tunayo Taasisi ya Saratani ya Ocean Road; Tunacho Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania, pia kuna Chama cha Afya ya Jamii Tanzania. Tumeambiwa hapa pia kwamba kuna Chama cha Kupambana na Tumbaku Tanzania, na leo tuna Asasi hii ya Saratani ya Matiti. Ni dhahiri hizi ni juhudi zinazoonekana za kutambua na kupambana na Ugonjwa huu. Inawezekana kila mmoja kufanya shughuli ki-vyake vyake, japo lengo ni kuwasaidia wenye matatizo ya Saratani ya Matiti. Tunahitaji kuunganisha nguvu hizi kwa pamoja. Kama tukijipanga vizuri na kushirikiana kufanya kazi kwa malengo ya pamoja, matokeo yanaweza kuonekana mazuri zaidi. Hili linawezekana!
 
Pili:    Ugonjwa wa Saratani ya Matiti unatibika kama ukipimwa na kugundulika mapema. Changamoto kubwa ni namna ya kukubali kupima mapema. Ni lazima sasa kuweka juhudi kubwa zaidi za kuelimisha Wananchi kuhusu umuhimu wa kupima mapema. MEWATA wametuonyesha njia na wanafanya kazi kubwa. Tuwaunge mkono wote. Tuwajengee Wananchi utamaduni wa kupenda kupima. Mimi ninaamini hili pia linawezekana kama tukijipanga vizuri.
 
Tatu: Bado kuna Woga na Hofu mtu anaposikia kwamba fulani ana Saratani ya Matiti. Hofu inayosababisha tabia ya Unyanyapaa wa aina yake. Tuwaelimishe Wananchi wajue kwamba Ugonjwa wa Saratani ya Matiti ni Ugonjwa unaotibika na kama tukijenga utamaduni wa kupima mapema, hofu hii itaondoka na madhara yake yatapungua.
 
Nne:   Tunayo Hospitali moja Maalum inayotoa Tiba ya Saratani hapa Nchini hivyo kusababisha wengi wa Wagonjwa kutopata huduma mapema. Hii ni Changamoto kwa Serikali na Wadau wake kufikiria namna ya kusambaza huduma hii sehemu zingine Nchini. Hili litasaidia kupunguza idadi ya Vifo vinavyotokana na Saratani ya Matiti.
 
Tano: Kuna tatizo kubwa la vifaa maalum vya kuwasaidia Wanawake wenye tatizo la Saratani ya Matiti. Bado hii ni Changamoto kubwa inayohitaji kufanyiwa kazi. Serikali iko tayari kushirikiana na Taasisi zote zenye kuonyesha nia katika kupambana na Ugonjwa huu.
 
Hitimisho
 
Ndugu Washiriki,
Nimalizie kwa kuwapongeza tena Viongozi na Wanachama wa Asasi ya Saratani ya Matiti  na wale wote wanaojitolea kufanya kazi mbalimbali za Asasi hii kwa juhudi zao katika kudhibiti Ugonjwa huu. Ugonjwa wa Saratani ya Matiti ni wa kawaida kama tukipima na kuutambua mapema. Tusiuogope. Nirudie kutoa Wito kwa Wananchi wote, hususan Wanawake kujenga tabia ya kujipima mapema ili kubaini ugonjwa mapema.
 
Tumeambiwa kwamba kuna asilimia ndogo ya Wanaume ambao wamebainika kuwa na Saratani ya Matiti. Kwa maana hiyo Wanaume nao wasijiweke pembeni katika kupima. Aidha, jukumu kubwa la Wanaume ni kushiriki katika kuhamasisha Wanawake ambao ndio Asilimia kubwa ya Waathirika ili waweze kupima na kubaini Ugonjwa huu mapema.
 
Mwisho niwashukuru tena kwa wote mlioamua kushiriki katika Matembezi haya Asubuhi ya leo. Tumetembea kwa pamoja kuonyesha kuunga mkono juhudi za kupambana na Ugonjwa huu. Tuendelee kuwa na Moyo wa Kusaidiana, Moyo wa Upendo na Moyo wa kuchagia huduma hii muhimu ya kuokoa maisha ya Binadamu wenzetu.
 
 
Asante sana kwa kunisikiliza.
 
 

 

 

 

Help | Disclaimer | Privacy | Site Feedback
Copyrights ©2008-2010, The United Republic of Tanzania, Prime Minister All Rights Reserved
Designed and published by DataVision International (T) Ltd